Vijana wakaidi wazee 2022

Na BENSON MATHEKA

SIASA za uchaguzi mkuu wa mwaka 2022 zinapoendelea kupamba moto, wazee wa jamii mbalimbali wamekuwa wakijitokeza kutoa misimamo yao inayotofautiana na vijana.

Wazee hao wamekuwa wakitawaza baadhi ya wagombeaji urais ambao vijana wanaonekana kutowachangamkia.

Wadadisi wa siasa wanasema kwamba hatua ya wazee hawa inaenda kinyume na misimamo ya vijana wanaohisi kwamba wana uhuru wa kuamua viongozi wanaowataka wawawakilishe.

“Kuna mgogoro wa uamuzi wa wazee wa baadhi ya jamii kutawaza wagombeaji na vijana wanaohisi kwamba wana uhuru wa kuchagua kiongozi wanayemtaka. Hii si kwa wanaogombea urais pekee bali hata wanaogombea viti vya ugavana, ubunge na useneta. Baadhi ya wazee wa jamii wanagawanya nyadhifa za uongozi kwa misingi ya ukoo jambo ambalo vijana hawafurahii,” asema Dkt Shadrack Ivuti, mtaalamu wa Masuala ya Jamii na Utawala.

Wazee wa Jamii ya Agikuyu wenyewe kwa wenyewe walitofautiana baadhi yao walipomtawaza Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi kuwa msemaji wa jamii ya Gema baadhi wakijitenga na hatua hiyo na hata kuandaa utakaso wa madhabahu ya jamii hiyo katika Kaunti ya Murang’a.

Kundi moja la wazee hao linasemekana kumchangamkia kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga na liliongoza ujumbe kumtembelea nyumbani kwake Bondo, Siaya ambapo lilikutana na wazee wa jamii ya Waluo.

Hatua ya wazee hao ilikuwa ya kuzika tofauti za kisiasa kati ya jamii hizi mbili kabla ya uchaguzi mkuu ujao mwaka 2022 na kumwidhinisha Bw Odinga kama mrithi wa Rais Uhuru Kenyatta.

Wafalme wa kuhadaa vijana

Na LEONARD ONYANGO

WANASIASA sasa wanatumia ahadi hewa kama chambo cha kunasa kura za vijana huku Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9, 2022 ukikaribia.

Naibu Rais William Ruto na kinara wa ODM Raila Odinga ni miongoni mwa wanasiasa wanaomezea mate urais mwaka ujao ambao wamekuwa wakitoa ahadi tele za ‘danganya toto’ kwa vijana.

Kati ya Wakenya milioni 19.6 waliojisajili kuwa wapigakura 2017, vijana wa kati ya umri wa miaka 18 na 35 walikuwa asilimia 51, kulingana na ripoti ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Katika shughuli ya usajili wa wapigakura kwa wingi inayoendelea kote nchini, IEBC inalenga kusajili wapigakura wapya milioni 6, wengi wao wakiwa vijana.

Karibu asilimia 60 ya wapigakura mwaka ujao watakuwa vijana –hali ambayo imefanya wanasiasa kuwang’ang’ania kwa kutoa ahadi ambazo hawatatimiza baada ya kuchaguliwa.

Jumamosi, Bw Odinga alipokutana na vijana mjini Naivasha, Kaunti ya Nakuru, aliahidi kutoa Sh6,000 za bwerere kwa kila kijana asiye na ajira kila mwezi iwapo atachaguliwa kuwa rais.

Shirika la Takwimu nchini (KNBS) linakadiria kwamba kuna watu milioni 2.49 – wengi wao wakiwa vijana – wasiokuwa na ajira.

Hiyo inamaanisha kwamba iwapo Bw Odinga atachaguliwa kuwa rais wa tano wa Kenya, atawapa vijana wasio na ajira Sh180 bilioni za bwerere kila mwaka.

Wataalamu wa masuala ya kiuchumi, hata hivyo, wametilia shaka ahadi hiyo huku wakisema kuwa itakuwa vigumu kuitekeleza.

Bw Odinga pia ameahidi kwamba vijana watakaoanzisha biashara hawatalipa ushuru kwa miaka saba kuwezesha biashara zao kukua.

Ameahidi kuongeza kiasi cha mikopo ya elimu ya juu (Helb) kwa kuzingatia gharama ya maisha na vijana wanaokamilisha masomo yao hawataingizwa kwenye orodha ya watu wanaoshindwa kulipa mikopo (CRB).

Iwapo Bw Odinga atashinda urais, zaidi ya vijana 1,000 wanaohitimu masomo yao, watakuwa wakipokea mishahara huku wakifanya mafunzo ya nyanjani katika mashirika ya kimataifa, ikiwemo Umoja wa Mataifa (UN).

Kinara wa ODM pia ameahidi kuunda wizara huru ya Vijana na kubuni hazina maalum ya wahudumu wa bodaboda.

“Nitabuni hazina spesheli ya kusaidia wahudumu wa bodaboda. Kiwanda cha kuunda pikipiki kitakuwa humu nchini. Hatua hiyo inalenga kuhakikisha kwamba zaidi ya vijana milioni 2.4 wanapata pikipiki kwa bei nafuu,” akasema Bw Odinga.

Kwa sasa vijana wako chini ya wizara ya Habari na Teknolojia ya Mawasiliano (ICT), Ubunifu na Masuala ya Vijana.?Dkt Ruto jana, huku akiwa ziarani katika Kaunti ya Isiolo, aliendelea kumimina ahadi zake kwa vijana.

“Chama cha UDA (United Democratic Alliance) ndicho kinachojali masilahi ya wananchi wa kawaida. Tutawapa vijana nafasi za ajira, mikopo nafuu na mazingira bora ya kuanzisha biashara,” akasema Dkt Ruto baada ya kuhudhuria ibada katika Kanisa Katoliki la Isiolo.

Bw Odinga, kiongozi wa Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi na Spika wa Bunge Justin Muturi –ambao wote wametangaza kuwania urais mwaka ujao – wameelezea kutoridhishwa na idadi ndogo ya vijana wanaojitokeza kujisajili kuwa wapigakura.

Wadadisi wanasema kuwa hali hiyo inasababishwa na hatua ya wanasiasa kutoa ahadi hewa kila baada ya miaka mitano.?Serikali ya Jubilee, kwa mfano, haijatekeleza kiasi kikubwa cha ahadi ambazo Rais Uhuru Kenyatta na Dkt Ruto walitoa 2013 na 2017.

Miongoni mwa ahadi walizotoa kwa vijana ni kubuni nafasi za ajira milioni 1.3 kila mwaka. Lakini ahadi hiyo haijatimizwa.

“Ahadi yetu kwa vijana ni kuhakikisha kuwa wanapata ujuzi unaohitajika kujiletea mapato humu nchini na ngazi ya kimataifa, kuwasamehe kulipa ushuru na kuwapa mikopo nafuu,” inasema manifesto za Jubilee 2013 2017.

Ahadi nyingine ambazo Rais Kenyatta na Dkt Ruto walitoa 2013 lakini hazijatimia ni kujenga vituo vya ICT na maktaba katika kaunti zote 47, viwanja vya michezo vitano katika kila kaunti, kujenga viwanja vya michezo vya kitaifa Kisumu, Mombasa, Nakuru, Eldoret na Garissa.

Wawili hao pia waliahidi kujenga Taasisi za Teknolojia katika kila wadi ili kuwezesha vijana kujiinua, mafunzo ya bila malipo katika vyuo vya ufundi, kutenga asilimia 2.5 ya mapato ya nchi kwa ajili ya Hazina ya Ustawishaji Vijana (YEF).

Serikali kutumia vijana na wanabodaboda kuendesha kampeni ya amani kuelekea 2022

Na CHARLES WASONGA

SERIKALI itatumia makundi ya vijana na waendeshaji bodaboda kuendesha mipango ya kudhibiti ghasia zinazohusiana na uchaguzi katika maeneo mbalimbali nchini kuelekea uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022.

Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i, Jumatano alisema wanachama wa makundi haya mawili watakodiwa kushiriki katika mipango ya kuhubiri amani na kutoa elimu ya uraia.

“Makundi hayo ya vijana na wanabodaboda watashirikiana na mashirika ya kidini na wadau wengine kuendesha shughuli hizo kuanzia ngazi za vijijini hadi mijini,” Dkt Matiang’i akaeleza huku akitoa hakikisho kuwa serikali itadhibiti usalama kote nchini katika kipindi hicho cha uchaguzi.

Waziri alisema kampeni hiyo ya kuhubiri amani italenga maeneo ambayo yametambuliwa kuwa katika hatari ya kushuhudia machafuko na maeneo mengine ambako utafiti wa kiusalama unaendeshwa.

“Sisi katika sekta ya usalama, huwa hatuendeshi chaguzi, tunaandaa mazingira kwa IEBC kuendesha shughuli hizo. Sharti tuhakikishe kuwa uchaguzi unafanywa kwa usalama sawa na upokezaji wa kimamlaka. Tumejitolea kuhakikisha kuwa hakuna risasi itakayofyatuliwa na hakuna raia atakayejeruhiwa; Wakenya wote watasaidiwa kushiriki katika mpango wa kuunda uongozi na demokraasia ya nchi yetu,” Dkt Matiang’i akaongeza.

Waziri huyo alisema hayo katika Kongamano la 64 la Baraza Kuu la Baraza la Kitaifa la Makanisa Nchini (NCCK) lililofanyika katika Ukumbi wa Mikutano ya Limuru, Kaunti ya Kiambu.

Dkt Matiang’i aliongeza kuwa washirika wa kimaendeleo pia watahimizwa kufadhili kampeni za vijana kuhubiri amani nchini “ili kuzima kabisa kero ya fujo ambazo hugubika chaguzi nchini kila mara.”

Waziri ambaye alikuwa ameandamana na mawaziri wasaidizi Mercy Mwangangi (Afya), David Osiany (Biashara) na Zack Kinuthia (Michezo) alitoa changamoto kwa vijana kujisajili kwa wingi kuwa wapigakura ili wawanie nyadhifa za uongozi katika uchaguzi ujao.

Vijana wataka vyuo vya kiufundi vianzishe masomo ya kidijitali

Na STEPHEN ODUOR

VIJANA katika Kaunti ya Tana River, wametaka mafunzo ya kisasa yatolewe katika taasisi na vyuo vya kiufundi ili kushawishi wengi wao kujiunga navyo.

Kulingana nao, taasisi hizo huchukuliwa kuwa za watu waliofeli katika elimu za msingi kwa vile mafunzo yanayotolewa yamejikita katika mbinu za zamani za utendakazi ilhali jamii ya sasa ni ya kidijitali.

“Hakuna mtu ambaye angependa kujifunza mambo ambayo yamepitwa na wakati katika enzi hizi,” akasema kiongozi wa vijana, Bi Asha Shehe.

Alidai kuwa, baadhi ya vijana waliopokea mafunzo kuhusu masuala ya umeme waliamua kufanya kazi ya bodaboda baada ya kukosa ajira zilizolingana na masomo yao, huku wengine kama vile fundi wa mifereji wakikosa ajira kwa vile mbinu walizofunzwa zilipitwa na wakati.

Waziri wa Elimu katika kaunti hiyo, Bw Abbas Kunyo alisema utawala uliopo unazingatia masuala hayo na tayari kuna mikakati ambayo ilikuwa imeanza kutekelezwa.

Bw Kunyo alisema mojawapo ya mikakati iliyoanzishwa ni kuwapa wahadhiri mafunzo ya kidijitali, ndipo wawe na uwezo wa kufunza mbinu za kisasa za utendakazi.

“Ukweli ni kuwa idadi ya wanafunzi katika taasisi zetu imekuwa ikiongezeka katika miaka ya hivi majuzi ikilinganishwa na zamani. Katika miezi ijayo, mtashuhudia wenyewe kozi mpya ambazo tutaanzisha,” akasema.

Nitawapa mashine za kisasa kuchapa kazi nikiingia Ikulu 2022, Raila aahidi vijana

Na SAMMY WAWERU

DALILI kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga kuwa debeni 2022 kuwania urais zinaendelea kudhihirika.

