Mjumbe wa Taliban anyimwa fursa kuhutubia kikao cha UN

Na AFP

MKUTANO wa Mataifa wanachama wa Umoja wa Mataifa (UNGA) ulimazilika jana, huku mwakilishi wa kundi la Taliban linaloongoza Afghanistan akizuiliwa kuhutubia kongamano.

Mwakilishi wa serikali ya Myanmar pia alinyimwa fursa ya kuhutubia viongozi wa nchi 100 walipokutana jijini New York, Amerika, kufuatia utata wa kisiasa katika nchi hiyo.

Mwakilishi wa Afghanistan katika Umoja wa Mataifa (UN), Ghulam Isaczai, aliratibiwa kuhutubia kongamano la UNGA kabla ya kufungwa baadaye jana.

Lakini kundi la Taliban lilimwandikia barua Katibu Mkuu wa UN, Antonio Guterres, likitaka Isaczai asiruhusiwe kuhutubu likishikilia kuwa halimtambui.Kundi la Taliban lilisema kwamba Isaczai aliteuliwa na Rais Ashraf Ghani aliyeng’olewa mamlakani mwezi uliopita, ‘hivyo kazi yake iliisha’.

Badala yake, kundi hilo lilimtaka Guterres kuruhusu waziri wa mashauri ya kigeni wa serikali ya Taliban, Amir Khan Muttaqi, aruhusiwe kuhutubia UNGA.

Kamati kuu ya UNGA inayojumuisha mataifa ya Amerika, China na Urusi iliahidi kufanya mkutano wa dharura kujadili ombi hilo la Taliban.

Mkutano huo wa kamati, hata hivyo, haukufanyika.Baadaye, maafisa wa UN walisema kuwa ombi hilo la Taliban lilichelewa na wakaruhusu Isaczai kuhutubia kongamano.Isaczai alitumia fursa hiyo kusihi UN kuongeza vikwazo dhidi ya serikali ya Taliban.

Mwakilishi wa Myanmar katika Umoja wa Mataifa, Kyaw Moe Tun, alizuiliwa kuhutubu kwa sababu nchi yake inakumbwa na msukosuko wa kisiasa.

Tun aliteuliwa na Rais Aung San Suu Kyi, aliyeng’olewa mamlakani kupitia mapinduzi ya kijeshi mnamo Februari, mwaka huu.Mnamo Mei, mwaka huu, wanajeshi waliteua jenerali wa jeshi wa zamani, lakini UN haijaidhinisha uteuzi wake.

Mwakilishi wa Guinea katika UN, Aly Diane, aliruhusiwa kuhutubia kongamano. Diane aliteuliwa na Alpha Conde aliyepinduliwa mapema mwezi huu na kundi la wanajeshi. Serikali ya jeshi inayoongozwa na Kanali Mamady Doumbouya, haikutuma mwakilishi wake katika kongamano la UNGA.

Shirika la Maendeleo la Mataifa ya Afrika Magharibi (Ecowas) tayari limewekea Guinea vikwazo huku likitaka wanajeshi wakabidhi mamlaka kwa utawala wa kiraia.

Hiyo ilikuwa mara ya kwanza kwa viongozi wa nchi mbalimbali kukutana ana kwa ana tangu kutokea kwa mlipuko wa virusi vya corona duniani.

Viongozi wa nchi kadhaa, akiwemo Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya na mwenzake wa Ufaransa Emmanuel Macron, walihutubia kongamano hilo kwa njia ya video.

Miongoni mwa viongozi waliohudhuria kongamano hilo na kupata fursa ya kuhutubu ni Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania na kiongozi mpya wa Zambia Hakainde Hichilema.

MARY WANGARI: Kongamano la UN litumiwe kuimarisha mifumo ya uzalishaji lishe

Na MARY WANGARI

UMOJA wa Mataifa (UN) umeonya serikali za dunia kuwa majanga yanayozidi kuchipuka kila uchao yataendelea kushuhudiwa iwapo mikakati thabiti ya kukabiliana na kiini cha matatizo hayo haitabuniwa.

