Habari za Kitaifa

Ruto amuomboleza Hakimu Kivuti muda mfupi baada ya kurejea nchini


RAIS William Ruto amemuomboleza Hakimu Mkuu Monica Kivuti ambaye aliaga dunia Jumamosi kutokana na majeraha ya risasi aliyopata baada ya kushambuliwa na afisa wa polisi kortini.

Kwenye taarifa Jumatatu, muda mfupi baada ya kuwasili nchini kutoka ziara nchini Italy na Uswizi, Rais alitaka polisi kulinda wahudumu wa mahakama, akisema kilichomtendekea Bi Kivuti hakikubaliki “na hakipaswi kutokea tena.”

“Naungana na familia, marafiki na idara ya sheria kuomboleza kifo cha kikatili cha Bi Monica Kivuti, ambaye alikuwa Hakimu Mkuu wa Mahakama ya Makadara. Kushambulia, kutishia afisa yeyote wa mahakama haikubaliki, ni kinyume cha sheria na ni tishio kwa utawala wa kisheria nchini,” akasema Dkt Ruto.

Alisema uwepo wa polisi ni kwa ajili ya kuhakikishia Wakenya usalama wao wakati wote.

“Kusiwasi kutokea hali kwamba wanatelekeza hili jukumu lao au kugeuka na kuwa tishio kwa usalama wa umma,” akasema.

“Tumepoteza mhudumu wa mahakama aliyekuwa na msimamo thabiti, aliyefanya kazi kwa bidii na aliyetumikia Wakenya kwa kujitolea. Bado alikuwa na mengi ya kuifaa nchi hii. Naomba Mwenyezi Mungu awape nguvu ya kuhimili pigo hili na kuwafariji,” akasema Bw Ruto.

Wakati huo huo, Inspekta Jenerali wa Polisi Japhet Koome ameahidi kutoa ulinzi kwa maafisa wote wa mahakama.