Afya na JamiiMakala

Wazazi wawadunga sindano mabinti zao kuzuia mimba

Na STEPHEN ODUOR August 18th, 2024 3 min read

WAKAZI wa Wema na Kulesa Eneobunge la Tana Delta, wanaishi kwa hofu kubwa ya mabinti zao huku visa vya mimba za mapema zikikithiri.

Baadhi ya wasichana wanaacha shule sababu ya mahusiano ya mapenzi na ndoa za mapema.

Baadhi ya wazazi wameamua kuchukua hatua, na sasa wanawadunga sindano za kupanga uzazi watoto wao waliobalehe.

“Mwanangu wa kwanza alipata ujauzito akiwa kidato cha pili, akajifungua nikamrudisha shuleni, ghafla alipofika kidato cha nne akapata ujauzito wa pili, ilinipa dhiki sana,” anasimulia Margaret Dhidha.

Bi Dhidha ana watoto wa kike wanne, wawili kati yao wametungwa ujauzito wakiwa shuleni na kwa sasa wanalea watoto nyumbani.

Anadhani kuna nuksi

Binti yake wa pili yuko katika kidato cha kwanza. Hofu ya mimba ya kwanza ilimchochea Bi Dhidha kumweka katika njia ya kupanga uzazi.

“Niliona itajirudia kama ile ya dadake kwa hivyo nikamdunga sindano ya miaka mitano, pamoja na dadake anayemfuata sababu tayari yuko kidato cha kwanza. Ni kama nuksi hii inawasubiri tu wakifika kidato cha pili. Imebidi niwe na tahadhari,” anasema kwa huzuni.

Japo uamuzi huu haumpendezi, hana budi ila kuwalinda wanawe wasitokomee katika dhiki milele.

Anaeleza kuwa ufukara katika jamii unasababishwa na mimba za udogoni, kwa hivyo anahofia mabinti zake watafuata mkondo huo.

“Maisha ya sasa yanahitaji bidii sana. Yana majukumu mengi kiasi cha kwamba hata wanaooa leo, wanataka mtu wa kuwasaidia kifedha sio kuketi tu na kulea. Nisipowasaidia wanangu kwa kuchukua hatua kama hizi, watapata dhiki sana maishani,” anasema.

Hayuko pekee yake

Bi Caroline Miche, naye anakabiliana na changamoto sawa, huku mabinti zake watatu kati ya wanne wakiwa tayari wameolewa sehemu mbalimbali.

“Wote walipata mimba wakiwa shule ya msingi, wawili wakatoroka nyumbani wakaenda kutumikia ndoa mbali sana, kwa mwanangu wa kwanza tayari mjukuu ana miaka miwili,” anasimulia kwa huzuni.

Amesalia na binti mmoja ambaye ndiye kitinda mimba wake, katika darasa la sita.

Huyu ndiye tegemeo lake la kujivunia na amemdunga sindano ya kupanga uzazi, akidai kuwa dalili za kutungwa mimba zilianza kumvizia.

” Nimepigana sana na wanaume huku mjini, wengine wanamsubiri nikimtuma sokoni, wengine wanaandika mpaka barua za mapenzi na wengine ni watu na hela zao wanajaribu sana kumdanganya,” anasema.

Anaomba haki itendeke

Bi Miche analaumu sana wafanyakazi wa serikali kwa tabia hiyo mbovu ya kuwanajisi watoto akidai wengi wao wanatumia pesa kuwahadaa na hata kusambaratisha hatua za haki.

Anasema haki imekuwa ya matajiri na wenye pesa, kwani wanaowadhulumu watoto hutumia pesa kuwahonga maafisi wa usalama na hata wakati mwingine kugawanya familia kukinzana katika ushahidi.

“Mume wangu alipewa laki tatu baada ya mwanangu wa pili kunajisiwa na afisa wa usalama, ghafla akanifukuza na akabaki na watoto, sasa kesi ile isingeenda popote, ilikufa, “anaeleza.

Mzazi mwingine, Joseph Kitsao, anaunga mkono hatua hiyo akidai kuwa mimba kwa watoto wachanga huleta aibu na dhiki kwa familia.

” Tunaishi katika jamii ambayo pindi mwanao anapotungwa mimba basi itabidi umuoze, sababu sasa bila kumuoza ataitwa malaya na majina mengine ya kushusha hadhi, “anasema.

Anaelezea kwamba, hofu hiyo ndio imemsababisha yeye na mke wake kutopuuza janga linalokumba vijiji hivi na kuchukua hatua hiyo ya kuwadunga wanao sindano ya miaka mitatu kila mmoja.

Akiwa baba wa binti wawili, tamanio la moyo wake ni kuwaona watoto wake wakipata ujauzito ndani ya ndoa.

Hisia ‘zalemea’ wasichana

“Wengine watasema tuwafunze watoto wetu tabia njema ili wajisitiri. Ni vyema, ila wajue kwamba hisia hazina uhodari; kwa watoto hawa kuna majaribu tele wasiyoyaweza,” anafunguka.

Chifu Mkuu wa Lokesheni ya Salama Peter Jilo anabainisha kuwa visa hivyo vimekuwa vikiongezeka huku vijiji husika katika eneo hilo vikirekodi visa vya juu zaidi katika kata hiyo.

“Watoto wamezidi, na ni kwa sababu wazazi wamezembea pia katika majukumu yao.  Wamewatelekeza mabinti zao na ndiyo sababu wananajisiwa,” anasema.

Zaidi, anaeleza kuwa wasichana wanaonajisiwa hawako tayari kuwafichua wanaowanajisi, na badala yake wanatoroka nao na hivyo kuchangia kusambaratika kwa kesi nyingi.

“Mengine yamekuwa kama kitega uchumi, ila wazazi wafahamu, kuna kupanga uzazi lakini pia kuna magonjwa ya zinaa yasoweza zuiwa na hizo sindano,” anaeleza.

Hatari ya sindano

Afisa wa Afya ya Uzazi katika Kaunti hiyo Hawaa Abdighafoor anabainisha kuwa japo dawa za kudhibiti uzazi ni suluhu, sio sawa kwa mabinti wachanga.

Kwa mujibu wa Dkt Hawaa, si vyema kuwaweka watoto kwenye vidhibiti mimba kama hatua ya tahadhari, bali kuna sababu ya kuwashirikisha katika vikao vya ushauri nasaha na kufahamu marafiki zao kwa kina.

“Mtindo huo wa kudunga sindano ya miaka mitano si salama kwa kila mtu, inaweza kusababisha hata utasa baadaye iwapo mwili utakuwa umezoea,” anasema.

Zaidi, anapendekeza kwamba wazazi wawaweke wanao kwenye vipindi vya ushauri pindi wanapopata mimba, badala ya kuwaoza mapema.

Mimba za mapema zimekithiri katika kaunti ya Tana River huku mamia ya wanafunzi wakiripotiwa kuacha shule kuolewa ama kulea mimba na watoto.

Kulingana na ripoti ya Idara ya Afya, zaidi ya watoto mia tatu hamsini waliripitowa kutungwa mimba.

Hata hivyo, katika rekodi za mahakama, kesi zinazohusu kunajisiwa kwa watoto wa kike zi chini ya ishirini kwa mwaka.

(Majina ya wazazi husika yamebadilishwa kuficha utambulisho)