Wetang’ula apinga mkutano wa Ford Kenya ulioitishwa na Eseli

Na Cecil Odongo

MZOZO wa uongozi ndani ya Chama cha Ford-Kenya unaendelea kutokota baada ya mrengo unaoongozwa na Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula kupinga kuandaliwa kwa Kongamano la Wajumbe mnamo Novemba 21.

Katibu Mkuu wa Ford Kenya Dkt Eseli Simiyu, ambaye ni hasimu wa kisiasa wa seneta huyo, alitoa notisi ya kuandaliwa kwa kongamano hilo ambalo linatarajiwa kurasimisha uongozi mpya ndani ya chama.

Hata hivyo, Bw Wetang’ula kupitia notisi iliyochapishwa kwenye gazeti moja nchini, aliwataka wanachama wa Ford Kenya wasusie mkutano huo, akisema Dkt Simiyu alifurushwa kama katibu mnamo Mei 31 na hana mamlaka ya kuitisha mkutano wowote wa chama.

“Dkt Simiyu hashikilii tena wadhifa wa katibu mkuu Ford Kenya na ni marufuku kwake kujishughulisha na masuala yoyote ya chama hiki. Pia mahakama ya Nairobi ilimzuia kuhusika au kuendesha suala lolote la chama hadi kesi iliyoko kortini isikizwe na iamuliwe,” ikasema notisi hiyo.

Aidha mrengo wa Bw Wetang’ula ulisisitiza kuwa kongamano hilo halikuidhinishwa na wanachama wa Ford Kenya au asasi zozote za uongozi wa chama jinsi alivyodai Dkt Simiyu kwenye notisi aliyotoa awali.

Ford Kenya imekuwa ikabiliwa na mzozo wa uongozi baada ya Dkt Simiyu na mbunge wa Kanduyi Wafula Wamunyinyi pamoja na wanachama wengine kutekeleza mapinduzi mnamo Mei 31 na kumwondoa Bw Wetang’ula kama kinara wa chama.

Mudavadi na Weta wapigania ubabe Magharibi

 BENSON AMADALA na DERICK LUVEGA

MIPANGO ya kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi na mwenzake wa Ford Kenya Moses Wetang’ula kukabili kampeni za Waziri wa Ugatuzi, Eugene Wamalwa na Gavana Wycliffe Oparanya wa Kakamega katika eneo la magharibi, zimeibua mvutano mpya.

Washirika wa Naibu Rais William Ruto sasa wametangaza kuwaunga mkono Bw Mudavadi na Wetangula katika makabiliano ya pande hizo mbili kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Wabunge wa ANC, Ford Kenya na Jubilee wamewashtumu Bw Wamalwa na Oparanya kwa kutumiwa na Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (COTU) kuwahujumu Bw Mudavadi na Wetangula, ambao wanachukuliwa kuwa wanasiasa waliobobea eneo hilo.

Bw Wamalwa na Oparanya katika muda wa majuma mawili yaliyopita, wamezuru kaunti za Bungoma, Busia na Vihiga na kufanya mikutano na wazee wa eneo hilo kutafuta mwelekeo wa kisiasa wakijaribu kuunga ajenda za maendeleo za Rais Uhuru Kenyatta.

Walisema lengo lao ni kutambua mahitaji ya kimaendeleo na kushinikiza ugawaji wa rasilmali kwa miradi ya kuimarisha maisha.

Mnamo Jumamosi, mkutano uliopangwa kuongozwa na viongozi hao wa ANC na Ford Kenya eneo la Malava, ulikatizwa na polisi kwa hofu ya kukiuka masharti ya kuzuia maambukizi ya corona.

Lakini wawili hao wameshtumu polisi kwa kutekeleza sheria kwa mapendeleo.

“Wakati waziri Wamalwa na Gavana Oparanya walikuwa wakikutana na wazee wakihutubia mikutano kwa dai la kusambaza chakula cha msaada kwa familia zilizoathiriwa na mafuriko na Covid-19, hawakuwa wanakiuka kanuni?” aliuliza Bw Mudavadi.

Mkutano wa Weta watibuliwa kwa vitoa machozi

BENSON AMADALA Na DERICK LUVEGA

POLISI Jumamosi walizima mkutano uliopangwa na kiongozi wa Ford Kenya Moses Wetang’ula nyumbani kwa mbunge wa Malava Malulu Injendi, kutoa mwelekeo wa kisiasa kwa jamii ya Waluhya kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Polisi wa kukabiliana na fujo waliweka vizuizi katika barabara ya Kakamega-Malava, na kukatiza magari yaliyokuwa yakielekea nyumbani kwa mbunge huyo.

Wakati wa makabiliano hayo, polisi walilazimika kurusha vitoa machozi ili kutawanya umati nyumbani kwa mbunge huyo.

Baadaye, Bw Wetang’ula na kundi la wabunge walikutana katika Kakamega Sports Club kwa mashauriano.

Viongozi hao walikuwa awali wamehudhuria mazishi ya mama Sofia Monyo wa mbunge wa Luanda, Bw Christopher Omulele kabla ya kuelekea Kakamega.

Kamanda wa polisi eneo la Magharibi, Bi Peris Kimani alisema mkutano huo haungefanyika kwa sababu ulikiuka kanuni za kuzuia kusambaa wa virusi vya corona.

Akizungumza katika mazishi hayo, Bw Wetang’ula alisema kuwa yeye pamoja na kiongozi wa ANC, Musalia Mudavadi wanashinikiza ajenda ya eneo lenye umoja.

“Kuna watu ambao wanafikiria kuwa ukiwa hauko upande wao, uko upande ule wanaopinga,” alisema Bw Wetangula katika kile kilichoonekana kuwa jibu kwa kambi ya Bw Odinga ambayo imewahusisha na Naibu Rais William Ruto.

Aliendelea, “Tutakuunga vipi mkono wakati tuna mmoja wetu. Tunaeleza Waluhya wote kujua kuwa siasa ni za nyumbani.”

“Inapofikia kwa umoja wa jamii yetu, lazima kusiwe na mipaka kati ya jamii ndogo zetu 18 na vyama tunavyoshiriki,”aliongeza.

Naye Bw Injendi alisema hatua hiyo haitamtisha kamwe.

“Tumefanya uamuzi na tunajua kila uamuzi una athari zake. Hatutarudi nyuma katika azma ya kuunga mgombeaji urais tunayetaka,” alisema.

Awali katika mazishi hayo, Mbunge wa Alego Usonga, Samuel Atandi, alijipata matatani kwa kuwashutumu baadhi ya viongozi wa jamii ya Waluhya waliomlaumu kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga kwa kugawanya jamii hiyo.

Bw Atandi aliyemwakilisha Bw Odinga katika mazishi ya mama Sofia Monyo, alilazimika kukatiza hotuba yake huku vijana waliokuwa na hasira wakimzomea.

Mazishi hayo yalifanyika chini ya ulinzi mkali wa polisi waliokuwa na mbwa wa kunusa silaha.

Masaibu ya mbunge huyo yaliendelea huku vijana hao wakijaribu kumshambulia kwenye lango alipokuwa akiondoka.

Alilazimika kurudi katika uwanja ambao mazishi yalifanyika hadi polisi wakamuokoa.

Bw Omulele alifika katika lango kuwatuliza waombolezaji waliomvamia Bw Atandi wakimlaunu kwa kudharau viongozi wa jamii ya Waluhya.

Kwenye hotuba yake Bw Atandi alilaumu viongozi wa Waluhya kwa kujadili muungano wa jamii yao wakati nchi inapigana na janga la corona.

“Hali ya baadaye ya nchi hii haitegemei mnachofanya kama jamii,” alisema Bw Atandi aliyepuuza wito wa umoja wa Waluhya na kukasirisha waombolezaji.

Polisi walikuwa na wakati mgumu kuthibiti umati na wakawaruhusu kuhudhuria mazishi hayo lakini wakazuia wanahabari.

Weta kuadhibu waliobadilisha uongozi chamani

BENSON MATHEKA na RICHARD MUNGUTI

CHAMA cha Ford Kenya kimebuni kamati itakayoamua hatua kitakachochukulia maafisa waliojaribu kufanya mapinduzi ya uongozi.

Kamati ya usimamizi wa chama hicho inayosimamiwa na Kiongozi wa Chama Moses Wetang’ula iliyokutana jana katika makao makuu jijini Nairobi iliamua kutumia mbinu za ndani kutatua mzozo wa uongozi chamani.

Mahakama kuu Jumatatu alasiri ilimzuia Msajili wa vyama vya kisiasa Anne Nderitu kumsajiili Wafula Wamunyinyi kuwa kinara wa Chama cha Ford-Kenya.

Jaji James Makau alipiga breki hatua ya Bw Wamunyinyi kunyakua uongozi wa Ford-Kenya akaamuru kesi kuhusu mzozo huo wa Ford-Kenya isikizwe Juni 29.

Alisitisha utekelezwaji wa Arifa ya Gazeti rasmi la Serikali ya Juni 8, 2020 iliyomtangaza Wamunyinyi kuwa kinara wa chama cha Ford-Kenya.

Ombi la kutotambuliwa kwa kundi la Wamunyinyi na Bi Nderitu liliwasilishwa na wakili Ben Millimo.

Ford Kenya sasa imeunda kamati ya kutatua mizozo inayosimamiwa na Naibu Kiongozi wa chama, Bw Richard Onyonka.

Katibu Mkuu Eseli Simiyu na Mbunge wa Kanduyi Wafula Wamunyinyi wanatarajiwa kuhojiwa na kamati nyingine ya nidhamu inayosimamiwa na Mbunge wa Mugirango Magharibi Vincent Kemosi.

Bw Simiyu analaumiwa kwa kumuondoa Bw Wetang’ula kama kiongozi wa chama. Kulingana na Seneta huyo wa Bungoma, Simiyu aliita mkutano haramu wa baraza kuu la kitaifa la chama kutekeleza mapinduzi.

Kamati simamizi ya chama ilipitisha kwamba Bazara Kuu la Kitaifa ya chama hicho itakutana hivi karibuni kuandaa mkutano wa wajumbe watakaochagua viongozi wapya.

Bw Onyonka aliyehudhuria mkutano wa jana alikariri uaminifu wake kwa chama na Bw Wetangula. Mbunge huyo aliahidi kutatua mzozo huo kwa kuzingatia katiba ya chama.

Chama hicho kilitangaza kitaandaa mkutano wa Kamati Kuu ya chama (NEC) hivi karibuni ili kuanzisha mipango ya kupanga uchaguzi wa viongozi wapya chamani.

Weta atishia wanaounga mkono kung’olewa kwake

NA SAMWEL OWINO

KUNDI la chama cha Ford Kenya linaloongwza na mbunge wa Kandunyi Wagula Wamunyinyi linalaumu seneta wa Bungoma Moses Wetangula kwa kutishia kamati ya chama hicho.

Bw Wamunyinyi pamoja na katibu wa chama hicho Eseli Simiyu alidai kwamba wanachama hao walikuwa wanalazimisha kukutia saini afidafiti ili kupinga saini zilizochukuliwa ili kumng’oa Bw Wetangula kama kiongozi wa chama wiki iliyopita.

Akiongea kwenye afisi ya msajili wa vyama Nairobi Ijumaa Bw Simiyu alisema kwamba madiwani wateuliwa ambao ni wanachama wa NEC walitishiwa kutolewa.

Wanachama wengine waliambiwa kwamba watatolewa kwenye kamati za kaunti kama hawatabadilisha msimamo wao kuhusu kutolewa kwa Bw Wetang’ula.

