Habari za Kitaifa

Wanaoenda haja kubwa na ndogo nyuma ya majumba kukiona

January 27th, 2024 1 min read

NA MWANGI MUIRURI

SERIKALI ya kaunti ya Murang’a imewaonya wakazi wenye mazoea ya kwenda haja kubwa na ndogo vichochoroni mjini Murang’a kwamba watakamatwa na kushtakiwa kwa kuvunja sheria za mazingira.

Waziri wa Maji, Usafi na Mazingira Mary Magocho alisema Ijumaa kwamba maafisa wa idara hiyo wameagizwa kushirikiana na bodi ya usimamizi wa mji wa Murang’a kuhakikisha kuwa wahalifu hao wanaadhibiwa.

Alilalamika kwamba wakazi wamegeuza maeneo kadha ya nyuma ya majengo kuwa sehemu za kuachilia haja kubwa na mkojo.

Bi Magocho pia aliongeza kuwa maafisa wa Idara ya Afya ya Umma watatumwa kukagua vyoo katika majengo ya burudani.

“Washukiwa ambao wamekamatwa kufikia sasa kwa kwenye haja vichorochoroni na nyuma ya majengo walisema mabaa na mikahawa wanayokwenda hayana vyoo hivyo wanalazimika kujisaidia barabarani,” akasema.

Waziri huyo alisema walevi huogopa vyoo vya kawaida kwa hofu wanaweza kukumbana na mabaya humo.

“Baadhi ya wakosaji ni walevi ambao wanaogopa kwamba huenda wakatumbukia ndani ya vyoo vya baa na mikahawa na badala yake wao huhiari kujisaidia nyuma ya nyumba hizo,” Bi Magochi akasema.

Lakini muungano wa maafisa wa mpango wa miji Kaunti ya Murang’a, kupitia mwenyekiti wao Adams Mwaura, unasema kutopangwa vizuri kwa mji huo ndiko kunachangia watu kwenda haja pahala wazi.

“Vyoo vya umma ni haba mno katika mji wa Murang’a kutokana na hali kwamba mji huu ulipangwa vibaya. Wenye majengo nao hawaruhusu raia kutumia vyoo vyao huku wengine wakilipisha ada kwa huduma hiyo,” akaongeza.