Sherehe zatuliza vita vya ubabe Kirinyaga

KENNEDY KIMANTHI na GEORGE MUNENE

SAWA na kaunti nyingine, Kaunti ya Kirinyaga inayoandaa sherehe za Mashujaa Dei mwaka huu 2021, imekumbwa na uhasama wa kisiasa wa kila mara, kushukiana na migogoro ya kila mara baina ya viongozi.

Hata kwa waangalizi wasio makini, dalili za ubabe wa kisiasa katika kaunti hiyo huwa wazi.

Katika miaka ya sabini, kulikuwa na tofauti za kisiasa kati ya wanasiasa wakuu wa Kirinyaga James Njiru (Kanu Moto) na Nahashon Njuno, waliokuwa wabunge wa Ndia na Gichugu mtawalia.

Wawili hao wanakumbukwa kwa kurushiana mangumi Bungeni wakati Njiru alikuwa akihudumu kama waziri msaidizi wa Afya huku Njuno akiwa waziri msaidizi wa wizara ya Uchukuzi na Mawasilino.

Pia, wanakumbukwa kwa kutishiana kwa bunduki mjini Kutus baada ya kutofautiana kuhusu mahali ambapo makao makuu ya Kanu yangejengwa.

Ingawa wawili hao waliacha siasa kitambo, ushindani mkali wa kisiasa ungali unashuhudiwa kaunti ya Kirinyaga.

Japo uhasama wa kisiasa Kirinyaga sio jambo geni, sherehe za Mashujaa Dei zinaonekana kutuliza hali na kuunganisha viongozi wa kaunti hiyo kwa wakati huu.

Wanakubaliana kwamba, kuna haja ya kuzika tofauti zao na kuhakikisha kaunti yao inapata maendeleo na ustawi. Ni azimio ambalo Rais Uhuru Kenyatta alisisitiza Jumatatu alipokutana na viongozi wa Kirinyaga katika ikulu ndogo ya Sagana kabla ya sherehe za leo Jumatano ambazo ni za kitaifa na zinazofanyika katika kaunti hiyo.

Rais Kenyatta aliwataka viongozi hao kuungana na kushirikiana kama kundi moja ili kuafikia maendeleo na ustawi was kaunti yao.

Kirinyaga ina maeneobunge manne Kirinyaga Ndia, Kirinyaga Central, Gichugu na Mwea ambayo kila moja limewahi kuwa mzozo wa viongozi.

Sherehe za Mashujaa Dei mwaka huu 2021 zitafanyika katika uwanja wa michezo wa Wang’uru dunia ikiendelea kupambana na janga la Covid-19.

Katibu wa usalama wa ndani, Karanja Kibicho na Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru walisema walipatana kwa ajili ya kufanikisha sherehe hizo ambazo zimefanya kaunti hiyo kupata miradi kadhaa ya miundomsingi.

Hofu ya siasa za urithi kutawala Mashujaa Dei

Na VALENTINE OBARA

SIASA za urithi wa urais mwaka wa 2022 zinahofiwa kuteka sherehe za Mashujaa Dei hii leo Jumatano katika Kaunti ya Kirinyaga, huku joto la kisiasa linapozidi kuenea nchini.

Hii itakuwa ni sherehe ya mwisho ya Mashujaa kuongozwa na Rais Uhuru Kenyatta, atakayekamilisha kipindi chake cha urais mwaka 2022.

Vigogo wakuu wa kisiasa ambao wanamezea mate urithi wa urais mwaka 2022 wanatarajiwa kukutana katika hafla hiyo ya kitaifa.

Joto la kisiasa tayari liliamshwa kufuatia ziara za Kiongozi wa ODM, Raila Odinga na Rais Kenyatta, ambao walifanya mikutano tofauti ya hadhara katika maeneo ya Kati wiki hii.

Viongozi wengine wanaotarajiwa katika hafla hiyo ni Naibu wa Rais William Ruto, na vinara wa Muungano wa One Kenya Alliance (OKA) ambao ni Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, mwenzake wa Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi, Mwenyekiti wa KANU aliye pia Seneta wa Baringo Gideon Moi, na Seneta wa Bungoma, Moses Wetang’ula anayeongoza Ford Kenya.

Rais Kenyatta amezidi kuonyesha ishara kuwa ataunga mkono azimio la Bw Odinga katika uchaguzi ujao, wandani wake wakidai Dkt Ruto alimsaliti alipomkaidi kama vile alipopinga Mpango wa Maridhiano (BBI).

Kwa mara ya pili katika kipindi cha chini ya mwezi mmoja, Rais Kenyatta aliashiria hayo alipohutubia wananchi alipokuwa katika msafara Jumatatu baada ya kukutana na viongozi wa Kaunti ya Kirinyaga.

Katika hotuba yake, Rais aliwasifu wakazi wa Mlima Kenya kwa kumkaribisha vyema “mgeni” wake, akionekana kumrejelea Bw Odinga, huku akiwaonya dhidi ya wanasiasa ambao hakuwataja aliodai wanataka kuwadanganya.

“Kuweni makini na yale ambayo wanakuja kuwaambia. Wakija na pesa, chukueni lakini ifikapo wakati wa uchaguzi fanyeni maamuzi kwa busara,” akasema.

Kura za eneo la Kati zimevutia wanasiasa wanaopanga kuwania urais 2022, ikizingatiwa kuwa kuna matarajio hapatakuwepo mgombeaji urais wa kutoa wengine jasho kutoka eneo hilo.

Katika ziara zake, Dkt Ruto hulaumu BBI kwa kuathiri utekelezaji wa miradi ya serikali wakati wa kipindi cha pili cha uongozi wa Jubilee, huku akitumia mafanikio yaliyopatikana katika kipindi hicho kujinadi kwa wananchi.

“Viongozi hawa wengine wanaotaka kuungwa mkono na Rais walimtoroka wakati alipowahitaji. Mimi pekee ndiye niliyesimama naye imara,” Naibu Rais alisema, alipokuwa katika ziara ya kaunti za Pwani aliyokamilisha Jumanne.

Kando na siasa, wananchi wengi wanatazamia kuona kama serikali itatangaza mpango wowote mpya wa kuwafaidi kimaisha.

Katika siku za hivi majuzi, kumekuwa na malalamishi mengi kuhusu kiwango cha juu cha ushuru wa mafuta ambacho kinafanya bei ya mafuta iwe ya juu kupita kiasi.

Hali hii imeongeza ugumu wa maisha ambao ulikuwa tayari umepanda tangu wakati janga la corona lilipotangazwa nchini mwaka 2020.

Kufikia Jumanne, baadhi ya kanuni zilizonuiwa kuepusha maambukizi ya janga la corona zilikuwa zinaendelea kutumiwa ikiwemo kafyu na masharti yanayoathiri shughuli za maeneo ya ibada na yale ya starehe.

Agizo la Joho kuhusu miraa lapingwa vikali

Na WACHIRA MWANGI

SERIKALI ya Kaunti ya Mombasa, italazimika kutafuta pesa kwingine baada ya Gavana Hassan Joho kuagiza kuwa magari ya kusafirisha miraa yasitozwe kodi.

Miraa na muguka ni miongoni mwa bidhaa zinazotozwa kiasi kikubwa zaidi cha kodi za usafirishaji kuingia Mombasa, miongoni mwa mazao ya kilimo.

Kulingana na Sheria ya Fedha ya 2021/22 iliyopitishwa na Bunge la Kaunti ya Mombasa, kiasi kidogo zaidi cha kodi ya kusafirisha miraa ni Sh5,000 kwa mkokoteni huku kiasi cha juu zaidi kikiwa Sh50,000 kwa malori na mabasi yanayozidi tani saba.

Bw Joho akiwa katika mkutano wa kisiasa Kaunti ya Meru ambapo aliandamana na Kiongozi wa ODM Raila Odinga mnamo Jumatatu, aliambia wakazi wa eneo hilo kwamba ameagiza kodi hizo ziondolewe ili kuwasaidia kiriziki.

Waziri wa Fedha katika Kaunti ya Mombasa, Bi Mariam Mbaruk, Jumanne alisema maafisa wa kaunti watatii agizo hilo.

“Hayo ni maagizo kutoka kwa Gavana kwa hivyo tayari tumeanza kuyatekeleza. Tuliacha kutoza kodi kwa miraa zinazoingia Mombasa tangu juzi (Jumatatu),” akasema Bi Mbaruk.

Haikubainika mara moja kama sheria zozote za fedha zilifanyiwa marekebisho kabla agizo hilo la Bw Joho kuanza kutekelezwa.

Wasiwasi

Kando na athari za agizo hilo kwa ukusanyaji wa kodi katika kaunti, baadhi ya mashirika yameeleza wasiwasi kwamba litasababisha ongezeko la bidhaa hiyo ambayo imekuwa ikilaumiwa kwa athari za afya na kijamii.

“Hili ni pigo kiuchumi na hakufaa kutoa agizo aina hiyo. Kodi hizo hutegemewa kutekeleza miradi kwa manufaa ya wakazi. Pia kuna changamoto nyingi za kiafya zinazosababishwa na matumizi ya miraa na muguka,” Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Reachout Centre akasema.

Afisa Mkuu Mtendaji wa Shirika la Kitaifa la Kukabili Uraibu wa Dawa za Kulevya (Nacada), Bw Victor Okioma, alitofautiana na wanasiasa wanaosema kuwa miraa haina madhara ya kiafya.

“Tumehamasisha umma kuhusu madhara ya miraa, na chaguo ni lao. Sawa na pombe, huwa tunatoa ilani kwa kuzingatia utafiti wa kisayansi. Uraibu wa miraa huathiri uwezo wa mtu kimwili, kiakili na hata kiuchumi,” akasema Bw Okioma.

Mshirika wa Bodi ya Nacada, Bi Farida Seif, alikosoa uamuzi wa kaunti kuondoa kodi ya kusafirisha miraa na kusema utasababisha ongezeko la matumizi yake.

“Tumekuwa tukifanya mashauriano na maafisa wa afya na wa kaunti ili kutafuta jinsi miraa na muguka inavyoweza kupigwa marufuku katika kaunti. Hii ni hasara kwa uchumi na afya ya watu wetu,” akasema Bi Farida.