Awali, Bw Raila amekuwa akikwepa kueleza bayana endapo atashiriki uchaguzi mkuu ujao, akisisitiza kwamba lengo lake kupitia mapatano ya Handisheki kati yake na Rais Uhuru Kenyatta ni kuunganisha taifa.

Amenukuliwa mara kadha akidai atatoa msimamo wake baada ya Ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI), ila hatma yake kwa sasa ipo mikononi mwa mahakama ya rufaa, kupita.

Kwenye ziara yake eneo la Nakuru kutangamana na vijana Jumanne, Waziri huyu Mkuu wa zamani, aliendelea kumsuta Naibu wa Rais William Ruto kwa sera zake kuinua uchumi kupitia mfumo wa bottom-up.

Akimcharura Dkt Ruto kwa kuwapa vijana wilibaro, Bw Raila alisema endapo ataingia Ikulu mwaka ujao, ataweka mikakati kabambe kuwapa mashine za kisasa kujiendeleza kikazi.

“Sisi tunataka kuona vijana wameinuka. Mazingira yangu nataka yawe ya vijana. Tutaboresha biashara kwa kuwapa mashine za kisasa, wajiendeleze na wengine waweze kuanzisha biashara,” akasema.

“Ninashangaa kuona wengine wakiwapa wilibaro,” Raila akasema akiuza sera zake, matamshi yake yakionekana kulenga Naibu wa Rais Ruto.

Katika ziara yake Nakuru kutangamana na baadhi ya vijana eneo hilo, Raila alikuwa ameandamana na gavana wa kaunti hiyo, Bw Lee Kinyanjui.

Kiongizi huyo wa upinzani na ambaye kwa sasa anashirikiana kwa karibu na Rais Kenyatta baada ya mapatano ya Handisheki, amekuwa akimsuta Dkt Ruto, akitaja ahadi zake kama hadaa tupu, na kwamba angezitekeleza wakati akiwa serikalini kama Naibu wa Rais.

Naibu Waziri aishangaa sekta ya matatu kunyima vijana nafasi za kazi

Na MWANGI MUIRURI

Naibu Waziri wa Spoti, Utamaduni na Turathi za Kitaifa Bw Zack Kinuthia ameteta kuwa sekta ya magari ya uchukuzi wa umma kwa sasa inawanyima vijana wa taifa hili Sh12.8 bilioni kwa mwaka kupitia kupiga marufuklu kazi ya utingo.

Akiongea Jumatano katika Kaunti ndogo ya Kigumo, alisema kuwa udadisi wa hali hiyo ni kwamba baadhi ya wamiliki wa magari hayo licha ya kusukumwa kufanya hivyo na athari za ugonjwa wa Covid-19 “kunao pia wengine miongoni mwao ambao wamefanya hivyo kimakusudi ili kiupounguza gharama za kazi na hivyo basi wajizidishie faida.”

Bw Kinuthia alisema kuwa kuna takriban magari 70, 000 ambayo ni kati ya yote 200, 000 ambayo katika uhudumu wayo, hayana huduma za kondakta na badala yake huwaelekeza abiria wakate tiketi za nauli kabla ya kuanza safari na katika steji barabani, dereva ndiye huwajibikia pia kazi ya Kondakta ya kusukisha na kubeba wengine.

“Ukizingatia mshahara wa chini kabisa wa kondakta ni Sh500 kwa kila mmoja wao kila siku, ina maana kuwa kwa siku wale vijana 70, 000 wangekuwa wameajiriwa kazi hiyo wangekuwa wanajipa Sh35 milioni ambazo kwa mwaka ni Sh12.8 Bilioni,” akasema.

Alisema kuwa hali hii inaangazia ule upungufu wa ushirika kati ya serikali na sekta ya kibinafsi katika kuunda nafasi za kazi.

“Ikiwa sekta hii ambayo kwa asilimia 80 iko mikononi mwa vijana inaweza ikawanyima wenzao 70, 000 nafasi za kujipa riziki, ina maana kuwa kuna shida kuu ambayo inafaa ijadiliwe na itafutiwe suluhu,” akasema.

Bw Kinuthia alisema kuwa wakati serikali inajizatiti kupambana na umasikini kupitia kutoa mazingara mwafaka ya kuunda ajira na mapato, kunafaa kuwe na mashauriano kati ya sekta hii ya uchukuzi pamoja na serikali ili kubaini hasa kinachozima nafasi hizo za kazi kupokezwa vijana.

Mwenyekiti wa Muungano wa Wamilki magari ya uchukuzi Mlima Kenya Bw Micah Kariuki alisema kuwa tangu sekta hii ya matatu iiwekwe chini ya uratibu wa vyama vya ushirika au makampuni, kanuni za utendakazi zilianza kuwekwa kwa mtazamo wa kibiashara.

“Maamuzi mengi kwa sasa huzingatia jinsi ya kuendesha biashara ili iunde faida kupitia kuvutia wateja wengi iwezekanavyo. Kazi ya utingo kwa wakati mwingine imekuwa changamoto kuu kufuatia tabia za matamshi na matendo kwa wateja ambapo husemwa na wengi hukera,” akasema.

Bw Kariuki aidha alisema kuwa tangu kuzuke ugonjwa wa Covid-19 na masharti yakawekwa kuwa magari ya uchukuzi wa umma yapunguze idadi ya abiria hadi asilimia 60 ya uwezo wa upakiaji, kiti cha kondakta kilionekana na wengi wa mameneja wa uchukuzi kuwa kinaweza kikaondolewa ili kiletee mwenye gari pesa.

Ni magari tu yale ambayo hayabebi kutoka steji maalum na kusafirisha wateja wake moja kwa moja almaaurufu “Express” ambayo yamekuwa yakiajiri makondakta kwa kuwa wanahitajika katika harakati za kuwasaka abiria kutoka steji moja hadi nyingine katika barabara ya uhudumu.

Bw Kariuki alisema kuwa ikiwa makali ya ugonjwa wa Covid-19 yatapunguka, nayo serikali ijizatiti na iteremshe bei ya mafuta, ipige msasa mfumo wake hasi wa ushuru na hatimaye iondoe ufisadi wa maafisa wa trafiki barabarani, basi biashara inaweza ikapanua utenda kazi wa faida na iishie kuunda nafasi hizo za kazi ambazo kwa sasa zimepotea.

Hazina za wanawake, vijana kuunganishwa

Na SIAGO CECE

Serikali itaunganisha hazina tatu za Uwezo, Wanawake na Vijana kuwa moja na kuongezea pesa hazina mpya itakayobuniwa kwa lengo la kufanya watu wengi kuchukua mikopo ambayo itakuwa na riba ya chini.

Waziri wa Fedha, Ukur Yatani, alisema kwamba wanabadilisha kanuni kadhaa, ya kwanza ikiwa kubuni Hazina ya Biashara ambayo itanufaisha wamiliki wa biashara ndogo.

Bw Yatani alisema kwamba serikali, kupitia hatua hiyo, itaongeza pesa za Hazina ya Biashara kutoka Sh2.4 bilioni hadi Sh14 bilioni.

“Kupitia Hazina ya Biashara, serikali itapunguza gharama kwa kupunguza idadi ya wafanyakazi na hazina itakua zaidi ya mara sita,” Yatani aliambia kamati ya bunge inayokutana Mombasa.

Aliongeza: “Tuko katika hatua za mwisho za kuunganisha hazina hizo ili kuziimarisha ziweze kuafikia malengo yake ya kutoa mikopo na kuondoa changamoto kama gharama ya kuziendesha,” alisema.

Kamati inayosimamiwa na mbunge wa Tiaty, William Kamket inaendelea kutoa mapendekezo kuhusu hazina hiyo ambayo Bw Yatani alisema yanamfurahisha.

“Tunachunguza sheria kadhaa na ya kwanza ni kubuniwa kwa Hazina ya Biashara. Tunataka kuimarisha mfumo wote,” alisema na kukiri kulikuwa na visiki awali.

Alisema miongoni mwa masuala wanayotaka kutatua ni pamoja na kuwa na maafisa wa hazina za vijana, wanawake na Uwezo katika miji mingi kote nchini wanaohudumu kivyao jambo linalofanya gharama kuwa kubwa.

Bw Yatani alisema kwamba wanataka kuhakikisha kuwa vyama vya akiba na mikopo na vyama vingine vinapatiwa nafasi ya kwanza kupata pesa hizo ili vijiimarishe.

Mnamo Agosti 2019, serikali ilisimamisha shirika lililokuwa likitoa mikopo kwa wanawake, vijana na biashara ndogo kwa riba ya asilimia sita.

Katika ripoti, kamati ya bunge kuhusu majukumu maalum ilisema kwamba sheria ya Hazina ya Biashara ya 2019 inakiuka Katiba na hivyo ikapendekeza ibadilishwe yote.

Kamati hiyo ilisema kwamba umma haukushirikishwa kikamilifu na hazina hiyo ingebuniwa kupitia sheria mpya wala si kubadilishwa kwa sheria iliyokuwepo.

Lakini Bw Yatani alisema Hazina ya Biashara inafaa kuanzishwa wakati huu kwa sababu tayari wamepata mafunzo kutoka hazina zilizotangulia na kutambua kuwa kulikuwa na shida.

Alisema itafaa zaidi kwa kuwa serikali itapunguza gharama na kuweka mikakati ili iweze kunufaisha watu wengi. Hazina hizo zilianzishwa na serikali kusaidia vijana na wanawake kuanzisha bishara kama mkakati wa kukabiliana na ukosefu wa ajira.

Uhuru aenjoi vijana

Na BENSON MATHEKA

RAIS Uhuru Kenyatta, Jumatatu alionekana kuwachezea vijana akili kwa kuwaambia kuwa angeteua baadhi yao katika Baraza la Mawaziri kama angekuwa na uwezo huo, na pia atakuwa mtetezi wao baada ya kung’atuka mamlakani.

Akihutubu wakati wa uzinduzi wa vuguvugu jipya la “Kenya ni Sisi” katika Ukumbi wa Boma jijini Nairobi, Rais Kenyatta alisema kuna vizingiti kwake kuteua vijana wakati huu.

“Mnajua ingekuwa katiba ya zamani ambapo ningeweza kuajiri na kufuta mawaziri, pengine tungekuwa na vijana wenye umri wa miaka 25 serikalini. Lakini sasa, taabu ni kuwa hii katiba inasema lazima niende Bunge, nipeleke majina huko wachunguze. Sasa sijui kama watapitisha, na kwa sasa sitaki kufanya mageuzi mengi kwa sababu unajua ukiwa mkondo wa lala salama haja yako ni kumaliza ile kazi umeanza,” akasema Rais.

Matamshi hayo ni kinaya kwani Rais Kenyatta ana uwezo wa kuteua yeyote wakati wowote anaotaka, hasa kutokana na kuwa teuzi zake nyingi zimekuwa zikipitishwa na Bunge bila matatizo kutokana na ushirikiano wa vyama vya Jubilee na ODM.

Matamshi ya rais pia ni kinyume na vitendo vyake vya awali kwani katika teuzi nyingi serikalini amekuwa akiwateua wazee na kutetea vikali msimamo huo wake.

Mwaka 2019 Wakenya walipolalamika kuhusu uteuzi wa wazee serikalini, Rais Kenyatta alijitetea akisema kuwa wazee wanaaminika na wana usimamizi bora ikilinganishwa na vijana ambao alidai wanapenda kupora mali ya umma.

Kati ya wakongwe katika serikali ya Rais Kenyatta ni aliyekuwa makamu wa rais Moody Awori, 93, aliyekuwa mkuu wa utumishi wa umma Francis Muthaura, 73, na mwekezaji Manu Chandaria, 90.

Rais alisema anachoweza kufanya kwa sasa na hata baada ya kuondoka mamlakani mwaka wa 2022 ni kuhakikisha maslahi ya vijana yatakuwa yakizingatiwa.

“Nitakuwa mtetezi wenu siku zijazo. Hata wale watakaokuwa mamlakani watakuwa na vijana wa umri wa miaka 25 na 30 katika baraza la mawaziri,” alisema.

Aliwataka vijana kuridhika na nafasi chache za manaibu waziri alizokabidhi vijana wachache mapema mwaka huu.

