Habari

Vukeni sakafu tumenyane, Ruto aambia mawaziri

September 7th, 2020 2 min read

Na JUSTUS OCHIENG

NAIBU Rais William Ruto amewataka mawaziri wanaomkosoa kujiuzulu ili waingie ulingo wa siasa apambane nao ikiwa wameshindwa kutekeleza majukumu yao serikalini.

Huku akionekana kumrejelea Waziri wa Mazingira na Misitu Keriako Tobiko aliyemdunisha hivi majuzi kwa kumtaja kama “karani” wa Rais Uhuru Kenyatta, Dkt Ruto aliwataka mawaziri kuepukana na siasa na wajikite katika ajenda za serikali za maendeleo.

“Maafisa wa serikali na haswa mawaziri waache siasa. Wasaidie katika utekelezaji wa ajenda nne kuu za Jubilee kama vile uzalishaji wa chakula, uimarishaji wa sekta za afya, nyumba na uzalishaji wa nafasi za kazi kwa vijana.” akasema.

“Lakini wakishindwa majukumu haya basi wajiondoe, waingie siasa tukutane huko tupimane nguvu msimu wa siasa utakapotimu,” Dkt Ruto akasema Jumapili wakati wa mchango wa fedha katika Kanisa la Kianglikana (ACK), Athi River.

Mnamo Jumamosi, Waziri Tobiko na Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen walirushiana cheche za matusi, waziri huyo alipomdunisha Dkt Ruto na kumtaka ajiuzulu.

Bw Tobiko alidai kuwa Naibu Rais alikuwa akimtumia Murkomen kumtusi Rais Uhuru Kenyatta huku akitaja seneta huyo kama mtu asiye na adabu.

“Murkomen anapaswa kuwa na adabu kwa sababu hana heshima kabisa. Amekuwa akitumiwa kuwatukana viongozi wengine akiwemo rais. Lazima aambiwe awe na adabu na amheshimu kiongozi wa nchi. Hata huyo mkubwa wake ni karani wa Rais kama mimi,” akafoka alipoongoza hafla ya uhifadhi wa msitu eneo la Loita, kaunti ya Kajiado.

Bw Murkomen, ambaye ni mwandani wa Dkt Ruto, juzi alitumia maneno makali dhidi ya Rais Kenyatta akidai ndiye chanzo cha masaibu yanayomzonga Naibu wake; ambapo ametengwa serikalini.

Lakini Jumapili, Dkt Ruto aliwataka mawaziri na maafisa wengine wa serikali kukomesha dharau na matumizi mabaya ya mamlaka ya afisi zao.

“Wale wanaochapa siasa, wakome kuwadharua wengine na kutumia mamlaka visivyo,” akasema.

Dkt Ruto pia alionekana kushambulia bosi wake, Rais Kenyatta na wandani wake wa kisiasa, kiongozi wa ODM Raila Odinga na mwenyekiti wa Kanu Gideon.