Habari

Wakulima wa majanichai Gatundu Kaskazini wataka malipo ya kuridhisha

June 13th, 2019 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

WAKULIMA wanaokuza majanichai katika eneo la Kanyoni, Gatundu Kaskazini, wanataka nyongeza ya fedha kwa bidhaa hiyo.

Walisema hata ingawa kwa wakati huu wanachuna majanichai kwa wingi, bado Mamlaka ya Ustawishaji Chai Nchini (KTDA) inawalipa pesa kidogo kwa bidhaa hiyo.

Mkulima Bi Margaret Kamau (pichani) anasema yeye ni mkulima wa majanichai kwa muda mrefu sasa lakini kwa siku za hivi karibuni malipo wanayopata sio ya kuwaridhisha.

“Sisi wakulima wa majanichai tunapitia masaibu mengi kila mara tunapotekeleza wajibu wetu wa kuchuma. Tunarauka asubuhi na mapema na wakati mwingi mvua inatunyeshea. Baada ya hapo tunaugua homa na maradhi ya kifua,” akasema Bi Kamau.

Anasema tayari amepeleka majanichai yake katika kituo maalum ili kupakuliwa na malori ya kuyapeleka kiwanda cha chai cha Mataara.

“Lakini ifikapo wakati wa malipo tunalipwa pesa kidogo mno. Sisi ni wazazi wenye watoto walio mashuleni, kwa hivyo hatungetaka kunyanyaswa hivyo,” alijitetea Bi Kamau wakati wa mahojiano na mwandishi wa makala haya.

Naye Bi Jecinter Gichiru ambaye pia ni mkulima wa majanichai katika eneo hilo, anamtaka Rais Uhuru Kenyatta aingilie kati kuona ya kwamba wao kama wakulima wanafaidika pakubwa kutokana na zao hilo.

“Wakulima wengi wameathirika na maradhi tofauti kama kifua kubana kutokana na kurauka kila asubuhi kwenda kuchuma zao huku kukiwa na baridi kali na mvua kunyesha,” anasema Bi Gichiru.

Anasema wakulima wengine wanatembea mwendo mrefu huku wakifika kwenye mashamba wakiwa wamechoka na kwa hivyo utendakazi wao unakuwa umeshuka kiasi.

“Sisi wengi wetu ni wazazi na tuna mahitaji mengi ya kutekeleza. Watoto wetu wako shuleni na pia wana mahitaji mengine ya kawaida. Kwa hivyo KTDA ifanye hima kuona ya kwamba maslahi ya wakulima yanashughulikiwa vilivyo bila ubaguzi,” akasema Bi Gichiru.

Malilio

Mkulima mwingine Bw Mburu Kamau anasema wao kama wakulima wana malilio mengi ambayo yanastahili kuzingatiwa haraka iwezekanavyo.

“Pesa tunayolipwa ni duni mno na halitoshelezi mahitaji yetu kama wakulima wa majanichai. Serikali kupitia KTDA ifanye kweli kuona ya kwamba sisi kama wakulima walio mashinani tunashughulikiwa vilivyo,” anasema Bw Kamau na kuongeza wangetaka bei ya kuiuza irekebishwe ili mkulima wa kawaida aweze kupata kitu cha kujivunia anaapoiuza.

Anasema wameweka nguvu zao zote kwa zao hilo na kwa hivyo hawawezi kutaka mchezo na hali ya malipo kwa wakulima.

“Mkulima wa kawaida ni mtu mnyenyekevu aliyejitolea kufanya kweli katika kilimo hicho na kwa hivyo ifikapo wakati wa kupewa haki yake, ifanywe kwa njia ya kuridhisha mkulima mwenyewe,” anasema Bw Kamau.