Habari za Kitaifa

Ukomavu wa EACC kulinda aliyefichua unyakuzi wa ardhi

Na JOSEPH OPENDA September 5th, 2024 2 min read

TUME ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) imeingilia kati kumlinda mwanaume mmoja aliyetoa habari muhimu kuhusu unyakuzi wa ardhi dhidi ya ukatili wa polisi.

Tume iliwaita maafisa wakuu wa polisi katika Kaunti ya Nakuru kusitisha kufunguliwa mashtaka kwa Simon Sankale Ole Nasieku.

Bw Nasieku, mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Vibanda na Wafanyabiashara Karimbux, Baringo, amekuwa akizungumzia unyakuzi haramu wa shamba la ekari 3 katika Jiji la Nakuru lenye thamani ya Sh100 milioni.

Alikuwa wa kwanza kutoa habari kuhusu mipango ya kunyakua shamba hilo.

Licha ya upinzani kutoka kwa wafanyabiashara na agizo kutoka kwa Waziri wa Biashara wa Kaunti ya Nakuru, Stephen Kuria, ubomoaji wa majengo uliendelea.

Matatizo ya Bw Nasieku yalianza Mei 1, 2024 wakati majambazi waliokodiwa walibomoa majengo kwenye sehemu mbili za ardhi.

Baada ya kupinga hatua hiyo, Bw Nasieku alikamatwa na kupelekwa katika Kituo Kikuu cha Polisi cha Nakuru na maafisa wakasema alitishia mtu kuhusiana na ubomoaji.

Baadaye ilibainika kuwa mlalamishi alikuwa na uhusiano na mwanasiasa mwenye nguvu katika kaunti.

Bw Nasieku aliachiliwa kwa dhamana ya pesa taslimu Sh30, 000 lakini alikabiliwa na vitisho vya mara kwa mara vya kushtakiwa na maafisa wa polisi na akaandikia EACC ili iingilie kati suala hilo.

Mnamo Agosti 28 2024, aliitwa na polisi ili afike katika kituo cha polisi.

Baadaye EACC iliwaita Afisa Mkuu wa Kituo Kikuu cha Polisi (OCS) na Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo hadi afisi zake Nakuru mnamo Septemba 3, 2024.

Wakati wa mkutano ulioongozwa na Meneja wa EACC eneo la South Rift Ignatius Wekesa, tume hiyo iliwataka polisi kuondoa mashtaka dhidi ya Bw Nasieku, ikisisitiza kuwa yeye ni mfichuzi.

Bw Wekesa alitoa wito kwa polisi wa Nakuru kulinda wafichuzi na walalamishi wanaofichua unyakuzi wa ardhi na aina nyingine za ufisadi, badala ya kuwafungulia mashtaka ya uwongo.

“Sheria inakataza kudhulumiwa kwa wanaotoa taarifa za kufichua ufisadi, na tunaomba sana polisi waondoe mashtaka yaliyokusudiwa dhidi ya Nasieku,” alisema Wekesa.

Msemaji wa EACC, Bw Eric Ngumbi alithibitisha kuwa wataenda kortini ili kurejesha ardhi ambayo ilinyakuliwa kinyume cha sheria na meya wa zamani.