“Tutaripoti vitisho hivyo kwa polisi ili wanchama wetu walindwe,” alisema Bw Simiyu..

Lakini mbunge wa Kimini Chris Wamalwa, katibu mkuu aliyeteuliwa na Bw Wetangula, alikana madai hayo. “Si ukweli. Ni uongo mtupu,” Dkt Wamalwa aliambia Taifa Leo.

Mapinduzi ya siasa ya Mudavadi, Weta yanukia Magharibi

LUCY KILALO na WANDERI KAMAU

KIONGOZI wa chama cha ANC Musalia Mudavadi na Seneta wa Bungoma, Moses Wetang’ula sasa wamejitokeza kumuonya Raila Odinga dhidi ya kugawanya jamii ya Mulembe.

Viongozi hao ambao walihutubia wanahabari jana wakiwa nyumbani kwa Bw Wetangula walimtaja Bw Odinga kama mgeni ambaye baada ya kukaribishwa vyema, anamgeuka mwenyeji wake.

“Inasikitisha kuwa baadhi ya wale ambao tumeunga mkono wanafikiria kuwa sisi ni punda. Wanadhani wanaweza kututumia kufika wanakotaka na baada ya kufika, wanatutupa na kututusi. Tumeona hili hasa kwa upande wa uongozi wa ODM chini ya Raila Odinga. Kushinda yeyote mwingine, Odinga amenufaika na nia njema ya watu wa Magharibi,” taarifa iliyotiwa saini na viongozi 21, saba wakiomba udhuru, ilisema.

Iliongeza, “Tumemruhusu mara kadhaa kuwa mwaniaji wa urais, hata wakati ambapo tulijua kuwa tuna wagombea bora zaidi. Tulimchukua kama ndugu mpendwa tuliyemthamini. Lakini amefanya nini? Amejiendesha kama mgeni mjeuri, na ameenda kila sehemu ya nyumba, pamoja na maeneo ambayo ni mwiko kufika. Amehimiza watoto kuwa wajeuri kwa wakubwa wao. Ameshawishi kuwatusi wazazi wao.”

Wakati huo huo, walisema kuwa Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (COTU), Bw Francis Atwoli, Gavana wa Kakamega, Wycliffe Oparanya na Waziri Eugene Wamalwa, hawawezi kuongea kwa niaba ya Waluhya.

“Haijalishi umepanda na kufikia nafasi gani kwa sababu ya nia njema ya watu wetu, tunakutahadharisha usifikirie kuwa unaweza kuongea kwa niaba yetu bila idhini yetu,” walisema kupitia taarifa hiyo iliyosomwa na mbunge wa Kiminini, Dkt Chris Wamalwa.

Waliohudhuria mkutano wa jana ni pamoja na wabunge Ben Washiali, Justus Murunga, Didymus Baraza, Ferdinand Wanyonyi, Tindi Mwale miongoni mwa wengine.

Aidha, mapinduzi ya kisiasa yanawaandama, kiongozi wa chama cha ANC, Bw Mudavadi na mwenzake wa Ford-Kenya, Bw Moses Wetangula, kama vigogo wakuu wa siasa katika jamii ya Abaluhya. Wawili hao ndio wamekuwa wakionekana kuwa wawakilishi na wasemaji wakuu kisiasa wa jamii hiyo, huku sauti zao zikiamua mwelekeo ambao jamii hiyo huchukua.

Hata hivyo, hatua ya baadhi ya wanachama wa Baraza Kuu (NEC) la Ford-Kenya kumng’oa mamlakani Bw Wetang’ula, ambaye pia ndiye Seneta wa Bungoma kama kiongozi wa chama mnamo Jumatatu, imeanza mchakato ambao wadadisi wa siasa wametaja kuwa “mapinduzi” ya kisiasa ya wawili hao katika jamii ya Mulembe.

Kwenye kikao kilichoongozwa na Katibu Mkuu wa chama, Dkt Eseli Simiyu, baraza hilo lilimng’oa mamlakani Bw Wetang’ula na kumchagua mbunge Wafula Wamunyinyi (Kanduyi) kama kaimu kiongozi.

Kikao pia kiliidhinisha kutolewa kwa Bw Chris Mandu kama Katibu Mashirikishi.

Hata hivyo, Bw Wetang’ula “alimjibu” Dkt Simiyu kwa kumtoa kama Katibu Mkuu na nafasi yake kuchukuliwa na mbunge wa Kiminini, Dkt Chris Wamalwa.

Lakini muda mfupi baadaye, Bw Mudavadi alitoa taarifa kali, akimlaumu mojawapo ya viongozi wa muungano wa Nasa kwa kupanga njama za kusambaratisha vyama tanzu kwenye muungano huo.

Na ingawa hakumtaja moja kwa moja, taarifa ya Bw Mudavadi ilimlenga kinara wa ODM, Bw Raila Odinga, hali iliyokifanya chama hicho kutoa jibu kali kwa Bw Mudavadi, iliyomtaja kama mwanasiasa ambaye hutegemea kuungwa mkono.

“Bw Mudavadi ni kiongozi ambaye daima amekuwa akitegemea kufaidika kwa kuungwa mkono na miungano ya kisiasa inayobuniwa. Lazima afahamu kujijenga,” ikasema ODM, kupitia Katibu Mkuu Edwin Sifuna. Kutokana na majibizano hayo, wadasisi wa siasa wanataja mwelekeo huo kama ishara ya mikakati ya wanasiasa wakuu nchini “kung’ang’ania” uongozi wa jamii ya Abaluhya.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo jana, mchanganuzi wa siasa, Bw Javas Bigambo, anasema kuwa mwelekeo huo unaashiria mwanzo wa mapambano makali ya kisiasa kati ya Bw Mudavadi, Bw Wetang’ula na wimbi la viongozi wapya wanaohisi kuwa wakati wao kuchukua uongozi wa jamii hiyo umetimia.

Kulingana na Bw Bigambo, wimbi hilo linawakilishwa na karibu viongozi 40 waliokutana na Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi (COTU), Bw Francis Atwoli katika makazi yake, Kajiado, Jumamosi.

“Mapinduzi ya kisiasa dhidi ya Mabwana Mudavadi na Wetang’ula yanaongozwa kichinichini ya Bw Atwoli kwa kuwatumia viongozi wapya na wachanga, ili kuleta mwamko mpya wa kisiasa katika eneo la Magharibi,” asema, akiongeza kuwa imefikia wakati wabuni njia mwafaka za kisiasa kuhimili wimbi hilo.

Wetang’ula alaumu Atwoli kwa masaibu yake

Na IBRAHIM ORUKO

SENETA wa Bungoma Moses Wetang’ula, amemlaumu Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (COTU) Francis Atwoli kwa madai ya kuchochea kung’atuliwa kwake kama kinara wa chama cha Ford-Kenya.

Bw Wetang’ula, ambaye alijitokeza baada ya kuondolewa kwake na Baraza Kuu la chama (NEC), alisema mipango ya kumtimua ilifanyika katika mkutano wa viongozi wa eneo la Magharibi nyumbani kwa Bw Atwoli katika Kaunti ya Kajiado.

“Hauhitaji kuwa mwanasayansi kujua kuwa kilichofanyika leo kilipangwa Ijumaa eneo la Kajiado. Hauwezi kuchagulia jamii viongozi,” akasema Bw Wetang’ula.

Hata hivyo, Bw Atwoli alipuuzilia mbali madai hayo akimtaja seneta huyo wa Bungoma kuwa mtu asiye na maendeleo, na ambaye anapenda kulalamika.

“Mkutano ambao ulimuinua Bw Musalia Mudavadi kuwa uongozi wa jamii ya Waluhya 2016 ulianzia kwa nyumba hii yangu,” alisema Bw Atwoli akizungumzia msururu wa mikutano ambayo iliishia na kutawazwa kwa kiongozi wa chama cha ANC kama msemaji wa jamii hiyo mnamo Disemba 2016 katika uwanja wa Bukhungu.

“Nakumbuka Bw Wetang’ula alikataa kuhusika na mikutano na pia alikosa kufika mkutano wa Bukhungu. Alikuwa ananishtumu kwa kumtumia Bw Mudavadi kumhujumu,” alisema Bw Atwoli.

Vita hivi vya maneno vilichipuka baadhi ya wanachama wa kamati kuu ya Ford Kenya walipopiga kura kumuondoa Bw Wetang’ula na Katibu Mtendaji Bw Chris Mandu Mandu kwa madai ya ukiukaji mkubwa wa katiba, sheria na maadili.

Seneta huyo pia anashtumiwa kwa kuingilia taratibu za mchujo wa chama mnamo 2017 ambazo inadaiwa ziligharimu chama nafasi bungeni pamoja na kukosa kupatanisha pande zilizokuwa zikizozana.

Jana, Mbunge wa Kanduyi, Wafula Wamunyinyi alichaguliwa kuchukua nafasi ya Bw Wetang’ula kama kaimu, Bi Josephine Maundu akishikilia cheo cha kaimu katibu mtendaji.

Akipinga mabadiliko hayo, Bw Wetang’ula alionekana kuhisi kusalitiwa na wale aliowataja kuwa marafiki wake wa karibu na kutangaza pia kuwang’oa katika nafasi walizoshikilia.

Alisema nafasi ya Dkt Eseli Simiyu ambaye ni katibu mkuu wa chama, itashikiliwa na mbunge wa Kiminini, Chris Wamalwa, na ya Wamunyinyi kuchukuliwa na mbunge wa West Mugirango, Vincent Mogaka.

“Bw Wamunyinyi amekuwa akitembea kwa kivuli changu kwani mimi ndiye nilimteua kuwa mjumbe maalum wa Kenya nchini Somalia,” alieleza.

Baadhi ya waliohudhuria mkutano wa NEC ni pamoja na Dkt Simiyu, mbunge wa Kisumu Magharibi Olago Oluoch, Gavana wa Bungoma Wycliffe Wangamati na aliyekuwa mwenyekiti wa baraza la wazee wa jamii ya Waluhya Patrick Wangamati.

“Tulichukua uamuzi huu kwa kuwa tunataka kuwa sehemu ya mipangilio ya kisiasa katika ngazi ya kitaifa. Tunaunga utaratibu wa BBI na handisheki,” alisema Bw Wangamati akipuuza madai kuwa walipanga mapinduzi hayo katika mkutano wa Kajiado mnamo Ijumaa.

Pia alisisitiza kuwa kuondolewa kwa Bw Wetang’ula hakuna uhusiano wowote na dhana kuwa yuko karibu na Naibu Rais William Ruto.

Msipore fedha za corona – Weta

Na DENNIS LUBANGA

KIONGOZI wa Chama cha Ford Kenya Moses Wetang’ula, amesema kwamba fedha zilizotengwa kusaidia kupigana na janga la corona zinafaa kutumika kwa uwazi badala ya kuporwa na watu wachache wenye tamaa serikalini.

Seneta huyo wa Bungoma alisema serikali kuu na zile za kaunti zinafaa kutumia fedha hizo vizuri ili kusitokee hali kama siku za nyuma ambapo ufichuzi wa sakata mbalimbali za ufujaji wa fedha zilitokea baada ya majanga nchini.

“Matumizi mabaya ya fedha za kupigana na janga la corona ni kosa la kihalifu,” akaeleza Taifa Leo jana.

Alitoa wito kwa afisi ya Mkaguzi wa hesabu za serikali, kamati za uhasibu bungeni na kwenye magatuzi mbalimbali pamoja na vitengo vya serikali kufuatilia kwa makini jinsi fedha hizo zinavyotumika.