“Kwa sasa, furahieni akina Nandia na wengine na muungane na mimi tuwatetee wateuliwe mawaziri kamili kwenye serikali ijayo,” alisema.

Kauli hii ni kejeli kwa vijana kwa kuwa katika utawala wake wa miaka saba, Rais Kenyatta amekuwa na uwezo wa kuteua vijana katika baraza la mawaziri na nyadhifa tofauti serikalini.

Jana, aliwataka vijana kujipanga wenyewe ili kupigania nafasi za uongozi badala ya kutumiwa na wanasiasa wanaowachochea kupigana na kuwasahau wanapoingia mamlakani.

“Mimi ninawaambia, na hakuna kura ninatafuta kwa hivyo ninaweza kuwaambia jinsi mambo huwa. Nyinyi ndio mnapiga kura kwa wingi, au mashini za kupiga kura mnavyoitwa. Lakini baada ya kupiga kura, kwa sababu ya tofauti za wale mnaopigia kura, tunajipata katika hali ambapo ghasia huzuka kati ya jamii, sio kwa sababu kuna tofauti kati yenu mliopiga kura, lakini ni kwa sababu wale mliopigia kura hawaridhiki, na huwachochea mpigane kisha wanaketi makwao na watoto wao na kuwatazama mkipigana,” alisema.

Alipigia debe BBI aliyoanzisha baada ya handisheki yake na kiongozi wa ODM Raila Odinga, akisema itatia kikomo ghasia za baada ya uchaguzi kwa kuhakikisha maslahi ya vijana yanazingatiwa.

Rais alisema vijana wanaweza kujiimarisha kiuchumi wakiungana kwa makundi

ONGAJI: Nani ataokoa maisha ya vijana?

Na PAULINE ONGAJI

Kila unapotembea katika mitaa na miji mingi hapa nchini Kenya, huenda umekutana na vikundi vya vijana –wa kike na kiume – wakiwa wamevalia magwanda ya kazi za sulubu, huku wakiwa na ala za shughuli hii kama vile vifagio, sepetu na kifyekeo miongoni mwa zingine.

Hapa, wanakumbwa na kibarua kigumu cha kufanya kazi za sulubu kama vile kukata nyasi, kuokota taka na kuzibua mitaro na mabomba ya majitaka, vyote chini ya mradi wa ‘kazi mtaani’.

Kupitia mradi huu naelewa kwamba wanapaswa kujipatia mapeni kidogo, huku nao wakitarajiwa kutoa huduma zao ili kunufaisha jamii.

Na sipo hapa kukosoa mradi huu, lakini bila shaka picha hii ya kuhuzunisha inathibitisha hali ngumu ya kiuchumi ambayo inaendelea kuwakumba vijana wetu.

Pengine utajiuliza kwa nini nasema hivi? Huku mataifa mengine ulimwenguni yakiwekeza mabilioni ya pesa kwa miradi ya kielimu, kiteknolovia na uvumbuzi ili kuwasaidia vijana, hii leo katika karne ya 21, sisi hapa tunawapa vijana wetu ala hizi kama mbinu ya kuwapa fedha kidogo.

Kuna baadhi ya watu wanaoohoji kwamba hii inasaidia kwa kuhakikisha kwamba vijana hawa wanapata hela mifukoni, lakini tena swali ni pesa ngapi hizo wanazolipwa kwa shughuli hii ya mchana kutwa?

Mradi huu unapaswa kuendelea kwa muda upi? Je pesa hizi zinatosha kuwasaidia kununua chakula chao cha kila siku, au hata kuanzisha mradi wa kujisaidia baadaye maishani?

Hii inanikumbusha kisa cha majuma machache yaliyopita ambapo nikiwa kwenye kiuo cha mabasi, niligundua kwamba kuna vijana ambao kwa shilingi kumi au 20, wako tayari kukuhifadhia kiti kwenye gari, hasa wakati wa jioni ambapo watu wengi wanarejea nyumbani.

Au kikundi cha wasichana niliokutana nao wakitembea mtaani katika harakati za kuuza sabuni.

Hii tu ni baadhi ya mifano ya masaibu ambayo yamekuwa maisha ya kawaida kwa vijana wengi humu nchini. Haya yanajiri huku kila siku vyombo vya habari vikiendelea kuangazia hadithi za vijana ambao licha ya kuelimika, wamesalia kufanya vibarua vya sulubu.

Kuna baadhi ya watu wanaohoji kwamba utakuwa upumbavu kutegemea tu masomo, badala ya ujuzi ambao waweza kukuletea riziki. Na mara ingine nakubaliana na wazo hili, lakini ikiwa hii ndio hatima ya asilimia kubwa ya vijana wanaohitimu kila mwaka, basi kuna tatizo kubwa sio tu kwa mfumo wetu wa elimu, bali jamii yetu kwa ujumla.

Lakini pia kwa upande mwingine, cha muhimu sio tu kuwa na hati za vyuoni, bali ujuzi wa kuweza kufanya kazi uliyosomea, na swali ni wangapi wanaohitimu kila mwaka wana uwezo wa kufanya walichosomea.

Kwa mfano, kila mwaka maelfu ya wanafunzi waliosomea uhandisi vyuoni uhitimu, ila ni wangapi tunaowaona wakitumia ujuzi wao kila kunapokuwa na miradi mikubwa ya uhandisi nchini. Sio suala la kupewa fursa, lakini swali ni je ni wangapi wanaoweza fanya kazi hii?

Nikirejelea suala la hatima ya vijana, ni wakati wa viongozi kuelewa kwamba kukosa kuwekeza katika vijana kutachochea masaibu ya kijamii, kisiasa na kiuchumi katika siku zijazo. Hii inamaanisha kwamba, jinsi mambo yalivyo, hali ilivyo sasa ni hatari sio tu kwa vijana, bali kwa jamii yote ya Kenya kwa ujumla.

 

Ni wazi sasa ahadi za Jubilee kwa vijana zilikuwa hewa

Na SAMMY WAWERU

Mei 2020 Rais Uhuru Kenyatta alipotangaza kuzindua mradi wa Kazi Mtaani ili kusaidia vijana wasio na kazi na ambao wameathirika kutokana na mkurupuko wa virusi vya corona nchini, mamia na maelfu walijitokeza kujaribu bahati yao.

Mpango huo na ambao mwezi Julai uliingia awamu ya pili, unasemekana kulenga kunufaisha zaidi ya vijana 270, 000 wasio na ajira, walio kati ya umri wa miaka 18 – 35.

Suala la ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana nchini linaendelea kuwa kikwazo na donda ndugu, mamia na maelfu wakifuzu kila mwaka kwa vyeti vya taaluma mbalimbali kutoka taasisi za juu za masomo.

Ukosefu wa kazi kati yao, umechangia wengi kushiriki visa vya uhalifu, unywaji wa pombe na matumizi ya mihadarati na dawa za kulevya, mitandao ya matukio inayowahatarishia maisha.

Ukizuru mitaa mbalimbali nchini, taswira ni ileile moja, hususan kwenye vibanda vya kutafuna miraa na pia kwenye vilabu. “Hiyo ni ishara ya kutelekezwa na serikali, kwa sababu hawana ajira. Ni picha inayopaswa kutia viongozi wasiwasi,” anaeleza Antony Kibui, 35.

Licha ya serikali ya Jubilee kudai inajikakamua kupiga jeki vijana, kulingana na Antony ambaye ni mfanyabiashara Nairobi, sauti ya vijana imepuuzwa.

Akitumia mfano wa uteuzi wa nyadhifa mbalimbali serikalini, haoni jinsi vijana wamewakilishwa. “Rais anapofanya uteuzi, hushangaa kuona ni wazee pekee wanaorejeshwa serikalini. Tutasikika lini? Suala la ukosefu wa kazi miongoni mwetu litatatuliwa lini ikiwa waliostaafu ndio wanaajiriwa tena na kuteuliwa?” Antony anashangaa.

Mashirika na kampuni mbalimbali, yakiwemo ya kiserikali yanapotangaza nafasi za kazi mahitaji ya tajiriba ya kutosha na ya muda mrefu ni kizingiti kikuu kwa vijana, Antony akihimiza bunge kupitisha sheria zitakazowasaidia kutofungiwa nje.

Kwa sababu ya ukosefu wa ajira, wengi wana ari ya kuwekeza kwenye biashara ila mtaji hawana. “Wakati wa usomaji bajeti kila mwaka, vijana hawakumbukwi katika mgao wa fedha. Pesa zinazosemekana ni za vijana hazitufikii,” analalamika Edward Kamangara, ambaye ni mchoraji hodari.

Mwanasanaa Edward Kamangara, ni mchoraji hodari. Anasema vijana waliojaaliwa vipaji mbalimbali wametelekezwa na serikali. Picha/ SAMMY WAWERU.

Serikali imekuwa ikihamasisha vijana kuchukua mikopo ya serikali, lakini kulingana na kijana Kamangara, taratibu na mikakati iliyowekwa inawafungia nje.

“Ukiniitisha dhamana ya hatimiliki ya shamba au cheti cha kumiliki gari ili unipe mkopo, nitatoa wapi? Hicho ni kichocheo cha ufisadi, unaoendelea kufuja fedha za umma na zinazoweza kutatua suala la ukosefu wa kazi kati yetu,” Kamangara anaiambia ‘Taifa Leo’.

Wengi wamejaaliwa vipaji tofauti, wanavyoweza kuvitumia kujiimarisha kimaisha na kimaendeleo, ila mtaji wa kuvipalilia hawana. Isitoshe, asasi husika zinaendelea kupuuza vijana wenye talanta, badala ya kufanya hamasisho kuwainua.

Ni mashirika machache mno nchini yaliyojitwika jukumu la kuangazia masaibu yanayokumba vijana.

Wakati wa kampeni, kabla ya uchaguzi mkuu wa 2017, kiongozi wa Amani National Congress (ANC), Musalia Mudavadi aliibua mjadala: “Ni jambo la kuatua moyo kati ya Jumatatu hadi Ijumaa viongozi wa kisiasa kuandaa mikutano ya hadhara wakitafuta kura, kisha ukumbi, nyanja au bustani kama Uhuru Park zinajaa vijana.”

Bw Mudavadi alisema hiyo ni ishara kuwa vijana nchini hawana kazi, na ni ujumbe kwa serikali kufanya hima kuangazia suala hilo kabla maji kuzidi unga.

Mada ya mwaka huu wa 2020 katika maadhimisho ya siku ya kimataifa kwa vijana ni “Kuhusisha Vijana katika Maendeleo Ulimwenguni”. Mada hii ikiwa wazi “kushirikisha vijana kwenye maendeleo”, hapa nchini Kenya vijana wanaendelea kupuuzwa.

Mpango wa muda wa Kazi Mtaani, unaotajwa kusaidia kupiga jeki vijana kimapato, hata hivyo, unakosolewa na baadhi ya watu wakisema serikali inapaswa kuwapa ajira ya kudumu.

Aidha, wakosoaji wanahisi vijana wanahitaji suluhu ya kudumu ili kutatua kikwazo cha ukosefu wa ajira miongoni mwao, badala ya suluhu ya muda mfupi tu, kisha warejelee maisha magumu ya hapo awali.

Mradi wa Kazi Mtaani unahusisha usafi wa mazingira, hasa ufyekaji wa nyasi kandokando mwa barabara na njia, kuzoa taka, kuzibua mitaro ya majitaka, kati ya majukumu mengine ya kusafisha mitaa.

Waliopata fursa hiyo, wanalipwa mshahara wa Sh455 kila siku.

Gideon aweka mikakati kuteka nyoyo za vijana

Na FRANCIS MUREITHI

SENETA wa Baringo Gideon Moi amebuni mbinu mpya ya kujivumisha kuwa Rais mnamo 2022, na wakati huo huo kuyeyusha umaarufu wa Naibu Rais Dkt William Ruto katika eneo la Bonde la Ufa na maeneo mengine nchini.

Ameunda Baraza la usimamizi wa vijana kwenye chama chake cha Kanu ambalo linaongozwa na Seneta wa Pokot Magharibi Samuel Poghisio, Cornelius Kipchumba na Mary Anne Njambi aliyewania kiti cha eneobunge la Molo katika uchaguzi mkuu wa 2017.

