Habari za Kitaifa

Wanjigi akosa kujibu shtaka la umiliki silaha mara ya pili

Na RICHARD MUNGUTI September 12th, 2024 2 min read

MKURUGENZI wa Mashtaka ya Umma (DPP) Renson Ingonga amepewa muda wa siku saba (7) kuthibitisha kuwepo kwa maagizo ya kumzuia asimfungulie mashtaka kinara wa chama cha Safina Jimi Wanjigi ya kupatikana na silaha kinyume cha sheria.

Hakimu mkuu wa mahakama ya Milimani Bi Susan Shitubi alimpa DPP muda wa siku saba kujibu madai ya Bw Wanjigi kwamba alimshtaki, kukiwa na agizo la mahakama kuu ya kuzuia kukamatwa na kushtakiwa kwa mwanasiasa huyo kwa umiliki wa silaha bila leseni.

Alipofikishwa kortini wiki tatu zilizopita, Wanjigi na msaidizi wake  David Kibe, mawakili zaidi ya 30 wakiongozwa na Kalonzo Musyoka, Kinara wa Azimio, Daniel Maanzo na Willis Otieno, walipinga washtakiwa wakijibu mashtaka wakisema hatua hiyo ni ya kisiasa na hakuna uhalifu wowote uliofanywa na kinara huyo wa chama cha Safina

Mnamo Alhamisi Septemba 12, Bw Otieno alimweleza Bi Shitubi kwamba Jaji Bahati Mwamuye alikuwa amezima hatua ya DPP kuwashtaki wawili hao.

Bi Shitubi aliahirisha kushtakiwa kwa wawili hao hadi Septemba 12, 2024 kuamua ikiwa washtakiwa wangejibu mashtaka au la.

“Kesi hii ilikuwa imeorodheshwa Alhamisi ili mahakama itoe uamuzi ikiwa washtakiwa watajibu mashtaka 11 ya kumiliki silaha bila leseni au la. Mahakama kuu ilizima kesi hii kuendelea hadi pale itakapoamua ikiwa Polisi na DPP walikaidi agizo Wanjigi asikamatwe na kushtakiwa kwa umiliki wa silaha bila leseni,” Bw Otieno alieleza korti.

Bw Otieno alimkabidhi agizo la Jaji Mwamuye akisitisha kushtakiwa kwa Wanjigi hadi kesi aliyoshtaki mahakama kuu isikizwe na kuamuliwa.

Aliomba mahakama ikome kusoma uamuzi iwapo wawili hao watajibu mashtaka hadi pale Jaji Mwamuye atakaposikiza na kuamua kesi ya kupinga kushtakiwa kwa Wanjigi.

“Tunaomba hii mahakama ikome kusoma uamuzi iwapo Wanjigi anapasa kujibu mashtaka au la,” Bw Otieno alisema.

Lakini viongozi wa mashtaka Wanjiku Waweru na Herbert Sonye waliomba muda kuthibitisha kutoka kwa afisi ya DPP kuhusu agizo hilo.

Bi Waweru alieleza mahakama kwamba hakuwa ameona agizo hapo mbeleni.

“Nimekabidhiwa hii agizo leo. Naomba muda wa siku saba nibaini ikiwa afisi ya DPP imewasilisha majibu katika mahakama kuu,” Bi Waweru alisihi hakimu.

Bi Shitubi aliahirisha kesi hiyo hadi Septemba 26, 2024 kuwezesha DPP kuthibitisha ikiwa kesi iliyoshtakiwa mahakama kuu na Wanjigi imesikizwa na maagizo kutolewa.

Wanjigi na msaidizi wake David Kibe walitiwa nguvuni Agosti 19,2024 baada ya maandamano ya kupinga maongozi mabaya ya serikali ya Rais Willliam Ruto.

Akiwasilisha ombi la kupinga kushtakiwa kwa Wanjigi, wakili Otieno alisema polisi walivamia makazi yake na kutwaa pesa na mali nyingine za thamani ya mabilioni ya pesa wakisaka silaha.