Habari za Kitaifa

Ukambani wajipanga kuungana, wanung’unika wametengwa serikalini

Na PIUS MAUNDU August 18th, 2024 2 min read

KIONGOZI wa Wiper Kalonzo Musyoka anasisitiza kuwa hatajiunga na serikali ya Rais William Ruto ambayo analaumu kwa utawala mbaya.

Akihutubia kongamano la uongozi wa wanawake lililoandaliwa na Baraza la Magavana katika Mji wa Machakos Ijumaa, Bw Musyoka alisema yuko tayari kubaki peke yake katika upinzani baada ya kiongozi wa ODM Raila Odinga kumchangamkia Rais Ruto.

“Iwapo mnadhani Gen Z wamezimwa, mnajidanganya. Nchi hii haitakuwa sawa tena katika masuala ya utawala. Hata nikibaki peke yangu nitasimama na watu wa Kenya na Gen Z,” Bw Musyoka alisema, akirejelea maandamano ya hivi majuzi dhidi ya serikali yaliyoongozwa na vijana.

Inasemekana Bw Musyoka anazungumza na wanasiasa sita katika eneo hilo ambao waliwania viti mbalimbali kwa tiketi ya United Democratic Alliance (UDA) katika Uchaguzi Mkuu wa 2022 au walijitambulisha waziwazi kuwa washirika wa Rais Ruto baada yake kuingia mamlakani.

Washirika wengi wa Rais Ruto katika Kaunti za Kitui, Machakos na Makueni wameamua kusubiri kufuatilia matukio ya kisiasa wakitaja hali ya suifahamu kufuatia kutikiswa kwa utawala wa Kenya Kwanza na maandamano ya vijana.

“Ukambani ni ngome ya Bw Musyoka. Ndiyo maana tumepanua mbawa katika maeneo mengine kote nchini. Katika siku zijazo, itakuwa nadra sana kutuona tukifanya kampeni Ukambani. Wale waliokuwa mrengo mwingine sasa wanarudi nyumbani,” Seneta wa Makueni Daniel Maanzo aliambia Taifa Leo Jumanne.

Mwanasiasa huyo alikuwa akirejelea mabadiliko ya wakosoaji wa Bw Musyoka katika eneo hilo.

Kamishna wa Tume ya Huduma za Bunge na aliyekuwa mwenyekiti wa UDA Johnson Muthama anaongoza kundi la washirika wa Rais Ruto katika kaunti za Ukambani ambao wameonyesha nia ya kushirikiana na Bw Musyoka ambaye kwa muda amekuwa hasimu wao kisiasa.

Bw Muthama anasema jamii ya Wakamba ina uwezo wa kutoa raisi kwa kuwa inajulikana kwa kutoa viongozi wengi bora.

Mwanasiasa huyo anasisitiza kuwa mkutano wa kuwaunganisha viongozi wa jamii hiyo aliotangaza Juni bado utafanyika – ulikuwa umepangwa kuwa Julai.

“Mkutano wa umoja wa Wakamba ulivurugika kutokana na maandamano yaliyotikisa nchi, kwa kuwa mimi niko upande wa serikali niliamua kuuchelewesha ili kuepusha dhana kuwa tunasherehekea wakati rais akikabiliana na matatizo na nchi ikikumbwa na umwagikaji wa damu. Mkutano bado utafanyika,” Bw Muthama alisema alipoungana na Bw Musyoka na aliyekuwa Seneta wa Kitui David Musila wakati wa mazishi ya Askofu Titus Kivunzi huko Winzyeei katika Kaunti ya Kitui wiki jana akisisitiza kuwa jamii ya Wakamba inahujumiwa.

“Kwa mfano, ukiangalia kile ambacho kimetokea hivi punde nchini Kenya, tumetengwa [katika uteuzi wa mawaziri] japo tunalipa ushuru kama Wakenya wengine wote,” alisema.

Bw Maanzo alithibitisha kuwa washirika wa Bw Musyoka wanazungumza na Bw Muthama kwa nia ya kuunganisha eneo hilo.

Ingawa Bw  Muthama anasisitiza kuwa mpango huo ni kuunganisha takriban kura milioni 2 za jamii hiyo kwa nia ya kuimarisha uwezo wake katika siasa za kitaifa, Bw Maanzo anasema nia kuu ni kuunga mkono azma ya urais ya Bw Musyoka 2027.

Ingawa Rais Ruto alirejelea ahadi zake za miradi ya barabara, maji na umeme mnamo Julai 12 alipokutana na wabunge wanane wa Ukambani, washirika wa Bw Musyoka wanaamini kwamba ana kile kinachohitajika kushindana na Rais Ruto.

Baadhi ya wachanganuzi wanahisi kwamba atajikwaa ikizingatiwa kuwa Rais Ruto anashirikiana na Bw Odinga.