Mwenyekiti wa kitaifa wa vuguvugu la wanawake wa Kanu Elizabeth Kimkung pia yupo kwenye baraza hilo.

Mbinu ya Bw Moi ya kuwakumbatia vijana inatumiwa wakati ambapo Dkt Ruto amekuwa akijivumisha kote nchini kupitia viongozi vijana.

Dkt Ruto tayari anatumia vijana kupenyeza kisiasa maeneo ya Nyanza na Mlima Kenya ili kujiweka pazuri kushinda Urais mnamo 2022.

Kwa kuwa Dkt Ruto amekuwa akikutana na ujumbe wa viongozi nyumbani kwake Karen na Sugoi, Bw Moi naye ameanza kuwapokea viongozi nyumbani kwa babake, marehemu Rais Mstaafu Daniel Arap Moi, Kabarak, katika Kaunti ya Nakuru.

Seneta wa Kajiado Philip Mpaayei aliongoza ujumbe wa vijana kumtembelea Bw Moi wikendi iliyopita.“Maandishi yapo wazi ukutani kwa kila mwenye macho kuyaona. Hauhitaji uambiwe ndio uyaone,” akasema Bw Mpaayei akizungumzia siasa za urithi.

Kulingana na waliohudhuria mkutano huo, Seneta Mpaayei na vijana kutoka Kajiado waliahidi kumuunga mkono Bw Moi kwenye kura ya 2022.Wandani wa Bw Moi nao wanasema mbinu hiyo mpya ya kukutana na vijana itaendelea huku wengine wengi wakialikwa wafike Kabarak hivi karibuni.

Hatua ya Bw Moi kukutana na vijana huku akijiimarisha kuwania uongozi wa nchi kwa mara ya kwanza mnamo 2022, inatokana na kile wandani wake wanasema ni kupanda kwa umaarufu wa Dkt Ruto miongoni mwa vijana nchini.

Hata hivyo, mmoja wa viongozi vijana kwenye mrengo wa Dkt Ruto Joseph Kibusia amesema mbinu hiyo haitamnufaisha Bw Moi kwa kuwa ameianzisha akiwa amechelewa na vijana wengi tayari wako kwa Dkt Ruto.

“Iwapo Gideon ataidhinishwa na Rais Uhuru Kenyatta au la, Dkt Ruto tayari yupo kifua mbele. Hawezi kufikia umaarufu wa Naibu Rais unaoenezwa nyanjani na vijana wengi wa makabila mbalimbali kote nchini,” akasema Bw Kibusia.

Kimani wa Kimani ambaye ni Katibu mtendaji wa Kanu mjini Nakuru hata hivyo alisema vijana hukimbilia tu kwa Dkt Ruto kupokea fedha na hawatamuunga mkono 2022.“Vijana wanaofurika kwa Ruto wana njaa na hukimbilia fedha zake.

Hata hivyo, sisi tunaounga mkono Gideon huwasaidia vijana kushiriki miradi ya kuwainua kiuchumi kama ufugaji wa kuku, ng’ombe na miradi ya kuchimba visima,” akasema Bw Kimani.

Mwanasiasa mkongwe na Waziri wa zamani Musa Sirma alisifu Bw Moi kwa mbinu yake mpya na akamshauri ashirikiane na viongozi wote nchini.

“Wale wanaomuunga mkono Naibu Rais wanajua haja yao ni pesa lakini sisi tuko nyuma ya Gideon ili taifa liwe bora na watoto wetu wahakikishiwe maisha mazuri. Hiyo ndiyo maana naunga mkono mbinu yake ya kukutana na vijana kujenga himaya yake kisiasa,” akasema mbunge huyo wa zamani wa Eldama Ravine.

Vijana wachoma picha

VALENTINE OBARA na MARY WAMBUI

MASAIBU yanayomkumba Seneta wa Nairobi, Bw Johnson Sakaja ambaye alikamatwa kwa kukiuka kanuni za kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona, yameibua upya mjadala kuhusu uwezo wa vijana kusimamia masuala ya nchi vyema kuliko wenzao wenye umri mkubwa.

Bw Sakaja, ambaye jana alitangaza kujiuzulu kutoka kwa uenyekiti wa kamati ya muda ya Seneti inayosimamia masuala ya Covid-19, alikuwa amenaswa na polisi katika baa saa za kafyu Jumamosi usiku.

Alipojisalimisha jana katika kituo cha polisi cha Kilimani, seneta huyo ambaye amekuwa akijizolea sifa kwa kuonekana kuwa kiongozi muungwana, aliweka dhamana ya Sh10,000 pesa taslimu akitarajiwa kufikishwa mahakamani leo.

“Nitafuata sheria, hakuna mtu ambaye ana mamlaka yanayozidi sheria. Sheria itatumiwa kwangu sawa na inavyotendeka kwa Mkenya mwingine yeyote,” akasema, akiandamana na wakili wake, Bw John Khaminwa.

Kisa hiki kimeongeza orodha ya viongozi vijana ambao wanakabiliwa na sakata mbalimbali ambazo zinatilia doa imani kuwa ni wakati wa vijana kuleta uongozi bora nchini.

Wakati huu, Gavana wa Nairobi Mike Sonko, 45, angali anakumbwa na kashfa ya ufisadi ambayo imemfanya kuzuiwa kuingia afisini mwake.

Bw Sonko, ambaye amewahi kukiri kuwa mfungwa zamani, hulaumiwa kwa mienendo yake ambayo huonekana kukiuka maadili ya uongozi ikiwemo kuonekana mlevi na kutumia matusi hadharani.

Katika kaunti hiyo hiyo, Mbunge wa Embakasi Mashariki, Bw Babu Owino, 30, anakumbwa na kesi kuhusu jaribio la mauaji.

Sawa na Bw Sonko, mbunge huyo alipata umaarufu kupitia kwa mienendo yake ya kuvuka mipaka ya maadili anapojitafutia umaarufu wa kisiasa.

Wakati mmoja, alijipata mashakani alipomtusi Rais Kenyatta wakati wa kampeni za uchaguzi.

Katika eneobunge jirani la Embakasi ya Kati, Mbunge Benjamin Gathiru pia alinaswa na polisi mapema Aprili alipopatikana katika baa Ruai.

Mbunge huyo mynyamavu alikamatwa pamoja na watu wengine waliokuwa naye kwani hilo lilikuwa ni ukiukaji wa kanuni za kuepusha maambukizi ya virusi vya corona.

Ingawa baadhi ya wananchi walimtetea Bw Sakaja na kusema hafai kuingizwa kwenye orodha ya watovu wa uadilifu kwa vile ‘kuteleza sio kuanguka’, wengine walisisitiza ameonyesha sura yake kamili.

“Seneta Sakaja ameomba msamaha kwa umma akakiri alikosea. Sote hukosea. Inahitaji ukuu kwa yeyote yule kukiri na kukubali kuadhibiwa kwa makosa yake. Yaishe,” akasema Afisa Mkuu Mtendaji wa Bodi ya Kuanisha Filamu Kenya (KFCB), Dkt Ezekiel Mutua.

Lakini mchanganuzi wa masuala ya uongozi, Bw Gabriel Oguda, alisema Wakenya wanapotoka wanapotetea viongozi kwa msingi kwamba hawakujua walichokuwa wanafanya wakiwa walevi.

“Johnson Sakaja ni sawa na Mike Sonko, isipokuwa tu kwamba hakutoroka kutoka gerezani. Wale wanaosema hakujua alichokuwa anafanya, ni wale wale ambao humwita Babu Owino muuaji kwa (kudaiwa) kufyatua risasi akiwa mlevi na bila kujua alichokuwa akifanya. Kwa mara nyingine, Wakenya wanakosa msimamo,” akasema.

Mbunge wa Starehe, Bw Charles Njagua almaarufu Jaguar pia amewahi kukamatwa mara kadhaa kwa madai ya uchochezi. Kando na hayo, alikumbwa pia na kesi za kusababisha ajali barabarani katika hali ya kutatanisha.

Tabia hizi za viongozi vijana hazionekani Nairobi pekee.

Katika Kaunti ya Nandi, Gavana Stephen Sang, 36, alikamatwa na kushtakiwa alipoongoza wakazi kuharibu shamba la kibinafsi la majani chai.

Na katika Kaunti ya Kilifi, Mbunge wa Malindi, Bi Aisha Jumwa, 45, alikamatwa alipohusishwa na ufyatuaji risasi ambapo mfuasi wa Chama cha ODM, Ngumbao Jola aliuawa.

Kisa hicho kilitokea usiku wa kuamkia uchaguzi mdogo wa Wadi ya Ganda, nyumbani kwa mgombeaji wa ODM, Bw Reuben Mwambire.

Katika Kaunti ya Murang’a, Mbunge wa Kiharu, Bw Ndindi Nyoro alikamatwa mwaka uliopita kwa kuhusishwa na rabsha zilizotokea kanisani.

Mbunge huyo alikuwa amelalamika kwamba, Mbunge Maalumu Maina Kamanda aliandaa harambee katika kanisa hilo lililo eneobunge lake bila kumwarifu.

Miongoni mwa mawaziri, aliyekuwa Waziri wa Michezo, Bw Rashid Echesa, alitimuliwa kwa sababu zisizojulikana na sasa anakumbwa na sakata ya kandarasi bandia ya silaha ya Sh39 bilioni.

Katika mwaka wa 2018, Rais Uhuru Kenyatta hakuficha hisia zake kuhusu vijana ambao wameshindwa kuafiki kiwango cha matarajio katika uongozi wao, akatetea anavyopenda kuajiri wazee kushikilia nyadhifa muhimu serikalini.

Vijana wa Makongeni mjini Thika wataka serikali iwajali

Na LAWRENCE ONGARO

VIJANA kutoka Makongeni mjini Thika, wanalalamika kuwa mpango wa kuajiri vijana wasio na kazi haujawafikia hadi sasa.

Vijana hao walishangaa ni mbinu ipi ilitumika kuajiri vijana 1,500 hivi majuzi katika Kaunti ya Kiambu.

Kiongozi wa vijana eneo la Makongeni Bw Philip Mwenda alisema wamekuwa wakiona vijana kadha wakifanya kazi za mikoni katika mitaa tofauti lakini hawajaelewa jinsi walivyoajiriwa.

“Sisi hapa Makongeni tunazidi kupambana na shida na hatuna njia yoyote ya kujikimu. Tungetaka serikali kupitia afisi ya naibu kamishna Bw Douglas Mutai, ituangazie ili nasi tupate angalau kibarua cha kutupa mkate wa kila siku,” alisema Bw Mwenda.

Alisema tangu homa ya corona ilipofika hapa nchini, wao kama vijana wamekosa hata vibarua walivyozoea kufanya.

Mkazi wa Makongeni mjini Thika, Bw Benson Njoroge, alisema wengi wao wamekosa pesa za kulipa kodi za nyumba.

“Malandilodi hawatuonei huruma kwani wao wanataka walipwe pesa za nyumba bila kujali hali ya maisha ilivyo,” alisema Bw Njoroge.

Alisema vijana wengi wamekosa mwelekeo ambapo sasa wameweka matumaini yao kwa serikali ili iwaokoe.

“Hapa mitaani tumebaki wapweke; twaomba usaidizi haraka iwezekanavyo. Mara nyingine ukifika Makongeni utapata vijana wameketi bure bila kufanya lolote,” alisema Bw Njoroge.

Naye Bi Catherine Wanjiru alisema wamekumbwa na shida kuwa kwa sababu hata chakula cha kila siku hakipatikani kwa urahisi.

“Iwapo tutatafutiwa angalau chochote cha kufanya tutashukuru. Hatutabagua kazi yoyote,” alisema Bi Wanjiru.

Vijana hao walitaka maslahi yao yaangaliwe haraka iwezekanavyo kwa sababu walisema wanazidi kuteseka.

Naibu kamishna Bw Douglas Mutai alisema kulingana na mpango huo wa kuajiri vijana kazi eneo la Thika Magharibi liliteua vijiji vya Kiandutu na Kiang’ombe, ambavyo ndivyo vina idadi kubwa ya wakazi.

