Akili MaliMakala

Uboreshaji kilimo, ufugaji kidijitali

Na SAMMY WAWERU September 20th, 2024 2 min read

UHABA wa mavetinari na maafisa wa kilimo wa umma ni mojawapo ya changamoto zinazozingira wakulima.

Tatizo hilo hasa linatokana na kustaafu kwa maafisa wa serikali, gapu wanazoacha zikikosa kujazwa.

Hatua hiyo inawaacha wakulima na wafugaji bila mbele wala nyuma.

Serikali inakiri uwepo wa uhaba wa maafisa wa umma, huduma za wataalamu wa kibinafsi zikiwa ghali.

Uhaba huo aidha unaathiri jitihada za uzalishaji chakula nchini, wakulima wakisalia kuwa watumwa wa kuendeleza kilimo bila ushauri.

Licha ya changamoto hizo, ukumbatiaji huduma za kidijitali unatajwa kuwa mbinu mwafaka kuziba gapu hiyo.

Jemimah Wanjiku, mwanzilishi wa DigiCow, apu ya kidijitali, akitoa mafunzo kwa mfugaji John Makumi wa ng’ombe wa maziwa. PICHA|SAMMY WAWERU

Hilo linaenda sambamba na sekta ya kilimo na ufugaji kukumbatia teknolojia za kisasa na bunifu.

Jemimah Wanjiku ni mmoja wa waanzilishi wa apu za kijiditali kutoa huduma za ufugaji, na anasema teknolojia hii itawafaa wakulima kwa kiasi kikubwa.

“Tuna apu inayojulikana kama DigiCow, ambayo madhumuni yake ni kuelimisha wafugaji,” Wanjiku anasema.

DigiCow inapatikana kwenye Google Playstore, na anachohitaji mkulima ni kuipakua (download) kwenye simu yake na kujisajili kuwa memba.

Jemimah Wanjiku akielezea jinsi apu ya DigiCow hutoa huduma kwa wafugaji. PICHA|SAMMY WAWERU

Hitaji kwa mtumizi, kando na kujiandikisha, ni kuwa na data.

Aidha, mtandao huo wa kidijitali hutoa kikamilifu huduma za ufugaji, kuanzia malezi ya ndama na matunzo, malisho, maji, matibabu hadi anapokomaa kuwa ng’ombe, kati ya mafunzo mengine.

Isitoshe, apu hiyo yenye wakulima 60, 000 ina jukwaa la kuunganisha wakulima na wataalamu wa mifugo, wakiwemo mavetinari walioidhinishwa na Bodi ya Huduma za Vetinari Kenya (KVB).

Mbali na kutumika kwenye simu, pia inatumika kwenye kompyuta au tarakilishi ya mpakato (laptop).

Kando na kutumika kwenye simu, apu ya DigiCow pia inatumika kwenye tarakilishi ya mpakato (laptop). PICHA|SAMMY WAWERU

Zipo apu zingine zinazotoa huduma za ukuzaji mimea, ambapo mkulima huelekezwa jinsi ya kuipanda, kutunza hadi wakati wa mavuno.

Ni mifumo ya kidijitali ambayo wakulima wakiikumbatia itatatua uhaba wa maafisa wa umma.

John Makumi, ni kati ya wakulima wanaotumia apu ya DigiCow na anasifia huduma za kidijitali zinazotolewa.

Makumi ni mfugaji wa ng’ombe wa maziwa Kiambu.

“Awali, nilikuwa mateka wa mavetinari bandia ila sasa ninapata mafunzo kwa njia ya kidijitali na ninapohitaji afisa ninamtoa kwenye apu,” anaelezea.

Mfugaji huyu, vilevile ameweza kupunguza gharama ya ufugaji.

John Makumi, mfugaji wa ng’ombe wa maziwa Kiambu. PICHA|SAMMY WAWERU