Habari za Kitaifa

Ukiona cha mwenzako chanyolewa…Makatibu wa wizara nao waingia baridi

Na COLLINS OMULO July 13th, 2024 1 min read

KAULI aliyoitoa Rais William Ruto mnamo Alhamisi Julai 11 kuwa atatangaza mageuzi zaidi katika utawala wake katika siku zijazo sasa imewatia hofu baadhi ya maafisa wakuu serikalini, wengi wao wakiwa makatibu wa wizara mbalimbali.

Marekebisho hayo huenda yakaathiri watumishi mbalimbali wa umma na hata wakuu wa mashirika ya umma.

Haya yalifuata hatua isiyotarajiwa ya kuwafuta kazi mawaziri wake wote jambo ambalo sasa limewatia wasiwasi baadhi ya watumishi wa umma.

Hatua hiyo kali ilifuatia shinikizo la kudumu kutoka kwa vijana wa GenZ, ambao wanataka mabadiliko makubwa katika serikali.

Masuala yaliyoibuliwa na vijana waliokuwa wakiandamana ni pamoja na ufisadi, viongozi kutowajibika, na uzembe, viongozi kuishi maisha ya kifahari, ukosefu wa ajira na kupanda kwa gharama ya maisha, miongoni mwa masuala mengine.

Akihutubia taifa katika Ikulu, Rais alisema amechukua hatua hiyo kwani amesikia kilio cha Wakenya.

Ni Mkuu wa Mawaziri ambaye pia ni Waziri wa Masuala ya Kigeni Musalia Mudavadi, ambaye amebaki madarakani.

Baada ya kuwatimua, Rais Ruto alitangaza kuwa wabunge na maafisa wengine wa serikali watasimamia shughuli za serikali ili kuhakikisha kila jambo linaenda sawa hadi Baraza jipya la Mawaziri litakapoundwa.

“Wakati wa mchakato huu, shughuli za serikali zitaendelea bila kukatizwa chini ya mwongozo wa Makatibu wa wizara mbalimbali na maafisa wengine husika,” alisema Rais Ruto.

“Nitakuwa nikitangaza hatua za ziada kwa wakati unaofaa,” aliongeza.

Hata hivyo, Rais alidokeza kwamba mabadiliko zaidi yanaweza kufanyika hivi karibu, akisema ataendelea kushiriki katika mashauriano ya kina katika sekta tofauti na mifumo ya kisiasa, kwa lengo la kuunda serikali yenye msingi dhabiti.

Kando na hayo, alisema ana nia ya kuifanya serikali kuwa bora, kupunguza gharama ya matumizi na kuunda serikali yenye ufanisi na manufaa kwa wananchi.

Mnamo Agosti mwaka jana, Rais Ruto aliwakashifu maafisa wake wakuu, akiwashutumu baadhi yao kwa kutokuwa na ufahamu wa kile kinachoendelea katika nyadhifa zao.