Habari

Utata zaidi wakumba nchi huku mafuta yakikauka

September 7th, 2018 2 min read

Na WAANDISHI WETU

GIZA limeendelea kutanda kuhusu gharama ya mafuta baada ya Mahakama Kuu mjini Bungoma kusimamisha ushuru mpya, siku chache tu baada ya Mahakama jijini Nairobi kuamua ushuru huo utaendelea hadi Rais Uhuru Kenyatta atoe uamuzi wake.

Kutokana na utata huo, hakuna mwelekeo kuhusu iwapo bei itashuka kama Mahakama ya Bungoma ilivyoagiza ama bei ya juu ya mafuta iliyowekwa na Serikali hapo Septemba 1 itaendelea.

Jana, Jaji Stephen Riechi wa Mahakama ya Bungoma alisimamisha kwa muda ushuru huo wa asilimia 16 kwa mafuta hadi Septemba 12 mahakama itakapotoa maagizo zaidi.

Walalamishi watatu Titus Alila, Jackline Otieno na Francis Ogada kupitia wakili wao Kenneth Amondi, walimwambia Jaji Riechi kuwa ushuru huo mpya unaumiza Wakenya kimaisha.

Watatu hao walisema Waziri wa Fedha Henry Rotich alikiuka Katiba kwa kufanya uamuzi ambao unakandamiza raia.

“Jaji ametoa maagizo ya kusimamisha ushuru mpya wa mafuta. Tutawasilisha maagizo hayo kwa Tume ya Kudhibiti Kawi (ERC) pamoja na Bw Rotich,” alisema Bw Amondi.

Uamuzi huo ulionekana kuleta utata kuhusu suala hilo la mafuta, kwani mnamo Jumanne Jaji Chacha Mwita wa Mahakama ya Juu jijini Nairobi alikataa kusimamisha ushuru huo akisema hatima ya mabadiliko ya Mswada wa Fedha bado haijulikani.

Kulingana na Wakili Thomas Maosa, ingawa inaonekana kama majaji waligongana kwenye uamuzi kuhusu suala hilo, kila kesi huamuliwa kwa kutegemea nguvu za maombi yanayowasilishwa kortini.

“Inategemea uzito wa ombi linalowasilishwa mbele ya jaji na hati za kuliunga mkono. Hatuwezi kusema kuwa kwa sababu kuna kesi nyingine katika mahakama tofauti, Jaji angekataa kutoa agizo,” alisema.

Kulingana na wakili huyo, agizo la mahakama likitolewa, ni lazima liheshimiwe iwapo hakuna lingine la kulisimamisha. Lakini kufikia jana jioni ERC na Serikali hawakuwa wamesema lolote.

Kulingana na wakili Soyianka Lempaa, kuna uwezekano kesi zote zilizoko mbele ya Mahakama Kuu kuunganishwa akisema agizo la Mahakama ya Bungoma ni la muda tu na haliwezi kuzua utata wowote.

Jana, Waziri Rotich alifanya kikao cha faraghani na Spika wa Bunge Justin Muturi, Kiongozi wa Wengi Bungeni Adan Duale, mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti Kimani Ichungw’a, Mwanasheria Mkuu Paul Kihara pamoja na Naibu Msimamizi wa Ikulu Njee Muturi kuhusiana na utata wa ushuru mpya.

Mkutano huo wa saa mbili haukuzaa matunda yoyote kwani Bw Rotich aliahidi tu ‘mashauriano zaidi’.

Utata huu unaendelea huku maeneo mengi nchini yakiendelea kushuhudia upungufu mkubwa wa mafuta kufuatia hatua ya baadhi ya wafanyabiashara wa bidhaa hiyo kusitisha usambazaji.

Katika miji mikubwa ikiwemo Nairobi, Mombasa, Kisumu, Nakuru na Machakos, kulishuhudiwa misongamano mikubwa ya magari huku madereva wakikimbilia vituo vichache vilivyokuwa na mafuta.

Wengi wa wamiliki wa vituo vya kuuzia mafuta walisema wamesalia na hifadhi kidogo ya mafuta na huenda vituo vyao vikakauka kufikia leo.

Rais Uhuru Kenyatta, ambaye anakabiliwa na shinikizo ya kutia saini marekebisho ya Mswada wa Fedha ili kusimamisha ushuru huo mpya, anatarajiwa kuwasili nchini Jumapili baada ya ziara zake nchini Uchina na Rwanda.

Taarifa Ya Dennis Lubanga, Wycliffe Muia, Benson Matheka Na Charles Wasonga