Habari

Helb yafafanua alichomaanisha Waziri Amina Mohamed

February 22nd, 2019 1 min read

Na CHARLES WASONGA

BODI ya kutoa Mikopo kufadhili Elimu ya Juu (Helb) imethibitisha kuwa itatumia maafisa wake kuwaandamana walionufaika kwa mikopo yake lakini wanaonekana kukwepa kulipa; na wala sio maafisa wa polisi.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari Ijumaa, Afisa Mkuu Mtendaji wa bodi hiyo Charles Ringera amesema habari zilizosambaa kwamba bodi hiyo itatumia polisi kuwaandama waliofeli kulipa madeni waliyopewa zilieleweka visivyo.

Waziri wa Elimu Amina Mohamed alinukuliwa akisema kuwa Helb itasaka usaidizi wa maafisa wa usalama katika jitihada zake za kusaka wale ambao wameajiriwa lakini hawataki kuwajibika kwa kulipa madeni waliyopewa.

“Tutashirikiana na maafisa wa usalama kuwatafuta wale ambao wameajiriwa lakini wanajivuta kusimama ili wahesabiwe kama wananchi wawajibikaji wanaolipa madeni yao,” Bi Mohamed akasema Jumatano wakati wa uzinduzi wa mpango wa Helb kati ya mwaka wa 2019 hadi 2023 jijini Nairobi.

Matamshi yake yaliibua mjadala mkubwa katika mitandao ya kijamii huku wanasiasa na wananchi kwa ujumla wakisema ukosefu wa ajira ndio sababu inayofanya watu hao kukosa kulipa mikopo ya Helb.

Idhini

Hata hivyo, akikana madai kuwa bodi hiyo itatumia polisi kusaka watu hao Bw Ringera alisema sheria ya Helb inaipa bodi hiyo idhini ya kutumia maafisa wake kuwafuata wale waliofeli kulipa mikopo yao kimakusudi.

“Kwa kusema maafisa wa usalama, Waziri Mohamed alimaanisha maafisa wetu. Sehemu ya 15 ya Sheria ya Helb ibara ya 2 inaipa bodi hii mamlaka ya kuwatumia maafisa wake kuwaandama wale ambao wameajiriwa lakini wanafeli kulipa madeni yao,” akasema Bw Ringera.

Waziri Mohamed alisema kuwa bodi ingali inadai jumla ya Sh7.2 bilioni kutoka kwa jumla ya watu 74,000 ambao wamekosa kulipa madeni waliopewa kufadhili masomo yao katika vyuo vikuu miaka ya nyuma.