• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 12:48 PM
Miti 20,000 kupandwa kando ya bwawa la Karimenu II Gatundu

Miti 20,000 kupandwa kando ya bwawa la Karimenu II Gatundu

NA LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa Gatundu Kaskazini na Gatundu Kusini kwenye Kaunti ya Kiambu, wamepata afueni baada ya serikali kuahidi kuweka vituo sita vya kusambaza maji kutoka bwawa la Karimenu II lenye thamani ya Sh24 bilioni.

Wakazi hao walikuwa wakilalamika kuwa kulikuwa na upungufu wa maji lakini serikali inapanga kujenga kituo kingine cha kusambaza maji katika msitu wa Kinale kitakachowasaidia wakazi hao kupata maji bila upungufu.

Kulingana na mkurugenzi wa kampuni ya Athi Water Service Bw Michael Thuita, serikali imeanza kujenga vituo hivyo vya kusambaza maji ambapo hivi karibuni watapata maji bila kuchelewa.

“Wakazi wa Gatundu hawastahili kuwa na hofu yoyote kwa sasa kwa sababu serikali imeanza kutekeleza wajibu wake,” alifafanua Bw Thuita.

Alisema maji kutoka Karimenu II sasa yanasambazwa hadi Ruiru na jijini Nairobi na maeneo jirani.

Aliyasema hayo jana Ijumaa kwenye hafla ya upanzi wa miti 20,000 iliyoongozwa na benki za Standard Chartered, KCB, Equity, na Postbank.

Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na jaji anayeamua mahakamani kesi za maswala ya ardhi na mazingira.

“Kutoka sasa miti 20,000 itapandwa kando ya eneo la bwawa la Karimenu ili kuboresha mazingira yawe safi,” alisema Jaji Oscar Angote.

Jaji wa mahakama ya mizozo inayohusu ardhi na mazingira Oscar Angote, (katikati) na mkurugenzi wa Athi Water Service Michael Thuita (kulia) wakihutubia waandishi wa habari katika bwawa la Karimenu II. PICHA | LAWRENCE ONGARO

Thuita alisema serikali inatafuta ardhi ekari 300 kwa ajili ya upanzi wa miti.

Alisema serikali imeanza mazungunzo na familia kutoka maeneo ya Mwimuto, Kanjuku, Gatei, Gathairi, na Githobokoni ili wakubali bwawa jingine lijengwe katika eneo la Ndarugu.

Hapo awali wakazi hao walidinda kuondoka maeneo hayo wakisema watakosa maeneo ya kufanyia shughuli za kilimo.

Lakini hata hivyo, Bw Thuita alisema serikali ilitumia mbinu nyingine ya kuwaacha wafikirie upya kwa undani ili waweze kujisahili na baadaye wakubali matakwa ya serikali.

Hata wakazi wengine waliwasilisha malalamiko yao mahakamani wakidai kuwa bwawa la Karimenu II liko kilomita tatu pekee kutoka makazi yao na kwa hivyo haikuwa sawa bwawa jingine kujengwa karibu na makazi yao.

Nalo shirika la Resource Outreach Development Initiative (RODI) litazuru vijijini na kuhamasisha wakazi jinsi ya kupanda miti kwa wingi.

Mkurugenzi wa shirika la RODI Bi Esther Bett, alisema licha ya kupanda miti kote nchini kuna haja pia ya kuhamasisha wakazi kupanda miti na kuhifadhi misitu ili kuongeza vyanzo vya maji katika maeneo hayo.
  • Tags

You can share this post!

Markstam Orwa asema bidii inaweza kumfikisha kwa viwango...

Shakahola: Idadi ya wanaotafutwa na familia zao ni 360

T L