Kwa mujibu wa shirika hilo la kimatiafa, kila wakati majanga yanapotokea, viongozi wa mataifa wamekuwa wakijishughulisha na suala la “nini” kilitendeka na kupuuza “ni kwa nini” kilitendeka.

Shirika hilo limeashiria hofu kuwa matatizo hayo kama vile mafuriko, maporomoko ya ardhi, ukame na njaa, mikurupuko ya maradhi, mioto nyikani na kadhalika, yatazidi kushuhudiwa iwapo mikakati jumuishi ya kudhibiti majanga hayo haitabuniwa.

Kauli yake imejiri wakati mwafaka baada ya hatua ya Rais Kenyatta wiki jana kutangaza ukame unaohangaisha wananchi Kaskazini ya Kenya kuwa janga la kitaifa.

Tangazo hilo lilijiri wakati kaunti 12 miongoni mwa 23 katika maeneo kame, tayari zinaathiriwa na makali ya ukame na ukosefu wa chakula.

Kwa miongo mingi, wadau katika sekta ya kilimo hawajakuwa wakitilia maanani michakato muhimu inayohusika wakati wakulima wanapoenda shambani na chakula kinapowafikia watu mezani.

Kuanzia upanzi wa mbegu za kiwango cha juu, vifaa bora vya kilimo, mifumo kabambe ya kuvuna na kuhifadhi mazao na usafirishaji ni baadhi tu ya masuala muhimu yanayohusika kuhakikisha kuwepo kwa chakula cha kutosha nchini.

Mbali na hayo, kuna suala nyeti kuhusu uhifadhi wa mazingira kwa kujiepusha na ukataji miti kiholela na kuvuruga chemchemi za maji ili kuzuia athari hasi za mabadiliko ya hali ya hewa.

Inavunja moyo kuwa licha ya maendeleo katika Sayansi na Teknolojia, Kenya hupoteza kiwango kikubwa cha mazao kutokana na mbinu duni za kuvuna na kuhifadhi mazao.

Mahangaiko

Si ajabu basi kwamba mwaka baada ya mwaka huwa tunashuhudia mamia ya raia wakihangaishwa na ukame hasa wakati ulimwengu unagubikwa na mabadiliko ya anga.Matokeo yake ni utapiamlo hasa miongoni mwa watoto na vita baina ya jamii za wafugaji na wakulima kung’ang’ania raslimali chache zilizosalia za malisho na maji.

Serikali imejitahidi kutimiza Ajenda Nne Kuu kuhusu Ruwaza 2030, mojawapo ikiwa kuhakikisha kuwepo kwa Chakula na Lishe ya Kutosha kwa Wakenya wote.Ili kufanikisha maazimio hayo, mikakati madhubuti inahitajika kubuniwa kwa dharura kuimarisha mifumo ya uzalishaji chakula.

Kongamano Kuu la UN kuhusu Mifumo cha Chakula Duniani litakaloandaliwa Septemba 23, litakuwa fursa kwa wadau kujadili mikakati ya kuimarisha mifumo ya chakula nchini.

mwnyambura@ke.nationmedia.com

Covid-19: UN yarai mataifa kuanza kufungua shule zao

Na AFP

GENEVA, Uswisi

UMOJA wa Mataifa (UN) umezirai nchi ambazo bado zinaendelea kufunga shule kutokana na janga la virusi vya corona kuzifungua, ili kuwaruhusu wanafunzi kurejelea masomo yao.

Umoja huo ulisema kuwa hali hiyo inawaathiri zaidi ya watoto 600 milioni kote duniani, ikivuruga pakubwa mpangilio wa masomo yao.

