Michezo

TONG-IL MOO-DO: Afisa aliyetia kibindoni medali ya fedha katika kitengo cha Sparring

May 29th, 2020 3 min read

Na ABDULRAHMAN SHERIFF

ALIKUWA miongoni mwa Wakenya waliotingisha wanamichezo wengine kutoka sehemu mbalimbali za dunia wakati wa mashindano ya Makala ya Pili ya 2019 Chungju Martial Arts Mastership Championship yaliyofanyika nchini Korea Kusini mwaka 2019.

Huyo si mwingine ila ni Rose Wacheke Muthui, afisa wa Polisi Tawala ambaye alikuwa miongoni mwa Wakenya walionyakuwa medali na kuifanya nchi yao kumaliza nafasi ya pili kwenye mashindano hayo ya dunia.

Ni jambo la kufurahisha kuona kuwa baadhi ya viongozi wa kaunti aliyotoka Rose, walitimiza wajibu wao wa kumtayarishia sherehe maalum mtu wao kwa kumfanyia mapokezi ya heshima aliporudi nyumbani kutoka mashindanoni.

Rose alisema kuwa mapokezi aliyopewa na watu wa sehemu anayotoka yalikuwa mazuri na ambayo yamempa moyo mkubwa wa kuendeleza kipaji chake ili ikiwa mashindano yatafanyika mwaka huu wa 2020 anatarajia kurudi na medali ya dhahabu moja ama mbili.

“Nimekuwa nikifanya mazoezi hata wakati janga la corona lilipoanza nikitambua mazoezi pia yanasaidia kumueka mtu katika hali ya afya mbali na kujitayarisha kwangu kwa ajili ya mashindano ya mwaka huu ikiwa yatafanyika,” akasema mwanaspoti huyo.

Viongozi na wakazi wa eneobunge la Kieni walimuonyesha Rose kuwa wametambua na kuheshimu ushindi wake katika mashindano hayo ya dunia kwa kumpokea kwa shangwe, hoihoi na vigelegele.

Rose Wacheke Muthui akishirikiana na wenzake kucheza ngoma walipofika kwao Kieni baada ya kutoka Korea Kusini aliposhinda medali ya fedha. Picha/ Abdulrahman Sheriff

Wakazi wa eneo hilo walijitokeza kwa wingi barabarani na njia zote ambazo mwanaspoti wao Rose alipitia akirudi nyumbani baada ya kuwakilisha nchi kwenye mashindano ya kimataifa huko Korea Kusini.

Katika mashindano ya makala ya Pili ya Dunia ya 2019 Cheongju Martial Arts Mastership Championship, Rose alikuwa miongoni mwa wana mchezo wa Tong-IL Moo-Do wa Kenya waliofanikiwa kupata medali akitia kibindoni medali ya fedha kwenye kitengo cha Sparring kwa wanawake wa uzani wa kilo +65.

Kamati maalum ya mapokezi ya mwanamichezo huyo yakiongozwa na Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga, Seneta Ephrahim Maina ilifanya mipango yote lakini siku ya kuwasili kwa Rose, hawakuwako kutokana na shughuli walizokuwa nazo kwenye Maonyesho ya Ukulima ya Nyeri.

Hata hivyo viongozi wa ngazi za juu wa kaunti hiyo ya Nyeri, walikawakilishwa kikamilifu na Mbunge wa sehemu hiyo ya Kieni, Kanini Kega.

“Ninawashukuru viongozi wa nyumbani kwa kuthamini matokeo mazuri niliyoyatekeleza huko mjini Chungju nchini Korea Kusini ambapo nilifanikiwa kuipatia nchi yangu medali ya fedha. Niliazimia kupata dhahabu, lakini ndio hali ya mchezo, nimetosheka na hiyo ya fedha,” akasema Rose.

Mbunge Kanini Kega ambaye amekuwa akijishirikisha na kuunga mkono vijana wanaoshiriki kwenye michezo mbalimbali aliahidi kuendelea kusaidia uimarishaji wa michezo katika eneo lake na akawaomba vijana na wakazi wa Kieni kujiunga na mchezo wa Tong-IL Moo-Do ambao mmoja wao sasa ni naibu bingwa wa dunia.

Rose ambaye ni Afisa Polisi Tawala anasema alifurahikiwa jinsi alivyopokewa kwa shangwe huko kwao.

Rose Wacheke Muthui akiwa ndani ya gari lenye sehemu ya juu ya wazi, akisalimiana na watu wa Kieni waliojitokeza kumpokea baada ya kushinda medali ya fedha kwenye mashindao ya dunia ya Tong-IL Moo-Do. Picha/ Abdulrahman Sheriff

Mwanamichezo huyo alifika huko kwao akisindikizwa na afisa wa cheo cha juu wa Polisi, Peter Mureithi ambaye naye pia alisema anaunga mkono kikosi cha Polisi Tawala kuchukulia umuhimu michezoni.

Katika hafla hiyo ya mapokezi ya kwao Rose, Shirikisho la Tong-IL Moo-Do la Kenya liliwakilishwa na Katibu Mkuu Master Hilary Wahanda aliyetoa ombi kwa viongozi wa kaunti nyingine waige mfano wa kaunti hiyo ya Nyeri kwa kuwathamini wanamichezo wao na kuwasherehekea wakirudi na ushindi.

“Leo nimefurahikia kuona wakazi wa eneo analotoka Rose wanampokea kwa shangwe na vifijo na hii inastahili kufanyika kote nchini kwa wanamichezo waliofanya vizuri wanaporudi na ushindi kwenye mashindano ya kimataifa. Kufanya hivi, kunawapa motisha na wengine kuchukua michezo kuwa ya muhimu,” akasema Wahanda.

Mbali na Mbunge Kega, viongozi wengine waliokuwako kwenye mapokezi hayo ni Joseph Nderitu, Lillian Wanjiku Gathua, machifu, viongozi wa makanisa na wakazi wa eneo la Kieni waliofika kwa wingi.

Waziri wa Michezo na Utamaduni, Balozi Amina Mohammed alituma risala za kuwapongeza viongozi wa Kieni kwa kuunga mkono juhudi za serikali za kuinua hali ya michezo yote nchini.

Kenya ilimaliza nafasi ya pili kwenye mashindano hayo ya dunia kwa kupata medali mbili za dhahabu (Gordon Ochieng na Lorna Abiero), mbili za fedha (Rose Wacheke na Form Team) na tano za shaba (Elvis Malipe, Evans Oduor, Patricia Lucky, James Njuguna na Salma Ali).