Makala

‘Ugonjwa wa wanawake’ uliofanya Lenolkulal aachiliwe kwa dhamana

Na RICHARD MUNGUTI September 1st, 2024 2 min read

ALIYEKUWA Gavana wa Samburu Moses Lenolkulal aliyefungwa Alhamisi kwa ufisadi aliachiliwa kwa dhamana Ijumaa Agosti 30,2024.

Hii ni baada ya ‘kufichulia’ mahakama kuu kuwa anaugua maradhi yanayohatarisha maisha  na ambayo huwapata kina mama wakiwa na ujauzito almaarufu kwa lugha ya kimatatibabu- pre-eclampsia.

Jaji Diana Kavedza alimwachilia Lenolkulal kwa dhamana ya Sh10,000,000 hadi Oktoba 31,2024 rufaa aliyokata itakaposikizwa.

Wakili Isaac Rene aliyewasilisha ombi la kuachiliwa kwa Lenolkulal kwa dhamana mbele ya Jaji Diana Kavedza alisema mfungwa huyo anaugua ugonjwa wa shinikizo la damu ,“na huenda kuzuiliwa gerezani hali yake ikadorora na hatimaye kupatwa na pre-eclampsia.”

“Gavana huyu wa zamani Samburu amekuwa akiugua mara kwa mara ugonjwa wa shinikizo la damu na kuna hatari kwamba akiendelea kuzuiliwa gerezani hali yake itadorora na kuhatarisha maisha yake. Madaktari wamesema huenda atapata pre-eclampsia,” Jaji Kavedza alielezwa na wakili Rene.

Kwa mujibu wa madaktari maradhi haya yanaweza kumfanya mtu kupatwa na hali ya kutetemeka kwa mwili, kuchanganyikiwa kimawazo na kiharusi na hatimaye kukata roho.

Lenolkulal aliachiliwa pamoja na mfanyabiashara Hesbon Ndathi.

Lenolkulal alitozwa faini ya Sh85,460,995 ama atumikie kifungo cha miaka minane gerezani.

Ndathi alitozwa faini ya Sh83,460,995 na hakimu mkuu wa mahakama ya kuamua kesi za ufisadi Thomas Nzioki.

Walikuwa wameshtakiwa pamoja na waliokuwa maafisa wakuu tisa katika kaunti ya Samburu kati ya 2013-2019.

Maafisa hao walitozwa faini ya Sh6.6milioni ama watumikie vifungo vya jumla ya miaka 36.

Kila mmoja wa maafisa hao walitozwa faini ya Sh700,000 isipokuwa mmoja Stephen Letinina aliyetozwa faini ya Sh1 milioni.

Lenolkulal na Ndathi walihukumiwa Alhamisi Agosti 29,2024 kwa kupokea kwa njia ya ufisadi Sh83,460,995.

Aliyekuwa Gavana Samburu Moses Kasaine Lenolkulal (kushoto) na Stephen Letinina waliofungwa jumla ya miaka 12 kwa ufisadi. PICHA | RICHARD MUNGUTI

Wawili hawa walikuwa hawajalipa faini hiyo ya jumla ya Sh168,821,990. Waliachiliwa kutoka gereza la Industrial Area Ijumaa alasiri baada ya kulipa dhamana hiyo ya Sh10m kila mmoja.

Hakimu mkuu mahakama ya kuamua kesi za ufisadi Thomas Nzioki aliamuru Lenolkulal, Ndathi na maafisa wa zamani wa kaunti hiyo wasichaguliwe katika wadhifa wowote wa umma  kwa muda wa miaka 10.

Wafungwa wenzao 9 walitozwa faini ya Sh6.6milioni ama kutumikia kifungo cha miaka minne kila mmoja.

Lenolkulal na Ndathi  waliachiliwa na Jaji Diana Kavedza wa Mahakama Kuu, Kibera, kwa dhamana ya  Sh10milioni  na mdhamini mmoja wa kiasi na hicho.

Jaji Kavedza aliamuru rufaa iliyowasilishwa na wakili Kennedy Kyalo na Isaac Rene itajwe October 31, 2024 kutengewa siku ya kusikizwa.

Lenolkulal na Ndathi walipinga uamuzi wa hakimu mkuu mahakama ya kuamua kesi za ufisadi Milimani Thomas Nzioki wakisema alipotoka kisheria alipofikia uamuzi kwamba walijinufaisha na pesa za umma Sh83,460,995.

Wawili hawa wanasema Nzioki alipotoka na kukosea alipofikia uamuzi kwamba waliilaghai kaunti hiyo pesa ilihali ilipokea mafuta na kulipa kampuni ya Oryx Service Station.

Lenolkulal alijitetea akisema hana hatia na kwamba alikuwa ameandikia kaunti hiyo barua Aprili 5, 2013 akifichua kwamba kampuni ya Oryx itakuwa inathibitiwa na Ndathi.

“Ndathi na Lenolkulal walikuwa na uhusiano wa karibu. Lenolkulal alijiondoa katika uendelezaji wa biashara ya kuuzia mafuta kaunti ya Samburu na kumpisha Ndathi. Ukweli ni kwamba alijificha nyuma ya Ndathi. Lenolkulal ndiye alikuwa akifanya biashara na kaunti aliyokuwa Gavana,” Nzioki alisema.

Katika rufaa yao wafungwa hao walisema hakimu alipotoka kufikia uamuzi  waliilaghai kaunti pesa.

Jaji Kavedza aliamuru kesi hiyo itajwe katika ya mahakama ya Milimani kwa maagizo zaidi.

Lenolkulal na Ndathi walikata rufaa kupinga adhabu watumikie kifungo kwa kujinufaisha na pesa za umma kati ya 2013 na 2019.

Kampuni ya Oryx iliyoandikishwa na Lenolkulal kabla ya kuchaguliwa kuwa Gavana ilishinda zabuni ya kuuzia kaunti ya Samburu mafuta ya petroli.