“Hali haiwezi kuendelea namna hii,” akaeleza James Elder, ambaye ndiye msemaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Maslahi ya Watoto (UNICEF) kwenye kikao na wahahabari jijini Geneva, Uswisi.

Ingawa alikubali nchi nyingi zinakabiliwa na wakati mgumu kufanya maamuzi kuhusu njia za kukabili janga hilo, alieleza “shule zinapaswa kuwa taasisi za mwisho kufungwa na za kwanza kufunguliwa.”

Alisema ni makosa kwa nchi kufungua upya baa na vituo vya burudani kabla ya kufungua shule.

“Si lazima walimu na wanafunzi wote kupewa chanjo ndipo shule ziweze kufunguliwa,” akasema.

Alizirai nchi kutopunguza fedha zinazoitengea sekta ya elimu licha ya changamoto za kiuchumi zilizosababishwa na janga hilo.

Barani Ulaya, wanafunzi wengi wako likizoni. Hata hivyo, inakisiwa kuwa karibu nusu ya wanafunzi wote katika maeneo ya mashariki na kusini mwa Afrika wamo majumbani mwao kutokana na athari za janga hilo.

Kijumla, zaidi ya watoto 32 milioni wanakisiwa kuwa nyumbani katika maeneo hayo baada ya shule kufungwa kutokana na athari zinazohusiana na janga hilo.

Nchi nyingi zimekuwa zikilazimika kufunga shule mara tu baada ya kiwango cha maambukizi kuanza kuongezeka.

Hilo linaifanya hali hiyo kudorora kwani kabla ya janga kutokea, ilikisiwa watoto karibu 37 milioni hawakuwa wakienda shuleni licha ya kufikisha umri unaohitajika.

Katika bara Asia na eneo la Pacific, shule katika eneo hilo zimefungwa kwa zaidi ya siku 200 kutokana na janga hilo.

Katika eneo la Amerika Kusini na Carribean, nchi 18 zimefunga shule zake ili kudhibiti maambukizi ya virusi hivyo.

“Kutokana na hali hiyo, nchi sasa zimelazimika kukabili visa vya ghasia za kinyumbani, hali ya wasiwasi na ongezeko la mimba za mapema miongoni mwa wasichana,” akasema Elder.

Alitoa mfano wa Uganda, ambapo kati ya Machi 2020 na Juni 2021, taifa hilo lilirekodi ongezeko la karibu thuluthi moja ya mimba za mapema miongoni mwa wasichana walio kati ya umri wa miaka 10 na 24. Kulingana na shirika hilo, idadi kubwa ya wanafunzi hawawezi kumudu gharama za kushiriki masomo kwa njia ya mtandao.

UN yakerwa na video ya ngono

CHARLES WASONGA na MASHIRIKA

UMOJA wa Mataifa (UN) umeelezea kukerwa na video moja inayoonyesha mwanamume katika kiti cha nyuma cha gari akishiriki ngono na mwanamke nchini Israel.

Katika video hiyo ambayo ilizungushwa mitandaoni, mwanamke mwenye nguo nyekundu anafanya mapenzi na mwanamume mmoja katika kiti cha nyuma cha gari leupe lenye alama za UN.

Inadaiwa kuwa video hiyo ilinaswa katikati mwa jiji la Tel Aviv.

UN ilisema inachunguza kisa hicho na inakaribia kuwatambua walioko katika video hiyo.

Inaaminika kuwa wahusika ni wafanyakazi wa kikosi cha wanajeshi wa kulinda amani nchini Israeli, umoja huo ulisema.

Stephane Dujarric ambaye ni msemaji wa Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres, alitaja kitendo kinachoonekana katika video hiyo kama “kisichokubalika”.

“Mwenendo huo unaenda kinyume na juhudi zetu za kupambana na utovu wa nidhamu miongoni mwa wafanyakazi wa UN,” akasema Bw Dujarric.

