Makala

Vipimo vya udongo shambani kuboresha uzalishaji wa chakula

Na SAMMY WAWERU August 19th, 2024 2 min read

WAKULIMA wametakiwa kuwa wakifanya vipimo vya udongo kwenye mashamba yao, ili kuwawezesha kuimarisha uzalishaji.

Hatua hiyo itawawezesha kujua virutubisho vinavyohitajika kuboresha shughuli za kilimo.

Katibu Mkuu wa zamani katika Idara ya Mimea, Wizara ya Kilimo, Profesa Hamadi Boga anaeleza wasiwasi wake kuhusu jinsi wakulima wengi nchini wanaendeleza kilimo cha mimea bila kujua hali ya udongo wa mashamba yao.

“Takwimu zinaonyesha ni asilimia 8 pekee ya wakulima Kenya ambao hufanya vipimo vya udongo mashambani mwao. Ningewasihi wakulima kuibukia mbinu hii ya kupeleleza udongo ili kuimarisha uzalishaji,” akasema Prof Boga.

Viazi vikuu, almaarufu nduma zikiendelea kukua shambani. Wakulima wanahimizwa kupima udongo ili kuboresha mazao. PICHA|SAMMY WAWERU

Prfesa Boga kwa sasa anahudumu kama Naibu wa Rais wa mpango wa utoaji huduma katika taasisi ya AGRA, shirika la Kiafrika linaloendeleza miradi mbalimbali ya kilimo Barani Afrika kuwasaidia wakulima wenye mashamba madogo (smallholder farmers) kuongeza mazao na mapato, kuinua maisha yao na kuimarisha usalama wa chakula.

Udongo kwenye ardhi nyingi nchini Kenya umegeuka kuwa na kiwango cha juu cha aside, kwa sababu ya matumizi ya fatalaiza na dawa zenye kemikali.

Sampuli za udongo kwenye maabara. PICHA|SAMMY WAWERU

Prof Boga anasema udongo Afrika umezeeka na kwamba kuimarisha mpango wa uzalishaji chakula, kunahitaji wakulima kukumbatia mbinu za kupima kiwango cha Asidi na Alikali (pH) ili kujua virutubisho vinavyohitajika.

“Cha msingi kwa wakulima ni kwamba kuna haja ya waelimishwe kuhusiana suala na hilo,” anaeleza.

Shirika la Utafiti wa Kilimo na Mifugo Kenya (Kalro)

na ile ya Mbegu na Ustawishaji wa Mimea (Kephis) ndizo asasi kuu za serikali zilizotwikwa jukumu la kufanya utafiti na vipimo vya udongo.

Mojawapo ya maabara za kupima udongo nchini, japo ni ya kibinafsi. PICHA|SAMMY WAWERU

Hata hivyo, maabara za kibinafsi pia hutoa huduma hizo japo kwa gharama ya juu.

Ripoti ya Kalro ya mwaka 2023 na ile ya Gatsby Africa ilibaini kuwa asilimia 63 ya ardhi za kilimo Kenya zina kiwango cha juu cha asili, jambo ambalo linatatiza uzalishaji.

Viazi vikuu, maarufu kama nduma shambani. PICHA|SAMMY WAWERU

Bw Boga, ambaye pia ni mtafiti aliyewahi kuhudumu katika Chuo Kikuu cha Masuala ya Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta (JKUAT), kama Mhadhiri wa Masuala ya Bayolojia, pia anaiomba serikali kuwekeza vya kutosha katika taasisi za utafiti wa kilimo.

Imetafsiriwa na Kalume Kazungu