Habari za Kitaifa

Ulimi wa Passy Ma Travor ulivyowaweka boksi Wakenya walio ng’ambo na kuwahadaa mamilioni

Na NYABOGA KIAGE September 22nd, 2024 1 min read

WAKENYA wanaoishi ng’ambo ni miongoni mwa watu wengi ambao wameandikisha taarifa na polisi baada ya kupoteza kima cha Sh350 milioni katika mpango bandia wa uwekezaji ambao wapelelezi wanasema unaendeshwa na Pascaline Peter almaarufu Passy Ma Travor.

Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai na Uhalifu (DCI) inasema inasaka ushahidi kutoka kwa stakabadhi nyingi baada ya makachero kuruhusiwa kumzuilia Bi Peter kwa siku 30.

Katika kile kinachotajwa kama uchunguzi tata, wapelelezi wanasaka stakabadhi, maelezo ya malipo na aina nyingine za mawasiliano kati ya mshukiwa na waathiriwa.

Mmoja wa walalamishi, Mkenya anayeishi Italia, ametoa maelezo kuhusu jinsi aliwekeza zaidi ya Sh5 milioni katika biashara hiyo haramu iliyokuwa ikiendeshwa na Bi Peter.

“Watu wanaoishi Italia ni miongoni mwa wawekezaji wakubwa wanaoaminika walikuwa wakitia kibindoni pesa nyingi kila mwezi lakini biashara hiyo ikaporomoka,” akasema afisa mmoja wa DCI ambaye aliomba jina lake limebanwe kwa sababu haruhusiwi kuzungumza na wanahabari.

Kufikia sasa, waathiriwa wengine zaidi ya 100 wamefikiwa na maafisa wa DCI.

Miongoni mwa walioingia katika mtego huo wa kuwekeza mamilioni ya pesa kwa biashara feki ni maafisa wakuu wa serikali na wafanyabiashara.

Afisa mkuu wa DCI katika eneo la Kasarani Justus Ombati aliambia Taifa Jumapili kuwa wanataraji kuwa waathiriwa zaidi watajitokeza na kuandikisha taarifa ili kuimarisha kesi dhidi ya mshukiwa mkuu.

Hii ni baada ya mahakama kutoa muda zaidi wa kuzuiliwa kwa Bi Peter korokoroni kutoa nafasi ya uchunguzi zaidi kufanywa.