Habari Mseto

Wanaofichua wauzaji bangi kutuzwa Sh500

January 21st, 2024 1 min read

NA PIUS MAUNDU

KAMANDA mmoja wa polisi kutoka Kaunti ya Makueni ameahidi kumpa Sh500 mtu yeyote ambaye atajitolea kutoa habari kuhusu wanaoendeleza biashara ya bangi kwenye gatuzi hilo.

Bw Albert Kipchumba, kamanda wa kituo cha polisi cha Salama, amesema kuwa biashara ya mauzo ya bangi imekuwa ikishamiri eneo hilo na inastahili kukomeshwa.

Kutokana na hilo, Bw Kipchumba alisema kuwa wameanza kuwashirikisha wanajamii kukabiliana na mauzo hayo ili kuokoa vijana ambao wapo hatarini kuangamizwa kimaadili kutokana na uvutaji bangi.

“Vijana na watoto eneo hili wanavuta bangi kwa kiwango cha kutisha. Binafsi nitampa Sh500 kwa yeyote ambaye atatoa maelezo yatakayosaidia kukamatwa kwa wale ambao wanauza bangi,” akasema Bw Kipchumba.

Soma pia https://taifaleo.nation.co.ke/habari/habari-za-kitaifa/wataalamu-wasema-bangi-haina-madhara

Alitoa nambari yake ya simu ambapo yeyote anaweza kutuma maelezo ya kusaidia kukamata wanaouza dawa hiyo ya kulevya.

Alizungumza hayo Jumapili, Januari 21, 2024 aliposhuhudia mechi ya soka kwenye kituo cha kibiashara cha Ngiini ambapo alitangaza kuwa atakayesaidia kusambaratisha mtandao wa kuuza bangi, atatuzwa Sh500.