Habari

Uhuru, Ruto wagongana

March 1st, 2019 2 min read

Na VALENTINE OBARA na NICHOLAS KOMU

NAIBU RAIS William Ruto na bosi wake Rais Uhuru Kenyatta, Alhamisi walitofautiana kuhusu uwezo wa Idara ya Upelelezi wa Uhalifu (DCI) kufanikisha vita dhidi ya ufisadi.

Akiongea mbele ya Rais Kenyatta na Jaji Mkuu David Maraga jijini Nairobi, Dkt Ruto alionyesha DCI kama inayowapotosha Wakenya alipokanusha madai ya Mkurugenzi wa DCI, George Kinoti kuwa, Sh21 bilioni zimeporwa katika miradi ya ujenzi wa mabwawa ya Kimwarer na Arror, Kaunti ya Elgeyo Marakwet.

Mwandani wake Seneta Kipchumba Murkomen wa Elgeyo Marakwet, naye alieleza Bunge Alhamisi alasiri kuwa DCI inatumiwa kumpiga vita Dkt Ruto kuhusiana na siasa za 2022.

Saa chache baadaye akiwa ameandamana na kiongozi wa ODM, Raila Odinga katika Kaunti ya Murang’a, Rais Kenyatta alieleza kuwa na imani kamili kwa Bw Kinoti na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji kuongoza vita dhidi ya ufisadi.

“Tumesafisha DCI na DPP na tumeweka watu wanaoweza kuchapa kazi. Kinoti anafanya kazi yake, naye Haji anasubiri kushtaki washukiwa,” akasema Rais.

Dkt Ruto kwenye kauli yake Alhamisi alitilia shaka DCI kwenye hafla ambayo Rais Kenyatta naye alieleza wasiwasi wa uwezekano wa wananchi kuchukua hatua mikononi mwao kutokana na ufisadi uliokolea serikalini.

“Lazima tutambue kwamba Wakenya wanaona na kusikia yale yote yanayotendeka. Tusipochukua hatua, wananchi watachukua hatua mikononi mwao na sidhani Wakenya wanataka kufikia hatua hiyo,” akasema Rais Kenyatta.

Pesa

Ingawa hajatajwa kuhusika katika kashfa hizo za Kimwarer na Arror, Dkt Ruto alisema ni “Sh7 bilioni pekee” ambazo zilitumiwa, akisisitiza kuwa hakuna senti hata moja iliyopotea.

Kauli ya Dkt Ruto inathibitisha kuna mabilioni ambayo tayari yamelipwa, licha ya kuwa hakuna ujenzi wowote ambao umeanza katika miradi hiyo.

“Katika vita vya kuangamiza ufisadi, ni muhimu kuzingatia ukweli ndipo wahusika halisi wakamatwe. Wakati mwingine unasikia Sh9 bilioni zimefujwa, kisha kesi ifikapo mahakamani inabainika ni Sh100 milioni. Wananchi hubaki wakijiuliza zingine zimeenda wapi. Ni muhimu tuwe waaminifu kuhusu habari tunazotoa ndipo haki itendeke,” akasema.

Spika Justin Muturi pia alionekana kuchukizwa na mbinu za DCI na EACC kwenye vita dhidi ya ufisadi aliposema kuwa kuna asasi zinazojitahidi kupata nafasi kubwa katika vyombo vya habari.

“Msipiganie kugonga vichwa vya habari, hilo tuachieni sisi wanasiasa. Ukitaka kumkamata Muturi, njoo umkamate badala ya kuambia ulimwengu mzima kwamba unapanga kumkamata Muturi baada ya wiki moja au mbili. Hilo halitakusaidia. Wewe fanya tu kazi yako,” akasema Bw Muturi.

Akiongea Bungeni, Bw Murkomen alirukia DCI akidai inatumiwa kumpiga vita Dkt Ruto kuhusiana na siasa za 2022.

“Bw Spika, nahimiza DCI kabla ya kuanzisha uchunguzi wa aina hii, kwanza ishauriane na watalaamu wanaoelewa miradi kama hii. Inasikitisha kuwa miradi hii imegeuzwa kuwa silaha ya siasa za 2022,” akasema Bw Murkomen.

“Inasikitisha sana kuona azma ya kisiasa ya mtu mmoja ikishambuliwa kiasi hiki. Vita hivi dhidi ya mtu huyu mmoja vina madhara sio tu katika eneo moja la nchi, mbali uchumi wa taifa zima. Naomba tukome kutumia ofisi za umma na raslimali kupigana vita vya kisiasa. Siasa zichezwe na wanasiasa, nayo masuala mengine kama vile vita dhidi ya ufisadi viendelezwe bila nia fiche,” akaongeza Bw Murkomen.

Hii si mara ya kwanza Dkt Ruto kuonyesha kutoridhishwa kwake na jinsi vita dhidi ya ufisadi vinavyoendelezwa, huku wandani wake wakiongozwa na Bw Murkomen wakidai juhudi hizo ni njama za kuvuruga mipango yake ya kushinda urais ifikapo 2022.

Desemba 2018 Naibu Rais alionya kuwa vita dhidi ya ufisadi havitafanikiwa ikiwa asasi husika za kitaifa zitakubali kutumiwa kisiasa.

Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, Bw Noordin Haji mnamo Jumatano alikanusha madai kuwa Dkt Ruto ndiye anayelengwa kwenye vita dhidi ya ufisadi.

“Inahitajika tukome kuingiza ukabila katika vita dhidi ya ufisadi au kutaja watu binafsi, ambao wakati mwingi hawahusiki hata kidogo. Tujishughulishe na watu waliotajwa na wale walioshtakiwa. Tuache kubahatisha,” akasema Bw Haji.