Msemaji huyo alisema uchunguzi unaendelea kubaini ikiwa kitendo hicho cha kufanya mapenzi kilikuwa cha hiari au kilihusisha malipo.

Umoja wa Mataifa umeweka sheria kali inayopiga marufuku vitendo haramu vya ngono miongoni mwa wafanyakazi wake wanaolinda usalama katika mataifa mbalimbali ulimwenguni.

Wafanyakazi wanaokiuka sheria hii huadhibiwa kisha wakarejeshwa katika mataifa yao na kupigwa marufuku kushiriki shughuli za kulinda amani chini ya mwavuli wa UN.

Vilevile, ni wajibu wa mataifa ya washukiwa kuwachukulia hatua zingine za kinidhamu na za kisheria.

Kenya yapata kiti muhimu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

NA AGGREY MUTAMBO

KENYA imepata kiti muhimu cha uanachama usio wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa baada ya kuishinda Djibouti katika awamu ya pili ya kupiga kura Alhamisi.

Kinyang’anyiro baina ya Kenya na Djibouti kililazimika kuendelea kwa siku ya pili baada ya awamu ya kwanza hapo Jumatano kukosa mshindi, Kenya ilipozoa kura 113 dhidi ya 78 za Djibouti, huku idadi ya kura zinazohitajika kutawazwa mshindi ikiwa 128.

Lakini Alhamisi, Kenya ipigiwa kura na mataifa 129 huku nchi zilizopigia Djibouti zikipungua hadi 62. Ili kupata kiti hicho, taifa linalowania linafaa kupata kura 128, ambazo ni thuluthi mbili ya mataifa yote 193, kulingana na sheria za baraza hilo.

Hii inamaanisha kuwa kuanzia Januari 2021, Kenya itarejelea uwepo wake katika asasi hiyo ya Umoja wa Mataifa baada ya miaka 23, ambapo itasaidia kufanya maamuzi muhimu kuhusu usalama na amani duniani. India, Mexico, Ireland na Norway zilichaguliwa hapo Jumatano.

Baadhi ya maamuzi ambayo Kenya sasa itashiriki ni kuhusu kupiga mataifa marufuku kama adhabu, kutoa kibali cha kutumia majeshi kudumisha amani pamoja na kuchagua majaji wa Mahakama ya Kimataifa kuhusu Haki.

Kenya sasa itashirikiana na wanachama watano wa kudumu wa baraza hilo – Amerika, Urusi, Uingereza, Uchina na Ufaransa, pamoja na wanachama wengine tisa wasio wa kudumu,. na huenda hata itakapata fursa ya kusimamia vikao vya baraza hilo.

Kenya ilikuwa imependekezwa na Umoja wa Afrika kwa nafasi hiyo, nayo Djobouti ikajitokeza kama mshindani.

Alhamisi, uchaguzi huo ulianza saa kumi alasiri ambapo Venezuela ilizuiwa kupiga kura kutokana na uanachama wake kukosa kuthibitishwa na Umoja wa Mataifa. Matokeo hayo yalitangazwa saa mbili usiku.

Kenya ilitumia kila mbinu kutwaa ushindi kwa kushawishi mataifa mengi kuipigia kura. Iliteua Bw Tom Amolo, Katibu wa Ubalozi na Siasa kama balozi wake maalumu, akisaidiwa na Mwakilishi wa Kudumu katika Umoja wa Afrika Bi Catherine Mwangi na Bw Lazarus Amayo, Mwakilishi wa Kudumu katika Umoja wa Mataifa jijini New York.

Kenya pia ilialika wawakilishi wengi humu nchini kutoka mataifa ya nje, na kuwashawishi kuipigia debe katika kila kongomano la kimataifa kabla ya ugonjwa wa Covid-19.

Ingawa juhudi hizo ziligharimu hela nyingi, kilikuwa kiti ambacho Kenya haikutaka kupoteza maanake jitihada za hivi majuzi za kutwaa uongozi katika ngazi za kimataifa zimekuwa zikigonga mwamba.

