Habari Mseto

'Wananchi wanataka maendeleo na wala sio majisifu ya viongozi'

October 22nd, 2019 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

MNAMO siku ya Mashujaa Dei kulishudiwa mengi, wananchi wakipata fursa ya kuhutubiwa na viongozi waliojieleza waziwazi kwa umati.

Diwani wa Ngoliba (MCA) Joachim Mwangi alijipata kona mbaya wakati alijaribu kumpigia debe Gavana wa Kiambu anayekabiliwa na kesi kortini, Ferdinand Waititu.

“Si mnajua vyema gavana wetu anapitia changamoto kadha? Tuzidi kumwombea ili mambo hayo yaishe na arejee kazini,” alisema Bw Mwangi.

Ni matamshi ambayo hayakufurahisha wananchi ambao walionekana kunung’unika bila kumpigia makofi jinsi alivyotarajia.

Baadaye alilazimika kukamilisha hotuba yake na kuwaachia wengine wajieleze.

Aliyekuwa wakati mmoja diwani wa Gatuanyaga, Thika Mashariki Bi Cecilia Wamaitha Mwangi aliwashutumu wazee wa eneo la Kilimambogo na vitongoji vyake ambao baada ya kupokea hatimiliki za vipande vya ardhi waligeuka kuuza tena kwa watu fulani.

“Iwapo unajua ulipokea cheti cha kumiliki kipande cha ardhi na baadaye ukauza, ole wako kwa sababu utakosa hata mahali pa kuzikwa ukifa. Nyinyi wazee mnataka usaidizi upi? Nyinyi mtajilaumu baadaye,” alisema Bi Mwangi.

 

Chuo cha walimu cha St Johns Teacher Training College, Kilimambogo kikitumbuiza wakazi wa Thika Mashariki. Picha/ Lawrence Ongaro

Alisema Kaunti ya Kiambu ina mikakati mizuri na kuna matumaini baada ya miaka mitatu kwamba maswala mengi yanayostahili kutekelezwa yatatimizwa.

Bw Chege Wagathu ambaye ni mshauri wa kisiasa wa Mbunge wa Thika, Patrick Wainaina, alisema tayari shule nyingi za msingi eneo la Thika zimefanyiwa ukarabati ambapo ni chache tu ambazo zimesalia.

“Mheshimiwa ameahidi kuleta maendeleo zaidi. Kwa sasa maji yamesambazwa katika maeneo kadha huku barabara pia zikikarabatiwa ndani na nje ya mji wa Thika,” alisema Bw Wagathu.

Alisema mji wa Thika utapata mafanikio iwapo wakazi wake watashirikiana na viongozi wote katika eneo hilo.

Diwani mteule wa mji wa Thika Bw John Njiru alisema tayari Kaunti ya Kiambu imetenga takribani Sh84 milioni ili kuona ya kwamba masoko yamejengwa na usambazaji wa maji kutekelezwa.

Alisema kwa sasa Kaunti ya Kiambu iko tayari kufanya kazi na wananchi walioko mashinani ili kufanikisha maendeleo kamilifu.

Hotuba ya naibu gavana iliridhisha wengi kwa sababu aliahidi kuwa hivi karibuni kampuni za maji katika kaunti hiyo zitalazimika kusambaza maji safi katika kila eneo.

Alisema kampuni ya kuchinja nyama ya nguruwe ya Uplands Bacon Factory, itafanyiwa ukarabati hivi karibuni ili iweze kufufuliwa rasmi.

Alizidi kusema ya kwamba wafugaji mifugo kwa ajili ya uzalishaji maziwa watapewa mwongozo wa jinsi ya kujiendeleza zaidi na biashara hiyo.