Miraa imeorodheshwa kama dawa ya kulevya na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), na matumizi yake yalipigwa marufuku katika baadhi ya mataifa ya Ulaya.Kulingana na utafiti, matumizi ya miraa kwa muda mrefu huweza kusababisha meno kuoza na pia kuangamiza hamu ya mraibu kushiriki tendo la ndoa.

Korti yaelezwa jinsi mwanamke alivyoibia mfanyabiashara

Na JOSEPH NDUNDA

MFANYABIASHARA raia wa Uganda aliibiwa Sh130,000 na mwanamke saa chache baada ya kukutana kwa mara ya kwanza katika baa moja eneo la Kilimani, Nairobi.

Mwanamke huyo, Clare Monyangi Moseti, 28, anakabiliwa na shtaka la wizi katika Mahakama ya Kibera baada ya kudaiwa kwamba alimlewesha mfanyabiashara huyo katika nyumba yake iliyoko barabara ya Muringa, Kilimani, Nairobi.

Inadaiwa kwamba alitenda kosa hilo kati ya Oktoba 14 na 16 mwaka huu wa 2021.

Mfanyabiashara huyo yuko Nairobi kwa shughuli za kikazi na alikuwa akinywa pombe katika kilabu kimoja kilichoko Adlife Plaza wanawake wawili walipojiunga naye.

Aliketi nao wakilewa na akaomba mmoja nambari ya simu.

Alienda naye katika nyumba yake walipoendelea kuburudika hadi siku iliyofuata mwanamke huyo alipomwambia hakuwa ametosheka na pombe na wakaenda katika baa nyingine.

WASONGA: Sherehe bila kusaidia familia za mashujaa ni kazi bure

Na CHARLES WASONGA

HUKU Kenya ikisherehekea Siku Kuu ya Mashujaa leo Jumatano, ni aibu kwamba jamaa za wapiganiaji ukombozi, wa kwanza, wa taifa hili wanaishi katika hali ya uchochole.

Ama kwa hakika watu hawa hawaoni thamani ya sherehe za leo kwa sababu hawafurahii matunda ya machozi, jasho na damu waliomwaga mababu zao waliopigania uhuru wa Kenya.

Isitoshe, serikali ya sasa imewatelekeza mashujaa wachache wa ukombozi ambao wangali hai, kutokana na kudura za mwenyezi Mungu.

Kile ambacho serikali hufanya kila mwaka ni kutaja majina yao katika sherehe za kitaifa kisha kuwaalika kwa dhifa ya chakula cha jioni katika Ikulu ya Nairobi.

Japo kuna sheria inayotoa mwongozo wa namna serikali inapaswa kushughulikia masilahi ya aina mbalimbali ya mashujaa, serikali haijafanya lolote.

Kwa mfano, kuna Baraza la Kitaifa la Mashujaa ambalo lilipaswa kutekeleza mapendekezo ya sheria.

Baraza hilo lenye wanachama 13 lilitarajiwa kutengewa Sh300 milioni za kusaidia mashujaa na familia zao lakini pesa hizo hazijatolewa tangu sheria hiyo ilipopitishwa mnamo 2014.

Juzi, kiongozi wa ODM Raila Odinga alimtembelea mjane wa shujaa wa ukombozi wa Kenya, Dedan Kimathi, Mama Mukami Kimathi akiahidi kumsaidia anunue kipande cha ardhi katika Kaunti ya Laikipia.

Bw Odinga aliungama kuwa serikali ilikuwa imeahidi kutoa Sh60 milioni kwa ajili ya ununuzi wa ardhi hiyo, lakini pesa hizo hazijatolewa hadi wakati huu.

Ama kwa hakika ni aibu kubwa kwamba mkewe Kimathi anaishi katika nyumba ya kukodisha katika mtaa wa Komarocks, Nairobi kwa kukosa ardhi ya kujengewa makazi ya heshima.

Kinaya ni kwamba, mumewe alipigania jino kwa ukucha hadi wazungu wakakubali kuachilia ardhi ya Waafrika walionyakua.

Mnamo Agosti 31, 2021 Rais Uhuru Kenyatta aliomboleza kifo cha bintiye Mama Kimathi, bila kutaja mipango yoyote ambayo serikali imeweka kuisaidia familia hiyo.

Mnara wa Dedan Kimathi ulioko katika barabara ya Kimathi, Nairobi hauna maana yoyote ikiwa familia ya shujaa itaendelea kuishi katika ufukara.

Isitoshe, ujenzi wa Mnara wa Mashujaa unaendelea katika bustani ya Uhuru Gardens, Nairobi hauna maana yoyote ikiwa familia za mashujaa mbalimbali nchini zitaendelea kutelekezwa na serikali iliyoko mamlakani sasa.

Sherehe za leo Jumatano katika Uwanja wa Michezo wa Wanguru, Kaunti ya Kirinyaga hazitakuwa na maana yoyote ikiwa mashujaa hawa watamiminiwa sifa bila serikali kutangaza mipango madhubiti ya kuwasaidia pamoja na familia zao.

NGILA: Tumia ufadhili wa Google kupiga jeki biashara yako

Na FAUSTINE NGILA

IWAPO wewe ni mjasiriamali katika sekta yoyote na unatumia teknolojia, basi huna budi kutabasamu kwa kuwa kampuni ya teknolojia ya Google imejiandaa kukupiga jeki.

Kwa kutambua umuhimu wa biashara za wastani na zile ndogondogo katika ukuaji wa uchumi, kampuni hiyo imetenga Sh1 bilioni kuinua biashara hizo ambazo zilipata pigo kuu kutokana na janga la corona.

Hii ni ithibati kuwa ukitia bidii katika ubunifu wako wa kila siku, kuna manufaa fiche ambayo utakumbana nayo katika safari yako ya ujasiriamali.

Tofauti na mikopo ya benki za humu nchini ambayo hutoza riba ya juu, fedha za Google zitapeanwa kwa riba ya chini, ikizingatiwa biashara nyingi zimekuwa zikipata hasara kutokana na kuporomoka kwa uchumi.

Ni bayana kuwa wafanyabiashara wengi wamekuwa wakitumia mitandao ya kijamii na majukwaa ya kidijitali kunadi bidhaa na huduma zao, lakini wengi wamefunga biashara hizo kutokana na ukosefu wa hela za kulipia kodi na umeme.

Mataifa mengine yaliyochaguliwa Afrika ni Afrika Kusini, Ghana na Nigeria, ishara kuwa wafadhili wako tayari kuwasaidia wananchi wanaojituma kila siku katika ubunifu wa teknolojia za kuziba changamoto zilizoko katika jamii.

Kwa wale ambao kazi yao ni kulalamika kuwa hakuna ajira, sasa waanze kufikiria kuhusu kuunda suluhu za kibiashara ambazo zinaweza kuchangia katika kubuni nafasi za kazi.

Nasema hivi kwa kuwa nimetangamana na vijana wengi waliohitimu elimu ya chuo kikuu lakini uzembe wa kufikiria umewatuma kusaka ajira katika kampuni huku wengine wakisalia mitaani kulia kuwa ufisadi serikalini ndio chanzo cha wao kukosa ajira.

Nawasikitikia sana vijana wanaofikiria hivi, kwa vile wana akili shupavu na elimu ya kutosha kuwawezesha kufikiria kuhusu miradi ya ubunifu ya kukabiliana na matatizo yaliyoko katika sekta za afya, elimu, uchukuzi, mawasiliano, fedha, kilimo, mazingira, sheria na hata uvuvi.

Kwa miaka minne, wahadhiri wao hawakuwaambia kuwa lengo kuu la kwenda chuoni ni kuunda nafasi za kazi na wala si kusaka ajira, na sasa bado wanaamini kuwa ipo siku wataajiriwa.

Kulingana na jinsi kasi ya teknolojia inavyotafuna nafasi za ajira viwandani, vijana wanafaa kufikiria kuwa katika mstari wa mbele katika uundaji wa teknolojia hizo, la sivyo watasalia kulia kuwa maisha ni magumu.

Utalemewaje kusajili biashara yako ndogo wakati wafadhili wa humu nchini na kigeni wamejaa kila kona wakisubiri kuona mapendekezo yako ya bishara ili wakupe mamilioni ya ufadhili?

Umaskini miongoni mwa vijana ni wa kujitafutia kwa kuwa wako na nguvu inayohitajika, lugha ya kuandika na kuelezea mapendekezo na akili ya kusimamia biashara hadi iimarike. Lakini wengi hawataonja hata shilingi moja ya Sh1 bilioni zilizotolewa na Google.

Usiniambie eti umetoka familia maskini na uko na digrii yako pale nyumbani na huna ajira.

Gutuka usingizini, ingia kwenye intaneti, saka changamoto zinazolemea serikali na jamii, fikiria kuhusu miradi ya kumaliza matatizo hayo.

Utanishukuru baadaye kwani utafiti wako utakuelekeza kwa mchakato wa kutengeneza pendekezo ambalo utatumiwa mamilioni kwenye akaunti yako ya benki ili uunde ajira kwa wenzako waliotekwa na laana ya kutofikiria. Kazi kwako.

Watu 26 wanaoishi na ulemavu Kiambu wapokea vifaa vya kazi kutoka NFDK

Na LAWRENCE ONGARO

WALEMAVU wapatao 26 kutoka Kiambu, wamenufaika na vifaa vya kazi kutoka kwa mfuko wa Hazina ya Kitaifa Maalum kwa Watu Wanaoishi na Ulemavu (PLWDs) yaani National Fund for the Disabled of Kenya (NFDK).

Prof Julia Ojiambo, mmoja wa maafisa katika kamati ya hazina hiyo na naibu kamishna wa Thika Bw Mbogo Mathioya walihudhuria hafla hiyo.

Prof Ojiambo, alisema vifaa hivyo vya kazi kwa walemavu viligharimu takribani Sh650,000

Baadhi ya vifaa vilivyotolewa ni vya kutumika kwenye kinyozi, vifaa vya ususi, vifaa vya kazi ya useremala, cherehani za kushona nguo, na viti vya magurudumu.

Baadhi ya wanufaika wa mpango wa NFDK. Picha/ Lawrence Ongaro

Alieleza kuwa serikali imejitolea kuzunguka kote nchini kuona ya kwamba walemavu wanasaidiwa vilivyo.

