Afya na JamiiMakala

Taka za sokoni zageuzwa kuwa kuni, makaa, mbolea na sabuni

Na LABAAN SHABAAN August 12th, 2024 3 min read

MAELFU ya wanabiashara sokoni Korogocho jijini Nairobi wamekuwa wakitupa uchafu kiholela katika mto wa Nairobi kwa miaka mingi.

Utupaji taka huu mtoni umehusishwa na uchafuzi, visa vya juu vya magonjwa na uharibifu wa mazingira.

Lakini haya yanabadilika baada ya kundi la vijana kugeuza uchafu wa soko kuwa mbolea, kuni na bidhaa nyingine kama vile sabuni na mafuta.

Kundi hilo kwa jina Korogocho Food Waste Management champions linapata mkate wa kila siku kutoka kwa shughuli hii.

Mbolea

Taka zinachakatwa na kuwa mbolea nzuri ya kunawirisha mazao ya shambani.

Kiongozi wa kundi hili Stephen Maina anaambia Taifa Leo kuwa mbolea hiyo imetathmnimiwa katika maabara kubaini kama ina virutubisho muhimu ya udongo.

“Vipimo vya maabara vimebaini kuna madini ya kutosha ya nitrogen, phosphorus, potassium na virurubisho vingine muhimu vya udongo kwa ajili ya upanzi,” anasema Maina huku akieleza kuwa mchakato huu hutumia wadudu kuvunjavunja taka za mazao ya shambani.

Wadudu hawa huachilia kioevu kwa jina vermicast na mbolea ambavyo hutumika katika kilimo.

“Sisi hutumia kioevu cha wadudu (worm juice) na mbolea kukuza sukuma wiki na mboga nyingine kwa matumizi yetu wenyewe na kuuza ziada kwa wateja eneo la Korogocho,” alieleza.

Wakijihami na shauku ya uendelevu, na kujitolea kufuata sera za kilimo hai, wakulima hawa wachanga wamezamia mbinu za kisasa za kilimo bila udongo na vijisahamba (kitchen gardens) kukuza mboga.

“Tunasisitiza matumizi ya mbolea hai kutoka kwa takataka za shambani ili kuhakikisha mazao yetu ni mabichi na salama kwa mazingira,” akasema Maina.

Haja ya vyakula salama nchini imeongeza uhitaji wa vyakula vinavyozalishwa kwa njia ya kilimo asili.

Maina anaripoti kuwa wateja wanatamani vyakula hivi hadi hulipia mboga kabla ya kukomaa ili wawe kipaumbele zitakapovunwa.

Aaron Titus katika kijishamba kinachokuza mboga kwa njia ya kilimo hai. PICHA | LABAAN SHABAAN

Kuni salama kwa mazingira

Vijana hawa kadhalika hutengeneza makaa na kuni kutoka kwa majani ya migomba ya ndizi, matunda yaliyoharibika, maganda ya mchele, nyanya, parachichi na sukuma wiki.

Kulingana na Sophie Nyaga, kiongozi mwingine wa kundi, wao huunda kuni na makaa maarufu briquettes kutoka kwa mbegu za avokado na majani ya migomba mtawalia.

Lakini wanapitia changamoto kutosheleza uhitaji unaokua kila kukicha

“Tunaziunda kwa mikono bila mitambo. Tutahitaji mashini ili kuongeza uzalishaji,” Sophie anakiri.

Kwa sasa wao husambaza kuni na makaa kwa wanachama na wahudumu wa hoteli eneo la Korogocho.

Hatua yao ya kupunguza unyevu kwenye kuni imesaidia kuondoa moshi wakati zinatumika.

Lakini makaa yanayotengenezwa hayatoi moshi. Kwa hivyo wateja wanaweza kuyapendelea.

“Utumizi wa kuni na makaa haya umechangia kupunguza utegemezi wa kuni za kawaida kwa hivyo kudhibiti ukataji miti na uharibifu wa misitu,” alisema.

Kiongozi wa kundi la vijana Stephen Maina aonesha makaa na kuni wanazotengeneza kutoka kwa taka za sokoni. PICHA | LABAAN SHABAAN

Mafuta ya Parachichi

Kundi hili bunifu linaminya mafuta kutoka kwa parachichi.

Aghalabu mafuta haya hutumika kutunza nywele na ngozi.

“Kazi hii haidhibiti tu hasara ya uzalishaji chakula bali pia kuzalisha bidhaa muhimu kwa jamii,” alisema Maina.

Mafuta ya avokado yana vitamini A, D na E pamoja na mafuta salama kwa afya.

Ni muhimu katika utunzaji wa nywele, ngozi na hupunguza uwezekano wa mtu kuzeeka haraka.

Sabuni kutoka kwa viazi

Viazi vilivyoharibika visivyouzika sasa vinatumiwa kutengeneza sabuni na mabingwa hawa wachanga.

Taka hizi hukusanywa kutoka sokoni na nyumbani na baadaye kuchakatwa kuwa sabuni.

Kiongozi wa kitengo hiki Loreen Nangila anaeleza kuwa walipokea mafunzo ili kuhakikisha sabuni hizi ni salama kwa afya na mazingira.

Mafunzo kutoka kwa mashirika

Mnamo Februari 2022, Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) lilishirikiana na mashirika ya kijamii kama vile Practical Action kusaidia wanajamii.

Hii ni kulingana na ajenda ya FAO kuhusu chakula na mazingira mijini maarufu FAO Urban Food Agenda na Green Cities Initiative.

Vijana hawa vile vile wanaeleza kuwa wamepokea mafunzo na misaada kutoka kwa Kampuni ya Oxfarm.

“Tunauza sabuni kwa bei nafuu kwa wanachama wetu kudumisha usafi na kuinua viwango vya uchumi,” Nangila aliambia Taifa Leo.

“Mashirika haya yametubadilishia maisha na kutupa maarifa. Vijana wengi ambao awali walikaa bila kazi wanapata mkate wa kila siku,” alikariri Maina.

Serikali ya Kaunti ya Nairobi imefanya kazi na vijana hawa kupunguza viwango vya uchafu kwa hadi asilimia 50 tangu kundi lianzishwe Aprili 2020

Mwanabiashara wa Soko la Korogocho Hannah Wangari akibeba ‘nyanya taka’ ambayo hutumiwa kutengeneza kuni na makaa. PICHA | LABAAN SHABAAN

Wanachama na tuzo

Maina anaarifu kuwa shirika lao lina wanachama 100 lakini wanaomakinika zaidi katika miradi ni 48.

Kwa sasa kina Maina huchakata tani tatu za taka za chakula kila wiki, ambazo ni sawa na kilogramu 500 kwa siku.

Shughuli zao za kufana zimewawezesha kushinda tuzo mbalimbali.

“Tulituzwa kombe na Serikali ya Kaunti ya Nairobi 2022 tulipoibuka kuwa vijana wabunifu zaidi katika Maonyesho ya Kilimo ya Nairobi. Baada ya hapo, Oxfarm walitutambua pia mwaka huo,” Maina alisema kwa tabasamu.

Tuzo hii iliambatana na ziara iliyolipiwa kwenda Tanzania kwa wiki moja kushiriki Maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani.

“Tulipata nafasi ya kunadi bidhaa zetu na kuwinda washikadau wapya,” alidokeza. “Vile vile, tulikutana na mashirika mengi na wateja mbali na kuwa upenyu wa kutufungulia milango kibiashara.”