“Hapa nchini wizi wa pesa za umma hukithiri sana wakati wa majanga kama haya. Mtindo huu wa mambo unafaa ukomeshwe kwa sababu pesa hizo zinafaa kusaidia Wakenya,” akaongeza Bw Wetang’ula.

Aidha alisema kwamba ziara yake kwenye baadhi ya hospitali za kaunti ilimdhihirishia kwamba hakuna vifaa vya kutosha za kuwahudumia wagonjwa.

“Lazima fedha zilizotolewa na Benki ya Dunia kwa serikali kuu pia zigawiwe kaunti ili kuimarisha sekta yao ya kiafya. Hii kaunti ina hospitali chache sana ambazo zina vifaa vya kutosha na iwapo hali itazidi kuwa mbaya basi tutakuwa taabani,” akasema.

Kauli ya seneta Wetang’ula linajiri wakati ambapo serikali inaendelea kupokea fedha kutoka masharika mbalimbali ndani na nje ya nchi ili kuisadia kupigana na janga la corona

Vilevile Bw Wetang’ula aliirai Wizara ya Afya kuanza kuwapima Wakenya katika maeneo mbalimbali ili kuzuia virusi hivyo visienee zaidi.

Weta apinga mpango kununua mahindi nje

Na DENNIS LUBANGA

KIONGOZI wa chama cha Ford Kenya Moses Wetang’ula, amekashifu mpango wa serikali wa kununua mahindi kutoka nje ya nchi, akisema wakulima wana mazao ya kutosha kwenye maghala yao.

Seneta huyo wa Kaunti ya Bungoma badala yake aliitaka serikali itumie fedha hizo, kununua mahindi kutoka kwa wakulima akisema kwa sasa kuna mahindi ya kutosha nchini.

Wiki jana, serikali kupitia Wizara ya Kilimo iliidhinisha uagizaji wa magunia milioni nne ya mahindi kutoka nje, ikisema imechukua tahadhari ya mapema kuepushia taifa hili janga la njaa wakati huu virusi vya corona vinaendelea kutatiza nchi.

Hata hivyo, Bw Wetang’ula kwenye mahojiano ya kina na Taifa Leo, alisema kwamba serikali inafaa ifutilie mbali mpango huo na badala yake iwakwamue wakulima kwa kuyanunua mahindi yao.

“Ninafahamu kwamba wakulima wa mahindi katika kaunti za Trans Nzoia na Uasin Gishu pamoja na maeneo mengine nchini wana mahindi ya kutosha kutokana na mavuno ya msimu jana. Iwapo kuna pesa ya kuagiza mahindi kutoka nje, basi serikali inafaa ihakikishe kwamba inanunua mahindi kutoka kwa wakulima ili kuwaepushia hasara,” akasema.

Bw Wetang’ula pia alimtaka Waziri wa Kilimo Peter Munya kuhakikisha mahindi yote yanayohodhiwa na wakulima, yananunuliwa kabla ya mengine kuletwa kutoka nje ya nchi.

“Kununua mahindi ya wakulima kuwasaidia kupunguza mazao ili wajiandae na msimu wa upanzi unaokuja. Litakuwa jambo njema iwapo tutaagiza mahindi kutoka nje ya nchi baada ya kuyanunua magunia yote ya wakulima,” akaongeza.

Seneta huyo ambaye ni Naibu Mwenyekiti wa kamati ya seneti kuhusu kilimo, alishangaa kwa nini serikali iagize mahindi kutoka Mexico, Brazil ama Ukraine na kuinua kiuchumi wakulima wa mataifa hayo ilhali jasho la wakulima nchini lipotee na wazamie mahangaiko tele maishani.

“Nafaka na mahindi si vyakula pekee ambavyo serikali inafaa kununua kutoka kwa wakulima. Kuna mihogo, viazi vitamu na ndizi zinazoendelea kuoza mashamabani. Tunaomba serikali inunue mazao hayo na kuyasambaza katika maeneo ambayo yanakabiliwa na ukame ambako hakuna vyakula vya kutosha,” akasema.

Wiki jana waziri Munya alisema serikali itanunua magunia ya mahindi milioni mbili kutumika kama chakula na Wakenya huku mengine milioni mbili yakisagwa na kutumika kutengeneza lishe kwa mifugo.

“Ningependa kuwahakikishia Wakenya kwamba serikali imeweka mikakati ya kutosha kuhakikisha hakuna ukosefu wa chakula nchini. Serikali ya kitaifa na ile ya kaunti zinafanya kazi pamoja kuhakikisha inaimarisha sekta ya kilimo nchini,” akasema Bw Munya.

Wafisadi wahukumiwe kifo – Wetangula

Na WANDERI KAMAU

CHAMA cha Ford-Kenya kinataka watu wanaopatikana kushiriki ufisadi nchini kuhukumiwa kifo na mali yao kutwaliwa na serikali.

Kwenye mapendekezo kilichowasilisha kwa Jopo la Mpango wa Maridhiano (BBI) jijini Nairobi jana, chama kilisema kuwa hiyo ndiyo njia ya pekee, ambapo vita dhidi ya ufisadi vitazaa matunda.

Kiongozi wa chama hicho, Bw Moses Wetang’ula alisema kuwa ufisadi umegeuka kuwa mojawapo ya changamoto kuu zinazoikumba nchi kwa sasa.

“Wakenya wanateseka sana kutokana na madhara ya ufisadi. Ni wakati tuimarishe vita hivyo ili kuhakikisha kuwa wanaoadhibiwa wanakuwa mfano kwa wengine,” akasema Bw Wetang’ula, ambaye pia ni Seneta wa Kaunti ya Bungoma.

Alisema kuwa serikali imekosa kuifadhili Idara ya Mahakama ifaavyo, hali ambayo imeyumbisha vita dhidi ya janga hilo.

Alitoa mfano kuhusu kesi ya ufisadi katika Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), ambapo washukiwa wakuu nchini Uingereza walihukumiwa baada ya kupatikana na hatia, huku kesi za wale washukiwa nchini zikiwa bado zinaendelea.

Aliyekuwa Afisa Mkuu Mtendaji wa tume hiyo, Bw James Oswago na Bw Trevy Oyombra ndio walitajwa kuwa wahusika wakuu kwenye sakata hiyo iliyoibuika mnamo 2014.

Chama pia kiliunga mkono mfumo ambapo Rais na Naibu Rais wanachaguliwa moja kwa moja na wananchi.

Chini ya utaratibu huo, Rais atamteua Waziri Mkuu na manaibu wake wawili kutoka chama kilicho na idadi kubwa zaidi ya wabunge, ambapo baadaye wataidhinishwa na Bunge la Kitaifa.

Chama kilipendekeza utathmini wa kina wa baadhi ya tume za kikatiba, kikizitaja kuwa “mzigo mkubwa kwa mlipa ushuru.”

Baadhi ya tume kilichopendekeza zifutiliwe mbali ni Mamlaka Huru ya Kuchunguza Utendakazi wa Polisi (IPOA), Tume ya Kitaifa Kuhusu Usawa wa Kijinsia (NGEC) na Tume ya Kitaifa Kuhusu Huduma za Polisi (NPSC).

Na ili kulainisha utungaji wa sheria nchini, kinapendekeza Seneti kupandishwa hadhi, kama ilivyo katika baadhi ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola kama Uingereza.

“Seneti inapaswa kutekeleza majukumu muhimu kama upigaji msasa wa maafisa wakuu wa serikali kama vile mabalozi, mawaziri, wakuu wa idara kati ya wengine kama ilivyo katika nchi zinazozingatia mfumo wa kidemokrasia,” akasema Bw Wetang’ula.

Ili kuharakisha mshikamano wa kikanda, kilipendekeza kuharakishwa kwa taratibu za uunganishaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa kuondoa vikwazo vyote vya kisiasa na kiuchumi vilivyopo kwa sasa.

Pia kilipinga pendekezo la kubuniwa kwa majimbo, badala yake kilipendekeza miungano ya kiuchumi iliyopo kupewa nguvu na kutambuliwa kikatiba.

Wetang’ula alia ODM inavuruga umoja Magharibi

Na SHABAN MAKOKHA

KINARA wa Ford Kenya, Moses Wetang’ula amewalaumu wafuasi wa ODM kutoka Magharibi mwa nchi kwa madai ya kutatiza kuunganishwa kwa chama chake na kile cha ANC cha Musalia Mudavadi.

Seneta huyo wa Bungoma amedai wafuasi hao wa Kinara wa ODM, Raila Odinga wamekataa kuunga mkono jitihada za jamii ya Waluhya kuungana ndani ya chama kimoja.

Alisema matumaini yaliyosalia kuishawishi ya muungano ni majadiliano wanayoendelea nayo na Gavana wa Kakamega, Wycliffe Oparanya ili kumshawishi aungane nao na kutoa mwaniaji moja wa urais 2022.

“Tunaendelea kuandaa mazungumzo na Oparanya ili ajiunge nasi na kuwaleta pamoja watu wa Magharibi. Sisi watatu tukiungana, basi tutakuwa na nafasi nzuri ya kumteua moja wetu kupeperusha bendera ya urais 2022,” akasema Bw Wetang’ula.

Alieleza masikitiko kwamba jamii hiyo imekuwa ikiwaunga mkono wawaniaji wa urais kutoka jamii zingine ambao wanapotwaa mamlaka huisahau.

“Tumewasaidia watu wengi kupata mamlaka na baadhi wamekuja kutushukuru ilhali wengine wamekuwa wakitupiga teke na hata kutuondoa kwenye nyadhifa muhimu. Wakati umewadia ambapo sisi kama jamii lazima tuweke mbele maslahi yetu kabla ya kuwaunga mkono watu kutoka nje,” akasema.

Hata hivyo, kauli ya Bw Wetang’ula imeshutumiwa vikali na baadhi ya wakazi ambao wanasema tabia ya viongozi wa jamii hiyo kukubali kutumiwa kwa maslahi yao wenyewe ndio imewafanya wasalie imara nyuma ya Bw Odinga.

“Viongozi wetu hushawishiwa kwa pesa na kutumiwa kutenganisha jamii,” akasema mkazi wa eneobunge la Matungu, Bw Fadhil Eshikwekwe.

Wameingia ‘box’ ya Jubilee?

Na MWANDISHI WETU

KIONGOZI wa ANC Musalia Mudavadi na mwenzake wa Ford-Kenya Moses Wetangula wameonekana kumezwa na Serikali ya Rais Uhuru Kenyatta, kama Raila Odinga alivyomezwa.

Wiki iliyopita, wawili hao pamoja na Kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka, walishirikiana na Rais Uhuru Kenyatta na Bw Odinga kuzindua usajili wa watu kidijitali na pia wakahudhuria hotuba ya rais bungeni.

Uwezekano kuwa hata Bw Mudavadi ameamua kufanya kazi na serikali umezua mjadala kuhusu kumalizwa kabisa kwa upinzani nchini.

Bw Mudavadi amekuwa akionekana kuwa mtu pekee aliyeweza kupuuza ushawishi wa Serikali na ndiye amekuwa sauti mpya ya kukosoa serikali.

Hii ni baada ya Bw Odinga kubadili msimamo na akakoma kukosoa serikali, na badala yake kuiunga mkono katika kila suala, kinyume na awali ambapo alikuwa sauti ya mwananchi.

Bw Kalonzo naye alitangaza mwaka jana kuwa atakuwa ‘mtu wa mkono’ wa Rais Kenyatta huku Bw Wetangula akibakia kimya.