Nairobi ilikuwa imepoteza fursa ya kuwa makao ya ukatibu wa Eneo Huru la Biashara la Afrika, nafasi iliyotwaliwa na Ghana. Pia ilipoteza nafasi ya kiongozi wake kuchukua hatamu za uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika. Pia ilikosa kuteuliwa kuwa makao makuu ya benki ya Afrexim.

 

UN yamteua Zainab Hawa Bangura awe Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Nairobi

Na MWANDISHI WETU

UMOJA wa Mataifa (UN) umetangaza kuteuliwa kwa Zainab Hawa Bangura wa kutoka Sierra Leone awe Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa jijini Nairobi (UNON).

Kwenye taarifa iliyochapishwa katika tovuti ya chombo hicho, Katibu Mkuu wa UN António Guterres alitangaza Jumatatu announced kwa Hawa Bangura katika wadhifa wa mkuu wa UNON.

“Katibu Mkuu anamtakia heri Katibu Mkuu mwenye Mamlaka wa Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Mpango wa Makao (UN-Habitat) Maimunah Mohd Sharif ambaye ataendelea kuwa kaimu mkurugenzi mkuu hadi Bangura achukue hatamu rasmi,” alisema Guterres jinsi alivyonukuliwa kwenye taarifa hiyo.

Bangura amefanya kazi kama mtetezi wa haki na msuluhishaji migogoro na mpatanishi kwa muda mrefu pamoja na kuwa mpiganiaji haki za kibinadamu ambaye hadi majuzi amekuwa Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu kuhusu Dhuluma za Kijinsia katika Migogoro tangu mwaka 2012 hadi 2017.

Alianzia nchini Liberia taaluma yake katika Umoja wa Mataifa ambapo alishughulikia na kusimamia chombo kikubwa zaidi kinacholenga raia cha UN majukumu yake yakiwa ni pamoja na kuchangia kulainika kwa asasi za serikali na upatanishi wa kijamii.

Aidha, Bangura amewahi kuwa Waziri wa Afya na Usafi (2010-2012) na Waziri wa Masuala ya Kigeni na Ushirikiano Kimataifa (2007-2010) katika serikali ya Sierra Leone.

Vilevile Bangura amehudumu kama Mkurugenzi Mkuu mwenye Ushawishi wa Makundi ya Kitaifa ya Uwajibikaji pamoja na kuwa Mshirikishi na mwasisi mwenza wa Kampeni ya Utawala Bora.

Ana shahada ya digrii baada ya kuhitimu kutoka Chuo cha Fourah Bay jijini Freetown, Sierra Leone, na diploma za juu katika usimamizi wa bima alizihitimu na kutunukiwa baada ya kusomea katika Chuo Kikuu cha London na kile cha Nottingham.

Walimu wa Kenya wapata tuzo za UN, AU

Na COLLINS OMULO na FAITH NYAMAI

WALIMU wawili wa humu nchini wamepata tuzo ya kimataifa wiki hii kwa kazi nzuri na kwa kuwasaidia wanafunzi kuweza kujisaidia katika mazingira wanamoishi.

Mwalimu Bora Duniani Peter Tabichi ametunukiwa heshima nyingine kwa kutawazwa na Umoja wa Mataifa (UN) kama Mkenya Bora Mwaka wa 2019.

Naye Mwalimu wa Masomo ya Hisabati na Kemia katika Shule ya Upili ya Wasichana ya Asumbi Erick Ademba Jumatano alikuwa miongoni mwa walimu watatu kutoka Afrika ambao walipewa tuzo ya Umoja wa Afrika (AU) kwa utendakazi wao wa mzuri.

Bw Ademba alipewa cheti na zawadi ya dola 10,000 za Amerika (sawa na Sh1 milioni) katika sherehe iliyofanyika katika Makao Makuu ya AU jijini Addis Ababa, Ethiopia.

