Habari za Kitaifa

Wanyonyi hoiyee! Mfalme mpya wa 800m Olimpiki

Na GEOFFREY ANENE August 10th, 2024 2 min read

BINGWA wa dunia mbio za mita 800 za chipukizi wasiozidi miaka 20 mwaka 2021, Emmanuel Wanyonyi, sasa pia ni bingwa wa Olimpiki baada ya kuponyoka na taji kwa dakika 1:41.19 jijini Paris, Ufaransa, Jumamosi usiku.

Wanyonyi,20, ni mshindi wa 800m mwenye umri mdogo kabisa tangu Olimpiki zianzishwe mwaka 1896.

Alitwaa nishani ya fedha kwenye Riadha za Dunia 2023 mjini Budapest, Hungary nyuma ya mzawa wa Sudan Marco Arop ambaye ni raia wa Canada.

Djamel Sedjati (Algeria), Wanyonyi (Kenya), Gabriel Tual (Ufaransa) na Mohamed Attaoui (Uhispania) waliwasili katika makala hayo ya 33 ya Olimpiki wakijivunia kuwa na muda nne-bora duniani mwaka huu katika umbali huo dakika 1:41.46, 1:41.58, 1:41.61 na 1:42.04, mtawalia.

Wanyonyi ampiku Marco Arop wa Canada kutwaa dhahabu hiyo ya 800m jijini Paris. PICCHA | REUTERS

Hata hivyo, ni Wanyonyi, ambaye alionekana kushika roho mkononi kwa kuingia uwanjani kwa maombi, aliibuka na ushindi kwa dakika 1:41.19 akifuatiwa na Arop (1:41.20) na Sedjati (1:4150).

Wanyonyi, ambaye hupenda kukaa mbele kwenye mashindano, alifanikiwa katika mbinu zake, ingawa alilazimika kufanya kazi ya ziada kuzima Sedjati kwenye laini.

Sasa, Wanyonyi ni mwanamume wa 12 tofauti kutoka Kenya kushinda medali katika 800m kwenye Olimpiki tangu Wilson Kiprugut anyakulie taifa medali ya kwanza katika umbali huo – shaba – mwaka 1964 mjini Tokyo, Japan.

Kiprugut kisha aliashinda fedha mwaka 1968 nchini Mexico. Mike Boit aliambulia shaba mwaka 1972 mjini Munich nchini Ujerumani kabla ya Kenya kupata dhahabu yake ya kwanza kupitia kwa Paul Ereng mwaka 1988 mjini Seoul, Korea Kusini.

William Tanui na Nixon Kiprotich walivuna dhahabu na fedha katika Olimpiki za Barcelona mwaka 1992 nchini Uhispania naye Fredrick Onyacha akaridhika na shaba mwaka 1996 mjini Atlanta, Amerika.

Hapa ubabe tu!

Kenya sasa imetawala makala matano mfululizo ya Olimpiki katika 800m – Wilfred Bungei (Beijing 2008, China), David Rudisha (London 2012, Uingereza na Rio de Janeiro 2016, Brazil), Emmanuel Korir (Tokyo 2020, Japan) na sasa Wanyonyi (Paris 2024, Ufaransa). Ferguson Rotich alinyakua fedha mjini Tokyo mwaka 2021.

Alfred Kirwa na Timothy Kitum walivuna shaba mwaka 2008 na 2012, mtawalia. Wanyonyi sasa ni wa tatu kwa muda bora katika historia ya 800m wanaume baada ya Rudisha aliyeweka rekodi ya dunia 1:40.91 mwaka 2012 na mzawa wa Kenya, Wilson Kipketer kutoka Denmark aliyetimka 1:41.11 mwaka 1997.