“Tunatoa wito kwa walemavu popote walipo wajitokeza ili waweze kusaidiwa na serikali kupitia hazina hiyo,” alisema Prof Ojiambo.

Alitoa wito kwa walemavu popote walipo wajitokeze wazi ili serikali iweze kujali maslahi yao bila ubaguzi.

“Sisi kama wanakamata walio katika afisi ya hazina ya kusaidia walemavu tunafanya juu chini kuona ya kwamba hakuna mlemavu anabaguliwa Kwa vyovyote vile,” alifafanua Prof Ojiambo.

Alitaja baadhi ya shule ambazo wamesambaza misaada. Nazo ni Thika School for the Blind, Salvation Army, Thika JoyTown, na shule ya Maria Magdalena.

Bw David Muiruri ambaye ana ulemavu kwenye mguu wake wa kushoto, alisema azma yake imetimia kwa kupokea vifaa vya useremala.

“Ninaishukuru serikali kwa kufanya jambo la kupongezwa kwa kujali walemavu,” alisema Bw Muiruri.

Naibu kamishna Bw Mathioya aliwaonya walemavu hao wasiuze vifaa hivyo kwa manufaa yao wenyewe.

Mumepewa vifaa hivyo ili muzisaidie familia zenu, wala sio vya kuuza,” alionya afisa huyo wa wilaya.

Alisema mtu yeyote atakayepatikana ameuza vifaa hivyo atachukuliwa hatua ya kisheria.

“Tayari nimewaagiza machifu wangu wawe makini na kuhakikisha vifaa hivyo vinatumika ipasavyo,” alifafanua Bw Mathioya.

Aliwahimiza walemavu wazuru hospitali zilizo karibu nao, ili wapokee chanjo dhidi ya Covid-19.

Alisema wako katika hali hatari ya kuambukuzwa kulingana na hali yao ya kiafya na kwa hivyo wafanye hima.

Bi Purity Nguli ambaye alipokea cherehani ya kushona nguo, alipongeza serikali kwa kuwajali PLWDs.

Wanufaika waliohojiwa walisema hali yao ya maisha itabadilika kutokana na msaada ambao walipokea kutoka kwa serikali.

KWA KIFUPI: Utakufa mapema ukihifadhi mlo kwenye vifaa vya plastiki – Utafiti

Na LEONARD ONYANGO

KEMIKALI za plastiki zinazotumika kutengeneza vyombo vya kuhifadhi vyakula, vipodozi na vifaa vya watoto kuchezea (toys) zinachangia katika vifo vya mapema.

Ripoti ya utafiti uliofanywa nchini Amerika inasema kuwa vifaa hivyo vina kemikali inayojulikana kama phthalates ambayo ikiwa nyingi mwilini husababisha maradhi ya moyo.

Kemikali hizo hatari pia zinadumaza uzalishaji wa homoni na ubongo.

Tafiti za awali, zimewahi kuhusisha kemikali hizo na kutatizika kwa ukuaji wa sehemu nyeti za watoto wa kiume.

Aidha, tafiti zinasema kemikali hizo zinaweza kusababisha wanaume kuwa na mbegu hafifu, ugonjwa wa pumu (asthma), unene kupindukia (obesity), kansa na maradhi ya moyo.

Watafiti hao wanasema kuwa kemikali hizo huingia mwilini watu wanapokula vyakula vinavyohifadhiwa kwenye vifaa vya plastiki.

Watu 5,000 waliohusishwa katika utafiti huo walipatikana na kiwango cha juu cha kemikali hizo.

Watafiti hao walibaini kwamba watu walio na kiwango cha juu cha kemikali hizo wanakufa kabla ya kufikisha umri wa miaka 65.

Angwenyi sasa ataja mizozo ya ardhi kama chanzo cha mauaji ya washukiwa wa uchawi Kisii

Na CHARLES WASONGA

MBUNGE wa Kitutu Chache Kaskazini Jimmy Angwenyi amedai mzozo wa ardhi ndio ulichangia mauaji wa akina nyanya wanne katika eneo hilo Jumapili.

Akiongea na wanahabari Jumanne katika Majengo ya Bunge, Nairobi Bw Angwenyi alisema japo ilidaiwa kuwa wanne hao walikuwa washukiwa wa uchawi, wauaji hao walitaka kuwapokonya akina nyanya hao vipande vya ardhi.

“Nakubali kuwa uchawi upo katika eneobunge langu. Lakini mauaji yaliyotokea Jumapili yalichangiwa na suala la mzozo wa ardhi wala sio uchawi kama ilivyoripotiwa,” akasema huku akilaani mauaji ya akina nyanya hao.

Hata hivyo, kiongozi huyo hakutoa maelezo zaidi kuhusu kauli yake.

Bw Angwenyi aliwaonya wakazi wa eneo hilo na Wakenya kwa ujumla kukoma kuchukua sheria mikononi mwao kwa kuwaua watu kwa tuhuma za uchawi.

“Ukweli ni kwamba vitendo vya uchawi haviruhusiwi katika jamii yoyote ile lakini washukiwa wa uovu huu wanapokamatwa wanafaa kuwasilishwa kwa maafisa wa polisi ili waadhibiwe kwa mujibu wa sheria. Mungu ndiye ana ruhusu ya kutoa uhai wa mtu wala sio mtu mwingine,” akasema.

Bw Angwenyi pia alitoa wito kwa maafisa wa polisi kuchukua hatua za haraka na kuwakamata washukiwa wengine ambao bado hawajakamatwa.

“Nafurahi kuwa washukiwa wanne wamekamatwa na watafikishwa mahakamani. Naomba polisi waendelee kuwasaka wengine wengi ambao walitoroka,” akaeleza.

Jumanne washukiwa wanne; Amos Nyakundi Ondieki, Chrispine Ogeto Mokua, Peter Angwenyi Kwang’a na Ronald Ombati Onyonka walifikishwa katika mahakama moja mjini Kisii kwa ajili ya kufunguliwa mashtaka kuhusiana na mauaji hayo.

Hata hivyo, Hakimu Mkuu Mwandamizi wa Mahakama hiyo Paul Mutai hakuwaruhusu kujibu mashtaka bali aliamuru wazuiliwe katika korokoro ya polisi kutoa nafasi kwa uchunguzi zaidi kuhusu kisa hicho.

Kesi hiyo sasa itatajwa mnamo Oktoba 29, 2021 ambapo ombi la dhamana kutoka kwa washukiwa hao wanne litashughulikiwa.

Uingereza waadhibiwa vikali kwa utovu wa nidhamu wa mashabiki wao kwenye fainali ya Euro 2020

Na MASHIRIKA

TIMU ya taifa ya Uingereza imeamrishwa kusakata mechi moja katika vibarua vijavyo vya kimataifa bila mashabiki uwanjani, hiyo ikiwa sehemu ya adhabu baada ya vurugu na fujo kushuhudiwa ugani Wembley wakati wa fainali ya Euro 2020 iliyowakutanisha na Italia mnamo Julai 11, 2021.

Shirikisho la Soka la bara Ulaya (Uefa) limepokeza Uingereza adhabu nyingine ya kucheza mchuano mwingine wa kitaifa bila mashabiki katika kipindi cha miaka miwili ijayo.

Mbali na adhabu hiyo, Shirikisho la Soka la Uingereza (FA) lilitozwa faini ya Sh13 milioni kwa utovu wa nidhamu uliodhihirishwa na mashabiki wa nyumbani wa Uingereza ndani ya uwanja wa Wembley kikosi chao kilipokuwa kikivaana na Italia waliotawazwa mabingwa wa Euro hatimaye.

“Japo hatukubaliani na ukubwa wa kiwango cha adhabu hiyo kutoka kwa Uefa, tunaheshimu maamuzi yao,” ikasema sehemu ya taarifa iliyotolewa na vinara wa FA.

Ni mara ya kwanza kwa adhabu ya kiasi hicho kutolewa dhidi ya Uingereza ambao sasa watalazimika kucheza mojawapo ya mechi zao zijazo za Uefa Nations League mnamo Juni 2022 bila mashabiki uwanjani.

Chini ya kocha Gareth Southgate, Uingereza wameratibiwa kuvaana na Albania mnamo Novemba 12, 2021 kabla ya kupimana ubabe na San Marino siku tatu baadaye katika juhudi za kufuzu kwa fainali zijazo za Kombe la Dunia mnamo 2022 nchini Qatar.

Mashabiki wa Uingereza walipigana na maafisa wa usalama ugani Wembley na kuharibu mali ya thamani kubwa wakati wa fainali ya Euro 2020 iliyoshuhudia Italia wakishinda 3-2 kupitia penalti baada ya sare ya 1-1 mwishoni mwa muda wa ziada.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

PATA USHAURI WA DKT FLO: Nitashikaje mimba ya mtoto mvulana?

Mpendwa Daktari,

Nataka kushika mimba ya mtoto mvulana. Hedhi zangu za mwisho zilikamilika Oktoba 9, 2021. Nitahesabu vipi siku ambazo kuna uwezekano mkubwa?

Naomi, Nairobi

Mpendwa Naomi,

Wakati ambapo yai linatolewa hutegemea na mzunguko wa hedhi, lakini kwa kawaida huwa siku 14 kabla ya kipindi kifuatacho cha hedhi.

Kwa mfano, ikiwa mzunguko wako ni wa siku 21, utatoa mayai siku ya 7; ikiwa mzunguko wako ni wa siku 32, utatoa mayai katika siku ya 18; ikiwa mzunguko wako ni wa siku 28, utatoa mayai siku ya 14.

Hata hivyo, kwa wale ambao mizunguko yao ya hedhi si ya kawaida, ni vigumu kutabiri siku ya kutoa mayai.

Kwa wale ambao hedhi zao si za kawaida, mabadiliko ya kimazingira na kimwili pia yaweza badilisha wakati wa kutoa mayai.

Kutokana na utofauti huu, inawezekana kushika mimba wakati wowote wa mzunguko, ikiwa ni pamoja na siku ya mwisho ya hedhi.

Pia, unaweza tabiri wakati wa kutoa mayai kwa kuangalia ute kwenye lango la uzazi.

