Habari za Kitaifa

Ujio wa Starlink utasaidia Safaricom na wenzake kuboresha intaneti – – Mkuu Mpya Mteule wa CAK

Na KEVIN CHERUIYOT September 16th, 2024 1 min read

MKURUGENZI Mkuu mteule wa Mamlaka ya Ushindani Nchini (CAK) David Kemei amewahakikishia Wakenya kwamba atazima mjadala kuhusu kampuni ya kutoa huduma za intaneti ya Sterlink baada ya Bunge kuidhinisha uteuzi wake.

Bw Kemei ambaye anatarajiwa kupigwa msasa na Kamati ya Pamoja ya Bunge la Kitaifa na Seneti kuhusu Fedha Jumanne, Septemba 17, 2024 alisema atashirikisha sekta zote katika kuleta maridhiano kati ya Starlink na kampuni zingine zinazotoa huduma hiyo nchini.

Kwenye mahojiano na Taifa Dijitali, Bw Kemei alisema anaelewa malalamishi yaliyowasilishwa dhidi ya kampuni hiyo ya Amerika na kampuni za humu nchini haswa Safaricom

“Hauwezi kutoa idhini kiholela. Sharti uangalie masuala yote, ushirikishe kampuni zote husika kabla ya kutoa mwelekeo utakaowafaa wadau hao wote,” Bw Kemei akasema.

Hata hivyo, mkurugenzi huyo mteule alizitaka kampuni za humu nchini na wadau wengine katika sekta ya mawasiliano kukumbatia teknolojia bora ili kuimarisha huduma kwa Wakenya.

“Uzuri wa ujio wa Starlink ni kwamba utazilazimu kampuni za hudumu nchini kuwa wabunifu na kukumbatia mbinu za kisasa katika utoaji huduma. Tunataka kampuni za hapa nchini zitikiswe ili zitupe huduma bora, ndipo kusema ni kampuni inayotangaza faida ya mabilioni ya fedha ilhali maeneo mengine ya nchi hayajaunganishwa na intaneti,” Bw Kemei akasema.

Alisema kuwa atahakikisha kuwa wadau wote wameshirikishwa katika kupatikana kwa mwafaka kuhusu suala hilo kuhakikisha kuwa kila mtu anapata nafasi ya kuhudumu huku kampuni za humu nchini zikilindwa dhidi ya ushindani usiofaa.

Kulingana na Bw Kemei, baadhi ya kampuni za humu nchini zimewekeza mabilioni ya fedha katika miundomsingi, rasilimali ambazo haziwezi kuruhusiwa zifutiliwe na ujio wa kampuni mpya ya kutoa huduma za intaneti.

Alisema masuala kama vile usalama wa nchini na ulinzi wa data yanapaswa kuzingatiwa kabla ya kuidhinisha Starlink kutoa huduma za intaneti kwa Wakenya.