Habari za Kitaifa

Whitman amkosoa Ruto kwa kudai Ford Foundation ilifadhili maandamano ya Gen Z

Na CHARLES WASONGA August 29th, 2024 2 min read

BALOZI wa Amerika Meg Whitman ameikosoa serikali ya Kenya kwa kuulaumu Wakfu wa Ford kwa madai ya kudhamini maandamano ya Gen Z kati ya Juni na Julai mwaka huu, 2024.

Kwenye mahojiano katika runinga ya Citizen Jumanne siku, Agosti 27, 2024, Whitman aliutetea wakfu huo akisema una rekodi nzuri ya kufadhili mipango ya serikali na mashirika ya kijamii nchini tangu ulipoanzishwa 1963.

Balozi huyo alisema viongozi wa Wakfu huo wako nchini kuhusiana na shutuma hizo na kujiondolea lawama ya kudhamini maandamano yaliyosababisha vifo vya zaidi ya watu 60.

“Nadhani shutuma hizo zilitolewa kwa nia mbaya na hazikufaa. Wakfu wa Ford umefanya kazi katika nchi hii kwa karibu miaka 60, wanasaidia idadi kubwa ya mashirika ya kijamii. Mashirika ya kijamii ni nguzo muhimu katika ukuzaji wa demokrasia sawa na vijana, viongozi wa kidini na wengine,” akaeleza.

“Mshauri mkuu wa Wakfu wa Ford na maafisa wake waliwasili nchini Kenya juzi na wanashughulikia suala hilo na ninaamini kuwa mwishowe watu wataamini kuwa Wakfu wa Ford haukuhusika na fujo hizo,” Balozi Whitman akaongeza.

Alikariri kuwa lawama dhidi ya wakfu huo ilitolewa kwa nia mbaya ikizingatiwa kuwa kuna mashirika mengi yenye makao yao Amerika, kama vile USAID ambayo hufadhili shughuli nyingi za mashirika ya kijamii.

“Kando na Wakfu wa Ford, kuna mashirika mengi kutoka Amerika, kama vile USAID, Welcome Trust na Wakfu wa Rockefeller ambayo hufadhili shughuli za mashirika ya kijamii. Kwa hivyo, haikuwa sawa kwa serikali kuelekeza kidole cha lawama kwa Wakfu wa Ford pekee,” Whitman akaeleza.

Mnamo Julai 15, 2024 Rais William Ruto alijitokeza na kulaumu Wakfu wa Ford kwa kufadhili maandamano ya vijana wa Gen Z waliopinga serikali yake.

Akiongea katika eneo la Keringet, Kaunti ya Nakuru Rais alishutumu wakfu huo kwa kudhamini maandamano hayo yaliyosababisha uharibifu wa mali na kuvuruga uthabiti nchini.

“Nataka niulize watu wa Ford Foundation watuambie hizo pesa wanazitoa kufadhili kusudi wapate faida gani?” akauliza.

“Nawaambia kuwa ikiwa hawataki demokrasia inawiri Kenya, ikiwa wataendelea kudhamini fujo tutawaambia wakome kufanya hivyo au waondoke Kenya,” Dkt Ruto akaonya.

Wakfu wa Ford ulijiondolea lawama ukisema kuwa maelezo kuhusu matumizi ya fedha zake yako wazi katika tovuti yake.

Kwenye taarifa, uongozi wa wakfu huo ulieleza kuwa fedha zake zimekuwa zikifadhili shughuli za kutetea haki za kibinadamu, uongozi bora na mipango mingine ya kusaidia jamii.

“Fedha za Wakfu wa Ford hazijawahi kutumika kufadhili ghasia tangu ilipoanza shughuli zake nchini Kenya 1963. Maelezo yote kuhusu matumizi ya fedha zetu yako katika tovuti yetu na mtu yeyote mwenye haja anaweza kufuatilia,” ikasema taarifa kutoka kwa uongozi wa wakfu huo.