Michezo

UNITED NJE: Manchester City yafuzu fainali ya Carabao

January 31st, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

MANCHESTER, Uingereza

MANCHESTER City wamefuzu kwa fainali ya Carabao Cup kufuatia ushindi wa jumla wa 3-2 dhidi ya majirani zao Manchester United.

Sasa, vijana hao wa kocha Pep Guardiola watakutana na Aston Villa fainalini mnamo Machi Mosi katika uwanja maarufu wa Wembley. Villa walifuzu baada ya kuibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya Leicester City, awali Jumanne usiku.

Huku wakijivunia mabao 3-1 ya mkondo wa kwanza, Manchester City walipoteza mkondo wa pili kwa kuchapwa 1-0, Jumatano usiku.

Bao hilo la ushindi la United lilifungwa na kiungo Nemanja Matic kabla ya wakati wa mapumziko, lakini ushindi huo haukuwafaidi.

Manchester United walihitaji kushinda mechi hiyo 2-0 ili kusawazisha matokeo ya awali, lakini mfungaji huyo alifukuzwa uwanjani dakika ya 76 baada ya kuonyeshwa kadi mbili za manjano kwenye mechi hiyo iliyochezewa Etihad Stadium.

Mastaa wa Manchester City Sergio Aguero, Kevin De Bryne na Raheen Sterling walipoteza nafasi nyingi mbele ya mashabiki wao wengi waliomiminika uwanjani humo.

Lakini akizungumzia kuhusu mechi hiyo, kocha Guardiola aliwapongeza vijana wake huku akidai kwamba walicheza vizuri kuliko wapinzani wao, licha ya kushindwa.

“Tulicheza vizuri mikondo yote miwili. Nimeridhika na mchango wa kila mtu, ikizingatiwa kwamba tulicheza tukiwa na matatizo kadhaa katika safu ya ulinzi.

“Aymeric Laporte na Fernandinho hawajarejea katika viwango vyao vizuri, hata Benjamin Mendy hajakuwa sawa. Tutangojea hadi mechi ijayo dhidi ya West Ham United tuone watakavyocheza.”

Katika nusu fainali ya Jumanne dhidi ya Leicester City, Aston Villa walifunga bao la ushindi wakati mashabiki wao walikuwa wameanza kukata tamaa.

Kiungo mahiri, Mahmoud Trezeguet Hassan alipachika bao hilo wavuni na kuiwezesha timu yake kutinga fainali. Raia huyo wa Misri alifunga bao hilo muhimu baada ya kuandaliwa pasi na Ahmed Emohamady.

Wakiwa nyumbani mbele ya mashabiki wao wengi, Villa chini ya kocha Dean Smith walitangulia kupata bao la kwanza kupitia kwa Matt Target kabla ya Kelechi Iheanacho kusawazisha kwenye mechi hiyo iliyochezewa Villa Park.

Villa wamekuwa na historia ya kujivunia katika michuano hii na itakuwa furaha kwa mashabiki wao iwapo watatwaa ubingwa wa mwaka huu, baada ya kulikosa taji hilo kwa muda mrefu.

Villa walionyesha kiwango cha juu licha ya nyota kadhaa kutocheza mechi hiyo ambayo pia kipa wao mpya, Pepe Reina hakuwa kikosini kutokana na jeraha dogo linalomsumbua.

Kocha wao, Smith anaamini ushindi wao dhidi ya Leicester City utawapata vijana wake matumaini makubwa ya kung’ara katika mechi za usoni.