Kauli ya mwanaTikTok Kakan Maiyo baada ya kuachiliwa na polisi
MwanaTikTok maarufu Godfrey Mwasiaga, anayejulikana kama Kakan Maiyo, Ijumaa aliachiliwa kwa dhamana ya Sh10,000 pesa taslimu baada ya kukamatwa kwa madai ya uchochezi na kusambaza taarifa za uongo kupitia mitandao ya kijamii.
Mwasiaga alikamatwa usiku wa Julai 9, na kufikishwa katika kituo cha polisi cha Muthaiga, ambapo alipewa dhamana huku Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) ikimwamuru kufika katika makao makuu ya DCI Jumatatu.
Kwa mujibu wa taarifa ya DCI, Mwasiaga alinaswa katika jengo la Kimathi House, Nairobi, ambapo alikuwa akiendesha biashara kwa jina la LetaPeleka Logistics.
Kukamatwa kwake kulichochewa na video iliyosambaa TikTok, ambapo alisikika akitoa matamshi yanayodaiwa kuwa ya uchochezi dhidi ya polisi na familia zao, akielezea ghadhabu ya wananchi dhidi ya madai ya utekaji na mauaji ya wakosoaji wa serikali.
Katika video hiyo, alisema miongoni mwa mengine:“Familia zenu zitalia kama familia hizi ambazo zimewapoteza wapendwa wao. Hakuna kiwango cha utekaji, mauaji au kukamatwa kutakaonyamazisha Wakenya.”
Wakili wake, Philip Maiyo, alisema hakuna msingi wa kisheria wa mashtaka hayo, na kwamba mteja wake alikuwa akitumia haki yake ya kikatiba ya kujieleza.
“Tunaitaka serikali iondoe mashtaka haya yasiyoeleweka wala kuwa na mlalamishi halisi,” alisema wakili huyo.
Licha ya mipango ya kumfikisha mahakamani Milimani, changamoto za kiufundi ziliripotiwa, na ndipo Mwasiaga akarejeshwa Muthaiga alikoachiliwa kwa dhamana ya polisi.
Mjomba wake, Peter Malande, alieleza furaha yake akisema familia imepata afueni.
“Tumepumua baada ya yeye kuachiliwa.”
Mwasiaga mwenyewe alisema hakudhulumiwa akiwa korokoroni.
“Walikuwa wa wataalamu, hawakunidhuru hata kidogo.”