Lakini bw Mudavadi amekanusha kuwa amemezwa na Serikali: “Sijamezwa. Kilichopo ni kuheshimu ustaarabu wa Rais kutualika kila mmoja kibinafsi katika shughuli hizo mbili za kitaifa.”

Baada ya hotuba ya Rais Kenyatta kwa Bunge mnamo Alhamisi, Bw Mudavadi ndiye pekee aliyemkosoa kwa kukosa kuwaondoa mawaziri wanaochunguzwa kwa madai ya ufisadi.

Mabwana Odinga, Musyoka na Wetangula kwa upande wao walimpa Rais sifa kochokocho kwa hotuba yake, ambayo ilipuuza masuala muhimu zaidi kwa wananchi kama vile gharama ya juu ya maisha na njaa.

Kwa upande wake, Bw Wetangula yanayoshuhudiwa ni matukio ya kisiasa, lakini akasisitiza kuwa taifa haliwezi kutawaliwa kwa handisheki, mbali kinachohitajika ni sera zinazokubalika na wote.

Lakini kulingana na Mbunge wa Pokot Kusini, David Pkosing, kuhusika kwa wawili hao kwenye shughuli za kiserikali ni mbinu ya kisiasa.

“Hatua ya Kalonzo, Mudavadi na Wetangula kuanza kumkaribia Raila ni ishara wazi kuwa kinara wao anaondoka kwenye siasa. Kama fisi anavyofuata mtu akidhani mkono utaanguka aukule, hata hao wanafanya hivyo wakitarajia kunufaika Raila akiondoka,” akasema Bw Pkosing.

Alieleza kuwa mbinu nyingine ni kuwa wanasiasa hao wanataka kukaa karibu na Rais, kwa matumaini kuwa atawaunga mkono kuwania urais 2022.

Mchanganuzi wa siasa, Prof Macharia Munene anasema kuwa uhusiano wa majuzi kati ya Rais Kenyatta na vinara wa upinzani ni jambo ambalo limepangwa vizuri.

Naye Prof Peter Kagwanja anasema kuwa hatua hiyo ni matunda ya handisheki: “Ni dhihirisho kuwa mbinu ya Rais ya kuleta umoja nchini inafanikiwa. Rais amelipatia suala la umoja umuhimu mkubwa katika utawala wake.”

Kwa upande mwingine, hatua ya wakuu wa upinzani kukaribia Rais Kenyatta imezua upinzani kutoka kwa mrengo wa Naibu Rais William Ruto, ambao wanaiona kama yenye lengo la kumtenga zaidi tangu.

Dkt Ruto alikosa kushiriki uzinduzi wa usajili wa kidijitali kutokana na kile wadadisi wanasema ilikuwa kuonyesha kutoridhishwa kwake na uamuzi wa Rais Kenyatta kuwashirikisha vinara wa upinzani.

JAMVI: Je, Uhuru amenasa Mudavadi na Weta?

PETER MBURU na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta sasa anaoenekana kudhibiti viongozi wote wa upinzani baada ya kuonekana kufaulu kuwanasa viongozi wa vyama vya Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi na wa Ford Kenya Moses Wetangula.

Bw Mudavadi ndiye alikuwa amesailia kuwa sauti ya upinzani baada ya kiongozi wa ODM Raila Odinga na mwenzake wa Wiper Kalonzo Musyoka kuamua kuhiari kufanya kazi na serikali ya Jubilee kwa moyo wa muafaka wa maridhiano, almaarufu ‘Handshake’.

Bw Wetangula pia naye amekuwa akisisitiza kuwa yuko upande wa upinzani, japo miezi kadha iliyopita amekuwa akionyesha ulegevu katika kazi ya upinzani, badala yake aidha akiwa kimya ama kuonekana katika hafla pamoja na viongozi wa serikali ya Jubilee.

Seneta huyo wa Bungoma hajakuwa mkakamavu kuikosoa serikali huku uvumi ukienea mwishoni mwa mwaka jana kwamba anaegemea mrengo wa Naibu Rais William Ruto katika chama tawala, Jubilee.

Mnamo Jumanne, viongozi hao wawili walitumwa na serikali kuongoza uzinduzi wa mpango mpya wa usajili wa watu kijidilitali ‘Huduma Namba’ katika kaunti ya Kajiado, katika shughuli hiyo ambayo kwayo Wakenya wote watapewa nambari maalum, “Huduma Namba” watakayotumiwa kufikia huduma za serikali.

Na kwa mara ya kwanza tangu uchaguzi mkuu wa 2017, mnamo Alhamisi Bw Mudavadi alihudhuria kikao cha pamoja cha bunge kusikiza hotuba ya Rais Kenyatta kuhusu Hali ya Taifa ambapo aliungana na wenzake, Bw Odinga, Musyoka na Wetang’ula kuunga mkono masuala kadhaa ambayo Rais Kenyatta alizungumzia.

Hata hivyo, alitofautiana na serikali kuhusu tangazo la Rais kwamba atafuta kazi wale ambao watafikishwa mahakamani pekee wala sio wale ambao bado wanachunguzwa kwa tuhuma za ufisadi.

Itakumbukwa kwamba baada ya Bw Odinga na Bw Musyoka kuamua kushirikiana na serikali mwaka jana, Bw Mudavadi alishikilia kuwa atasalia kuwa sauti ya upinzani ili kukosoa serikali.

“Sitageuka kuwa mtu wa mkono wa Rais Kenyatta kama hao wenzangu. Kama mwasisi wa NASA nitakuwa na umuhimu mkubwa kwa kutoa msimamo mbadala na kuwa mtetezi wa wanyonge,” akawaambia wanahabari.

“Nikitangaza kuwa ninaunga serikali, nitadhibitiwa. Sitakuwa na nafasi ya kuzungumzia masuala kama kupanda kwa madeni ya serikali, masaibu ya wakulima wa mahindi na miwa na ufisadi,” Bw Mudavadi akasema huku akiongeza kuwa msimamo huo haumaanishi kuwa yeye sio mzalendo.

Na mapema mwaka huu kiongozi huyo wa ANC alijitangaza kuwa kiongozi rasmi wa upinzani na kutisha kuitisha maandamano kuishinikiza serikali iwaadhibu vikali maafisa wake waliotajwa katika sakata za ufisadi.

Bw Wetangula naye Alhamisi alisifu hotuba ya Rais, akihimiza asasi za kuchunguza ufisadi sasa kufanya kazi ya ziada ili watu fisadi wakamatwe na kufungwa.

“Hotuba ya Rais imekuwa ya kuunganisha, ya kuunganisha taifa, kubaini makosa ya mbeleni na ya kuahidi kuwa tunahitaji kufanya mengi zaidi ili kuponya taifa tunaposonga mbele,” Bw Wetangula akasema baada ya hotuba hiyo.

Kiongozi huyo aidha aliungama na Rais kuwa idara za kuchunguza kesi za ufisadi zinafaa kupewa nguvu zaidi.

Viongozi hao wawili ndio walikuwa wakionekana kuwa sura halisi ya ufisadi nchini, lakini kwa kuongoza shughuli ya serikali katika kaunti ya Kajiado wiki hii na matamshi yao baada ya hotuba ya Rais, wadadisi wanasema Rais Kenyatta sasa amefaulu kuwaweka “box” viongozi wote wa upinzani na hivyo serikali yake kukosa mkosoaji mkuu.

“Hali hii inaweza kupalilia utawala mbaya na hata kurudisha nyumba vita dhidi ya maovu serikalini kama vile ufisadi,” anaonya Bw Barasa Nyukuri, ambaye ni mtaalamu katika masuala ya uongozi.

Wakati wa hotuba hiyo ya Rais Alhamisi, aliyekuwa mwenyekiti wa Jubilee David Murathe na ambaye ni mwandani wa karibu wa Rais Kenyatta alimsifia Bw Mudavadi kuwa kiongozi pekee ambaye anaweza kufananishwa na Rais kwa kujitolea kukabiliana na ufisadi.

Bw Murathe alisema japo haoni kiongozi mwingine mwenye uwezo wa kupigana vita dhidi ya ufisadi, anafahamu kuwa Bw Mudavadi anaweza.

“Rais anataka kuacha taifa lililoungana na ni yeye tu mwenye uwezo wa kushinda vita dhidi ya ufisadi. Ana uwezo wa kuvishinda kwa kuwa huu ni muhula wake wa mwisho, hana kitu cha kupoteza na hahitaji kuiba,” akasema.

“Ni yeye tu, kama rafiki yangu huyu (Mudavadi, ambaye alikuwa kando yake) ambaye anaweza kumaliza ufisadi. Na tunatumai kuwa atakayechukua hatamu baada yake ataendeleza vita hivi,” Bw Murathe akasema.

Bw Mudavadi akizungumza hakumlaumu Rais Kenyatta kwa kukosa kumfuta yeyote kazi ama kwa kusema watakaofikishwa kortini ndio watahitajika kujiuzulu, ila shoka lake alilielekeza kwa washukiwa wenyewe.

“Amesema kwamba yeye hatafuta watu, atasubiri waingie kortini, lakini ikiwa wewe umekuwa mgeni wa DCI na umekuwa mgeni wa EACC wewe pia huoni unapeana aibu kwa serikali, na kwa Rais na ujiondoe. Usingoje upelekwe kortini ndio utoke,” akasema kiongozi huyo wa ANC.

Viongozi hao (Murathe na Mudavadi) baadaye walionekana wakicheka na kupiga gumzo nje ya makao ya bunge.

Macho sasa yanaangaziwa Bw Mudavadi ambaye ndiye amekuwa akijitaja kuwa sura ya upinzani na ambaye amekuwa akikosoa serikali tangu mwaka jana baada ya Bw Odinga na Bw Musyoka kunyakuliwa na Rais, kuona ikiwa atashikilia kauli yake kuwa yeye ni kiongozi wa upinzani asiyeweza kunyakuliwa na serikali.

Risasi mazishini ililenga kuniangamiza – Wetang’ula

Na WAANDISHI WETU

POLISI wanachunguza madai kwamba Seneta wa Bungoma, Bw Moses Wetang’ula ndiye aliyekuwa akilengwa na risasi zilizofyatuliwa katika mazishi aliyohudhuria Jumatatu.

Bw Wetang’ula alikuwa miongoni mwa viongozi katika mazishi ya dereva wa Mbunge wa Likuyani, Bw Enock Kibunguchy, katika Kaunti ya Trans Nzoia.

Kiongozi huyo wa Chama cha Ford-Kenya na kiongozi mwingine wa eneo hilo aliyejeruhiwa katika fujo hizo walidai risasi zilizofyatuliwa zililenga kumwangamiza.

“Niliona polisi ambaye alimpiga risasi diwani na alikuwa akinyoosha bunduki upande wetu. Ninaamini risasi hiyo ililenga kuniangamiza,” akadai Bw Wetang’ula.

Dereva wa Bw Kibunguchy alipigwa risasi akafariki wiki iliyopita katika mkahawa ulio soko la Soy, Kaunti ya Kakamega alipokuwa na mbunge huyo.

Wapelelezi jana walimwagiza mbunge huyo kuandikisha taarifa kuhusu madai yake kwamba mauaji ya dereva wake hayakutokana na uhalifu wa kawaida bali ilikuwa ni njama ya kisiasa kumwangamiza.

Walimtaka aeleze zaidi kile alichomaanisha alipodai kuwa wapinzani wake wa kisiasa ndio walihusika katika shambulio hilo.

Afisa wa Upelelezi wa Jinai katika kaunti hiyo, Bw John Onyango, alisema wanamtarajia Bw Kibunguchy aende katika makao makuu ya polisi hii leo kuandikisha taarifa.

