Habari za Kitaifa

Wito serikali ifidie Gen Zs walioathirika wakati wa maandamano

Na WINNIE ONYANDO August 23rd, 2024 1 min read

RAIS wa Bunge la Mwananchi Francis Awino ametoa wito kwa serikali iwafidie waathiriwa wa maandamano yaliyofanyika miezi michache iliyopita ya kupinga serikali ya Kenya Kwanza.

Bw Awino alisema hayo baada ya kuwasilisha kesi yao ya kuishutumu serikali kwa kutumia nguvu kupita kiasi, maafisa wa polisi kuwaua waandamanaji na ukiukaji mkubwa wa haki za kibinadamu wakati wa maandamano katika Mahakama ya Haki za Kibinadamu.

“Serikali inafaa kufidia waathiriwa wote wa ukatili wa polisi. Kuna wale ambao walijeruhiwa, wengine waliuawa. Familia ya waliouawa inafaa kufidiwa pia,” akasema Bw Awino.

Kando na hayo, aliitaka serikali kuzingatia Katiba ya Kenya na kukoma kudhulumu Wakenya.

“Wakati wa maandamano, vijana wa Gen Z walikuwa wakiandamana bila vurugu. Hata hivyo, polisi walitumia nguvu kupita kiasi kuwatawanya jambo ambalo lilifanya mamia kuumia na wengine kupoteza maisha yao,” akaongeza.

Rais wa Bunge la Mwananchi Francis Awino akihutubia wanahabari Niarobi. PICHA|WINNIE ONYANDO

Isitoshe, aliishutumu serikali kwa kuendelea kuwateka watu nyara.

“Hata jana (Alhamisi, Agosti 22, 2024) tuliskia kuna wengine walitekwa nyara Kitengela. Hii inafaa kukoma,” akasema.

Matamshi hayo ya Bw Awino yanajiri siku moja tu baada ya Kiongozi wa chama cha Narc Kenya, Martha Karua kusema kuwa ataendelea kupigania haki za Wakenya na kuishutumu serikali kukiuka haki za binadamu wakati wa maandamano.

“Msimamo haubadiliki. Tutaendelea kutetea Wakenya. Japo Bw Odinga (kiongozi wa upinzani) ameachana na siasa za humu nchini, sisi bado tupo imara na tutaendelea kuiwajibisha serikali ya Kenya Kwanza. Kuwa katika upinzani hakutegemei uwepo au kutokuwepo kwa ndugu yetu (Bw Odinga). Ni jukumu tunalochukua kwa uzito,” Bi Karua alisema.