Kwa kawaida huwa mzito kisha mwepesi sawasawa na ute wa yai katika kipindi cha mayai kutoka. Njia nyingine, japo ni adimu, ni kutumia vifaa maalum vya kutambua halijoto ya sehemu ya chini ya mwili au kipimajoto cha sehemu hii (ni tofauti na vipimajoto vya kawaida).

Japo kuna nadharia nyingi kuhusu jinsi ya kubainisha jinsia ya mtoto, hazijathibitishwa kisayansi na hivyo siwezi pendekeza kwa ujasiri.

Mbinu ya Shettles inahoji kwamba, kwa sababu shahawa za mvulana (Y sperm) kwa kawaida huwa ndogo, zenye kasi na hazidumu, basi ikiwa unataka kushika mimba ya mtoto mvulana, ushiriki tendo la ndoa unapokaribia wakati wa kutoa mayai.

Hii inabidi basi uwe na kipimajoto cha mwili, vilevile vifaa vya kutabiri wakati wa mayai kutolewa ili ufuatilie mzunguko wako kwa karibu. Mtindo huu umepingwa na wanasayansi wengi.

Njia ya kipekee ya kutambua ni kwa kuchambua jinsia wakati wa kupachikwa mimba kupitia upandikizaji mimba (in vitro fertilization-IVF), ambao ni ghali mno, na uchambuzi wa shahawa haukuhakikishii kwa asilimia mia kwamba utapata matokeo unayotaka.

Aidha, mbinu hii imeibua masuala mengi ya kimaadili. Kushika mimba kwa njia ya kawaida kunakupa uwezekano wa 50-50 kupata mtoto wa jinsia unayotaka, na hiyo yatosha.

Mpendwa Daktari,

Nimekuwa nikikumbwa na upele katika sehemu kadhaa mwilini ikiwa ni pamoja na puani. Najikuna katika sehemu zilizoathirika. Je, huu waweza kuwa mzio?

Jane, Mombasa

Mpendwa Jane,

Huenda upele huu wenye mwasho unasababishwa na mzio, au pengine unatokana na matumizi ya dawa fulani; maambukizi ya ngozi; maambukizi ya helminth infection (mnyoo); kisukari; maradhi ya tezi; ugonjwa wa ini; maradhi ya figo; ugonjwa wa neva; anemia inayosababishwa na utapiamlo wa madini ya chuma; virusi vya HIV au hata wakati mwingine maradhi ya kansa.

Litakuwa jambo la busara kwenda hospitalini ili ufanyiwe chunguzi zinazohitajika.

Haya yakijiri, epuka kujikuna kila mara. Unaweza tuliza sehemu zilizoathirika kwa kuweka kitambaa kilicholoweshwa majini au hata barafu katika sehemu zilizoathirika.

Tumia sunscreen unapoenda nje kwenye jua. Tumia sabuni isiyo na harufu kali kuoga. Pia, badala ya kuoga kwa maji ya moto, tumia yale yaliyo na uvuguvugu. Tumia losheni baada ya kuoga. Usivae nguo wala kulalia malazi yaliyoundwa kwa vitambaa vinavyochochea kujikuna, kama vile sufu (wool).

Badala yake, tumia bidhaa zilizoundwa kwa kitambaa cha pamba, valia mavazi yasiyobana, kunywa maji kwa wingi na dumisha uzani ufaao.

Kuna aina ya krimu ambazo zaweza tumika kupunguza mwasho kama vile antihistamine au hydrocortisone.

Ujanja wa kahaba wazimwa na mganga

Na JOHN MUTUKU SAMUEL

DEMU aliyesifika mtaani hapa kwa ujanja wake wa kuwatapeli wanaume maelfu ya pesa baada ya kula uroda nao, alibanwa asijue la kufanya baada ya kukutana ana kwa ana na mjanja wa wajanja.

“Kisu kimegusana na mfupa! Hapa kwangu utakula huu na hasara juu. Ondoka sasa ama niambie ‘vijana’ wangu wakufanyie kazi,” demu alitishwa na jamaa aliyelenga kumpora.

Demu ambaye alikuwa akifanya kazi ya ukahaba alikuwa ametafuna pesa za wanaume kwelikweli.

Kila alipotembea na mwanamume, alimtisha kwa kisu na kudai kulipwa pesa nyingi. Mwanamume aliyekosa pesa alinyang’anywa simu au chochote cha thamani ndani ya nyumba.

Siku ya arubaini ya demu ilipofika, alikutana na polo katika baa usiku.

Walikata maji kisha polo akaamua kumpeleka kwake. Walikula uroda usiku kucha kisha alfajiri, demu akadai alipwe Sh5,000. Polo alikuwa na Sh500 pekee mfukoni.

“Nitoe wapi pesa hizo jamani? Nina Sh500 tu!” Polo alimpasulia mbarika.

“Utajua hujui! Unajua unacheza na nani wewe? Mimi huminya mwanamume akanipigia magoti na kunililia,” demu alimtisha akimrushia kofi lakini likadakwa.

“Leo umepatana na dume lisiloogopa visu wala bastola. Tazama humu kabatini. Waona nini?” polo alimfungulia kabati.

Demu alishangaa kuona mifupa mingi ya aina tofauti, jambo lililomtia woga usio wa kawaida.

“Ukiendelea kunitishatisha, hutatoka katika nyumba hii. Nitahakikisha umekuwa chizi,” polo ambaye alikuwa mganga alimlipukia demu.

Demu aliondoka polepole akafungua mlango na kutoweka bila kutazama nyuma tena.

Aliapa kutokanyaga kwa polo tena akijua fika kuwa pwagu hupata pwaguzi.

Arsenal na Palace watoshana nguvu katika gozi la EPL ugani Emirates

Na MASHIRIKA

KOCHA Patrick Vieira amesema bao la sekunde za mwisho ambalo Arsenal walifunga dhidi ya kikosi chake cha Crystal Palace katika sare ya 2-2 mnamo Jumatatu usiku ugani Emirates lilimsikitisha zaidi.

Fowadi Alexandre Lacazette alitokea benchi katika kipindi cha pili na kunyima Palace ushindi muhimu dhidi ya Arsenal waliotangulia kufunga kupitia nahodha Pierre-Emerick Aubameyang.

Chini ya kocha Mikel Arteta, Arsenal walianza mchuano huo kwa matao ya juu huku Aubameyang na Nicolas Pepe wakimfanyiza kipa Vicente Guaita kazi ya ziada.

Ingawa hivyo, Palace walirejeshwa mchezoni na Christian Benteke aliyesawazisha katika dakika ya 50 baada ya ushirikiano wake na Jordan Ayew kumwacha hoi kiungo mkabaji Thomas Partey.

Palace walipachika wavuni bao la pili katika dakika ya 73 baada ya Conor Gallagher kumpokonya Albert Sambi Lokonga mpira kirahisi na kumwandalia Odsonne Edouard pasi safi.

Nusura Kieran Tierney asawazishie Arsenal katika dakika ya 80 ila akapaisha mpira licha ya kusalia peke yake na kipa wa Palace.

“Ilikuwa vigumu kuamini. Nilisikitika sana kuhusu jinsi masogora wangu walivyolegea katika sekunde za mwisho na kuwapa Arsenal fursa ya kusawazisha,” akasema Vieira.

Matokeo hayo yaliwapaisha Arsenal hadi nafasi ya 12 kwenye msimamo wa jedwali baada ya kutandaza mechi ya sita mfululizo ligini bila kushindwa. Kwa sasa wanajivunia alama 11, tatu zaidi kuliko Palace wanakamata nafasi ya 14.

Sawa na Palace, Arsenal pia walishuka ugani wakipania kujinyanyua baada ya kuokota alama moja pekee katika mechi ya awali. Arsenal walikuwa wameambulia sare tasa dhidi ya Brighton uwanjani Amex huku Palace wakikabwa koo na Leicester City kwa sare ya 2-2 ugani Selhurst Park kabla ya kipute cha EPL kusitishwa kupisha michuano iliyopita ya kimataifa kwa mujibu wa kalenda ya FIFA.

Japo Arsenal walilemewa na Palace katika kipindi cha pili, alama 11 kutokana na mechi tano zilizopita ni ishara ya kuimarika pakubwa kwa miamba hao wa zamani wa soka ya Uingereza walioanza kampeni za muhula huu kwa kusuasua.

Ushindi uliosajiliwa na Arsenal katika mechi tatu mfululizo za EPL dhidi ya Norwich City (1-0), Burnley (1-0) na Tottenham Hotspur (3-1) mwezi uliopita ni matokeo yaliyomvunia Arteta, 39, taji la Kocha Bora wa EPL mwezi Septemba.

Ufanisi huo uliwezesha mabingwa hao mara 13 wa EPL kujiondoa katika orodha ya vikosi vitatu vya mwisho jedwalini baada ya mwanzo mbaya uliowashuhudia wakipoteza mechi tatu za ufunguzi wa msimu dhidi ya Brentford (2-0), Chelsea (2-0) na Manchester City (5-0) kwa usanjari huo.

Arteta aliyechezea Arsenal mara 150 katika kipindi cha miaka mitano (2011-2016), aliteuliwa kuwa mrithi wa kocha Unai Emery mnamo Disemba 2019 na akaongoza klabu hiyo kutwaa Kombe la FA miezi mitano baadaye.

Kufikia sasa, ni pengo la alama tatu ndilo linatamalaki kati ya Arsenal na Palace ambao chini ya Vieira, wameshinda mechi moja, kuambulia sare mara tano na kupoteza michuano miwili kati ya minane iliyopita.

Vieira, 45, aliondoka Arsenal na kuyoyomea Italia kuvalia jezi za Juventus mnamo 2005, mwaka mmoja kabla ya kikosi hicho kutoka uwanjani Highbury na kuhamia Emirates. Nyota huyo wa zamani wa Ufaransa alikuwa nahodha wa kikosi cha Arsenal kilichonyakua ufalme wa EPL bila kushindwa katika mechi yoyote mnamo 2003-04.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

TAHARIRI: Mauaji ya kiholela ya wazee yakomeshwe

KITENGO CHA UHARIRI

INASIKITISHA sana kwamba visa vya mauaji ya kiholela ya wazee vinaendelea nchini bila hatua kali kuchukuliwa dhidi ya washukiwa.