Baadhi ya madiwani katika kaunti hiyo wakiongozwa na Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kaunti, Bw Joel Otwoma, walimlaumu Bw Kibunguchy kwa kuchochea waombolezaji kumfurusha Waziri wa Huduma za Kijamii, Bw Robert Kundu Mukhanu, punde alipowasili mazishini na kusababisha vurugu.

Mwana mpotevu atarudi nyumbani?

Na BENSON MATHEKA

Kiongozi wa chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka, Jumanne alikutana na kinara mwenza wa NASA, Moses Wetangula, katika juhudi za kumshawishi asihame muungano huo wa upinzani.

Wawili hao walikutana katika afisi za chama cha Wiper mtaani Karen jijini Nairobi siku tatu baada ya Bw Musyoka kuahidi kuwa atampatanisha kiongozi huyo wa chama cha Ford Kenya na kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga ili kuokoa NASA.

Bw Wetangula amekuwa akimshambulia Bw Odinga tangu chama cha ODM kilipompokonya wadhifa wa kiongozi wa wachache katika seneti siku chache baada ya waziri huyo mkuu wa zamani kujiapisha kuwa rais wa wananchi Januari 30.

Bw Wetangula, Bw Musyoka na kiongozi wa chama cha Amani National Congress Musalia Mudavadi, walisusia hafla ya kumuapisha Bw Odinga katika bustani ya Uhuru Park jijini Nairobi.

Tofauti za Bw Wetangula na Bw Odinga zilizidi kiongozi huyo wa ODM alipoacha vinara wenza wa NASA katika mazungumzo yake na Rais Kenyatta.

Alitangaza kuwa muungano wa NASA ulikufa na umebaki gofu akisisitiza kuwa, hatashirikiana kisiasa na Raila japo Bw Musyoka na Bw Mudavadi wanasisitiza muungano ungali imara.

“Ndoa yangu na Bw Raila imekufa. Ni mwanasaisa anayetumia watu na kuwatupa. Tunajua alikuwa Kanu, akaibomoa, tulikuwa naye Narc, akaivunja, tukaunda Cord akaibomoa pia na sasa amevunja NASA,” alisema alipohojiwa na runinga ya Citizen wiki moja lililopita.

Wanasiasa wa chama cha ODM wamekuwa wakimkashifu Bw Wetangula wakimtaka aondoe wabunge wa chama chake kutoka kamati za bunge iwapo amehama NASA.

Bw Kalonzo ambaye alikuwa ng’ambo uhasama kati ya Wetangula na Raila ulipozidi, aliahidi kuwapatanisha.

Jana, duru katika Wiper zilisema kwamba, Bw Musyoka aliahidi kuendelea kuwa gundi inayounganisha muungano huo na kwamba, hatalegeza juhudi za kuhakikisha vinara wenzake wanazungumza kwa ustawi na amani nchini.

Kwenye taarifa, chama hicho kilisema Bw Wetangula alipongeza Wiper kwa kufungua ofisi mpya mtaani Karen.

“Vyama vya Ford-Kenya na Wiper vina malengo sawa ya siku zijazo kuhusu nchi hii , tutaendelea kujitolea na kuungana,” taarifa ilisema ikinukuu Bw Wetangula alivyoandika katika kitabu cha wageni katika ofisi za Wiper.

Kwenye anwani yake ya Twitter, chama hicho kilipakia picha za Bw Wetangula akitabasamu huku akisalimiana na Bw Musyoka.

Wakenya wanasubiri kuona iwapo juhudi za Bw Musyoka kufufua NASA zitafaulu kwa sababu Bw Wetangula alinukuliwa akiapa kutoshirikiana tena na Bw Raila.

Chama cha Wiper kimetangaza kuwa kitashirikiana na chama cha Jubilee sawa na ODM cha Bw Raila, huku Bw Wetangula akijitangaza kiongozi rasmi wa upinzani. Duru zinasema Bw Musyoka anafanya juhudi za kukutanisha vinara wote wa NASA waweze kuzika tofauti zao.

Mudavadi na Weta watakiwa kujiunga na Jubilee

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE wa Jubilee kutoka magharibi mwa Kenya wamewataka vinara wa NASA Musalia Mudavadi na Moses Wetang’ula ‘kuondoka kwenye baridi’ na kujiunga na serikali.

Mbw Emmanuel Wangwe (Navakholo), Dan Wanyama (Webuye Magharibi) na Didmus Barasa (Kimilili) waliwataka wawili hao kuiga mfano wa wenzao Raila Odinga na Kalonzo Musyoka kwa kufanya kazi na Rais Uhuru Kenyatta.

“Kalonzo alihudhuria Maombi ya Kitaifa na kuwasalimiana na Naibu Rais William Ruto na Bw Odinga licha ya kuachwa nje katika mwafaka wa hapo awali. Sasa Musalia na Wetang’ula hawana budi kujiunga kufuata nyayo za wenzao na kujiunga na Jubilee,” akasema Bw Wangwe.

Naye Bw Wanyama alisema endapo wawili hao wanajiunga na serikali watajiweka katika nafasi nzuri kupata vyeo vya juu katika uchaguzi wa mwaka wa 2022.

“Ikiwa Mudavadi na Wetang’ula watajiunga na serikali watakuwa katika nafasi bora kujadiliana na Naibu Rais William na viongozi kutoka maeneo mengine katika siasa zijazo,” akasema.

Kwa upande wake Bw Barasa alisema njia ya kipekee ya Mudavadi na Wetang’ula kumpinga Raila chenga kisiasa ni kushirikiana na Rais Kenyatta na naibu wake Ruto katika mipango yao ya kuwahudumia Wakenya.

“Njama fiche za Raila zitaambulia patupu ikiwa viongozi hawa wawili watajiunga na serikali katika mchakato wake wa kuunganisha nchi kwa ajili ya maendeleo. Kupitia njia hiyo sisi kama Waluhya tutafaidi,” akasema Bw Barasa ambaye anahudumu muhula wake wa kwanza.

Wabunge hao watatu walikuwa wakiongea Jumamosi katika hafla ya mazishi katika eneo bunge la Navakholo.

Mbw Mudavadi na Wetang’ula hawakuhudhuria hafla ya maombi ya kitaifa katika mkahawa wa Safari Park, Nairobi. Hata hivyo, Bw Musyoka aliwataka Rais Kenyatta na Bw Odinga kuhusisha wawili hao katika mchakato wa kuunganisha taifa.

“Leo ni siku muhimu zaidi kwa sababu sisi kama viongozi tumeungana hapa kwa ajili ya kupalilia umoja na uthabiti wa taifa letu. Ingekuwa bora zaidi ikiwa wenzetu, Mudavadi na Weta pia watajumuishwa katika mchakato huu ili sote tutembee pamoja,” akasema kiongozi huyo wa chama cha Wiper.

Kalonzo, Mudavadi na Weta wapinga kubuniwa kwa jopo la kuzima ufisadi

Na VALENTINE OBARA

VINARA watatu wa Muungano wa NASA wamejitenga na msimamo wa mwenzao Raila Odinga, kuhusu vita dhidi ya ufisadi.

Kiongozi wa Chama cha Wiper Kalonzo Musyoka, mwenzake wa Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi na Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula (Ford Kenya), Jumatano walipinga pendekezo la kubuniwa kwa jopokazi maalumu la kupambana na ufisadi nchini.

Pendekezo hilo lilikuwa limetolewa mwishoni mwa wiki na Bw Odinga ambaye uhusiano wake wa kisiasa na watatu hao umeonekana kudorora tangu alipoamua kushirikiana na Rais Uhuru Kenyatta miezi miwili iliyopita.

Kwenye taarifa ya pamoja, watatu hao walisema asasi za kupambana na ufisadi zilizopo kwa sasa zinahitaji tu kutekeleza majukumu yao ipasavyo na kupewa uhuru wa kutosha ili zifanikiwe kuangamiza janga hilo sugu.

“Huu si wakati wa kuunda taasisi nyingine kwa minajili ya kupambana na ufisadi. Kuunda taasisi inayofanana na zile zilizopo na kuchukua hatua za kisiasa kutachangia tu kuficha wahusika wakuu, kutoa nafasi zaidi ya wahusika kupeana bakshishi na kuadhibu tu wahusika wadogo,” wakasema.

Hii ilikuwa ni mara ya kwanza kwa vinara hao kutoa taarifa ya pamoja kuhusu ufisadi nchini baada ya sakata mpya kufichuliwa katika shirika la Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS), wiki chache zilizopita.

Tofauti na jinsi ilivyokuwa wakati Bw Odinga alipokuwa akishirikiana pamoja na watatu hao, upande wa upinzani umeonekana kukosa makali ya kushinikiza serikali ibadilishe mienendo yake inapokosea.

Mbali na kumpinga kiongozi huyo wa Chama cha ODM, watatu hao pia walikosoa hatua zilizochukuliwa na serikali kufikia sasa kupambana na ufisadi. Kulingana nao, serikali haijadhihirisha kujitolea kukamata wahusika wakuu wanaopora mali ya umma licha ya kutoa ahadi za kufanya hivyo mara kwa mara.

“NASA itaamini serikali imejitolea tu ikiwa wale walio na ushawishi ndani na nje ya serikali watapelekwa mahakamani kwa msingi wa ushahidi wa kutosha ili wafungwe, na wala si sarakasi tunazoshuhudia ambapo washtakiwa ni mawakala tu,” wakasema.

Idara ya Upelelezi wa Jinai (DPP) ilipeleka washukiwa 24 wa ufisadi wa NYS mahakamani Jumanne ingawa wengi wao ni watu wa vyeo vya chini isipokuwa Katibu wa Wizara ya Utumishi wa Umma, Vijana na Jinsia Lilian Mbogo-Omollo na Mkurugenzi Mkuu wa NYS Richard Ndubai.

Wetang’ula atisha kutoboa siri zote za Raila Odinga

Na PATRICK LANG’AT

KIONGOZI wa Ford-Kenya Moses Wetang’ula ametisha kuanika hadharani siri za kiongozi wa ODM Raila Odinga iwapo ataendelea kuwachokoza.

Hii ni baada ya kinara huyo wa ODM kudai kuwa mpango wa kutaka kuunganisha vyama vya Ford Kenya na ANC chake Musalia Mudavadi ni wa kikabila.

Mnamo Jumapili Bw Odinga alipuuzilia mbali hatua ya Bw Mudavadi na Bw Wetang’ula kutaka kuunganisha vyama vyao kwa lengo la kuleta pamoja jamii ya Waluhya.

Bw Odinga alisema mpango huo unalenga kugawanya Wakenya kwa misingi ya kikabila.

Lakini, jana, Bw Wetang’ula alisema kuwa Bw Odinga anahofia kuwa muungano wa vyama vya ANC na Ford-Kenya utasambaratisha azma yake ya kutaka kuwa rais 2022.

“Tunamtaka Bw Odinga kukoma kutuchokoza. Asiturushie mawe ilhali anaishi kwenye nyumba ya vioo. Akiendelea kueneza madai ya uongo kutuhusu, tutafichua siri zake kwa kueleza ukweli kumhusu,” akasema Bw Wetang’ula.

Mabwana Odinga, Bw Mudavadi na Wetang’ula na Bw Kalonzo Musyoka wa Wiper walikuwa vinara wenza wa muungano wa National Super Alliance (Nasa) uliobuniwa Januari 2017 kwa ajili ya maandalizi ya uchaguzi wa Agosti 8, mwaka jana.

Lakini muungano huo ulisambaratika baada ya Bw Odinga kuafikiana kufanya kazi na Rais Uhuru Kenyatta mnamo Machi 9, mwaka huu.

