Habari za Kitaifa

Tangu niwe waziri ni nadra kwangu kulala ama kupumzika wikendi – Kindiki

Na LABAAN SHABAAN August 1st, 2024 1 min read

WAZIRI mteule wa Usalama wa Ndani Prof Kithure Kindiki amefunguka kuwa uzito wa kazi ya kudumisha usalama nchini haujawahi kumpa muda wa mapumziko.

“Tangu niwe waziri siku hizi imekuwa vigumu kulala na hata kupumzika wikendi,” alikiri alipojibu maswali ya wanajopo wa kamati ya uteuzi bungeni.

“Kwangu mchana na usiku ni sawa.”

Prof Kindiki amehudumu katika wadhifa wa Waziri wa Usalama kwa takriban miaka miwili kabla ya kupigwa kalamu mnamo July 11.

Aliteuliwa tena na Rais William Ruto katika wadhifa uo huo.

Seneta huyo wa awali wa Tharaka Nithi anakashifiwa kwa maafa ya watu 60 yanayodaiwa kutekelezwa na polisi waliokuwa wanadhibiti maandamano dhidi ya serikali.

Haya ni kwa mujibu wa Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu Kenya (KNCHR) ambayo iliripoti kuwa watu 66 wamepotea ndani ya majuma matano ya maandamano.

Takwimu hii ilitolewa na KNCHR mnamo Julai 25.

Mwezi mmoja uliopita, serikali ilikabiliwa na maandamano makubwa ya kihistoria yaliyochochewa na malilio ya vijana wa kizazi cha Gen Z kuhusu Mswada wa Fedha 24 uliosheheni ushuru mpya, pamoja na uongozi mbaya.

Maelfu ya vijana kutoka angalau kaunti 35 walifurika barabarani na mijini kupinga utawala wa serikali ya Kenya Kwanza.