Kisa cha hivi punde ni mauaji ya watu wanne katika Kaunti ya Kisii kwa tuhuma kwamba walikuwa wachawi. Visa kama hiki vimewahi kushuhudiwa awali katika maeneo kama vile Nyamira, Kwale na Kilifi.

Cha kushangaza ni jinsi makundi ya watu hujitokeza tu na kuchukua sheria mikononi na hatimaye hawachukuliwi hatua zozote na vyombo vya dola.

Kutochukuliwa kwa hatua kumewapa ujasiri wahusika kuendeleza mauaji zaidi.

Uchunguzi katika vingi vya visa hivi umeonesha kwamba wauaji huwa na sababu fiche za kuendeleza unyama huu na badala yake uchawi hutumiwa tu kama kisingizio.

Mathalan, uhasama baina na koo pamoja na tofauti nyinginezo za kijamii ndizo huwa baadhi ya vyanzo vya mauaji haya.

Kwa mfano kumewahi kuripotiwa hali ambapo vijana huwasingizia wazee wao kuwa wachawi na kushiriki katika mauaji yao kisha wawanie mali ya urithi.

Katika kaunti ya Kwale, walengwa huwa ni wazee wenye mvi na macho mekundu.

Jamii pana haifai kunyamazia ukatili huu.

Kimya cha jamii pamoja na asasi za serikali ndicho kichocheo cha mauaji zaidi. hatua za dharura zinafaa kuchukuliwa kukomesha uhayawani huu.

Inasikitisha hata zaidi kubaini kwamba ipo sheria inayoweza kutumiwa kukabili tuhuma za uchawi au ushirikina.

Kwa mujibu wa Sheria Kuhusu Uchawi sura ya 67, ni hatia kwa mtu kujifanya kuwa na nguvu za uchawi au ushirikina, hali inayotumiwa kuwasababishia watu wengine woga au majeraha.

Mtu kama huyo atapewa adhabu ya miaka mitano gerezani. Mtu kama huyo atahukumiwa kifungo cha miaka 10 gerezani endapo atapatikana na hatia ya kumwelekeza mtu mwingine jinsi ya kudhuru mwenzake au mali yake kwa kutumia nguvu za uchawi.

Kwa upande mwingine, sheria iyo hiyo pia inasema kwamba mtu yeyote ambaye atapatikana na hatia ya kumsingizia mwenzake kuwa mchawi atatozwa faini ya Sh500,000 au asukumwe gerezani kwa miaka mitano, au adhabu zote mbili.

Maadamu sheria ya kukabili uchawi au ushirikina ipo na vile vile sheria hiyo pia inaeleza hatua ambazo wanaowatuhumu wengine kuwa wachawi ipo, ina maana kwamba polisi na jamii pana ndiyo inazembea na hivyo kuchochea mauaji ya wazee katika jamii.

Kibicho aonya wahuni wanaopanga kusambaratisha sherehe za Mashujaa Kirinyaga

Na SAMMY WAWERU

SERIKALI imetoa onyo kali kwa wahuni wanaopanga kuzua fujo wakati wa maadhimisho ya Sikukuu ya Mashujaa 2021, yatakayoandaliwa kesho Kaunti ya Kirinyaga.

Katibu katika Wizara ya Usalama wa Ndani, Dkt Karanja Kibicho ametahadharisha kwamba wenye mipango ya aina hiyo watakabiliwa kisheria.

“Tumepata habari kuna watu wanaopanga kuleta fujo, tunawaambia kuwa watu wa Kirinyaga hawatakubali na serikali haitakubali,” Dkt Kibicho akaonya.

Akitaja fujo hizo kama zinazolenga kuchochewa kisiasa, Katibu alisema serikali imepata taarifa za kijasusi wahuni hao watatolewa nje ya Kaunti ya Kirinyaga.

Rais Uhuru Kenyatta ataongoza taifa kuadhimisha sherehe hizo zitakazofanyika, katika Uwanja wa Wanguru, Kirinyaga.

Tayari kiongozi huyo wa nchi ametua katika kaunti hiyo, ambapo anaendelea kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo.

Naibu wa Rais Dkt William Ruto na kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga ambaye anaendeleza kampeni zake Meru kuwania urais 2022, pia watahudhuria.

Kufuatia athari za ugonjwa wa Covid-19, serikali imepiga marufuku hafla za maadhimisho hayo kuandaliwa katika kaunti zingine, kinyume na miaka ya awali ambapo kila kaunti imekuwa ikiandaa.

Kulingana na Dkt Kibicho, maandalizi ya hafla hiyo yamekamilika.

Awali, Mashujaa Dei ilitambulika kama Kenyatta Dei, ila ikabadilishwa chini ya Katiba ya sasa, iliyoidhinishwa 2010.

Kanu yaimarisha kampeni mashinani

ERIC MATARA na BARNABAS BII

WIKI mbili baada ya wajumbe wa Kanu kumwidhinisha kwa pamoja Seneta wa Baringo Gideon Moi kuwania urais katika chaguzi za mwaka 2022, chama hicho kimeimarisha kampeni mashinani kikilenga urithi wa Rais Uhuru Kenyatta 2022.

Huku ikiwa imejasirishwa na hatua hiyo ya hivi majuzi, Kanu imeanzisha usajili na uhamasishaji wa wanachama mashinani kote nchini kwa lengo la kuvutia umaarufu kwa mwenyekiti wake.

Wandani wa Bw Moi wanasema hatua ya kuidhinishwa kwake na Kanu ilijiri wakati mwafaka kwa sababu ilimweka katikati ya kinyang’anyiro cha kumrithi Rais Kenyatta.

Katika hafla ya kufana iliyoandaliwa Bomas of Kenya, Nairobi, wiki iliyopita, wajumbe hao zaidi ya 3,000 vilevile walimpa Seneta Moi kibali cha kwenda na kuunda miungano na vyama vingine kwa lengo la kushinda chaguzi za 2022.

Bw Moi tayari ni mwanachama wa One Kenya Alliance (OKA) ambao ni muungano unaowaleta pamoja viongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka, Amani National Congress, Musalia Mudavadi, na Ford Kenya, Moses Wetang’ula.

Taifa Leo imebaini kuwa Kanu imeanzisha misururu ya kampeni mitandaoni kote nchini katika juhudi za kupigia debe ugombeaji wa kiongozi wa chama chao kabla ya Uchaguzi Mkuu 2022.

Katibu wa Kanu Nick Salat amesema chama hicho kimeandaa kampeni zitakazofanyika kote nchini katika majuma yajayo ili kumpigia debe Seneta Moi.

“Sasa tuna mpeperushaji bendera na tunataka kuhakikisha atamrithi Rais Uhuru Kenyatta 2022. Tutaendesha shughuli za kumpigia debe kuanzia eneo la Bonde la Ufa wiki ijayo,” alisema Bw Salat.

Yamkini mikakati hiyo inanuia kukusanya Bonde la Ufa, eneo linalochukuliwa kuwa ngome ya Naibu Rais, William Ruto, kuunga mkono azma ya Bw Moi.

Taifa Leo imefahamu kuwa Kanu imebadilisha mikakati yake eneo la Bonde la Ufa na sasa inawafikia moja kwa moja wapigakura na kujadili masuala tata ikiwemo kilimo ambacho kimetawala siasa za eneo hilo ili kuwavutia wakazi kabla ya Uchaguzi Mkuu.

Katika mpango kabambe unaolenga kubadilisha mizani dhidi ya Naibu Rais ambaye amekuwa kigogo wa eneo hilo kwa muda mrefu, Kanu imebuni timu ya maafisa 18 katika viwango vya maeneobunge kuhamasisha uungwaji mkono mashinani.

DPP ataka kesi za Kimwarer, Arror ziunganishwe

Na RICHARD MUNGUTI

MKURUGENZI wa Mashtaka ya Umma (DPP), Noordin Haji sasa anataka kesi za ufisadi wa Sh63 bilioni zinazowakabili aliyekuwa waziri wa Fedha Henry Rotich na mkurugenzi mkuu wa zamani Shirika la Ustawi wa Kerio Valley (KVDA), David Kimosop ziunganishwe.

Kesi hizo mbili zinahusu kufujwa kwa pesa katika ujenzi wa mabwawa ya Kimwarer na Arror.

Katika ombi hilo, DPP amepunguza idadi ya washtakiwa kutoka 18 hadi tisa.

Pia amepunguza mashtaka kutoka 40 hadi 30.

Akiwasilisha ombi hilo, kiongozi maalum wa mashtaka, Bw Taib Ali Taib na naibu wa DPP, Bw Alexander Muteti, walimweleza Hakimu Mkuu wa mahakama ya Milimani, Bw Lawrence Mugambi, kuwa idadi ya mashahidi imepunguzwa kutoka 104 hadi 52.

“Lengo la kuwasilisha ombi hili la kuunganishwa kwa kesi hizi mbili dhidi ya Bw Rotich na Bw Kimosop ni kuhakikisha imekamilishwa kwa haraka,” alisema Bw Muteti.

Kesi hiyo itatajwa tena Oktoba 26.

Miraa: Raila aahidi kutafutia wakuzaji soko akiingia ikulu

Na MARY WANGARI

KIONGOZI wa Orange Democratic Movement (ODM) Raila Odinga ameahidi kutafutia wakulima wa miraa soko katika nchi za kigeni iwapo atachaguliwa kama rais 2022.

Waziri mkuu huyo wa zamani alisema haya Jumatatu katika Kaunti ya Meru wakati wa ziara yake ya siku tatu katika eneo la Mashariki mwa Mlima Kenya, huku Rais Uhuru Kenyatta naye akizuru Kaunti ya Kirinyaga katika maandalizi ya Sherehe za Sikukuu ya Mashujaa itakayoadhimishwa hapo kesho Jumatano.

Rais wa Malawi Lazarus Chakwera akiandamana na mkewe Bi Monica Chakwera ni miongoni mwa wageni mashuhuri wanaotarajiwa kuhudhuria sherehe za Sikukuu ya Mashujaa, kulingana na taarifa kutoka Ikulu iliyofikia Taifa Leo.