Bw Wetang’ula pia alipokonywa wadhifa wake wa Kiongozi wa Wachache katika Seneti.

“Raila anapoungwa mkono na jamii ya Waluo si ukabila, lakini jamii nyingine zinapounga mkono viongozi wao anawaita wakabila. Huku ni kujikanganya.

Nilisema kuwa talaka yetu itakuwa yenye kelele na vurugu na sasa Raila ameanza kuhisi joto,” Bw Wetang’ula akaambia Taifa Leo afisini kwake jijini Nairobi.

“Raila amegundua kwamba amepoteza uungwaji mkono katika eneo la Magharibi. Wafuasi wamemkimbia. Naona akiwania urais tena 2022 lakini tutakutana kwa debe,” akaongezea.

Bw Wetang’ula alisema kuwa muungano wa vyama vya Ford-Kenya na ANC huenda ukajumuisha chama cha Wiper.

Vyama vya ANC na Ford Kenya tayari vimebuni jopo la watu 10 linaloongozwa na Dkt Boni Khalwale na Katibu Mkuu wa ANC Barrack Muluka kuandaa mikakati ya kubuni chama kipya.

Orengo aanza kazi huku Wetang’ula akilia

Na VALENTINE OBARA

SENETA wa Siaya, Bw James Orengo, Jumatano ameanza kuchapa kazi kwenye afisi ya kiongozi wa wachache katika seneti huku Seneta wa Bungoma, Bw Moses Wetang’ula, ambaye ni mtangulizi wake akizidi kulalamikia jinsi alivyong’olewa kutoka kwa wadhifa huo.

Bw Orengo alichaguliwa na maseneta wa upinzani katika wadhifa huo baada ya madai kuwa Bw Wetang’ula hakuwa akiwahudumia ipasavyo.

Mwandani huyo wa Kiongozi wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga, amekuwa akikutana na mabalozi mbalimbali afisini mwake.

Mnamo Jumanne, alikutana na Balozi wa Uingereza, Bw Nic Hailey, na jana akakutana na Naibu Balozi wa Australia, Bw Jonathan Ball.

“Tulijadiliana kuhusu hatua za kiuchumi na kisiasa, na umuhimu wa kudumisha uwiano,” akasema Bw Orengo.

Kwa kawaida mabalozi hukutana na viongozi mbalimbali wa bunge la taifa na wale wa seneti kwani asasi hizo mbili ndizo hutegemewa kupitisha sera na sheria ambazo hutoa mwongozo kuhusu jinsi taifa linavyoendeshwa.

Kufuatia ushirikiano wa Rais Uhuru Kenyatta na Bw Odinga, mabunge hayo yatategemewa zaidi kupitisha sheria ambazo zitawezesha utekelezaji wa makubaliano yatakayofanywa na viongozi hao wawili kuhusu masuala tofauti yanayogusia uongozi na utendaji wa haki kwa wananchi.

 

Amponda Raila

Ingawa Bw Wetang’ula alisema hana haja tena na wadhifa huo wa kiongozi wa wachache, Jumatano alizidi kumshambulia Bw Odinga kwa madai kuwa ndiye alichochea maseneta kumtimua.

Alimtaka kinara huyo mwenzake wa NASA aondoke katika muungano ili ubaki chini yake na vinara wengine ambao ni Kiongozi wa Wiper, Bw Kalonzo Musyoka, na Bw Musalia Mudavadi anayeongoza Chama cha Amani National Congress (ANC).

“Ulifanya uamuzi wako ukasonga mbele na vuguvugu la NRM, kwani inafahamika huwa unabadilisha vyama katika kila uchaguzi,” akasema, kwenye mtandao wa Twitter.

Taarifa ya kwanza iliyotolewa na Bw Orengo kwa niaba ya maseneta wenzake ilitoa wito wa umoja na ushirikiano kutoka kwa seneta huyo wa Bungoma.

“Huu ni wakati wa siasa za maendeleo na ni lazima tuwe katika safari hii kwa pamoja kama taifa moja la Kenya,” akasema Bw Orengo.

Alitoa wito kwa viongozi waeke ubinafsi kando ili kupigania malengo ya kuleta haki uchaguzini, kulinda ugatuzi, mamlaka ya mahakama na sheria, kuleta usawa kitaifa, kupambana na ufisadi, kudumisha haki za binadamu na uongozi bora.

Masaibu ya Weta ni mwiba wa kujidunga – Raila

Na VALENTINE OBARA

KIONGOZI wa Chama cha Ford Kenya, Bw Moses Wetang’ula, ametakiwa akome kumlaumu mwenzake wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga, kwa masaibu ya kisiasa anayopitia.

Maseneta wa Muungano wa NASA na Bw Dennis Onyango, ambaye ni msemaji wa Bw Odinga, Jumanne walipuuzilia mbali madai ya Seneta huyo wa Bungoma kwamba Bw Odinga ndiye alipanga njama na maseneta hao kumpokonya mamlaka ya kiongozi wa wachache katika seneti.

Kulingana na Bw Onyango, uamuzi wa kumg’oa Bw Wetang’ula ulifanywa na maseneta ambao hawakupendezwa na mitindo yake ya uongozi kwa hivyo anapaswa kujilaumu mwenyewe.

“Kufikia leo, hakuna seneta wa NASA ambaye amejitokeza kumtetea Bw Wetang’ula. Hatujawahi kushuhudia kiongozi akikataliwa jinsi hii kwa hivyo ni ishara inayoonyesha kulikuwa na tatizo kubwa kati yake na wenzake,” akasema kwenye taarifa kwa vyumba vya habari.

Seneta wa Siaya, Bw James Orengo wa ODM, alichaguliwa kuchukua nafasi ya Bw Wetang’ula.

Bw Wetang’ula amekuwa akidai kuwa kinara mwenzake, Bw Odinga, alifahamu kuhusu mipango ya kung’olewa kwake kwani anaamini wanachama wa ODM hawawezi kuchukua hatua kubwa kama hiyo bila kiongozi wao kujua.

 

Suala la kikabila 

Lakini Bw Orengo alisema inasikitisha jinsi suala hilo limegeuzwa kuwa la kikabila ilhali uamuzi ulifanywa kidemokrasia.

“Raila Amolo Odinga hafai kuhusishwa kwa suala hilo kwa kuwa hakuna seneta yeyote kutoka kwa vyama tanzu ambaye alipinga mabadiliko ya uongozi katika seneti,” akasema.

Bw Onyango alifichua kuwa wakati wa mkutano ulioitishwa na Bw Odinga kumpatanisha seneta huyo na wenzake, maseneta walimlaumu kwa “kutofahamu mambo, kuwa mbinafsi, mjeuri na mwenye uzoefu wa kuwalazimishia maamuzi kwa kudai yalikuwa maagizo ya wakuu wa NASA ilhali wakati mwingi huo ulikuwa ni uongo”.

Bw Wetang’ula jana alinukuliwa kusema Bw Odinga alikutana kisiri na maseneta wa ODM ambapo mpango wa kumng’atua ulifanywa.

 

Viongozi wa kidini: Weta na Mudavadi wakomeshe siasa za ukabila

Na JUSTUS OCHIENG’

VIONGOZI wa dini eneo la Nyanza wamewalaumu vinara wawili wa Nasa- Musalia Mudavadi na Moses Wetenga’ula kwa kuendeleza siasa za ukabila kumlenga kiongozi muungano huo wa Nasa Raila Odinga katika eneo la magharibi.

Wahubiri hao wa baraza la viongozi wa kanisa waliwashutumu Mudavadi na Wetang’ula kwa kuendeleza kampeini za mgawanyiko na uchochezi dhidi ya Bw Odinga.

“Tunamtaka Bw Wetang’ula aendeleze kampeni zinazolenga kuwaunganisha wakenya. Hii ni kwasababu nchi hii inahitaji kuletwa pamoja baada ya siasa za migawanyiko na chuki kutokana na kampeni za mwaka uliopita,” kiongozi wa baraza hilo Askofu Washington Ongonyo-Ngede alisema.

Mnamo Jumamosi, Mabw Mudavadi na Wetang’ula waliambia jamii ya Walhuya wamkatae Bw Odinga na kumlaumu “kwa kuitumia jamii hiyo na kuitema.”

Shambulizi hili dhidi ya Bw Odinga linatokana na kung’atuliwa kwa Bw Wetang’ula kutoka wadhifa wake wa kiongozi wa walio wachache katika bunge la Seneti.

Wadhifa huo umetunukiwa Seneta wa Siasa James Orengo.

Lakini jana viongozi wa dini kutoka Nyanza wakiongozwa na Askofu Ngede walimtahadharisha dhidi ya madai kwamba ataimbua kampeini za kumpinga Bw Odinga.

Katika taarifa iliyotiwa saini na maaskofu saba Ogonyo-Ngede, Julius Otieno, Dkt Hesbon Omwandho Njera, Habakuk Abogno, Dkt William Abuka, Geoffrey Owiti na Rev Job Othatcher viongozi walimtakaka Bw Wetang’ula akome “mara moja kuendeleza kampeni za mgawanyiko na badala yake aanze mikakati ya kuwaunganisha wananchi kwa minajili ya maendeleo.”

Maaskofu hao waliwashauri wakenya wakumbatie uhusiano uliozinduliwa na Rais Uhuru Kenyatta na Bw Odinga kuimarisha nchi hii.

Wahubiri hao walisema Bw Odinga yuko huru kushauriana na Rais Kenyatta kutafuta namna ya kuleta uuwiano nchini.

“Seneta Wetang’ula anapasa kujua aliyekuwa waziri mkuu ni kiongozi wa kitaifa anayeongoza watu na wala sio wananchi wanaomwongoza,” alisema Askofu Ngede.

Sitaki kiti chenu, nitawapa dawa yenu, Weta aiambia ODM

Na WYCLIFF KIPSANG

Kwa ufupi:

  • Bw Wetang’ula asema hatahudhuria kongamano la maseneta la kujadili na kutatua masuala yanayotisha kusambaratisha NASA
  • Amshambulia kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga kwa kudharau eneo la Magharibi licha ya kumuunga mkono kwa miaka mingi
  • Nilidhani hali ingedumishwa lakini nilitusiwa na kudhalilishwa. Matamshi yaliyotolewa yalionekana kuwa yaliyopangwa kuniabisha -Wetang’ula
  • BwMudavadi asema kuna mipango ya vyama vyote vya kisiasa eneo la Magharibi kuungana kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.

MPASUKO katika muungano wa NASA ulipanuka wazi Jumapili baada ya Seneta wa Bungoma, Moses Wetangula kukata tamaa ya kupigania kiti cha Kiongozi wa Wachache katika Seneti na kutangaza kwamba hatapigania tena wadhifa huo.

Bw Wetangula alisema hatahudhuria kongamano lililopangwa la maseneta wa NASA la kujadili na kutatua masuala yanayotisha kusambaratisha muungano huo.

“Ni nini cha kujadili (katika kongamano hilo)? Sitahudhuria. Nikienda itakuwa kama kondoo kujipeleka katika mahakama ya fisi,” alisema Bw Wetangula.

“Hata nikipewa kiti hicho sitakichukua, wakae nacho; asante. Sasa mchezo uanze; tutawapa dawa yao polepole lakini hatari sana,” aliongeza kiongozi huyo wa chama cha Ford Kenya.

Alisisitiza kuwa hakuomba kiti hicho cha Kiongozi wa Wachache katika Seneti lakini akiwa mmoja wa vinara wa NASA, uamuzi wa kumpa wadhifa huo ulinuiwa kutia nguvu shughuli katika bunge hilo.