“Maeneo hayo mawili yana zaidi ya wakazi 35,000 na ndiposa yakawekewa zingatio. Hata hivyo, bado vijana hao wa Makongeni hawajasahauliwa,” alisema Bw Mutai.

Vijana wapatao 1,500 waliajiriwa wiki mbili zilizopita kama njia mojawapo ya kutii agizo la Rais Uhuru Kenyatta.

Kulingana na mpango uliopo, vijana hao watakuwa wakifyeka mitaa tofauti mjini Thika, na kuzibua mitaro hya majitaka maeneo tofauti huku wakilipwa Sh600 kila siku.

SERIKALI: Kazi kwenu vijana

Na JUMA NAMLOLA

SERIKALI sasa inawaomba vijana wawe kwenye mstari wa mbele kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona. Waziri wa Afya, Bw Mutahi Kagwe Jumamosi aliwataka vijana watumie nguvu zao kuhamasisha jamii pamoja na kuleta mabadiliko ya maana kwenye juhudi za kuzuia Corona kusambaa nchini.

“Natoa ombi maalumu kwa vijana wetu ambao ndio sehemu kubwa ya jamii. Takwimu zinaonyesha kuwa vijana ndio wanaoambukizwa virusi kwa wingi na wanavisambaza kwa wazee na wakongwe,” akasema.

Aliwahimiza wachukue hatua za kuhakikisha hawaendelei kusambaza virusi hivyo kupitia tabia yao ya kutojali.

“Najua vijana damu inawachemka na wanafurahia kusafiri hapa na pale. Nawaomba msijipeleke mashambani, kwa sababu kwa kuenda huko, mnaweza kuwaua wazazi au babu na nyanya zenu,” akasema.

Badala yake, waziri anawataka vijana watumie mikakati na nguvu zao za kujiweka katika makundi kushawishiana na kufanya shughuli zinazoweza kumaliza kabisa maambukizi hayo, ambayo kufikia jana yameathiri watu 126 nchini.

“Tunajua haitakuwa rahisi, itakuwa ngumu. Hii si safari ambayo mnatarajiwa kuimaliza peke yenu. Ni jukumu lenu kama vijana kuliokoa taifa hili. Mungu kwa hekima zake ameamua kuwa nyinyi muwe hai wakati huu ambapo nchi inahitaji vijana, ili mchukue jukumu la kumaliza ugonjwa huu,” akasema.

Bw Kagwe aliwakumbusha vijana kwamba, kama ambavyo katika historia kulikuwa na vijana waliopigania uhuru na wengine wakaleta mageuzi, vijana wa sasa ni nafasi yao kumaliza corona.

Kauli hiyo ya Bw Kagwe ina maana kuwa, vijana wanapaswa kuwajiika kwa makosa watakayofanya, yatakayosambaza virusi hivyo nchini. Takwimu za wizara ya Afya zinaonyesha kuwa, asilimia kubwa ya watu walioambukizwa corona nchini ni watu wa chini ya miaka 35.

Katika baadhi ya maeneo ya nchi, vijana wengi bado wanashiriki michezo ya kuwaleta karibu kama vila Kamari. Wengine wanasafiri kutoka mji mmoja hadi mwingine au kuzuru mashambani, jambo ambalo linachangia kwa wingi usambazaji wa virusi.

Jana, waziri alionya kuwa, iwapo vijana wataruhusu uchumi wa nchi uathiriwe na virusi hivyo, ni wao watakaoumia zaidi.

“Msipoiokoa nchi, hakutakuwa na ajira na uchumi utaanguka. Ni nyinyi mtakaotuzika siku kwa mamia. Suluhisho kwa tatizo hili mnalo. Mkitaka, mnaweza kujipanga na kuzuia watu kukaribiana, miongoni mwa kanuni tulizotangaza,” akasema Bw Kagwe.

Kati ya watu 372 waliopimwa, wanne walipatikana kuwa na virusi hivyo.

“Wanaume wawili na mwanamke mmoja, wameambukizwa. Wawili walisifiri kutoka Malawi na Pakistani mtawalia,” akasema.

Waziri pia alizima mpango wa Idara Simamizi ya Nairobi kuwakusanya zaidi ya watu 600 katika jumba la Mikutano ya Kimataifa la Kenyatta (KICC) Jumatatu.

Vijana watatiza hotuba ya Aisha Jumwa

MOHAMMED AHMED na CHARLES WASONGA

KUNDI la vijana mjini Mombasa, Ijumaa limemzomea Mbunge wa Malindi Aisha Jumwa alipokuwa akiwahutubia wanahabari kuhusu mkutano wa Jumamosi wa BBI mjini humo.

Vijana hao walianza kurusha mawe hali iliyowalazimisha wanahabari kutoroka kujisalimisha.

Bi Jumwa, ambaye alikuwa ameandamana na viongozi wengine wa Mombasa amelazimika kukatiza hotuba yake, japo kwa muda tu.

Mbunge huyo wa Malindi ni mwandani wa Naibu Rais William Ruto.

Utulivu uliporejea Bi Jumwa alisema kuwa hatatishwa na wahuni waliokodiwa.

“Sitatishwa na vijana kama hawa ambao wamelipwa pesa ili waingilie uhuru wangu wa kuzungumzia masuala yanayowahusu Wapwani,” amesema Jumwa.

Mkutano huo ulivurugwa kwa mara pili pale vijana hao walishikilia kuwa viongozi hao walifaa kuondoka.

Mbunge wa Nyali, Mohammed Ali ambaye alifika baada ya dakika chache aliwakaripia viongozi waliopanga kuvurugwa mkutano huo na kushambuliwa kwa Bi Jumwa.

Ali alidai kuwa wahuni hao walikodiwa na Gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho.

“Ana haki kama Mkenya mwingine kusema yaliyo moyoni mwake. Hamwezi kumshambulia kiongozi mwanamke kwa sababu ana msimamo tofauti,” akasema Bw Ali

Jumwa na Ali ni wanachama wa mrengo wa ‘Tangatanga’ ambao wameahidi watahudhuria mkutano huo BBI katika uwanja wa Tononoka.

Hii ni licha ya wao kususia mikutano miwili ya awali katika miji ya Kisii na Kakamega.

Taharuki imetanda mjini Mombasa saa chache kabla ya kuanza kwa mkutano huo huku ikitarajiwa kuwa wandani wa Naibu Rais William Ruto na wale wa mrengo unaounga mkono Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga, watakabiliana kwa maneno makali.

Uhuru awapa vijana vyeo vya juu kuwatuliza

Na PETER MBURU

RAIS Uhuru Kenyatta Jumanne alionekana kutaka kuwatuliza vijana ambao wamekuwa wakimkosoa kwa kuwapa wazee kazi, alipoteua vijana saba kuwa mawaziri wasaidizi (CAS).

“Ningependa Wakenya kutambua kuwa saba kati ya wale nimewapa kazi za manaibu waziri (CAS) ni vijana, wengine wa chini ya miaka 30. Natumai watafanya kazi na kujifunza kutoka kwa wenzao wenye uzoefu serikalini kwa lengo la kujiandaa kwa kazi za juu zaidi serikalini siku zijazo,” Rais Kenyatta akasema.

Hatua hiyo ni kufuatia malalamiko kutoka kwa vijana kuwa Rais Kenyatta anawapa kazi wazee waliostaafu huku maelfu ya vijana waliohitimu wakiwa hawana kazi.

Walioteuliwa kuwa Manaibu Waziri (CAS) ni Nadia Ahmed Abdalla na Maureen Magoma (Habari, Mawasiliano na Teknolojia), Ann Mukami Nyaga (Kilimo), Mumina Bonaya na Zacharia Kinuthia Mugure (Elimu), Abdul Bahari (Leba) na Lawrence Karanja (Viwanda).

Wengine ni Peter Odoyo (Ulinzi), Winnie Guchu (Afisi ya Sheria Serikalini), Wavinya Ndeti (Uchukuzi), Lina Chebii (Kilimo) na Mercy Mwangangi (Afya).

Vilevile, miongoni mwa Mawaziri Wasaidizi (CASs), Patrick Ole Ntutu alihamishwa kutoka Wizara ya Usalama wa Ndani hadi ya Leba, badala yake akiingizwa Hussein Dado ambaye alikuwa wizara ya Ugatuzi.

Rais pia alifanya mabadiliko miongoni mwa makatibu wa wizara, ambapo aliwateua Jwan Ouma kuwa katibu wa idara ya Mafunzo ya Kiufundi, Mary Kimonye (idara ya Huduma za Umma), Simon Nabukwesi (Masomo ya Vyuo vikuu na Utafiti), Solomon Kitungu (Uchukuzi), John Weru (Biashara) na Enosh Momanyi Onyango (Miundomsingi).

Baadhi ya makatibu waliohamishwa ni Joe Okudo (Utalii hadi Spoti), Kevit Desai (idara ya Mafunzo ya Kiufundi hadi wizara ya EAC), Kirimi Kaberia (wizara ya Spoti hadi ya Uchimbaji Madini), Esther Koimett (idara ya Uchukuzi hadi ya Utangazaji) na Colleta Suda (idara ya Masomo ya Vyuo Vikuu na Utafiti hadi idara ya Jinsia).

Mazungumzo baina ya Kanisa na vijana yachangia kuimarika kwa usalama

Na SAMMY KIMATU

KANISA linafurahia matunda ya mazungumzo na vijana yaliyochangia kuimarika kwa usalama wakati wa msimu wa sherehe.

Aidha, hakuna ripoti zilizotolewa kuhusiana na uhalifu Desemba 2019 katika maeneo ya Ngelani na Kisekini.

Akiongea mwishoni mwa wiki katika Kanisa la Africa Inland Ngelani katika Kaunti ya Machakos, Mchungaji Bonface Kyalo Nthenge alisema nidhamu ilisisitizwa kwa vijana kupitia mikutano na kambi.

“Kama kanisa, tunashirikisha vijana wetu katika kujikimu katika kambi za vijana na programu zingine za kanisa kupitia Idara ya Elimu ya Kikristo almaarufu CED,” Rev Nthenge aliambia Taifa Leo.

Alimshukuru mtoto wa kike kwa kuwapiku wavulana katika KCPE na KCPE na kuongeza kwamba wasichana walizoewa kwa kuonekana wadhaifu wakilinganishwa na wavulana.

“Siku za hapo nyuma, kasumba ilikuwa ni wavulana wanaongoza katika mitihani lakini wakati huu, mambo yamebadilika,” akasema.

Afrika yashauriwa kukoma kuwanyima vijana nafasi maishani

NA ALLAN OLINGO

VIONGOZI wa bara Afrika wamehimizwa kupatia kipaumbele masuala yanayohusu vijana.

Suala hilo lilijitokeza katika kongamano linaoendelea nchini Rwanda la Kusi Ideas Festival, kuhusiana na masuala ya Bara Afrika katika kipindi cha miaka 60 ijayo.

Katibu Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Biashara na Maendeleo (UNCTAD), Dkt Mukhisa Kituyi aliwasisimua waliohudhuria kongamano, akisema kizazi cha sasa kinatilia maanani ushirikiano badala ya mashindano ili kufanikiwa.

Dkt Kituyi alisema bara hili linafaa kuwaruhusu vijana kutangamana, kuwekeza na kuhamia taifa moja hadi jingine bila kuwekewa vikwazo vya usafiri na kutangamana.

“Hawa vijana wanatafuta nafasi ya kupata riziki si katika mataifa yao ya kuzaliwa pekee bali hata nchi za mbali. Wanaangalia mbali wanapojizatiti kutimiza ndoto zao na hulazimika kuelekeza macho yao kwenye nafasi za kujiinua zinazopatikana kwingine. Serikali za mataifa ya Afrika zinafaa kutambua hilo kisha kuondoa vikwazo vya usafiri au kutangamana,” akasema Dkt Kituyi.

Marais wa nchi mbalimbali barani pia waliombwa kushirikiana na kufungua mipaka ya mataifa yao kwa raia kutoka nje ili kuwaruhusu kufanya biashara na kuinua uchumi wa nchi husika.

