Habari Mseto

Wafuasi wa Arati wateketeza jeneza wakimkashifu Osoro ‘kwa kukosa heshima’

January 15th, 2024 1 min read

NA WYCLIFFE NYABERI

Wafuasi wa Gavana wa Kisii Simba Arati hivi leo Jumatatu Januari 15, 2024 wanafanya maandamano ya kumkashifu mbunge wa Mugirango Kusini Silvanus Osoro kwa kile wanasema mbunge huyo  “anamkosea heshima” kiongozi wa kaunti.

Maandamano hayo yanayofanyika pakubwa katika eneobunge la Bobasi, yanaongozwa na madiwani ambao ni wandani wa Arati. Mamia ya wanabodaboda wanatumiwa kufunga barabara nyingi za eneobunge hilo.

Katika mji wa Nyamache, waandamanaji hao waliliteketeza jeneza lililokuwa na picha ya mbunge huyo wa UDA.

Kumekuwa na purukushani baina ya viongozi hao wawili kufikia viwango ambapo maisha ya raia yameanza kuwa hatarini.

Tukio la kufyatua risasi katika mkutano wa gavana Jumatatu iliyopita, mnamo Januari 8, 2024, katika eneobunge la Mugirango Kusini ndilo lililoteka sana hisia za Wakenya kitaifa.

Ufyatulianaji huo uliwaacha raia wanne na majeraha ya risasi.

Gavana alidai Osoro ndiye aliyepanga fujo hizo lakini Kiranja huyo wa Wengi katika Bunge la Kitaifa alikanusha madai hayo.

Tayari chama cha ODM kimezungumzia kisa hicho cha wiki jana na vingine vingi vya hapo awali.

Kupitia katibu wake Edwin Sifuna, ODM walisema maisha ya Naibu Mwenyekiti wao wa kitaifa yamo hatarini.

Polisi kwa sasa wanakabiliana na vijana katika makutano ya kuingia Nyamache, kwenye barabara kuu ya Kisii-Kilgoris.

Vijana hao wanawatupia Polisi mawe huku walinda usalama nao wakijibu mapigo kwa kuwarushia vitoa machozi.