Habari Mseto

Wanachama wa Urithi Housing Co-operative wahimizwa kuchukua hatimiliki zao

May 10th, 2019 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

WANACHAMA wa Urithi Housing Co-operative Society wanazidi kupokea vyeti vya umiliki wa vipande vya ardhi walivyonunua  kwa lengo la kujiendeleza.

Mnamo Ijumaa chama hicho kimetoa vyeti 400 kwa wanachama wake ambao wamepata mali kupitia chama hicho.

Mwenyekiti wa chama hicho Bw Samuel Maina, amesema wanachama wake wengi wamenufaika kwa kununua vipande vya ardhi katika sehemu tofauti za nchi kwa lengo la kujiendeleza kimaisha.

Amesema chama cha Urithi kimenunua ardhi katika sehemu tofauti za nchi na kuwauzia wanachama wake vipande vya ardhi vilivyoko kwenye maeneo hayo.

Ametaja baadhi ya maeneo wanakomiliki mashamba ni kama Kiambu, Nakuru, Murang’a, Gilgil, Machakos, Kilifi, Kajiado, Embu, na Malindi.

“Tumepiga hatua kubwa ya kuwapa matumaini wanachama wetu ambao wamefanya hima kununua vipande vya ardhi katika maeneo mbalimbali ya nchi hii. Hiyo ni njia moja ya kuwaleta Wakenya ili kutangamana vyema,” amesema Bw Maina.

Ameyasema hayo wakati amewapa wanachama hao vyeti vyao ili waweze kumiliki vipande vya ardhi kikamilifu.

Amewahimiza wanachama wao ambao hawajachukua vyeti vyao vya umiliki wafanye hivyo haraka kwa sababu kuna vyeti 900 ambavyo bado viko afisini na hazijachukuliwa na wanachama husika.

“Ninawahimiza wale ambao hawajachukua vyeti vyao wafanye hima waje wachukue haraka iwezekanavyo,” akatoa mwito.

Amesema kila mwanachama yuko huru kufanya lolote apendalo katika kipande chake cha ardhi mara baada ya kumiliki.

Matumizi hayo ni kama vile kupanda chakula, na hata shughuli za ufugaji.

Alisema kwa wakati huu wana wanachama wapatao 27,000 na tayari wameuza eneo la ekari 3,000 na kutoa vyeti 6,500 kwa wanachama wao.

Bw Maina alipozuru eneo la Juja Farm kunakowekwa barabara ya lami alisema watu walio na ardhi eneo hilo watanufaika pakubwa kwa sababu maji na umeme ni huduma zitakazopatikana kwa urahisi.

Alisema Urithi imenufaisha wanachama wao wengi kwa kuwajengea nyumba za kuishi.

“Ningetaka kuwahimiza wakazi wa hapa wachukue nafasi hii kuona ya kwamba wamejiendeleza kwa sababu ya barabara ya kilomita 12 kutoka Juja mjini hadi Juja Farm inayoendelea kujengwa.Itafungua biashara kwa wingi,” alisema Bw Maina.