“Tunafaa kuelewa kwamba asilimia 53 ya raia wanaohamia mataifa yetu mbalimbali hapa barani ni Waafrika wenzetu. Wahamiaji hawa ni wa manufaa kwa nchi zao asili na zile wanazohamia kutokana na uwezo wao wa kuwekeza. Haya ndiyo masuala yanayofaa kupigiwa debe badala ya mashindano yasiyozalisha chochote,” akaongeza Dkt Kituyi.

Afisa Mkuu Mtendaji wa Bodi ya Maendeleo Nchini Rwanda(RDB), Bi Clare Akamanzi alisema mataifa hayafai kuhofia kuondoa vikwazo vya mipaka, akisema uhuru wa kufanya biashara utasaidia kustawisha nchi za Afrika.

“Hakuna sababu maalum ya kuogopa kufungua mipaka yetu. Kama Rwanda tumekuwa tukipigia upato suala hili kwa muda wa miaka mitano iliyopita na limetufaa sana kwa kuwa tumewavutia wageni na wawekezaji wengi,” akasema Bi Akamanzi.

Mwanachama wa bodi ya kampuni ya Msingi East Africa, Bw Linus Gitahi naye alitaka serikali za Afrika kuelekeza macho katika uundaji wa mtaala mpya unaosisitiza matumizi ya teknolojia kuendesha masuala ya nchi.

Wazee mnaovuta bangi mnachangia vijana kupotoka – kamishna

Na LAWRENCE ONGARO

KUNA haja ya wazee kuwa kielelezo kwa vijana ili waweze kuiga mfano wao.

Hayo yalitajwa na Naibu Kamishna wa Thika Mashariki Bw Thomas Sankei.

Alisema Jumapili kwamba uchunguzi wake umebainisha ya kwamba katika eneo la Makutano, Kilimambogo, wazee wameonekana wakivuta bangi na hiyo ni ‘tabia mbaya’ mbele ya vijana.

“Nyinyi wazee inaonekana mmevuka mpaka sasa. Badala ya kutoa mfano mwema, nyinyi ndio mnavuta bangi,” alisema Bw Sankei.

Alisema wazazi wana jukumu kubwa la kuwapa vijana mawaidha ili waweze kuwa raia wema wa kutegemewa.

Alisema imefika wakati kila mmoja awe mstari wa mbele kuwaleta vijana karibu na kuwapa mawaidha na mwelekeo ufaao.

“Kila mara tunaposhuhudia mambo mabaya ni sharti tuseme hapana kwa sauti ya juu. Vijana hawa walio mbele yenu wanataka kusikia mengi kutoka kwenu,” alisema Bw Sankei.

Alisema vijana wamejaliwa vipaji tofauti na kwa hivyo wanastahili kuvitumia vilivyo kwa sababu ndivyo vitawainua katika maisha ya baadaye.

“Nimefurahishwa na vipaji vya vijana hawa na iwapo watakuza talanta hizo, bila shaka watafanikiwa katika siku zijazo,” alisema afisa huyo mkuu.

Aliyasema hayo wakati wa sherehe za Mashujaa Dei ambazo katika Kaunti ya Kiambu zilifanyika katika mkao makuu ya naibu wa Kamishna eneo la Kilimambogo.

Aliwataka wakazi wa eneo la Kilimambogo na maeneo jirani wawe na umoja na washirikiane kwa jambo lolote lile.

Alisema umoja ndiyo nguvu kwa umma.

Mabadiliko kadhaa

Mwakilishi wa naibu gavana wa Kiambu Dkt James Nyoro, Bw Peter Kang’ethe alisoma hotuba ya kaimu gavana huku kukiwa na mikakati ya kuleta mabadiliko kadhaa katika Kaunti hiyo.

Kulingana na mipango hiyo, Kaunti ya Kiambu iko tayari kufanya kazi kwa pamoja na serikali kuu.

Mipango hiyo inaelezea wamiliki wote wa baa za kuuza pombe watabuni vyama vya ushirika kama njia mojawapo ya kujiendeleza na kuwa pamoja.

Alieleza ya kwamba hospitali zote – kuanzia kiwango cha Level 5 hadi Level 2 zitapata dawa bila kukosa na hii inatokana na kampuni ya kusambaza dawa ya Kemsa kutoa hakikisho kuwa dawa zitapatikana.

Alisema sekta za chai na kahawa zinafanyiwa uangalizi mpya ili kuziboresha zaidi.

Ripoti ya naibu gavana ambaye kwa sasa ndiye kaimu gavana wakati Gavana Waititu akikabiliwa na kesi mahakamani, ilidai ya kwamba kwa muda mrefu kumekuwa na usimamizi mbaya wa sekta hizo mbili na kwa hivyo, ni sharti jambo la dharura lifanywe.

Alikariri ya kwamba kila mfanyakazi atapewa nafasi yake kutekeleza wajibu wake bila kutishwa na yeyote.

WANGARI: Serikali imepuuza maslahi ya vijana wa Kenya

Na MARY WANGARI

MAJUZI kumekuwa na misururu ya visa na masimulizi ya kutamausha kuhusu vijana waliosoma na kupata shahada za digrii na hata uzamili, wanaoishi maisha ya uchochole kwa kukosa ajira.

Ripoti hizo zimewaacha Wakenya wakijiuliza nini hasa umuhimu wa elimu katika kizazi cha leo.

Idadi kubwa ya vijana walioathiriwa ni werevu katika masomo na walipata alama za juu zilizowawezesha kufanya kozi tajika. Ole wao! Hawakuwa tayari kwa kilichowasubiri katika ulimwengu usio na huruma uliochekelea ushauri waliopatiwa kwamba ‘elimu ndio ufunguo wa maisha!

Kisa cha Kevin Ochieng aliyekuwa akiishi barabarani bila makao baada ya kukosa kazi licha ya kufuzu kwa daraja ya kwanza katika Sayansi ya Hisabati na Takwimu, ni mfano mzuri.

Kinaya ni kwamba iligharimu masaibu yake kuangaziwa na vyombo vya habari, ndipo mashirika chungu nzima mashuhuri ya kiserikali na kibinafsi, yalipojitokeza kumpa kazi, ikiwemo kampuni zilizokuwa zimemkataa hapo mbeleni, na kuwaacha wengi wakishangaa zilikotoka ghafla nafasi hizo za kazi.

Hii ni ishara thabiti kwamba tatizo si vijana bali ni sera mbovu na unafiki katika jamii kwa jumla iliyowasaliti vijana wetu.

Ni kinaya na unafiki wa kiwango cha juu kuwasikia baadhi ya watu waliojitwika ghafla cheo cha ujuzi kuhusu masuala ya kiuchumi, wakiwashauri vijana kufikiria mbinu nyinginezo za kujipatia riziki badala ya kutegemea ajira etu kwa sababu hakuna nafasi za kazi nchini.

Inakera mno kuwasikia baadhi ya watu wakiwasuta vijana kwa kuzembea na kukosa ubunifu wa kuvumbua mbinu nyinginezo badala ya kusaka ajira ilhali wanaowakashifu vijana hao wameajiriwa.

Wa kulaumiwa ni nani wakati mfumo wa elimu waliopitia vijana hao uliwaandaa kwa ajira? Ni vigumu mno kubadili ghafla mawazo ya kijana aliyeandaliwa kwa zaidi ya miaka 15 tangu shule ya chekechea hadi chuo kikuu ‘kusoma kwa bidii’ ndipo ‘apate kazi nzuri.’

Ikiwa ni biashara, ni wazi kwamba unahitaji mtaji kuanza pamoja na mazingira mwafaka ili biashara inawiri. Baadhi ya vijana waliobahatika kupata mtaji na kuanza biashara kwa lengo la kuunda ajira, wamesimulia masaibu waliyopitia kutokana na sera mbovu zilizowalazimu kufunga biashara zao na kurejea walipoanzia.

Ukweli mchungu ni kwamba, serikali na jamii kwa jumla imewasaliti vijana na ndiposa tunashuhudia idadi kubwa ya vijana gerezani kwa kutenda uhalifu baada ya kukata tamaa maishani. Ni sharti tubuni sera mwafaka zitakazowezesha kuwepo kwa mazingira bora kwa vijana kupata nafasi za kujipatia riziki na kujiendeleza kimaisha, la sivyo, mustakabali wetu kama taifa unaning’inia hatarini.

mwnyambura@ke.nationmedia.com

OBARA: Tutatue vikwazo vya ajira badala ya kuimbaimba ‘Vijana Wajiajiri’

Na VALENTINE OBARA

MAHALI tulipofika sasa, wimbo huu wa ‘Vijana Wajiajiri’ wasinya!

Kila mara mdahalo unapoibuka kuhusu janga la ukosefu wa ajira kwa vijana Kenya, utasikia sauti nzito kutoka pembe tofauti zikiwika: “Vijana wajiajiri.”

Wakati mwingi, sauti hizo huwa zinatoka kwa watu waliokalia viti vya kifahari afisini walimoajiriwa. Wengine wao ni watumishi wa umma, kumaanisha ni waajiriwa wa raia wale wale ambao wanashurutisha kujiajiri.

Sina pingamizi kuhusu umuhimu wa ujasiriamali katika enzi hizi ikizingatiwa kwamba hali ya maisha imebadilika na hakuwezi kuwepo nafasi za kutosha kuajiri afisini kila kijana anayekamilisha elimu ya juu.

Lakini jinsi mdahalo kuhusu ukosefu wa ajira unavyoendeshwa, ni kama kwamba tunalaumu vijana kwa uzembe na upumbavu unaowakosesha uwezo wa kujiajiri wenyewe.

Changamoto zinazokumba vijana kikazi zimesababishwa na masuala tofauti ambayo yanastahili kuzingatiwa kwa uzito zaidi kuliko kujaribu kulazimisha kila kijana kuwa mjasiriamali hata kama hana uwezo huo.

Ujasiriamali stadi hauhitaji tu mafunzo ya darasani wala ya kiufundi au hela za kuwekeza. Kuna ujuzi fulani ambao mtu huzaliwa nao ndipo afanikiwe, na ukitaka kujua ukweli huu, tazama tu wajasiriamali waliobobea kimataifa na ukague wasifu wao.

Mwaka uliopita, Benki Kuu ya Kenya ilifichua kwamba zaidi ya asilimia 61 ya biashara ndogo ndogo huwa hazikamilishi miaka miwili kabla kufungwa. Waimbaji wa ‘Vijana Wajiajiri’ wameamua kufumbia macho takwimu hizi!

Mfumo wetu wa elimu umebainika kuwa ovyo na unaohitaji mabadiliko. Itachukua muda kabla tuone mafanikio ya juhudi zinazoendelezwa sasa kubadilisha mfumo wa elimu, hivyo basi hebu tuangalie masuala mengine yatakayoboresha hali kwa dharura.

Ufisadi ni mojawapo ya vikwazo vinavyozuia vijana kujiendeleza kimaisha hata wakijitosa katika biashara. Kisheria, asilimia 30 za zabuni serikalini zinafaa ziende kwa vijana. Lakini kufikia sasa, tunachoshuhudia ni zabuni kutolewa kwa njia za ufisadi na kujuana kisha viongozi wao hao wanaohusika ndio huja kutuambia vijana wajiajiri!

Vilevile, mandhari ya kufanya biashara katika nchi hii ni duni mno. Mashirika mengi makubwa ya kimataifa yalishindwa kustahimili mandhari magumu ya kuendesha biashara Kenya, sembuse vijana ambao ndio wanajaribu bahati yao kwa biashara ndogo ndogo!

Zaidi ya hayo, sheria za uhamiaji zinastahili kutekelezwa kikamilifu ili kuzuia raia wa kigeni kunyakua kazi zinazoweza kufanywa na Wakenya.

Pendekezo vijana wasio na kazi wapewe Sh48,000 na serikali

Na PETER MBURU

WABUNGE wawili wanapendekezea bunge kubadili sheria, ili vijana ambao hawajaajiriwa wawe wakipewa kiwango fulani cha pesa na serikali, kama mbinu ya kuwakinga kutokana na hali ngumu ya maisha.

