Habari Mseto

Baraza jipya la wazee kubuniwa Mlima Kenya

July 19th, 2020 1 min read

Na Gakuu Mathenge

BARAZA jipya la wazee wa jamii ya Wakikuyu latarajiwa kuzinduliwa wiki hii kumsaidia Rais Uhuru Kenyatta ambaye anakumbwa na misukosuko ya kisiasa katika ngome yake.

Kumekuwa na mgawanyiko wa viongozi katika eneo la Kati, wakati ambapo Rais anahitaji uungwaji mkono kuacha sifa bora atakapokamilisha hatamu yake ya uongozi 2022 na vile vile kutekeleza Mpango wa Maridhiano (BBI).

Baraza hilo jipya linatarajiwa kuunganisha mabaraza yote ambayo yako katika jamii za Gikuyu, Embu na Meru (GEMA).

Hii inalenga kufanya kuwe na sauti imara mashinani ya kutetea maazimio ya Rais Kenyatta, na kukabili pingamizi kutoka kwa wandani wa Naibu Rais William Ruto katika eneo hilo.

Wawakilishi wa Baraza la Wazee wa Kikuyu (KCE), Njuri Ncheke, Kiama Kia Ma na makundi mengineyo yamekuwa yakikutana kuandaa uzinduzi wa baraza jipya Alhamisi.

‘Tumeonelea hatua hii ni muhimu baada ya wazee kutambua kuwa wanasiasa tuliowatuma bungeni wamemsaliti Rais ambaye ndiye kiongozi wetu,’ akasema Katibu Mkuu wa KCE, Bw Peter Munga.

Mkutano wa maandalizi ulihudhuriwa pia na Mzee Phares Ruteere ambaye ni afisa wa ngazi ya juu katika Njuri Ncheke.