Makala

TUONGEE KIUME: Usitumie maisha ya zamani ya mwanamke kumhukumu

Na BENSON MATHEKA July 18th, 2024 2 min read

UNATAKA kuoa au kuolewa na malaika? Mtu mkamilifu anayetimiza yote unayotaka? Samahani, hautampata. Kila unayedhani ni mkamilifu, ana udhaifu wake na iwapo hauoni udhaifu wake, una kasoro au ana kasoro.

Hakuna mtu aliye mkamilifu katika ulimwengu, hakuna. Inahitaji juhudi kufanya mtu kuwa malaika unayetaka. Kwa ufupi, ni lazima uwajibike kujenga uhusiano imara wa mapenzi. Mungu hatateremsha malaika kutoka mbinguni kuwa mume au mkeo. Tumia udhaifu wa mtu wako kumfanya awe utakavyo awe na hautajuta kwa kuwa utakuwa umemuunda wewe binafsi kuwa wako.

Tazama, uhusiano wa kimapenzi unaodumu, hata ndoa, ni wa wale wanaokuzana kwa kutumia udhaifu wa kila mmoja.

Kila mtu ana historia yake ya mambo mabaya na mazito ambayo hawezi kufunguka mara moja. Unapooa au ukitaka kuolewa, acha kutumia maisha ya zamani ya mtu kumhukumu. Kilicho muhimu zaidi ni maisha ya sasa na ya mbeleni na mtu wako. Ya zamani yalipita. Zingatia ya sasa na yajayo mnayojenga pamoja.

Kila uhusiano una changamoto zake. Ndoa sio kitanda cha waridi. Kila ndoa nzuri imepitia mtihani wake wa moto mkali. Upendo wa kweli unathibitishika wakati wa changamoto. Pigania penzi na ndoa yako.

Usiige uhusiano wa mtu mwingine. Kufanya hivi ni kukosa mwelekeo.

Kila ndoa ina viwango tofauti vya mafanikio. Usilinganishe ndoa yako na mtu mwingine yeyote.  Unayodhani ni tamu inaweza kuwa imejaa machungu na dhiki kuliko yako.

Ndoa mbili zinaweza kuonekana sawa, lakini kamwe haziwezi kuwa sawa. Kamwe usilinganishe kiwango cha upendo kutoka kwa ndoa nyingine na yako. Jifunze kuwa na subira. Na ukumbuke siri za ndoa hazianikwi kwa kila mtu.

Hii ni kwa kuwa, kuoa ni kutangaza vita. Naam, hata kabla ya ndoa, lazima uwe tayari kupigania mpenzi wako. Hakuna kizuri kinachojiri rahisi. Unapooa au kuolewa, lazima utangaze vita dhidi ya maadui wa ndoa. Baadhi ya maadui wa ndoa ni ujinga, kutokusamehe, uzembe, uchafu, ukaidi, uongo, tuhuma na hatari kabisa, kukubali maoni ya watu wa nje wakiwemo mashemeji na marafiki. Sio kwamba ushauri ni wa jamaa na marafiki ni mbaya, inategemea aina ya ushauri, nia yao na uamuzi unaofanya.

Mungu hawezi kukupa mtu kamili unayemtaka. Anakupa mtu huyo katika mfumo wa malighafi ili umtengeneze mtu unayetamani. Ndio umfinyange huku mkijengana kwa mawasiliano ya dhati,  maombi, upendo na subira.

Usisahau kwamba ndoa sio mkataba. Ni ya kudumu. Inahitaji kujitolea kabisa. Upendo ni gundi inayowaunganisha wanandoa.

Kila ndoa ina gharama ya kulipa. Ndoa ni kama akaunti ya benki. Ni pesa unazoweka ambazo unazitoa. Usipoweka upendo, amani na kutunza ndoa yako haitakuwa na furaha.