Wabunge Caleb Amisi (Saboti) na Didmus Barasa (Kimilili) wanalitaka bunge kubadili sheria kuhusu Uajiri na Huduma za Kijamii, ili vijana ambao hawana kazi wawe wakipewa Sh48,000 kila mwaka na serikali, sawa na Sh3,000 kila mwezi.

Viongozi hao aidha wamependekeza kuwa wanafunzi wanaofuzu kwa Diploma ama Shahada ya kwanza wawe wakilipwa Sh25,000 wanapochukuliwa kufanya kazi za kimafunzo (internship).

Endapo bunge litapitisha pendekezo hilo, ambalo mwanzilishi wake ni Bw Amisi, kila kijana asiye na kazi atakuwa akipewa Sh12,000 na serikali kila baada ya miezi minne.

“Watu wasio na kazi Kenya hawalipwi marupurupu ya kukosa kazi na misaada yoyote ya kimaisha kama jinsi ilivyo katika mataifa mengine. Vijana wengi hawawezani na maisha ya mijini ambapo ndipo nafasi za ajira zinapatikana,” Bw Amisi akasema.

Mbunge huyo alijutia kuwa vijana wengi wanakosa kupewa misaada na ufadhili ambao utawawezesha kupata ajira ili wajitegemee wenyewe.

Kulingana na ripoti ya punde zaidi kutoka kwa shirika la kimataifa la UNDP, vijana wapatao milioni 2.6 hawana kazi nchini, licha ya kuwa wengi wao wana ujuzi wa kufanya kazi mbali mbali na wanazitafuta.

Hii ni kumaanisha kuwa serikali itatumia jumla ya Sh93.6 bilioni kuwalipa vijana hao mwaka wa kwanza, kiwango ambacho kitapanda hadi zaidi ya Sh100 bilioni mwaka wa pili.

Bw Barasa naye anataka wanafunzi wa Diploma na Shahada wanaofuzu wawe wakipewa kazi za kimafunzo na mashirika ya serikali na ya kibinafsi, na kulipwa Sh25,000 kila mwezi.

“Mswada huu unataka wanafunzi hao walipwe pesa chache zaidi ambazo zinaruhusiwa kwao,” Bw Barasa akasema.

Kulingana na sheria ya sasa kuhusu utoaji wa misaada ya kijamii kwa watu, watu wenye uhitaji wa misaada hiyo pekee ndio wanaruhusiwa.

Watu waliotajwa ni mayatima, watoto wasio na uwezo, wazee maskini, wasio na kazi, walemavu, wajane na wengine ambao waziri anaweza kuruhusu.

Wabunge hao walikuwa mbele ya Kamati ya Bajeti bungeni Jumanne ambapo waliwasilisha miswada yao, na kutetea jinsi itafadhiliwa.

‘Vijana wanaofanya kulihali kuepuka maovu katika jamii wanastahili pongezi’

NA SAMMY WAWERU

UKOSEFU wa ajira miongoni mwa vijana nchini unanyooshewa kidole cha lawama kama njia mojawapo inayochangia visa vya uhalifu.

Vijana wanalalamikia kufungiwa nje katika nafasi za kazi licha ya serikali ya Jubilee kudai inaendelea kubuni ajira.

Wahalifu kuuawa hasa mijini, si suala geni asasi za usalama zinapoarifiwa ili kukabiliana nao.

Licha ya kwamba kuna wanaoshiriki uhalifu si kwa sababu ya kukosa kazi, ila ni mazoea, wengi wanadaiwa kuushiriki ili kuzimbua riziki.

Ni kutokana na hilo ambapo baadhi ya mashirika ya kijamii na yasiyo ya kiserikali yanajaribu kadri yawezavyo kushirikisha vijana katika gange, zingine zikiwa kutoa huduma bila malipo.

Kwa kufanya hivyo, yanawaepusha kushiriki maovu. Pia, baadhi ya mashirika yanawapendekeza kwa kampuni ili kupata ajira.

Mbali na kuhamasisha jamii kuhusu maambukizi ya Ukimwi na magonjwa ya zinaa, Kikundi cha Liberty na ambacho ni cha kijamii, pia kinajaribu kunasua vijana dhidi ya kushiriki uhalifu.

Paul Kahiro, mmoja wa waasisi wacho anasema kinalenga vijana wa kaunti ya Nairobi na Ruiru, Kiambu.

“Tumefanikiwa kubadili mienendo ya vijana kadhaa ambao awali walishiriki uhalifu. Kuna baadhi yao wameweza kuweka kazi,” anaeleza Bw Kahiro.

Kulingana na mwenyekiti Ezra Aswani, Liberty Group hutumia sanaa kama vile michezo ya kuigiza na kukariri mashairi yenye mada husika kupasha ujumbe na kuhamasisha jamii.

“Tunanoa vijana waliobadili mienendo kuvutia walioshikwa na minyororo ya matendo maovu. Waonapo wenzao wanaishi maisha huru na ya kujitegemea, wanayatamani na hawana budi ila kujiunga nasi,” anafafanua Bw Aswani.

Kando na mashirika ya kijamii, kuna wananchi wazalendo wanaotumia vipaji vyao kunusuru vijana. Jamal Njambe, kutoka kaunti ya Nyeri ni mmoja wao.

Historia ya kaunti hiyo ikiandikwa, jina la Bw Jamal halitakosa kujumuishwa kwa juhudi zake kudhibiti visa vya uhalifu katika mtaa wa Majengo, ambao awali uligonga vichwa vya habari kwa kukita mizizi uhalifu.

Barobaro huyu amekuwa akitumia sanaa kubadilisha mawazo ya vijana.

Ni mkufunzi wa michezo ya kuigiza na sarakasi, malenga na mwanamasumbwi hodari, na anatumia vipaji vyake kuwateka dhidi ya kushiriki matendo haramu.

Jamal pia ni muundaji hodari wa bidhaa za urembo na utanashati kwa kutumia shanga.

“Kwa muda wa miaka mitano sasa nimekuwa nikiwashirikisha katika sanaa zote nilizobobea. Furaha yangu ni kuona vijana wanabadili mienendo na tabia, na kujiimarisha kimaisha kwa kufanya kazi halali,” anaelezea.

Kazi ipo

Hata hivyo, juhudi za kukabiliana na visa vya uhalifu nchini si rahisi.

Waliofanikisha wanahoji safari hiyo inahitaji uvumilivu na uzalendo.

Ukosefu wa fedha za kutosha ni baadhi ya changamoto ambazo wazalendo waliojituma hukumbana nazo.

“Wakati mwingine tunalazimika kuchangana kama wanachama ili kusafiri mitaa tunayolenga,” anasema Paul Kahiro wa Liberty Group.

Kwa upande wake Jamal Njambe, anasema wakati mwingine hutumia mapato yake kugharimia lishe kwa vijana anaokomboa kutoka kwa minyororo ya uhalifu.

Lingekuwa jambo la busara kwa serikali kutambua wazalendo na makundi yanayobeba mzigo huo na kuwapiga jeki kifedha.

Madhehebu ya dini pia yanahimizwa kushirikiana nao kwa karibu ili kudhibiti visa vya uhalifu.

JARED OUNDO: Anahakikisha vijana wamesalia nguzo ya jamii

NA PAULINE ONGAJI

Alianza kujihusisha na masuala ya kunasihi vijana akiwa katika kidato cha pili na miaka kumi baadaye mchango wake katika kuimarisha maisha ya vijana unahisiwa katika fani mbalimbali katika jamii.

Huo ulikuwa mwaka wa 2008 ambapo Jared Oundo, 26, wakati huo akiwa katika kidato cha pili, alizamisha akili yake katika masuala ya kusaidia jamii na hasa vijana huku akianzisha shirika la Jubilant Stewards of Africa.

Ni mwito ambao aliuendesha hata baada ya kukamilisha shule ya upili ambapo katika kipindi cha mwaka mmoja pekee alisajili shirika hili na kuanza rasmi kunasihi vijana kuhusu jinsi ya kufanya vyema shuleni, kuwahamasisha kuhusu athari za matumizi ya mihadarati na jinsi ya kukabiliana na virusi vya HIV, umuhimu wa kutangamana na watu, miongoni mwa mambo mengine.

Kufikia sasa, anajivunia kuendesha shughuli hii katika mataifa 23 barani Afrika ikiwa ni pamoja na Kenya, Sierra Leone, Zambia, Afrika Kusini, Zimbabwe, Malawi na Sudan Kusini.

Bw Oundo akihutubia wanafunzi wa Taasisi ya Uzuri. Picha/ Hisani

Kadhalika ameshiriki katika kuanzisha vyama katika shule za msingi na upili na vyuo vikuu ambapo anatumia jukwaa hili kunasihi wanafunzi. “Hapa ndipo suala la kufanya vyema masomoni, vile vile jinsi ya kuchagua taaluma zinazowafaa huzungumziwa,” aeleza.

Shughuli zizi zimempeleka katika mamia ya taasisi za kielimu katika Kaunti mbalimbali. “Baadhi ya taasisi hizo ni pamoja na shule za upili za Highway, Moi Girls, Upperhill School, Ruai Boys (Nairobi); shule za msingi kama vile Buyende Primary School, Kaunti ya Busia, na Chuo Kikuu cha Masai Mara, miongoni mwa taasisi zingine,” aeleza.

Ni ujumbe huu unaopitishwa kupitia kitabu chake Awakening the Academic Giant kinachohimiza wanafunzi kuimarisha matokeo yao shuleni. Kupitia jitihada hizi wanafunzi wengi ambao awali walikuwa na alama za chini shuleni wamezidi kuimarika.

Kampeni zake hazijakomea tu hapo kwani amejihusisha vilivyo katika vita dhidi ya maradhi ya zinaa na hasa virusi vya HIV. “Nimehusika katika vikao vya kuwashauri vijana, kuwahamasisha kuhusu maradhi ya zinaa na mbinu za kuhakikisha usalama wao,” aeleza.

Bw Oundo akiwashauri wanafunzi wa shule ya upili. Picha/ Hisani

Mafunzo haya yameendelezwa katika sehemu mbalimbali ikiwa ni pamoja na vitongoji duni kadha jijini Nairobi kama vile Mukuru Kwa Reuben, Kwa Njenga na Kayole. Pia wameendesha shughuli hizi katika Kaunti za Uasin Gishu, Kisumu, Busia, Meru, Narok na Homa Bay miongoni mwa zingine, ambapo pia madhumuni ni kukabiliana na tatizo la unyanyapaa kwa wale ambao tayari wana virusi hivi.

Mradi huu ulianza kama chama kidogo pindi baada ya kuondoka sekondari huku ari yake ikichochewa na aliyekuwa Rais wa Amerika Barack Obama na mwanaharakati wa mazingira, marehemu Prof Wangari Maathai. “Nilishuhudia vijana wengi wakitaabika kwani walikuwa wametekwa na mihadarati, na hivyo nikatumia nafasi hiyo kukuza ndoto zao,” aeleza.

Lakini sasa japo anahisi kwamba hajaafikia lengo lake, kupitia jitihada zake vijana wengi wamebadilisha mienendo kwani visa vya ulevi, matumizi ya mihadarati, mimba za mapema na maambukizi ya virusi vya HIV vimepungua.

Kwa sasa ndoto yake ni kuona bara la Afrika likikuza vijana wanaowajibika na watakaochukua uongozi katika siku zijazo na hivyo kuimarisha maisha ya raia wa bara hili.

Ukimwi: Maambukizi kwa vijana yanatisha

VERAH OKEYO na ANGELA OKETCH

WATAFITI na wataalamu wa afya wanaadhimisha Siku ya Ukimwi Ulimwenguni hii leo wakitoa wito kwa taifa kuangazia zaidi vijana wachanga, ambao wamekuwa wakichangia pakubwa katika maambukizi mapya ya Ukimwi nchini.

Kiwango cha kitaifa cha maambukizi ya virusi hivyo ni asilimia 7.7, na kuifanya Kenya kuwa miongoni mwa mataifa sita yanayolemewa mno na janga la Ukimwi barani Afrika.