“Rais Lazarus Chakwera, akiandamana na mkewe Monica Chakwera, Mama Taifa wa Malawi, atakuwa Mgeni Mheshimiwa katika sherehe za mwaka huu za Sikukuu ya Mashujaa zitakazoandaliwa katika Uwanja wa Wang’uru, Kaunti ya Kirinyaga mnamo Jumatano, Oktoba 20, 2021,” taarifa ilisema.

Iliongeza, “Mnamo Alhamisi, Oktoba 21, 2021, Rais Chakwera na wajumbe wake watapokewa rasmi katika Ikulu, Nairobi na wenyeji wake Rais Uhuru Kenyatta na Mama Taifa Margaret Kenyatta.”

Sherehe hizo zinatarajiwa Kirinyaga huku juhudi za kuwapatanisha viongozi mahasimu kutoka eneo hilo zikishika kasi kabla ya hafla hiyo ya kitaifa.

Wakenya wanasubiri Sikukuu hiyo kwa hamu huku wengi wao wakitumai kwamba serikali hatimaye itafutilia mbali kafyu ya kitaifa iliyotangazwa katika juhudi za kukabiliana na Covid-19.

Akijibu wito huo, Kiongozi wa Taifa alidokeza kwamba serikali itaondoa kafyu hiyo hivi karibuni bila kufafanua ni lini hasa.

Mnamo Jumatatu, Rais Kenyatta alikutana na viongozi wa Kaunti ya Kirinyaga, wakiongozwa na Gavana Anne Waiguru, katika Sagana State Lodge, Kaunti ya Nyeri.

Rais Kenyatta aliwahimiza viongozi hao kuungana na kufanya kazi pamoja ili kufanikisha maendeleo ya haraka katika kaunti hiyo.

Aidha, alitahadharisha dhidi ya siasa za uongo na maneno matupu akisisitiza kuwa njia pekee ya kuwezesha ustawi ni kupitia amani na utangamano unaopatikana kupitia uongozi mwema.

Alitaja mradi wa Bwawa la Thiba unaogharimu Sh8.5 bilioni kama mojawapo ya miradi mikuu inayotekelezwa na serikali na inayotazamiwa kubadilisha uchumi wa kaunti hiyo na taifa kwa jumla.

“Tumetekeleza miradi hii kwa sababu ya ushirikiano na amani miongoni mwa viongozi ambao umehakikisha kwamba hatubadilishi tu maisha ya wakazi wa Kirinyaga ila pia raia wote wa Kenya. Wakulima wetu wa mpunga sasa wanapata bei bora kwa mazao yao. Kupitia Bwawa la Thiba tutaweza kupanua kilimo cha mpunga ili kukidhi mahitaji ya humu nchini. Tunafaa kukuza na kula kitokacho humu nchini mwetu,” alisema Rais Kenyatta.

Kuhusu zao la miraa, Kiongozi wa ODM aliapa kusuluhisha mzozo mkali kuhusu mpaka kati ya Kenya na Somalia ili kuhakikisha zao la miraa linaendelea kuuzwa katika taifa hilo la Afrika.

Aliahidi pia kutafutia zao hilo ambalo ni maarufu katika Kaunti ya Meru, soko katika mataifa ya kigeni ikiwemo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ikiwa juhudi zake za kumrithi Rais Kenyatta 2022, zitafua dafu.

“Ninajua wakulima wa miraa wamepata shida kubwa kwa kukosa soko. Soko letu la Somalia linadidimia, mara wamefunga mara wamefungua… Nitahakikisha ya kwamba Somalia inafungua mipaka yake na miraa inaenda huko. Kuna sehemu ya Somalia ambayo imekuwa huru, inaitwa Somaliland, tayari wamekubali kuchukua miraa kwetu, lakini Somalia imezuia ndege zetu kupita na kupeleka miraa huko. Tutatatua shida hiyo, ndege zetu zitoke hapa hadi zifike Somalia,” alieleza.

Bodi yasaka chanzo cha jengo kuporomoka

Na WINNIE ONYANDO

BODI ya wahandisi nchini (EBK) inaendelea kuchunguza mkasa wa kuporomoka kwa jengo mjini Ruiru, Kaunti ya Kiambu wikendi, huku ikiwaonya wakandarasi wasiotumia vifaa thabiti katika ujenzi.

Bodi hiyo pia imesema itayaondoa kwenye orodha majengo yote yanayoendelea kujengwa nchini, ikiwa hayatasajiliwa ifikapo mwisho wa Novemba.

Akizungumza na wanahabari Jumatatu, Mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Kitaifa ya Ujenzi (NCA), Bw Maurice Akech, alitoa wito kwa wakandarasi wote wafanye usajili wa haraka kwa majengo yote yanayoendelea kujengwa kabla ya ukaguzi kuanzishwa rasmi.

Mshukiwa wa mauaji ya Tirop kuzuiliwa siku 20

Na TITUS OMINDE

MSHUKIWA mkuu katika mauaji ya mwanariadha chipukizi, Agnes Tirop atazuiliwa kwa siku 20 katika kituo cha polisi cha Eldoret baada ya mahakama kukubali ombi la kumzuilia ambalo liwasilishwa katika mahakama ya Iten na maafisa wa jinai.

Hakimu mkuu mwandamizi wa Iten, Charles Kutwa alitoa agizo hilo baada ya mshukiwa huyo, Ibrahim Rotich kufikishwa mahakamani mjini Iten, Jumatatu.

Rotich anashukiwa kumuua Bi Tirop Jumatano wiki jana.

Mshukiwa huyo alifikishwa kortini mwendo wa saa tatu unusu asubuhi chini ya ulinzi mkali wa zaidi ya maafisa 10 wa polisi, ambao walikuwa wamejihami.

Kulitokea kizaazaaa katika lango la mahakama hiyo, pale umati wa wananchi wenye ghadhabu ulipotaka kuruhusiwa ndani ya mahakama ili kujionea mshukiwa huyo.

Maafisa wa polisi walilazimika kuzuia raia kuingia kortini humo, ila waliruhusu tu mawakili na wanahabari kwa kuhofia usalama wa mshukiwa.

Hakimu Kutwa aliamuru mshukiwa azuiliwe katika kituo cha polisi cha Eldoret kwa siku 20, ili kufanikisha uchunguzi kabla ya kusomewa mashtaka husika.

Vile vile mahakama iliamuru mshukiwa kufikishwa hospitalini ili kufanyiwa uchunguzi wa kiakili, kubaini iwapo atafunguliwa mashtaka ya muaji.

“Kwa kuwa hili ni suala linalohusu kesi ya mauaji, ninaelekeza kwamba litajwe katika Mahakama Kuu ya Eldoret hapo Novemba 9 kwa maagizo zaidi,” aliamuru hakimu.

Agizo hili lilitokana na ombi la Mkurugenzi Mwandamizi wa Mashtaka ya Umma, Judith Ayuma, ambaye aliambia mahakama kuwa uchunguzi wa polisi bado haujakamilika.

Polisi wanalenga kuwakamata washukiwa zaidi kuhusiana na mauaji hayo.Kwa mujibu wa polis, mshukiwa huyo mkuu katika mauaji hayo, alikamatwa Alhamisi katika eneo la Changamwe Kaunti ya Mombasa, wakati akijaribu kukimbilia nchi jirani.

Turkana kifua mbele katika usajili wa kura

Na KENYA NEWS AGENCY

KAUNTI ya Turkana imeorodheshwa ya kwanza nchini katika shughuli inayoendelea ya usajili wa wapigakura.

Kulingana na ripoti ya hivi punde ambayo Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ilitoa mnamo Oktoba 16, 2021, kaunti ya Turkana imesajili wapigakura wapya 10,539 kutoka kwa wapigakura 62,500 waliolengwa.

Hii ni sawa na kiwango cha ufanisi usajili cha asilimia 16.9

Meneja wa Uchaguzi katika kaunti ya Turkana George Oyugi alisema licha ya kwamba tume hiyo imefikia idadi hiyo ya usajili, uhamasisho duni na ukosefu wa usaidizi kutoka kwa viongozi, utaathiri kuafikiwa kwa lengo hilo.

“Nawaomba viongozi kujitokeza wawahimize watu wajitokeze ili tuweze kuwasajili wote waliosalia ndani ya wiki mbili zilizosalia. Watu wasisubiri hadi dakika za mwisho,” akasema Bw Oyugi.

Meneja huyo wa Uchaguzi pia alisema idadi kubwa ya watu hawana vitambulisho vya kitaifa licha ya kwamba baadhi ya stakabadhi hizo zimetengenezwa.

Bw Oyugi, alitoa wito kwa Shirika la Usajili wa Watu (NRB) katika kaunti ya Turkana liwasilishe vitambulisho kwa wenyewe ili waweze kujisajili kuwa wapigakura.

Alitoa wito kwa viongozi wa serikali ya Turkana kusaidia IEBC kufikia lengo la usajili wa wapigakura.

Bw Oyugi alisema serikali zingine za kaunti zinashirikiana na IEBC kwa kuwasafirisha watu katika vituo vya usajili pamoja na kutoa uhamasisho kuhusu zoezi hilo.

“Viongozi wa kaunti ya Turkana wanafaa kuiga mfano wa kaunti hizi. Inavunja moyo kwamba viongozi wa hapa hawajitokeza kupiga jeki shughuli hii,” akalalamika afisa huyo.

Wanaotaka ugavana wamsuta Wetang’ula kupendekeza Lusaka

Na BRIAN OJAMAA

WANASIASA wanaolenga kuwania ugavana Kaunti ya Bungoma, wamemtaka Seneta Moses Wetang’ula, kukoma kuelekeza wakazi kuhusu mgombea wanayefaa kuchagua katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2022.

Wakiongozwa na Bw Zacharia Baraza, walilalama kuwa watu ambao wamekuwa wakipendekezwa kwa wadhfa huo hugeuka kuwa watepetevu katika utendaji kazi wao.

Akiongea Jumatatu mjini Bungoma, Bw Baraza alisema wakazi wanafaa kuachwa wajiamulie wawaniaji wa ugavana wanaowataka.

“Mnamo 2013, Wetang’ula alimleta Spika wa sasa Seneti, Bw Ken Lusaka kwa sababu waligawana vyeo katika kaunti kwa usawa. Baadaye alimtupa mnamo 2017 na akamleta Bw Wycliffe Wangamati ambaye tena amemtelekeza kwa kuamua kuunga mkono Bw Lusaka,” akaeleza Bw Baraza.

