Uncategorized

Macho kwa bingwa mtetezi Sheila Chepkirui akiwinda taji la New York Marathon

Na BERNARD ROTICH Na GEOFFREY ANENE October 29th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

SHEILA Chepkirui wa Kenya anarejea kwenye barabara za mji wa New York siku ya Jumapili, Novemba 2, 2025, akiwa na lengo moja kuu: kutetea taji lake la TCS New York City Marathon.

Baada ya mbio za kuvutia mwaka jana ambazo zilimpa ushindi wake wa kwanza katika ligi ya Marathon Kuu Duniani (WMM), Chepkirui yuko New York akiwa na imani tele na umakini mpya.

Mtimkaji huyo mwenye umri wa miaka 34 ana azma ya kushinda tena katika barabara hizo zenye milima na hali ya hewa isiyotabirika, mbio zinazohitaji uvumilivu na nguvu kwa wakati mmoja.

Akijifua kwenye milima ya Kaunti ya Kericho, Chepkirui ameinuka kutoka kuwa bingwa wa mbio za uwanjani hadi kuwa mmoja wa watimkaji mahiri wa marathon duniani, akijulikana kwa akili yake ya kimkakati na kasi yake ya kumalizia mbio. Uzoefu wake New York unamweka pazuri kwa sababu anajua ni wakati gani wa kuongeza kasi na ni wakati gani wa kuhifadhi nguvu.

Akiwa na muda bora wa saa 2:17:29, Chepkirui ataingia makala hayo ya 54 akiwa na muda wa tatu-bora kwa kasi katika orodha ya wanawake watakaoshiriki. Lakini bingwa huyo mtetezi anakabiliwa na wapinzani wakali wanaotaka kumvua taji, wakiwemo mabingwa wa New York Marathon Sharon Lokedi (2022) na Hellen Obiri (2023).

Lokedi aliyemaliza wa tisa mwaka jana New York, ataingia akiwa na muda bora zaidi wa 2:17:22 aliopata akitawala Boston Marathon mwezi Aprili.

Obiri, ambaye alimaliza wa pili mwaka jana New York, naye amerejea ulingoni kutafuta taji tena.

Mwaka 2024, Chepkirui aliibuka mshindi kwa saa 2:24:35, akifuatwa kwa karibu na Obiri (2:24:49) na Vivian Cheruiyot (2:25:21). Ushindi huo wa 1-2-3 ulithibitisha tena ubabe wa Kenya duniani, na mwaka huu huenda tukashuhudia tena hali kama hiyo.

Katika mahojiano kabla ya kusafiri Jumanne, Chepkirui aliambia Taifa Leo kwamba maandalizi yake yameenda sawa kama ilivyopangwa. Baada ya miezi mitatu ya mazoezi makali, ikiwemo mbio za milimani kuiga mandhari magumu ya New York, yuko tayari kwa kibarua mbele yake.

“Orosha ya washiriki ni kali sana, lakini nitakimbia mbio zangu mwenyewe,” alisema. “Barabara za mashindano ni ngumu, na kila mtu amejitayarisha vizuri. Si rahisi kubaki kileleni, lakini nataka kurudi kwenye jukwaa la washindi, ikiwezekana kama mshindi tena,” alisema.

Msimu wa Chepkirui mwaka 2025 ulianza vyema alipotawala Nagoya Women’s Marathon mwezi Machi, akimaliza kwa 2:20:40 mbele ya Mjapani Sayako Sato (2:20:59) na mzaliwa wa Kenya anayewakilisha Bahrain, Eunice Chumba (2:21:35). Anasema ushindi huo ulimpa imani na muda wa kutosha wa kujiandaa kwa New York Marathon.

“Kushinda Nagoya kulinipa imani. Kulinikumbusha kwamba kila kitu kinawezekana ukijiandaa vizuri,” alisema. “Sina presha, bali motisha ya kufanya vizuri tena.”

Zaidi ya washiriki wa Kenya, mbio za wanawake zimevutia nyota wa kimataifa akiwemo Sifan Hassan, mzaliwa wa Ethiopia anayewakilisha Uholanzi, mwenye muda bora zaidi katika kundi hilo (2:13:44). Bingwa huyo wa Sydney Marathon, Sifan, atakuwa tishio kubwa bila kusahau bingwa wa dunia 2022, Gotytom Gebreslase wa Ethiopia (2:18:11), na Waamerika Emily Sisson (2:18:23), Sara Hall (2:20:32), na Susanna Sullivan (2:21:56).

Makala hayo yatamkosa Edna Kiplagat, 45, ambaye ni bingwa wa mwaka 2010. Kiplagat amejiondoa New York Marathon baada ya kufiwa.

“Ninajua haitakuwa rahisi,” alisema Chepkirui. “Lakini niko tayari kwa chochote kitakachonijia katika mitaa ya New York.”