Walimu wengine waliozawidiwa ni Augusta Lartey kutoka Shule ya Upili ya Presbyterian ncjhini Ghana na Gladys kutoka Uganda.

Mnamo Machi mwaka huu Tabichi aliandikisha historia kwa kuwa mwalimu wa kwanza kutoka Afrika kushinda tuzo ya Mwalimu Bora Ulimwenguni kwa mara ya kwanza miaka mitano baada ya tuzo huyo kuanzishwa. Alitia kibindoni Sh100 milioni .

Kwa kutambuliwa na UN kama Mtu Bora Mwaka huu, Mwalimu Tabichi amejiunga na orodha ya watu wachache ambao wamewahi kutawazwa Mtu Bora wa Mwaka na umoja tangu mwaka wa 2002.

Tabichi alituzwa kwa kielelezo cha umuhimu wa elimu na thamani na heshima ya taaluma ya elimu kama chombo ya kukabiliana na changamoto za maisha.

Akipokea tuzo hiyo, Tabichi ambaye ni mwalimu wa Hisabati na Fizikia katika Shule ya Upli ya Kerika katika Kaunti ya Nakuru alitoa wito kwa serikali kuhakikisha kuwa inaipa kipaumbele elimu ya mtoto wa kike.

Na Bw Ademba, na wenzake wawili, walituzwa kwa kuwasaidia watoto kutimiza matamanio yao, kutoa mafunzo yenye ubora na kupalilia mienendo hitajika shuleni kati ya mambo mengine.

Akiongea baada ya kupata tuzo hiyo, Bw Ademba, alisema itaimarisha heshima na taadhima ya ualimu barani Afrika.

“Tuzo hii pia itawatia shime walimu kuwa wabunifu. Hii ni kando na kuimarisha hadhi ya kazi hii kwa sababu sasa walimu barani Afrika watahisi wanathaminiwa,” akasema Bw Ademba.

Mwalimu huyo aliwasili nchini Alhamisi na kulakiwa kwa nderemo, vifijo na furaha tele na maafisa wa Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA), Nairobi.

Akiongea katika hafla hiyo Beatrice Njenga, ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Elimu katika AU, alisema kuwa tuzo hiyo ya walimu ni muhimu kama chombo ambacho kitachangia ufanisi wa Agenda ya 2063 ya AU.

Vile vile, akaeleza, tuzo hiyo inafanikisha kufikiwa kwa Mkakati wa kustawisha Elimu barani Afrika (CESA).

“Tuzo hii itaimarisha hadhi ya heshima ya Mwalimu Afrika katika ngazi zote; kuanzia chekechea hadi chuo kikuu, na hata vyuo vya kiufundi (TVET). Pia itawapa wanafunzi mshawasha na msukumo wa kuteua ualimu kama taalamu ya kwanza vyuoni,” akaongeza Bi Njenga.

Watu 500 wameuawa katika mashambulio nchini Syria – UN

Na AFP

UMOJA WA MATAIFA

KATIBU Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Antonio Guterres amesema kwamba watu 500 wakiwemo watoto 120, wameuawa katika muda wa wiki moja katika mashambulio ya ndege mashariki ya Ghouta nchini Syria na kutaja hali hiyo kama jehanamu ulimwenguni.

Bw Guterres alisema hayo wakati ambao Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, likiungwa na Urusi, lilipitisha kwa kauli moja amri ya kusitishwa kwa vita nchini Syria kwa siku 30 kuruhusu misaada ya kibinadamu na dawa kufikia waathiriwa.

Azimio la kusitisha mapigano hayo mara moja lilipitishwa wakati wanajeshi wa serikali ya Syria walipokuwa wakiendelea kuponda ngome za waasi eneo la Mashariki ya Ghouta, ambapo mamia ya watu wameuawa katika mashambulio ya wiki moja.