Mwanasiasa huyo, alidai Bw Wetang’ula ndiye wa kulaumiwa kwa ukosefu wa maendeleo katika Kaunti ya Bungoma “kwani huleta magavana wasio wachapa kazi.”

Ni hatia kumsingizia mtu kuwa mchawi

Na WAANDISHI WETU

HUKU visa vya wazee kwa tuhuma za uchawi vikiendelea kukithiri haswa katika kaunti ya Kwale, Kilifi na Kisii, imebainika kuwa watu wanaotekeleza vitendo hivyo wanavunja sheria yenye adhabu kali.

Kulingana na sheria iliyopo sasa yeyote ambaye atapatikana na hatia ya kumsingizia mwenzake kuwa mchawi atatozwa faini ya Sh500,000 au asukumwe gerezani kwa miaka mitano, adhabu zote mbili.

Hii ni kulingana na Sheria za Kuhusu Uchawi sura ya 67 ambayo pia inaharamisha vitendo vya uchawi au ushirikina.

“Mtu yeyote ambaye atamtuhumu mwenzake kuwa mchawi au kuendesha shughuli za uchawi bila kutoa ithibati atakuwa ametenda kosa na atatozwa faini isiyozidi Sh500,000 au kifungo kisichozidi miaka mitano gerezani au adhabu zote mbili,” inasema sheria hiyo katika ibara yake ya sita.

Kulingana na sheria ni hatia kwa mtu kujifanya kuwa na nguvu za uchawi au ushirikina ambayo hutumia kuwasababishia watu wengine woga au majeruhi. Mtu kama atapewa adhabu ya miaka mitano gerezani.

Isitoshe, mtu kama huyo atahukumiwa kifungo cha miaka 10 gereza endapo atapatikana na hatia ya kushauri mtu mwingine jinsi ya kudhuru mwenzake au mali yake kuwa kutumia nguvu za uchawi.

Lakini licha ya kuwepo kwa sheria hii maafisa wa usalama hawajawashtaki watu wanaowaua wazee kwa tuhuma za uchawi.

Kwa mfano katika kaunti ya Kwale, jumla ya wazee 12 wameuawa kwa tuhuma za kuwa wachawi kuanzia Januari mwaka huu.

Akithibitisha visa hivyo, Kamishna wa Kaunti ya Kwale Josepha Kanyiri, Jumatatu alisema visa hivyo vimekithiri zaidi katika maeneo bunge ya Lunga Lunga na Kinango.

Aliongeza kuwa wazee wenye mvi na macho mekundu ndio hulengwa zaidi haswa na makundi ya vijana, wengine wakitoka familia zao.

“Uchunguzi wetu umebaini kuwa wazee wanaolengwa ni mwenye umri wa zaidi ya miaka 70 kwenda juu; wengi wakiwa ni wale ambao wamemea mvi. Inasikitisha kuwa mauaji hayo yanatekelezwa na watu wa familia za wahasiriwa,” akasema Bw Kanyiri.

Kamishna huyo alikariri kuwa ni kinyume cha sheria kwa mtu yeyote kumsingizia mzee kuwa mchawi au mshirikina akisema “kuota mvi au kuwa na macho mekundi sio ithibati kuwa mtu ni mchawi.”

Katika eneo bunge la Rabai, kaunti ya Kilifi Mzee Mwinga Lwambi Mwinga, 69, akishambuliwa na kuuawa Jumapili usiku na watu wasiojulikana kwa tuhuma za uchawi.

Kulingana na polisi, visa 67 vya mauaji ya wazee viliripotiwa mwaka uliopita na inahofiwa idadi itaongezeka mwaka huu.

Katika kaunti ya Kisii, wazee waliuawa mwishoni mwa wiki kwa madai ya kuwa wachawi.

Kulingana na kamishna wa kaunti ndogo ya Marani Patrick Murira, wanne hao wanawake watatu na mwanamume mmoja walidaiwa kumroga mwanafunzi mmoja ambaye ni mtahiniwa wa mtihani wa kidato cha nne (KCSE).

RIPOTI ZA: SIAGO CECE, MAUREEN ONGALA, WYCLIFFE NYABERI na CHARLES WASONGA

ODONGO: Tusifuate vyama 2022 ila falsafa za wawaniaji

Na CECIL ODONGO

CHAGUZI ndogo ambazo zimefanyika nchini tangu 2017 zimeonyesha kuwa Wakenya hufanya maamuzi bora na kutofuata mawimbi ya vyama vikubwa jinsi inavyokuwa wakati wa uchaguzi mkuu.

Upigaji kura katika chaguzi ndogo ambazo zimefanyika mara nyingi umedhihirisha kuwa wananchi wanapigia kura kiongozi kutokana na falsafa yake wala si kutokana na chama chake.

Tatizo pekee ni kuwa wengi huwa hawajitokezi kutekeleza wajibu wao wa kidemokrasia ikilinganishwa na uchaguzi mkuu.

Wiki jana, wakazi wa wadi ya Nguu/Masumba walipuuza umaarufu wa chama cha Wiper katika eneo la Ukambani na kumpigia kura mwaniaji huru Timothi Maneno huku mgombeaji wa chama cha Wiper, Eshio Mwaiwa akimaliza katika nafasi ya tatu nyuma ya mwaniaji wa UDA pia.

Uamuzi huo wa raia uliafikiwa licha ya vigogo wa Muungano wa OKA, Bw Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi na Moses Wetang’ula, wiki jana kukita kambi katika wadi hiyo wakiwarai raia wampigie kura Bw Mwaiwa.

Bw Maneno alikuwa akiungwa mkono na Gavana wa Makueni Prof Kivutha Kibwana na wanasiasa ambao ni mahasimu wa Bw Musyoka katika kupigania ‘ufalme’ wa kisiasa za Ukambani.

Wengi wa wapigakura wa Nguu/ Masumba walisema kuwa walimchagua Bw Maneno ambaye amewahi kuhudumu kama diwani wao, kulingana na rekodi yake ya maendeleo wala hawakuwa wakizingatia umaarufu wa chama cha Wiper.

Vivyo hivyo, ODM imewahi kupitia masaibu kama ya Wiper mnamo 2019, mwaniaji wake Chris Karan alipobwagwa na mbunge wa sasa David Ochieng’ katika uchaguzi mdogo wa eneobunge la Ugenya.

Hii ni licha ya kinara wa chama hicho, Bw Odinga na wanasiasa wengine wakati huo, kumvumisha Bw Karan kama mwaniaji bora baada ya ushindi wake kufutwa 2017 kortini.

Katika ngome ya Bw Odinga ya Pwani, mwaniaji huru Feisal Bader alimbwaga Omar Boga wa ODM mnamo Disemba 2020.

Mnamo Mei 2021, Bw George Koimburu, kwa chama cha People Empowerment Party (PEP) alishinda kiti cha eneobunge la Juja licha ya serikali na baadhi ya viongozi wa Jubilee kumpigia kampeni kali mwaniaji wao Susan Waititu.

Ingawa hivyo, kuna baadhi ya chaguzi ndogo ambazo raia waliwachagua viongozi kwa msingi wa vyama kama ushindi wa Majimbo Kalasinga (Kabuchai), Agnes Kavindu (Machakos) na Pavel Oimeke (Bonchari).

Mara nyingi Wakenya wameonyesha ukomavu zaidi wanapowachagua viongozi katika chaguzi ndogo kuliko uchaguzi mkuu.

Mtindo huu unafaa kuendelea hata 2022 kwa kuwa utasaidia katika kuwachagua wanasiasa ambao wanazingatia maslahi ya raia.

Baadhi ya wanasiasa ambao walichaguliwa 2017 kutokana na mawimbi ya vyama hawajatimiza ahadi walizotoa kwa wapigakura na sasa wanatumai kuwa watatumia umaarufu wa wa vyama vyao 2022 kurejea tena mamlakani.

Hii ndiyo maana sasa wanajigawanya katika mirengo jinsi ilivyoripotiwa kuwa baadhi ya wanasiasa washajitengea vyeo wanavyolenga kuvitwaa kupitia ODM katika Kaunti ya Siaya 2022.

Imani ya wanasiasa hawa ni kuwa hawatapoteza uchaguzini baada ya kupokezwa tiketi ya ODM.

Ni vyema iwapo wapigakura watamakinika zaidi jinsi wanavyofanya katika chaguzi ndogo kisha kuwapa nafasi za uongozi wanasiasa bora 2022.

Wapigakura wasikubali kushawishiwa kuwapigia kura wanasiasa wa vyama vikubwa kama ODM na UDA 2022 iwapo kwa mtazamo wao wanawaona kama wanasiasa ambao hawatawawajibikia kwa kuwapa miradi.

Vyama hivi vikubwa huwa pia vinaendeleza ubaguzi wakati wa uteuzi, kwa hivyo ni aula raia wamfuate kiongozi bora hata kama watahamia vyama vingine au kugombea kama wawaniaji huru

Maswali Ruto akiidhinisha wawaniaji ugavana Pwani

Na WAANDISHI WETU

CHAMA cha United Democratic Alliance (UDA) kinachoongozwa na Naibu Rais William Ruto, kina kibarua kizito kuamua watakaowania uongozi wa kaunti za Pwani katika uchaguzi ujao.

Licha ya chama hicho kuhakikishia wanasiasa mara kwa mara kwamba kutakuwa na haki kuchagua wagombeaji wa UDA, Dkt Ruto aliidhinisha wazi baadhi ya wanasiasa wanaotaka kuwania ugavana wakati wa ziara yake Pwani.

Chama hicho kimefanya mkutano na wagombeaji watarajiwa leo Jumatatu jijini Mombasa, na inatarajiwa kwamba maafisa wa chama wamejitahidi kutuliza wasiwasi kuhusu uwezekano wa mapendeleo katika mchujo.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Dkt Ruto alimwidhinisha Naibu Gavana wa Kwale, Bi Fatuma Achani, kurithi kiti cha Gavana Salim Mvurya. Wawili hao walichaguliwa kupitia kwa Jubilee.

Ijapokuwa Bi Achani alihudhuria mkutano ulioongozwa na Dkt Ruto, hakutangaza kujiunga na UDA.

