Kibarua kwa Kindiki kubomoa ushawishi wa Gachagua Mlima Kenya
HOTUBA ya Naibu Rais Kithure Kindiki kwa taifa Alhamisi ilifichua kwamba ana ajenda ya kubomoa umaarufu wa mtangulizi wake Rigathi Gachagua huku akipigia debe Rais William Ruto kwa Wakenya.
Katibu Mkuu wa Chama cha Jubilee Jeremiah Kioni anasema Kindiki anaingia ofisini akiwa na mtazamo hatari.
‘Kama ningekuwa yeye, ningefanya uchambuzi huru wa kina kuhusu hali halisi kitaifa bila kutegemea ripoti rasmi ambazo maafisa wa usalama wanapasha serikali. Ripoti hizo wakati mwingine hazisemi ukweli kwa walio mamlakani,” alisema.
Aliongeza kuwa ‘hisia zilizopo ni kwamba ama anasaidia watu kuepuka utawala wa Kenya Kwanza au anaisaidia kuendelea kuwafanya watu kuwa maskini’. Aliyekuwa Mbunge wa Gatanga, Nduati Ngugi, ambaye amekuwa mmoja wa watu wanaompigia debe Gachagua katika Kaunti ya Murang’a, alisema Kindiki hana tofauti na Rais Ruto.
“Nilipomsikiliza Kindiki, nilielewa kile Rais Ruto alimaanisha aliposema alikuwa mpweke uongozini. Kindiki katika hotuba yake alifichua kwa njia isiyo ya moja kwa moja kwamba Rais Ruto alimtakia mafanikio pale ambapo Gachagua alidaiwa kushindwa,” alisema Ngugi.
Kindiki alisema atamsaidia Rais Ruto kutekeleza ajenda ya uchumi wa kuanzia mashinani kuenda juu, kuunganisha nchi na kutekeleza maendeleo. Aidha, aliahidi kuhakikisha ufadhili wa ugatuzi unafanyiwa marekebisho ili kuondoa ucheleweshaji katika utoaji mgao kwa kaunti.
Aliyekuwa Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu asema Kindiki anafaa kufahamu ukweli kuwa Wakenya wanaweza kusoma hadaa ya sheria.
Aliyekuwa mgombea urais Peter Kenneth naye asema serikali hii itapatwa na mshtuko mbaya kwa vile wapigakura wamepoteza imani waliyokuwa nayo kwayo 2022.
Kiongozi wa vijana wa chama cha Democratic Congress Gladys Njoroge asema Kindiki anahitaji kwanza kurekebisha uhusiano wake ulioharibiwa na vijana na familia zinazoomboleza kufuatia kutekwa nyara na kuuawa kiholela kwa wapendwa wao alipokuwa Waziri wa Usalama wa Ndani.
Kindiki anapaswa kujua kwamba ikiwa serikali itajaribu kuwasilisha Mswada wa Fedha wa 2025, kutakuwa na upinzani,’ alisema.
Wazee katika Mlima Kenya wakiongozwa na mlezi wa Kiama kia Ma Kung’u Muigai waliambia Taifa Jumapili kwamba wazee wameazimia kumuunga mkono Kindiki.
Mchambuzi wa siasa Gasper Odhiambo anasema kazi ngumu zaidi inayomkabili Kindiki ni ile ya kuchafua ushawishi wa Gachagua ambao umeongezeka kufuatia kuondolewa kwake madarakani.
“Kindiki ameteuliwa kuwa Naibu Rais kwa azma ya kujaribu kuwaunganisha wapigakura wa Mlima Kenya wamuunge Ruto 2027. achagua alikuwa wazi na kwa ujasiri akichukua eneo hilo kutoka kwa Ruto.
Siasa ni mchezo wa idadi na wagombea-wenza lazima waje na kura,” Odhiambo alisema. Anasema ikiwa Kindiki atapata ugumu wa kumhakikishia Rais Ruto angalau kura milioni mbili kutoka Mlima Kenya, basi ataaga siasa 2027.
IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA