Habari Mseto

Viongozi wakosoa kukamatwa kwa mlinzi aliyeitisha mshahara

October 22nd, 2018 1 min read

Na ALEX NJERU

BAADHI ya viongozi wa kaunti ya Tharaka-Nithi wamekashifu hatua ya kukamatwa kwa mlinzi wa hospitali ya Gaceeraka ambaye alifunga kituo hicho Jumanne iliyopita akilalamikia kutolipwa mshahara kwa miezi 14.

Bw Josphat Mutiiria alikamatwa na polisi nyumbani kwake katika kijiji cha Gaceeraka, wadi ya Chiakariga Ijumaa usiku na kupelekwa katika kituo cha polisi cha Marimanti.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye kituo hicho, diwani wa Chiakariga, Bw Njagi Murandi alisema hawataruhusu viongozi wa serikali ya kaunti kuendelea kutesa wafanyakazi bila malipo.

Madiwani, Mwenda Gataya (Mukothima), Susan Ngugi (Marimanti), Gitonga Kithuka (Nkondi) na Mutegi Ruujia (Gatunga) walisema hawataruhusu viongozi wa kaunti kuendelea kudhalilisha wafanyakazi kwa kuamuru kukamatwa kwao wanapodai malipo.

Bi Ngugi ambaye pia ni Naibu Spika alisema watatafuta wakili wa kumsaidia mlinzi huyo katika kesi hiyo na kushtaki serikali ya kaunti kwa kutomlipa mshahara.

“Bw Mutiiria alifunga kituo hicho kwa sababu alikuwa amejaribu njia nyingine zote ambazo hazikufaulu,” alisema Bi Ngugi.

Bw Kithuka na Ruujia walisema walinzi wanaofanya kazi kama walinzi katika kaunti nzima hulipwa kwa kutegemea uhusiano wao na viongozi wakuu wa kaunti.

Wawakilishi hao walibainisha kuwa kuna mfanyakazi mmoja wa kaunti anayemiliki kampuni ya usalama ambaye tayari imepewa kadarasi ya kutoa huduma za usalama katika vituo vyote vya kaunti na kwamba walinzi walioko kwa sasa walikuwa wakisumbuliwa ili waache kazi.

“Tunafahamu kuwa kuna kampuni ya kulinda usalama inayomilikiwa na mfanyakazi wa kaunti ambayo imepewa kadarasi ya kutoa huduma za usalama,” alisema mwakilishi wa Chiakariga.