Bw Wetangula alimshambulia kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga kwa kudharau eneo la Magharibi licha ya kumuunga mkono kwa miaka mingi.

Wiki iliyopita, maseneta wa ODM walimng’oa Bw Wetangula katika wadhifa wa Kiongozi wa Wachache na kumteua Seneta wa Siaya James Orengo kuchukua wadhifa huo. Bw Wetangula alisema Ford Kenya iliungana na ODM kwenye uchaguzi wa 2013 sawa na 2017.

“Tuliweka mali na nguvu zetu kwa suala hili lakini kama jamii ya Mulembe hakuna la kutufaidi,” Bw Wetangula alisema alipohutubia wanahabari mjini Bungoma.

“Imesemekana ninapigwa vita. Ninataka kutangaza hapa na sasa kwamba nina amani katika moyo wangu,” alisema Bw Wetangula.  Alitaja mkutano wa vinara wa NASA na maseneta wa muungano huo Alhamisi kama duka la kelele.

“Nilidhani hali ingedumishwa lakini nilitusiwa na kudhalilishwa. Matamshi yaliyotolewa katika mkutano huo yalionekana kuwa yaliyopangwa kuniabisha,” alisema Bw Wetangula.

Alikuwa ameandamana na kiongozi wa chama cha ANC ambaye ni mmoja wa vinara wa NASA Musalia Mudavadi, Gavana wa Bungoma Wycliffe Wangamati na aliyekuwa seneta wa Kakamega, Bonnie Khalwale.

Wengine walikuwa wabunge Wafula Wamunyinyi (Kanduyi), Eseli Simiyu (Tongaren), Ayub Savula (Lugari).

Bw Mudavadi alikosoa mazungumzo kati ya Bw Odinga na Rais Uhuru Kenyatta wa kuwatenga vinara wenza wa NASA.

“Hatupingi mazungumzo lakini tunataka yahusishe watu wote. Hakuna aliye na haki ya kushiriki mazungumzo. Canaan yetu si harambee house, bado tunaendelea mbele, “ alisema Bw Mudavadi.

Hata hivyo, akiongea katika kanisa la CITAM, mjini Rongai Jumapili, Bw Odinga alisema mwafaka wake na Rais Kenyatta ni wa kuunganisha Wakenya.

Bw Mudavadi alisema kuna mipango ya vyama vyote vya kisiasa eneo la Magharibi kuungana kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.

“Maeneo mengine yamefanya hivyo. Sioni sababu yetu kukosa kuungana hapa. Sisi kama viongozi wa Magharibi tunamuunga Bw Wetangula,” alisema Bw Mudavadi.

Alisema walipoungana katika NASA lengo lao lilikuwa mageuzi, kuimarisha uhuru wa asasi za kikatiba na mageuzi ya polisi. “ Tunasikitika kusema kwamba ndoto ya NASA haijatimizwa, nchi yetu inakabiliwa na changamoto tele ikiwa ni pamoja na vijana kukosa ajira,” alisema.

 

Weta na Mudavadi waapa kusambaratisha ndoa ya Uhuru na Raila

Na DERRICK LUVEGA na JUSTUS OCHIENG’

Kwa ufupi:

  • Mudavadi asema Raila ni msaliti na kama jamii ya Waluhya inafaa kuepukana kabisa na chama chake kinachoshirikiana na Jubilee
  • Wetang’ula alimsuta kwa kumsaliti yeye pamoja na vinara wenzake Kalonzo Musyoka (Wiper) na Musalia Mudavadi akisema: “tumeungana ili kukufunza adabu”
  • Wetang’ula alisema ni makosa kwa chama cha ODM kuendelea kueneza propaganda kwamba vinara watatu walikwepa sherehe ya kuapishwa kwa Raila 
  • Ingawa Bw Odinga amekuwa akidhani kuwa washindani wake wake wako ndani ya Jubilee, atashangaa atakapogundua kuwa vinara wa NASA ambao amewasaliti ndio watammaliza kisiasa

VINARA wa NASA kutoka jamii ya Waluhya sasa wametangaza vita vikali vya kisiasa dhidi ya kiongozi wa ODM, Raila Odinga na kuwataka wafuasi wao kukataa chama hicho kuelekea uchaguzi wa 2022.

Wakihutubia mikutano ya hadhara katika vituo kadha vya kibiashara kaunti ya Vihiga, kiongozi wa Ford Kenya Moses Wetang’ula na mwenzake wa ANC Musalia Mudavadi, walisema Bw Odinga ameikosea heshima jamii ya Waluhya kwa kuisaliti na kuitelekeza.

Walitaja kuondolewa kwa Bw Wetang’ula kutoka wadhifa wa kiongozi wa wachache katika seneti na wao kutajwa kama waoga kama ishara tosha kuwa ODM imetelekeza jamii ya Waluhya.

“Mliona vile alituhepa na kwenda kuzungumza na Uhuru Kenyatta. Na juzi mliona alivyochochea kuondolewa afisini kwa ndugu yangu Weta kama kiongozi wa wachache katika seneti.

Huyo ni msaliti na sisi kama jamii ya Waluhya tuepukane kabisa na chama chake kinachoshirikiana na Jubilee,” Bw Mudavadi akawaambia wafuasi wake mjini Mbale bila kumtaja Bw Odinga kwa jina.

Aliandamana na wabunge, Alfred Agoi (Sabatia), Ernest Ogesi (Vihiga), aliyekuwa seneta wa Kakamega Dkt Bonny Khalwale, Katibu Mkuu wa ANC Barrack Muluka miongoni mwa wengine.

Nao viongozi wa ODM wakiongozwa na Katibu Mkuu Edwin Sifuna na mbunge wa Ugunja Opiyo Wandayi, waliwajibu kwa kupuuzilia mbali malalamishi yao.
“Watu wanafaa kuungana kwa masuala yenye umuhimu kwa wananchi kama vita dhidi ya umasikini unaowazonga watu wetu.

Sio masuala potovu kama kuwashambulia wanasiasa wengine,” akasema Bw Sifuna.

Naye Bw Wandayi akasema: “Hakuna aliyeisaliti jamii ya Waluhya. Hakuna mwanasiasa aliye na uwezo kama huo. Hili suala la mabadiliko ya uongozi katika seneti linashughulikiwa na maseneta wenyewe, haifa kutumiwa kumchafulia jina kinara wetu Bw Odinga”.

 

Kusambaratisha ndoa

Na akiongea mjini Chwele awali, Bw Wetang’ula alisema yeye na vinara wengine wa NASA watafanya juu chini kusambaratisha ushirikiano kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Bw Odinga ambaye ni kiongozi wa ODM.

Bw Wetang’ula alimsuta kwa kumsaliti yeye pamoja na vinara wenzake Kalonzo Musyoka (Wiper) na Musalia Mudavadi akisema: “tumeungana ili kukufunza adabu”.

Migawanyiko imekuwa ikitokota katika muungano wa NASA baada ya Bw Odinga kukutana na Rais Uhuru Kenyatta kwa mazungumzo Machi 9 bila kuwahusisha vinara wenzake.

Akiwahutubia walimu katika kituo cha kibiashara cha Chwele wakati wa kongamano la wajumbe wa chama cha ushirika cha Ngarisha, Bw Wetang’ula alisema uamuzi wa Bw Odinga kukutana na Rais bila kuwafahamisha na kuondolewa kwake kutoka wadhifa wa kiongozi wa wachache katika seneti ni usaliti “ambao hauwezi kuvumiliwa”.

 

Kulipiza kisasi

“Licha ya sisi kupambana kwa bidii na baadhi ya watu kupoteza maisha yao, mienendo ya mgombea wetu wa urais inashangaza na inaashiria usaliti wa kiwango cha juu,” akasema Bw Wetang’ula huku akiapa kulipiza kisasi.

Alisema ingawa yeye, Mudavadi na Kalonzo wamekuwa wakihimiza kuandaliwe mazungumzo ya kitaifa, utaratibu ufaao haukutumika kuanzisha mchakato huo.

Bw Wetang’ula alisema ni makosa kwa chama cha ODM kuendelea kueneza propaganda kwamba vinara watatu walikwepa sherehe ya kuapishwa kwa Raila mnamo Januari 30.

Alisema ni Raila mwenyewe aliyewashauri kutohudhuria halfa hiyo katika bustani ya Uhuru, Nairobi, ili waweze kumtetea endapo angekamatwa.

“Ni Raila aliyetushauri kukaa kando, kwa hivyo ni makosa kwa wanachama wa ODM kututaja kama waoga kwa kutohudhuria sherehe hiyo ambayo kwa kweli haikuwa na maana,” Bw Wetang’ula akasema.

 

Fisi

“Kama fisi anataka kuwala wanawe, kwanza huanza kuwashutumu kwamba wananuka harufu inayofanana na ya mbuzi,” akaeleza kwa mafumbo.

Kiongozi huyo wa Ford Kenya alisema yeye na wenzake hawatakubali kutolewa kafara na Raila, akisema wamejipanga kukabiliana naye na Rais Kenyatta bila woga.

“Sasa hafai kujihushisha na masuala ya NASA. Aelekeze nguvu zake katika ushirikiano kati yake na Jubilee na sasa tuko tayari kuendelea na ajenda za upinzani,” Bw Wetang’ula amasema.

Seneta huyo alisema ingawa Bw Odinga amekuwa akidhani kuwa washindani wake wake wako ndani ya Jubilee, atashangaa atakapogundua kuwa vinara wa NASA ambao amewasaliti ndio watammaliza kisiasa.

“Kondoo amekuwa na wasiwasi kuhusu mbwa mwitu kwa miaka mingi lakini aliishia kuliwa na mchungaji,” Wetang’ula akasema.

 

Raila anamwadhibu Wetang’ula kwa kususia ‘kiapo’, asema mbunge

Na CHARLES WASONGA

MBUNGE mmoja wa Ford Kenya ameelekeza kidole cha lawama kwa kiongozi wa ODM Raila Odinga kufuatia kuondolewa kwa Moses Wetang’ula kama kiongozi wa wachache katika seneti.

Bw Vincent Kemusi Magaka (pichani juu) ambaye ni mbunge wa Mugirango Magharibi  Jumatano alidai Bw Odinga ndiye alitoa idhini kwa maseneta wa ODM, walio wengi, kuchukua hatua hiyo kama njia ya kulipisha kisasi kufuatia hatua ya Wetang’ula na wenzake wawili kufeli kuhudhuria sherehe ya “kuapishwa” kwake katika bustani ya Uhuru, Nairobi.

“Raila alikuwa akilipisha kisasi dhidi ya Wetang’ula kwa kutohudhuria ile halfla ya Uhuru Park. Hii ndio maana aliwashauri maseneta 20 wa ODM kupiga kura na kumwondoa kiongozi wa chama changu,” akasema  kwenye kikao na wanahabari katika majengo ya Bunge, Nairobi.

Bw Mogaka alisema kufuatia hatua hiyo, vinara watatu wa NASA, Musalia Mudavadi (ANC), Kalonzo Musyoka (Wiper) na Wetang’ula watakutana juma lijalo kupanga mkakati wa kufurusha ODM kutoka Muungano wa NASA.

“Hatuwezi kuendelea kushirikiana na watu ambao wanalenga kuporomosha muungano. Hatutawavumilia watu wenye kiburi na wanaolenga kuhujumu vinara wa NASA.

