Wanahabari wa bungeni wachagua viongozi wapya
Na CHARLES WASONGA
CHAMA cha wanahabari wanaoripoti masuala ya bungeni (KPJA) Ijumaa kiliandaa uchaguzi wa viongozi wake wapya ambapo ripota wa gazeti la The Standard Moses Njagi alichaguliwa kuwa mwenyekiti.
Bw Njaji ambaye alipata kura 26 alifuatwa kwa umbali na ripota wa runinga ya Citizen Stephen Letoo aliyezoa kura nane. Wa tatu alikuwa mwenzao wa runinga ya KBC Kevin Wachira aliyepata kura tano pekee.
Bi Halima Osman, mwanahabari wa redio ya Baraka FM naye alichaguliwa bila kupingwa, kuwa naibu mwenyekiti katika uchaguzi huo ulioendeshwa katika majengo ya bunge, Nairobi.
Wadhifa wa katibu mkuu nao ulivutia wagombeaji wawili; Bi Elizabeth Mutuku wa idhaa ya Kikristo, ATG Radio, na mwenzake Edward Kabasa, mtangazaji wa runinga ya KBC. Bi Mutuku alipata ushindi mkubwa kwa kujizolea kura 30 huku Kabasa akipata kura tisa.
Na wadhifa wa katibu mratibu ilimwendea James Murimi wa gazeti la The People Daily aliyepata ushindi kwa njia rahisi baada ya Hillary Mageka wa gazeti la Xnews kujiondoa kinyang’anyironi.
Baada ya kukamilika kwa zoezi hilo, lililosimamiwa na Afisa Mshirikishi wa Wanahabari Bungeni Washington Otiato, walioshindwa walikubali matokeo hayo, na kuwapongeza washindi huku wakiahidi kushirikiana nao kusukuma gurudumu la KPJA.
“Pongezi mwenyekiti. Nimekubali kwamba ulikuwa na ushawishi mkubwa na kunishinda. Sasa tufanye kazi pamoja kwa manufaa ya KPJA,” Bw Letoo akamwambia Bw Njagi huku akimsalimia kwa furaha.
Bw Wachira naye alimpiga Njagi pambaja akimwambia, “Pongezi Kaka. Ushindi wako ni wa kweli. Sasa kazi kwako…sote tutashirikiana nawe kuhakikisha kuwa KPJA imefikia ufanisi.”
Bi Mutuku na Bw Kabasa nao walikumbatiana kwa furaha punde tu matokeo yalipotangazwa.
Katika hotuba yake Bw Njagi aliahidi kufanya kazi na wanahabari kutoka vyumba vyote vya habari ambao huripoti kutoka bunge huku akiwapongeza wenzake alioshindana nao.
“Kwanza nawapongeza ninyi wanachama wote KPJA kwa kunipa heshima ya kuwa mwenyekiti wenu kwa kipindi cha mwaka mmoja ujao.
Naahidi kuwahudumia kwa bidii na moyo wa kujitolea na bila ubaguzi wote. Mimi sio bora zaidi kuliko wenzangu ambao niliwashinda… kwa hivyo nitashauriana nao kila wakati,” akasema Bw Njagi huku akishangiliwa na wanachama.
Kwa upande wake, mwenyekiti anayeondoka Bw Gedion Keter wa gazeti la The Star aliwapongeza maafisa wapya waliochaguliwa na kuahidi kuwaelekeza ili waweze kuwahudumia wanachama ipasavyo kulingana na katiba ya chama hicho.
“Ni furaha yangu kwamba uchaguzi wa Ijumaa umeendeshwa kwa njia nzuri na wagombea wote wameridhishwa na matokeo. Napongeza wenzetu walioshinda, wakiongozwa na Bw Njagi, na kuahidi kuwa nitawapa ushauri wowote ambao watahitaji. Nawahongera pia wale walioshindwa kwa kuonyesha ukomavu,” akasema.
Mojawapo ya malengo ya KPA ni kushirikiana na asasi ya bunge kuwawezesha wanahabari kupata habari, kuhusu shughuli za bunge kwa njia faafu.
Chama hicho pia kinashirikiana na mashirika mbalimbali kwa lengo la kutoa mafunzo ya kila mara kwa wanahabari ili waimarishe utendakazi wao.
Viongozi na wanachama wa KPJA pia huandamana na Spika wa Bunge Justin Muturi, wabunge na maafisa wa bunge katika ziara zao nje ya nchi kwa shughuli mbalimbali muhimu za kikazi.
Kwa mfano, wiki iliyopita mwenyekiti anayeondoka Bw Keter na mwanachama John Nyaga (mpiga picha wa runinga ya K24) waliandamana na Spika Muturi katika ziara ya kikazi jijini Gaborone nchini Botswana.
Bw Muturi alikuwa amehudhuria Kongamano la 46 la Shirikisho la Mabunge ya Mataifa Wanachama wa Jumuiya Madola, ukanda wa Afrika (CPA-A).
Spika Muturi alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati Kuu ya shirikisho hilo wakati wa kongamano hilo ambalo lilidumu kwa siku kumi.
Orodha Rasmi ya Wanachama wa KPJA 2018
1. Edward Kabassa, KBC TV
2. Crane Senteman, Ebru Tv
3. Laban Wanambisi, Capital FM
4. Geofrrey Mosoku, The Standard
5. Josphine Karani, Bunge TV
6. Simon Macharia, Inooro TV
7. Stephen Letoo, Citizen TV
8. Anthony Mwangi, The People Daily
9. Mercy Mwai, The People
10. Carol Korir, Baraka Fm
11. Lucy Kilalo, Taifa Leo/ Taifa Jumapili
12. Lynette Igadwa, Business Daily
13. Ruth Njuguna, Radio Citizen
14. Grace Njihia, Kameme TV
15. Chris Nyamuta, Baraka FM
16. Kennedy Mureithi, NTV
17. Grace Ndungu, Ebru TV
18. David Mwere, Daily Nation
19. Elizabeth Mutuku, ATG Radio
20. Dina Ondari, The People Daily
21. Jane Goin, K24 TV
22. Patrick Amimo, KTN News
23. John Nyaga, K24
24. James Murimi, The People Daily
25. Charles Wasonga, Taifa Leo/Taifa Jumapili
26. Glady Mungai, Inooro Tv
27. Joseph Njane, Redio Citizen
28. Ibrahim Oruko, Daily Nation
29. Hillary Mageka, Xnews
30. James Mbaka, The Star
31. Boniface Okendo, The Standard
32. Moses Njagi, The Standard
33. Edwin Obuya, Redio Citizen
34. Aaron Kinamaso, ATG Redio
35. Halima Osman, Iqra FM
36. Zainab Ismael, Iqra FM
37. Dancan Khaemba, KTN News
38. Chris Thairu, KTN News
39. Cecilia Wakesho, KTN News
40. Eric Munene, Inooro Fm
41. Daniel Psirmoi, The Standard
42. Samwel Owino, Daily Nation
43. Kevin Wachira, KBC TV
44. George Okachi, Ebru TV