Habari za Kaunti

Urafiki wa Joho, Omar wazua joto kisiasa

March 31st, 2024 2 min read

NA WINNIE ATIENO

JUHUDI za aliyekuwa Gavana wa Mombasa, Hassan Joho kuunganisha viongozi wa Pwani waliokuwa mahasimu wake kisiasa akiwemo Naibu Mwenyekiti wa chama tawala cha UDA, Bw Hassan Omar, zimeanza kuzua joto la kisiasa miongoni mwa wafuasi wa UDA.

Hii ni baada ya viongozi wa chama hicho kinachoongozwa na Rais William Ruto, eneo la Pwani, kuanza kuuliza maswali kuhusu usuhuba wa Bw Omar na Bw Joho, ambao umeshuhudiwa siku za hivi karibuni.

Wakiongozwa na Bw Samir Omar, viongozi wa UDA Mombasa, walisema hatua ya Bw Omar kuungana na viongozi wa ODM ni kinaya.

“Huwezi kwenda kuleta muungano kwa chama pinzani na chama chako kimekushinda kuleta muungano. Unatuaibisha. Ikiwa nyumba yako umeiachilia na imekushinda kuiunganisha, basi hufai cheo hicho cha uenyekiti,” alisema Bw Omar.

Alisema Omar anafaa kuleta maendeleo na si siasa za mapema.

Bw Omar alisema viongozi hao wa Pwani wameanza siasa mapema badala ya kupelekea wakazi maendeleo.

“Leteni maendeleo kwa Wapwani. Wacheni ubinafsi kwa uchoyo wa maendeleo. Mnaangalia matumbo yenu mkigawanya vyeo vya kisiasa kama mbunge, waziri, na hata Rais,” aliongeza.

Bw Joho ameonekana kupenyeza siasa zake UDA, baada ya kumnasa Bw Omar ambaye ni mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA).

Bw Omar pia amekuwa akitetea biashara za familia ya Bw Joho akisisitiza ipo haja ya Wapwani kushirikiana.

“Niliwaambia hata watu wa UDA katika hili suala tutasimama kama Wapwani. Hakuna kubaguana twende pamoja kama Wapwani na tunakutakia kila la kheri,” alisema Bw Omar majuzi kwenye hafla ya futari nyumbani kwa Bw Joho eneo la Nyali.

Bw Joho ameanza kampeni zake Pwani ili kurejesha hadhi yake kama kigogo eneo hilo kabla ya kupenyeza sehemu zingine nchini.

“Tubebane, tukikoseana, tuwe wepesi wa kusameheana, na tushirikiane kwa karibu ili tujenge umoja wetu,” Bw Joho aliwaambia Wapwani.

Viongozi wa kaunti za Taita Taveta, Kwale, Tana River, Kilifi, Mombasa na hata Lamu wamejitokeza kumuunga mkono, wakiamini ni wakati wa Pwani kutoa rais.

Bw Joho ambaye ni kiongozi wa ODM, ameelezea nia yake kutaka kumrithi kiongozi wa chama hicho, Bw Raila Odinga katika kuwania urais 2027.

Bw Odinga anamezea mate wadhifa wa mwenyekiti Tume ya Muungano wa Africa (AUC).

Mbunge wa Changamwe, Bw Omar Mwinyi amemtaka Bw Joho kuendeleza kampeni za kutaka kuwa rais wa Kenya kote nchini ili kuonyesha umahiri wake kisiasa.

Mwenzake wa Kilifi Kusini, Bw Ken Chonga alisema azma ya Bw Joho itabadilisha taswira ya siasa eneo la Pwani.

Bw Joho alisema ni sharti amrithi babake wa kisiasa, Bw Raila Odinga.

Joho amekuwa akiendeleza kampeni za kuunganisha wanasiasa wa Pwani kutoka mirengo ya upinzani na chama tawala cha Kenya Kwanza.