Kulingana na ripoti iliyochapishwa wiki jana na Baraza la Kitaifa la Kudhibiti Ukimwi (NACC), vijana wachanga 17,667 wenye umri wa kati ya miaka 15 na 24 waliambukizwa Virusi vya Ukimwi (HIV). Hii ni asilimia 40 ya maambukizi yote mapya 52,800 yaliyoshuhudiwa nchini Kenya.

Mbali na kuchangia visa viwili kati ya kila vitano vya maambukizi, sababu kuu ya vifo vinavyoshuhudiwa miongoni mwa vijana wachanga ni magonjwa yanayotokana na makali ya Ukimwi.

Ndiyo hali ya kutamausha inayojitokeza hususan ukiongeza matineja walio na umri wa miaka kati ya 10 na 19 katika kundi hilo la vijana wachanga, kwa mujibu wa Mkuu wa Kitengo cha Kiufundi katika NACC, Dkt Celestine Mugambi.

“Matineja wengi na vijana wachanga hawajui hali yao ya HIV. Vilevile, hawana maelezo sahihi kuhusu HIV na Ukimwi,” Dkt Mugambi aliambia Taifa Leo.

Dkt Patrick Oyaro, mtafiti na Afisa Mkuu Mtendaji wa RCTP -Faces, ambalo ni shirika lisilo la kiserikali linaloendesha utafiti wa HIV eneo la magharibi mwa Kenya, alisema ingawa vijana wachanga hupimwa HIV na kupewa matibabu, bado wanakabiliwa na changamoto ya kufuatilia kwa makini taratibu za matibabu.

Alitaja unyanyapaa miongoni mwa vijana hao, hususan shuleni, kama moja ya sababu zinazowafanya kutomeza dawa hizo za kukabiliana na makali ya virusi (ARVs) kwa utaratibu.

Dkt Abdhalah Ziraba, mtaalamu wa afya ya umma katika shirika la

African Population and Health Research Centre (APHRC) alihimiza wadau kuangazia suala la jinsia katika vita dhidi ya Ukimwi akisema juhudi zaidi zinafaa kuelekezwa katika miradi inayowalenga wasichana na wanawake.

Aliandika: “Mengi ya maambukizi yanashuhudiwa katika kundi hili kwa sababu mbalimbali za kijamii.”

Inavunja moyo kuona viongozi vijana wafisadi – Uhuru

RUTH MBULA Na BENSON MATHEKA

RAIS Uhuru Kenyatta Jumatatu aliwaingilia vijana walio katika nafasi za uongozi akisema wale waliokabidhiwa nyadhifa mbalimbali wamemvunja moyo yeye mwenyewe na taifa lote kwa jumla.

Akihutubu katika eneo la Sotik, Kaunti ya Bomet alipofungua kiwanda cha maziwa, Rais Kenyatta alisema vijana waliopewa nafasi za uongozi wameshindwa katika majukumu yao na kuwa ndio wanaoongoza katika ufisadi.

Aliongeza kuwa vijana hao hawana cha kuonyesha katika vyeo walivyopewa na akawatetea wazee akisema wamekuwa wakifanya kazi bora na ya kuridhisha wakilinganishwa na vijana, na pia wanazingatia maadili.

Rais alisema vijana wengi hulalamika kila mara kuhusu uhaba wa nafasi za kazi lakini wanashindwa kutumia fursa wanazopewa.

“Kila mara wanahimiza viongozi wazee kuondoka kwenye vyeo, lakini tukitazama mahala walipo vijana, tunaona shida tupu,” akasema

Aliwapatia changamoto vijana kuchukua fursa ya vyeo wanavyopewa kuonyesha wanaweza kufanya kazi inavyohitajika na pia wanaweza kutegemewa.

Kumekuwa na malalamiko katika teuzi ambazo Rais amekuwa akifanya vijana wakilalamika kuwa anapendelea wazee.

Rais alionekana kuwalenga magavana vijana ambao kaunti nyingi wanazosimamia zinakumbwa na matatizo na siasa duni.

Lakini ikiwa Rais Kenyatta alimaanisha maafisa wa serikali walioshtakiwa kwa ufisadi, wazee waliofikishwa kortini ndio wengi.

Tangu atangaze vita dhidi ya rushwa, maafisa wa wizara, idara na mashirika ya serikali walioshtakiwa kwa ufisadi ni walio na umri wa zaidi ya miaka 35 ambao kulingana na Katiba hawawezi kuitwa vijana.

Maafisa wa Shirika la Vijana wa Huduma kwa Taifa (NYS), Hazima ya Vijana, kampuni ya stima nchini (Kenya Power) na Shirika la ukadiriaji ubora wa bidhaa nchini (KEBS) walioshtakiwa kwa ufisadi wako na umri wa zaidi ya miaka 40.

Katika Baraza la Mawaziri hakuna waziri aliye na umri wa chini ya miaka 40. Mawaziri wanaohudumu kwa sasa wako na umri wa kati ya miaka 46 na 60.

Miongoni mwa waziri wenye umri wa chini ni waziri wa Kilimo Mwangi Kiunjuri aliye na umri wa miaka 49, Eugene Wamalwa aliye na umri wa miaka 49, Charles Keter (Kawi) aliye na umri wa miaka 48 na Joe Mucheru, waziri wa Tekinolojia ya Habari na Mawasiliano ambaye ana umri wa miaka 46.

Huenda ikawa Rais alikuwa akizungumza kuhusu vijana kwa kutozingatia umri unaowafafanua kikatiba, na badala yake wale wanaoonekana vijana machoni pa umma.

TAHARIRI: Wadau watatue shida za vijana

NA MHARIRI

KUONGEZEKA kwa visa vya kujitoa uhai miongoni mwa vijana ni jambo ambalo linatishia msingi na mustakabali wa jamii ya sasa.

Ni suala nzito ambalo linahitaji kushughulikiwa kwa haraka, kwani mkondo huu unaendelea kupanuka kadri siku zinavyosonga.

Kulingana na takwimu ambazo zimetolewa na mashirika kadhaa ya kijamii, vijana wengi wanaojipata katika hali hii ni wale walio kati ya miaka 18 na 35.

Nayo Idara ya Polisi inasema kuwa karibu visa 1,400 vya vijana waliojitoa uhai ama waliojaribu kujitoa uhai viliripotiwa katika vituo mbalimbali vya polisi mwaka uliopita.

Tafiti kadhaa zimebaini wazi kwamba changamoto za kiuchumi, ukosefu wa ajira, matatizo ya kimapenzi ama ndoa ni baadhi ya viini vikuu vya vifo hivyo.

Ni dhahiri kwamba vijana wengi wanakabiliwa na changamoto za kiuchumi, hasa wanapobaini kwamba matumaini makubwa waliyokuwa nayo wakisoma ni kinyume na uhalisia wanaokumbana nao wanapoanza kutafuta ajira.

Wengi hutamauka wanapokumbuka juhudi nyingi walizoweka wakiwa vyuoni ama taasisi nyingine za masomo ili kufanikiwa wanapomaiza taaluma zao. Kwa haya yote, imefikia wakati ambapo lazima wadau husika wabuni sera ambayo itahakikisha kwamba kuna mpango wa kuwasaidia vijana wanaohitimu kutoka vyuo mbalimbali.

Ingawa serikali imefanya juhudi kuimarisha Hudma ya Kitaifa ya Vijana (NYS) mikakati hiyo imeonekana kutofaulu kutokana na sakata za ufisadi ambazo zimekuwa zikiripotiwa kila mara.

Hata hivyo, hilo halimaanishi kwamba juhudi hizo zinapaswa kuachwa, kwani idadi ya vijana itazidi kuongezeka.

Mfano mmoja serikali inapaswa kuiga ni kubuni hazina maalum ya kushughulikia vijana wote wanaomaliza masomo yao kama ilivyo katika nchi kama Denmark.

Chini ya mpango huo, vijana hao hupewa kiasi fulani cha pesa kujiendeleza ili kuhakikisha kwamba wanaepuka changamoto zitokanazo na ukosefu wa ajira. Kwa mfano huu, lazima Kenya iondoe hali ambapo vijana wengi huanza kulipa mikopo ya Halmashauri ya Elimu ya Juu (HELB) ilhalo wengi wao huwa hata hawana ajira.

Kwa mkakati kama huo, huenda ukawa mwanzo wa kutatua changamoto za kiuchumi ambazo zinawakumba mamilioni ya vijana nchini.

OBARA: Kinaya cha mwaka vijana kumrai Raila awakomboe

Na VALENTINE OBARA

HAYAWI hayawi hatimaye huwa. Licha ya kilio kutoka kwa wananchi wengi hasa wenye mapato ya chini, mswada wa fedha hatimaye uliidhinishwa na Rais Uhuru Kenyatta ukiwa na ushuru mpya kwa Wakenya.

Dalili zilikuwa wazi kwa yeyote anayefahamu vyema siasa za nchi hii kwamba mswada huo ungepita kwa njia yoyote ile. Na hivyo ndivyo ilivyokuwa kwani sauti ya mwananchi ilipuuzwa hata bungeni.

Kwanza ningependa kuchukua fursa hii kuwapongeza wabunge waliosimama kidete na wananchi wengi wanaolemewa kiuchumi kupinga sheria hiyo ya ushuru mpya.

Wakati wote ambapo kulikuwa na mdahalo mkali kuhusu mswada huo ambao sasa ni sheria, kuna baadhi ya watu ambao walimlaumu Kiongozi wa Upinzani Raila Odinga kwa kutoupinga kwa msingi wa muafaka wake na rais.

Kinachonisikitisha ni kuwa miongoni mwa waliokuwa wakimlalamikia Bw Odinga ni idadi kubwa ya vijana hasa katika mitandao ya kijamii.

Vijana wanafaa kufahamu kuwa huu ni wakati wao wa kuamua jinsi serikali inavyosimamiwa na ni aibu kubwa wanapomlalamikia mwanasiasa mkongwe bila kujitolea wenyewe kupigania haki wanayotaka.

Katika enzi hii, kizazi cha sasa kina uwezo bora zaidi wa kutetea haki za wananchi wote. Lakini hilo halitatendeka kama vijana wataendelea kujificha nyuma ya skrini za simu zao na tarakilishi wakipiga kelele mitandaoni bila kuchukua hatua yoyote mwafaka.

Vijana wengi wamekuwa wazembe. Hawataki kutoa jasho, na hili sio tu katika masuala ya kupigania uongozi bora bali pia kujiendeleza maisha yao wenyewe.

Tumekuwa kizazi cha kutafuta mtu wa kulaumu kila mara tunapokumbwa na changamoto yoyote maishani mwetu. Hatutaki kujikagua nafsi zetu wenyewe ili tutambue hila tulizo nazo na kujirekebisha.

Tofauti na ilivyokuwa zamani, tuna katiba ambayo imelinda haki zetu kwa njia inayotupatia mandhari bora ya kupigania haki za kijamii.

Vile vile, tumejaliwa teknolojia za kisasa ambazo tunaweza kutumia kujifahamisha mengi ya kutusaidia katika juhudi hizi na pia kueneza ujumbe huo kwa umati mkubwa zaidi kwa kasi.

Lakini tumeamua kwamba teknolojia ni ya burudani, na kwa wengine ni mfumo wa kufanya vitendo vya ulaghai kujipatia riziki huku wengine wakipata nafasi ya kumtusi Bw Odinga kupitia mitandao hiyo.

Kuna mataifa mengi ambako vijana wametumia mitandao ya kijamii kuleta mabadiliko wanapohisi kukandamizwa. Hata kama walisaidiwa na wanasiasa wakongwe, hawakukaa kitako wakilialia jinsi tufanyavyo.

Hakika, hata humu nchini kuna masuala kadhaa ambayo yametimizwa kufuatia kilio cha wananchi mitandaoni.

Hizi ni ushahidi tosha kwamba vijana wana uwezo wa kufanya serikali isikilize na itekeleze maoni yao kuhusu uendeshaji wa taifa.

Huu si uchochezi wa mapinduzi, bali ni uchochezi unaolenga kuhamasisha vijana wachukue nafasi yao katika masuala ya uongozi wa taifa. Wakome kutumia nguvu na maarifa zao isivyostahili huku wakisubiri ukombozi ambao hauonekani karibu upeoni mwa macho yetu.