Habari

Wakulima wa maembe Murang'a walia

February 19th, 2019 1 min read

Na MWANGI MUIRURI

WAKULIMA wa maembe katika Kaunti ya Murang’a wameteta vikali kuwa utawala wa Gavana Mwangi Wa Iria wa miaka sita hadi sasa umewatunuku hasara ya zaidi ya Sh10 bilioni kupitia ukosefu wa kiwanda cha uongezaji ubora.

Mwenyekiti wa Wakulima hao, James Musau, akiongea na Taifa Leo Dijitali alisema kuwa  punde tu baada ya Wa Iria kuapishwa kuwa gavana mwaka wa 2013, walimwendea na kujadiliana naye kuhusu kiwanda cha uongezaji ubora.

“Tuliafikiana kuwa maembe mawili tu ndiyo huhitajika kuunda juisi lita moja na ambayo inaweza ikauzwa kwa Sh1,000 sokoni. Maembe hayo mawili kwa sasa yanauzwa kwa madalali kwa chini ya Sh2,” akasema Bw Musau.

Aliteta kuwa maembe yakiongezwa ubora yanaweza yakatengeneza hata mivinyo, hali ambayo kwa ujumla inaweza ikabuni nafasi za ajira na utajiri kwa wakulima na pia serikali ya Kaunti ijipe umaarufu na utajiri wa ushuru.

“Hali ni tofauti kabisa ambapo sasa kazi yetu imekuwa ya kulia kila mwaka kuhusu hasara. Kila Januari hadi Machi katika kanda za chini za Kaunti ya Murang’a huwa ni msimu wa maembe lakini utapata kuwa badala ya uwezo wetu kamili wa kujitajirisha, ni madalali ndiyo wanaonufaika,” akasema.

Maembe. Picha / Hisani

Hata hivyo, hivi majuzi  Wa Iria alilalama kuwa serikali kuu haijakuwa ikituma pesa za ugatuzi kwa wakati ufaao na kwa kiwango cha kushirikisha maendeleo mashinani.

“Tumekuwa katika shida ya ugavi wa rasilimali na ni hivi majuzi tu serikali ilitangaza kupunguza migao kwa serikali za Kaunti kufuatioa ukosefu wa fedha. Kwa sasa tuko na changamoto ya migomo ya wauguzi lakini bado niko na imani hili la viwanda litatimia,” akasema.

Alisema kuwa serikali yake inasaka mikataba ya kimaelewano na serikali za Morocco, Misri na Canada ili kujenga viwanda vitano vya uongezaji ubora hasa kwa mazao yatokanayo na kilimo.