Tikiti hiyo inawaniwa pia na Bw Mangale Lung’anzi.

“Namshukuru Mama Achani kwa sababu yeye atashikilia ile kazi ambayo ndugu yangu Mvurya amefanya. Sisi wote tunasema kazi iendelee,” akasema naibu rais.

Bw Mvurya ni mmoja wa magavana watatu wanaotumikia kipindi cha pili katika ukanda huo, wengine wakiwa ni Hassan Joho (Mombasa) na Amason Kingi (Kilifi).

Katika Kaunti ya Mombasa, Dkt Ruto alimwidhinisha aliyekuwa seneta Hassan Omar kuwania ugavana kupitia kwa UDA alipohutubu katika uwanja wa Allidina.

Baadhi ya wafuasi wa chama hicho humtaka Mbunge wa Nyali, Bw Mohamed Ali, ndiye apeperushe bendera ya UDA katika kinyang’anyiro hicho.

“Sisi kama mahasla Kenya nzima, tumejipanga kupambana na mabepari na mabwanyenye. Ni sisi mahasla ambao tutahakikisha tumeleta mabadiliko ya kiuchumi kwa manufaa ya kila Mkenya,” Bw Omar alisema Jumapili.

Mbunge wa Malindi, Bi Aisha Jumwa, kufikia sasa ndiye anayetarajiwa kuwa mgombeaji ugavana Kilifi kupitia UDA.

Hata hivyo, bado anakumbwa na kesi zinazohusu madai ya kushiriki ufisadi na mauaji, hali inayotishia azimio lake iwapo masuala hayo yatatumiwa dhidi yake na wapinzani.

“Tuingie katika mambo muhimu ambayo yanatuumiza. Kwanza tuwekane wazi kuhusu njaa hapa Kilifi, hatujawahi kuona gavana Amason Kingi hata siku moja akija mahali hapa na kuwauliza wala kuwaletea chochote,” alisema Bi Jumwa, wakati wa mkutano wa UDA Kilifi.

Katika Kaunti ya Lamu, mwanzilishi wa shirika la kutoa misaada ya kimatibabu la Safari Doctors, Bi Umra Omar ndiye ameonyesha nia ya kuwania ugavana kupitia kwa UDA.

Dkt Ruto alipokuwa Kaunti ya Taita Taveta, imebainika alikutana na aliyekuwa Gavana John Mruttu na Bw Stephen Mwakesi ambao wote wanawania tikiti ya UDA wakitaka kumwondoa Gavana Granton Samboja mamlakani.

Duru zilisema mkutano huo ulinuiwa kuwapatanisha ili kuwe na mgombeaji mmoja, kuzuia mpasuko chamani.

Hata hivyo, mratibu wa UDA katika kaunti hiyo, Bw Scaver Masale, alisema hakuna aliyeshinikizwa kuweka kando maazimio yake ili kuunga mkono mwenzake.

Katika mahojiano ya awali, Mbunge Mwakilishi wa Wanawake kaunti hiyo, Bi Lydia Haika, alisema kuna mazungumzo yanaendelea ili Mabw Mruttu na Mwakesi wakubaliane kushirikiana.

“Wakishindwa kukubaliana basi watalazimika kuingia katika kura ya mchujo ambayo itakuwa huru na wa haki,” Bi Haika aliambia Taifa Leo.

Ripoti za Siago Cece, Alex Kalama, Lucy Mkanyika na Valentine Obara

TANZIA: Colin Powell afariki

Na AFP

WASHINGTON, Amerika

MWEUSI wa kwanza kabisa kuwahi kuwa Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Amerika, Colin Powell alifariki Jumatatu kutokana na kile kilichotajwa kama changamoto za Covid-19.

Kulingana na taarifa kutoka kwa familia yake iliyotumwa kupitia mtandao wa Facebook, Powell aliyekuwa na umri wa miaka 84, alikuwa amepewa chanjo.

“Tumempoteza mume mzuri, baba na babu,” familia yake ikisema.

Poweli ndiye mtu mashuhuri wa hivi punde kufariki kutokana na ugonjwa wa Covid-19 ambao umesababisha maafa makubwa kando na kuvuruga chumi za mataifa ya ulimwengu kwa ujumla.

Marehemu anakumbukwa kwa kuongoza vita vya Ghuba mnamo mwaka wa 1991. Vita hivyo, vilimpa Powell umaarufu mkubwa kiasi kwamba wakati mmoja alidhaniwa angefaulu kuchaguliwa Rais wa kwanza mweusi Amerika.

Hata hivyo, miaka ya baadaye alitupilia mbali wazo la kuwania urais, akatofautiana na chama chake cha Republican na kuunga mkono azma ya Barack Obama.

Powell alizaliwa mnamo Aprili 5, 1937 katika mji wa Harlem.

Alilelewa na kusoma jijini New York hadi akapata shahada katika taalamu ya sayansi ya ardhini (Geology).

Alihudumu katika jeshi la Amerika na kupanda cheo hadi kuwa Luteni Jenerali. Aliwahi kuhudumu katika mataifa kama vile Ujerumani, Vietnam, miongoni mwa mengine.

Tafsiri: CHARLES WASONGA

‘Kenya imefanikiwa kuwakabili kikamilifu nzige waharibifu’

Na SAMMY WAWERU

KENYA imefanikiwa kukabili kikamilifu nzige waharibifu, serikali imetangaza.

Tangazo hili limejiri miaka miwili baada ya Kenya hasa maeneo kame kuvamiwa na nzige, 2019 na 2020.

Katibu katika Wizara ya Kilimo, Mifugo na Samaki Prof Boga Hamadi alisema wadudu hao wamekabiliwa chini ya athari haba kwa mimea, malisho ya mifugo na kwa mazingira.

Akizungumza jijini Nairobi, Prof. Boga alisema hatua hiyo imefanikishwa kwa ushirikiano wa karibu na Shirika la Chakula na Kilimo (FAO-UN) na Benki Kuu ya Dunia.

“Ninathibitisha kuwa Kenya sasa ni salama, haina nzige,” katibu akaambia Taifa Leo kupitia mahojiano katika Kilimo House, Nairobi.

Hata hivyo, alidokeza kwamba nchi jirani ya Somalia na Ethiopia baadhi ya maeneo yamethibitishwa kuvamiwa na nzige.

“Tupo makini kama taifa wadudu hao wasirejee,” Prof Boga akaahidi.

“FAO kwa ushirikiano na Benki Kuu ya Dunia inaendelea kutoa msaada kukabili wadudu hao Somalia na Ethiopia,” akasema.

Zaidi ya kaunti 32 zilikumbwa na nzige hao waharibifu, ambao walivamia mimea na malisho ya mifugo.

ONYANGO: Mchujo ufanywe siku moja kubana nje wanaorukaruka

Na LEONARD ONYANGO

PENDEKEZO la Msajili wa Vyama vya Kisiasa, Bi Anne Nderitu, kwamba vyama vya kisiasa viandae kura za mchujo siku moja ili kufungia nje wanasiasa walio na mazoea ya kuruka kutoka chama kimoja hadi kingine baada ya kubwagwa, linafaa kuungwa mkono.

Hatua ya wanasiasa kukimbilia vyama vingine baada ya kushindwa katika kura za mchujo, imetia doa siasa za humu nchini.

Kufanyika kwa mchujo siku moja kutapunguza joto la kisiasa ambalo huletwa na kura hizo katika baadhi ya maeneo nchini.

Japo wanasiasa hao wana uhuru wa kisiasa wa kujiunga na chama chochote wapendacho, kutangatanga huko baada ya kubwagwa ni ithibati tosha kwamba siasa za humu nchini hazijakomaa na wanasiasa wanaongozwa masilahi yao ya kibinafsi na wala si sera.

Ulafi huo ndio umefanya karibu kila mwanasiasa anang’ang’ania kuunda chama chake.Kufikia sasa, Kenya ina vyama vya kisiasa 75 ambavyo vimesajiliwa kikamilifu.

Vyama 10 vimetuma maombi ya usajili na vingine 22 vimepewa cheti cha muda vikiendelea na harakati za kusajiliwa kikamilifu.Chama kinafaa kuongozwa na sera na wala si uchu wa vyeo.

Kwa mfano, hakuna tofauti ya sera baina ya chama cha ODM chake Raila Odinga na United Democratic Alliance (UDA) cha Naibu wa Rais William Ruto.

Ni vigumu kutofautisha sera zao ambazo wamekuwa wakieleza Wakenya katika kampeni zao ambazo wamekuwa wakifanya katika maeneo mbalimbali nchini.

Bw Odinga akiondoka ODM huo ndio utakuwa mwisho wa chama cha Chungwa kwani wanachama wote wataondoka na kumfuata anakoenda.

Kadhalika, Dkt Ruto akiondoka UDA, huo ndio utakuwa mwisho wa chama hicho cha Wilibaro.

Wanasiasa wanaodai kuwa wanachama wa UDA hawaamini chochote ndani ya chama hicho. Hiyo ndiyo maana mbunge wa Kandara Alice Wahome, miezi michache iliyopita alishindwa kuelezea maana ya mfumo wa ‘Bottom Up’ ambao Dkt Ruto amekuwa akidai kuwa utaangamiza umaskini unaohangaisha zaidi ya asilimia 90 ya Wakenya.

Katika ripoti yake iliyotolewa hivi karibuni, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) pia inalalamikia idadi kubwa ya wawaniaji wa kujitegemea kama moja ya changamoto kuu zinazotatiza maandalizi yake.

Katika uchaguzi wa 2017, wawaniaji 3,752 wa kujitegemea waliwania viti mbambali kama wagombea wa kujitegemea. Kati yao 2,918 waliwania udiwani huku 605 wakigombea ubunge.

Lakini idadi kubwa ya wawaniaji hao wa kujitegemea waligura vyama baada ya kushindwa katika kura za mchujo.Kuna haja ya kubadilisha sheria itakayozuia wanasiasa kuhama vyama vyao mwaka mmoja kabla ya uchaguzi mkuu ili kudumisha nidhamu vyamani.

Wanaotaka kuwania kama wagombea wa kujitegemea pia wanafaa kutangaza msimamo mwaka mmoja kabla ya uchaguzi mkuu.