“Tumechelewa kukabiliana na mzozo huu, tumechelewa sana,” Balozi wa Amerika aliambia baraza baada ya kura na kulaumu Urusi kwa kuwa kikwazo kwa kura hiyo.

Azimio hilo linataka kusitishwa kwa vita mara moja kote Syria ili kuruhusu misaada kuwafikia wagonjwa na waliojeruhiwa bila kutatizwa.
Ili Urusi iweze kuunga mkono azimio hilo, ilibidi lugha iliyotumiwa ibadilishwe kufafanua kuwa lingetekelezwa bila kuchelewa badala ya kuwa lingeanza kutekelezwa saa 72 baada ya kupitishwa.

Mabalozi walisema walikuwa na hakika kwamba hatua hii isingefungua milango ya kuahirisha kusitishwa kwa vita, kwa sababu wanachama wa baraza walikuwa wameweka wazi kwenye majadiliano kwamba amri ingetekelezwa haraka.

Mabalozi hao walisema kwamba Guterres ataarifu baraza kuhusu hali ya utekelezaji wa azimio hilo katika muda wa siku 15.

Inasemekana Russia ilikubali kuunga azimio hilo baada ya kuthibitishiwa kuwa halitaathiri mashambulio dhidi ya kundi la kigaidi la Islamic State au Al-Qaeda, pamoja na watu, makundi na mashirika yanayohusishwa na vitendo vya kigaidi.

Hatua hii itaruhusu serikali ya Syria kuendelea kushambulia magaidi wanaoshirikiana na Al-Qaeda eneo la Idlib, mkoa wa mwisho unaodhibitiwa na magaidi nchini Syria.

Kulingana na azimio hilo, mashambulio yatakomeshwa maeneo ya Ghouta Mashariki, Yarmouk, Foua na Kefraya.

Tanzania kujitoa katika mpango wa UN kuwapa wakimbizi uraia

Rais wa Jamhuri ya Tanzania Bw John Pombe Magufuli. Picha/ Maktaba

DAR ES SALAAM, TANZANIA

Na AFP

Kwa Muhtasari:

  • Tanzania ilijiondoa kutokana na ukosefu wa fedha na utovu wa usalama
  • Nchi hiyo imekuwa ikiwahifadhi raia kutoka Burundi na DRC
  • Kulingana na UNHCR, wakimbizi wanafaa kupewa uraia wa nchi wanazokimbilia hifadhi

RAIS wa Tanzania, John Magufuli, ametangaza kuwa nchi yake itajiondoa kutoka mpango wa Umoja wa Mataifa wa kushughulikia wakimbizi ambao unatoa suluhisho la kudumu kwa wakimbizi ikiwa ni pamoja na kuwapa uraia.

“Tanzania imeamua kujiondoa kwa sababu za usalama na ukosefu wa fedha,” ilisema taarifa ya serikali.

Rais Magufuli alitoa tangazo hilo Ijumaa katika mkutano na mabalozi wa nchi za kigeni jijini Dar es Salaam.

Mnamo Januari, Tanzania ilifahamisha shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR), kuwa ilisimamisha kuwapa uraia baadhi ya wakimbizi kutoka Burundi na kuwa isingekubali maombi mapya kutoka kwa wakimbizi.

Nchi hiyo imekuwa ikiwahifadhi raia kutoka Burundi na Jamhuri ya Demokrasia ya Congo.

Kulingana na gazeti la serikali la Tanzania Daily News, Magufuli analaumu jamii ya kimataifa kwa kukataa kuipatia pesa ilizoahidi kusaidia wakimbizi.

Kulingana na UNHCR, wakimbizi wanafaa kupatiwa uraia wa nchi wanazokimbilia hifadhi.

Shirika hilo linaamini kwamba wakimbizi wakipatiwa elimu na haki ya kufanya kazi kisheria, wanaweza kupata maarifa na kujitengemea huku wakichangia katika uchumi wa nchi wanazoishi.