Bobi Wine kutibiwa London, maumivu yamzidi
NA PETER MBURU
Mwanasiasa Bobi Wine pamoja na mwenzake Francis Zaake wa Uganda watasafirishwa hadi Jijini London kwa matibabu, kutokana na majeraha mabaya ya mwilini waliyopata baada ya kuteswa wakiwa korokoroni.
Mawakili wa wabunge hao wamesema wamezungumza na daktari wa hospitali ya kifahari huko London, ambaye atawahudumia wabunge hao wa Kyadondo Mashariki na Mityana.
“Tumezungumza na daktari Martin Griffin ambaye anafaa kuwapokea wabunge hao,” akasema Bw Mao, wakili wao baada yao kuwachiliwa huru kwa bondi.
Gazeti moja la Uganda liliripoti kuwa Bw Zaake yuko kwenye hatari ya kupata ulemavu wa maisha, likirejelea ripoti ya siri aliyowasilisha daktari mmoja kwa familia ya mbunge huyo na kwa maafisa wakuu wa bunge la nchi hiyo.
“Ana uchungu mwingi kwenye uti wake wa mgongo kuanzia shingoni kuteremka. Majeraha yake yanahitaji ukaguzi zaidi kutoka kwa mtaalam,” Dkt Andrew Ssekitoleko akaandikia spika wa bunge la nchi hiyo, Rebecca Kadaga.
Alisema majeraha ya mbunge huyo yasipotibiwa ipasavyo na kwa umakini yanaweza kumsababishia ulemavu milele.
Mkewe Bobi Wine naye alieleza kuwa mumewe alikuwa akishangaa ilikuaje bado alikuwa uhai, baada ya mateso ya aina hiyo.