Ni heri kusalie na wabunge wachache katika upinzani lakini wawe ni wale ambao wataendelea kuikosoa serikali  iliyoko mamlakani,” akasema huku akitoa mfano wa Afrika  Kusini ambapo chama cha Julius Malema chenye wabunge 17 kilichochea kung’olewa mamlakani kwa Rais wa zamani Jacob Zuma.

NASA yapinga Wetang’ula kutimulilwa

Na CHARLES WASONGA

VINARA wawili NASA wamepinga kuondolewa kinara mwenza Moses Wetang’ula kama kiongozi wa wachache katika Seneti ukisema hatua hiyo ilikwenda kinyume na kinyume cha sheria.

Hata hivyo, kiranja wa wengi katika bunge la kitaifa Bw Benjamin Washiali alionekana kuunga mkono kuondolewa kwa Wetang’ula akisema “mtu yeyote ambaye ataonekana kutounga mkono huu mwafaka kati ya Rais Kenyatta na Raila Odinga atawekwa kando,”

Bw Washiali alikuwa akizungumzia suala hilo jijini Nairobi jana baada ya kuungana na Gavana wa Kakamega na wabunge wengine wa kutoka kaunti ya Kakamega kuunga mkono mwafaka huo.

Vigogo hao; Mabw Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi pamoja na Wetang’ula Ijumaa walisema hawatambui hatua hiyo iliyochukuliwa na chama cha ODM kupitia barua kwa Spika wa Seneti Kenneth Lusaka.

Chama hicho kinachoongozwa na kiongozi wa NASA Raila Odinga, kilisema wadhifa huo sasa utashikiliwa na Seneta wa Siaya James Orengo.

“Vinara watatu wamekutana leo (jana) asubuhi jijini Nairobi kufuatia yale yaliyotokea katika bunge la Seneti jana (Alhamisi). Wameelezea imani yao kwa Wetang’ula kama Kiongozi Rasmi wa Wachache,” ikisema taarifa hiyo iliyotiwa saini na Katibu Mkuu wa ANC Barrack Muluka.

Barua ya kumvua Bw Wetang’ula wadhifa wake iliwasilishwa kwa Spika Lusaka na kiranja wa wachache Mutula Kilonzo Junior ambapo alieleza kuwa uamuzi huo ulifikiwa kwenye mkutano wa ODM uliofanyika Machi 14 na kuungwa mkono na maseneta 16 wa chama hicho.

Bw Kilonzo Junior pia aliwasilisha kumbukumbu za mkutano huo ambao ulisemekana kuhudhuriwa na Bw Odinga katika makao makuu ya ODM, jumba la Orange, Nairobi.

Hata hivyo, Bw Wetang’ula ambaye ni seneta wa Bungoma aliapa kutobanduka akisema kuwa alipewa wadhifa huo na NASA wala sio ODM.

“Hii ndio itavunjika kwa fujo ikiwa ODM itapanga njama chafu kama hii. Ikiwa mnataka talaka basi sharti muwe tayari kwa sababu itakuwa na vurumai kubwa,” akasema katika ukumbi wa bunge la seneti.

Kiongozi huyo wa Ford Kenya alimlaumu Bw Orengo kwa kupanga njama ya kumwondoa.

Japo Spika Lusaka alisema hatua ya kumwondoa Wetang’ula ilikuwa halali alisema haitatekelezwa wakati huu hadi pale afisi yake itakapopokea barua ya kuidhinisha kutoka kwa muungano wa NASA.

“Seneti inatambua NASA wala sio ODM. Kwa hivyo, utekelezaji wa hatua hiyo itasimamishwa hadi pale Seneta aliyechaguliwa na NASA kwa njia ambayo inatambuliwa na kanuni nambari 20 (1).

Kumbukumbu za mkutano wa kuidhinisha uamuzi huo pia sharti iwasilishwe kwa afisi yangu na ile ya kiranja wa chache,” akasema Spika.

Ndoa ya NASA yaingia doa: ODM yampiga Wetang’ula mjeledi

Na LUCY KILALO na IBRAHIM ORUKO

CHAMA cha ODM kimemuondoa Seneta wa Moses Wetangula kama kiongozi wa Wachache katika Seneti, hatua ambayo huenda ikaashiria kuwa ndoa ya muungano wa NASA imesambaratika kabisa.

Chama hicho kilimwandikia barua Spika wa Seneti, Kenneth Lusaka kikieleza kuwa nafasi hiyo sasa itashikiliwa na Seneta wa Siaya, Bw James Orengo.

Spika baadaye alikubali ombi hilo na kusema lilifuata kanuni zote. Uamuzi huo ni kinyume na awali ambapo alikuwa ametoa pingamizi.

Hata hivyo, Seneta Wetang’ula ambaye ni kinara mwenza katika muungano huo na kiongozi wa chama cha Ford Kenya, aliapakutobanduka huku akionya ODM kuwa ndoa hiyo “itavunjika kwa fujo”.

“Ikiwa mnataka talaka, basi lazima muwe tayari kwa sababu itakuwa na vurumai na haitakuwa rahisi,” alisema.

Seneta huyo wa Bungoma alimshtumu mwenzake Bw Orengo kwa kupanga njama hiyo ya kumuondoa.

Kiranja wa Wachache, Seneta wa Makueni Mutula Kilonzo Junior, aliwasilisha barua hiyo kwa spika, ambapo alielezea kupokea kumbukumbu za mkutano wa chama cha ODM wa Machi 14, ambapo maseneta 16 waliidhinisha uamuzi huo.

Spika Lusaka alifafanua jana kwamba utaratibu kulingana na kanuni ambayo imeonyesha mkutano ulifanywa, kuna kumbukumbu na kuna maseneta waliotia saini, Seneta Wetangula ameondolewa kihalali kutoka kwa afisi hiyo.

Hata hivyo, alieleza kuwa Seneti inatambua muungano wa NASA na si chama cha ODM, kwa kuwa awali ilijitambulisha hivyo, matakwa ya kanuni ya bunge hayajatimizwa, na hatua hiyo itasimamishwa hadi “seneta aliyechaguliwa na Muungano wa NASA kwa njia ambayo imeelezwa na Kanuni 20(1) ya Bunge na mawasiliano kuhusiana nao, pamoja na kumbukumbu kuonyesha ushahidi kwamba uamuzi umefanywa kwa kuandika barua kwa afisi yangu na Kiranja wa Wachache wa Seneti.”

Uhusiano baina ya ODM na vyama vya Ford Kenya, Wiper na ANC umeendelea kuzorota katika siku za hivi karibuni tangu Bw Raila Odinga alipojiapishwa Januari 30, na wenzake kukosekana kwa hafla hiyo.

Mbali na hivyo, Bw Odinga hata baada ya kupinga vikali ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta akisema kuwa amenyang’anywa ushindi wake, ameonekana tena kuchukua msimamo wa kibinafsi kwa kufanya mkutano na mpinzani wake, na wawili hao kuafikiana kufanya kazi pamoja, ili kuunganisha nchi.

Maelezo kamili ya mkataba wa wawili hao ungali kitendawili ambacho waliokuwa vinara wenza wameshindwa kukitegua huku Wakenya pia wakishindwa kubaini ikiwa kuna njama nyingine hasa ya kisiasa kando la kilichowekwa wazi.

 

 

Wetang’ula: Lengo letu ni kuwaunganisha Wakenya

Na CECIL ODONGO
VIONGOZI mbalimbali wameunga mkono juhudi za kuunganisha taifa hili haswa baada ya mkutano wa Ijumaa iliyopita kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa NASA Raila Odinga.
Akizungumza Jumatano kwenye misa ya kumuaga msomi marehemu Prof Oeri Tumbo katika kanisa la Consolata Shrine Mtaani Westlands, Kiongozi wa wachache kwenye Bunge la seneti Moses Wetang’ula alisema kwamba wanalenga kuunganisha taifa na kuleta maridhiano.
Kiongozi huyo aliyefikisha rambirambi za vinara wenzake alimsifu marehemu kama msomi aliyeshirikiana nao kupigania mfumo wa vyama vingi mapema miaka ya 90.
“Prof akishirikiana na wengine kama Marehemu Job Omino na Ooko ombaka walitufaa kwa mawaidha ya kuikomboa nchi kutoka kwa uongozi wa chama kimoja,” akasema Wetangu’la.
Kwa upande wake, Seneta wa Kisii Prof Sam Ongeri alisema kwamba amani ni kiungo muhimu nchi inapokua na kusifia mwelekeo ambao nchi imechukua tangu mkutano kati ya viongozi hao wakuu.
Akimwomboleza marehemu Prof.Ongeri alisema kwamba jamii ya Abagusii wamempoteza shujaa aliyetumia ujuzi alionao kuwasaidia bila kubagua .
“Alikuwa msomi,mwanafamilia na mchanganuzi wa maswala ibuka katika jamii na tunashukuru Mungu kwa maisha yake hapa duniani,” akaongeza Seneta huyo.
Misa hiyo pia ilihudhuriwa na Jaji Mkuu David Maraga na Wasomi kutoka Vyuo Vikuu mbalimbali nchini na nje na wanafamilia akiwemo Mbunge wa Kitutu Chache Kusini Richard Onyonka ambaye ni mpwa wa mwendazake.
Marehemu ambaye kwa wakati moja alikuwa Mkuu wa Kitengo cha Sayansi ya Bayolojia Chuo cha Chiromo bewa la Chuo Kikuu cha Nairobi alitambuliwa mno kutokana na kushiriki mijadala ya kuchanganua maswala yanayoathiri taifa kwenye Vyombo vya habari haswa runinga.
Atazikwa Ijumaa nyumbani kwake katika Kaunti ya Kisii, eneobunge la Kitutu Chache Kusini.

Atwoli anagawanya jamii ya Abaluhya, aonya Wetang’ula

Kinara wa muungano wa NASA na kiongozi wa chama cha Ford Kenya Bw Moses Wetang’ula. Picha/ Maktaba

Na LEONARD ONYANGO

KINARA mwenza wa muungano wa NASA Moses Wetang’ula ameitaka jamii ya watu wa Magharibi kupuuzilia mbali Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi (Cotu) Francis Atwoli huku akisema kuwa analenga kugawanya jamii ya Waluhya.

Bw Wetang’ula alimshambulia Bw Atwoli saa chache baada ya kiongozi huyo wa Cotu kutangaza Jumapili kwamba kiongozi wa chama cha Amani National Congress (ANC) ambaye pia ni kinara mwenza wa NASA Musalia Mudavadi ataendelea kuwa msemaji wa jamii ya Waluhya.

Bw Atwoli alisema kwamba amemsamehe Bw Mudavadi, kwa kuhepa hafla ya kumuapisha kiongozi wa muungano huo Raila Odinga mnamo Januari 30, 2018.

Bw Mudavadi, Bw Wetang’ula na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka walisusia hafla ya kuapishwa Bw Odinga kuwa ‘rais wa wananchi’.

Bw Atwoli aliyesema hayo baada ya mkutano wa faragha nyumbani kwa  Bw Mudavadi alisema: “Tumekubaliana kwamba Bw Mudavadi ataendelea kuwa msemaji wa jamii ya Waluhya bila kutatizwa na yeyote.”

Lakini matamshi hayo yalimkera Seneta wa Bungoma Wetang’ula huku akiyataja kuwa ‘sarakasi’.

“Sarakasi za Atwoli hazitasaidia kwa lolote kuunganisha jamii ya Waluhya na badala yake anatugawanya,” akasema Bw Wetang’ula kupitia Twitter.

“Mbona Bw Atwoli anaangazia Mudavadi kwani hakuna Waluhya waliochaguliwa katika maeneo Bungoma, Trans Nzoia naNairobi?” akauliza Bw Wetang’ula.