• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 7:55 PM
China kuondoa faini ya kuzaa watoto wengi

China kuondoa faini ya kuzaa watoto wengi

MASHIRIKA NA PETER MBURU

BEIJING, UCHINA

Huenda Uchina ikalazimika kuondoa vizingiti kwa wanandoa kuhusu idadi ya watoto watakaopata, baada ya gazeti moja la serikali nchini humo kuripoti Jumatatu kuwa kuna sheria inayoandaliwa.

Kwa miaka mingi, sheria nchini humo imekuwa ikielekeza idadi ya watoto wanaofaa kupata wanandoa, watu wakizuiliwa kuzaa kupita kiwango fulani.

Wengi wanaokiuka sheria hiyo wamekuwa wakipigwa faini ama wengine kulazimishwa kuavya mimba, huku wengine wakipewa dawa za kufunga uzazi wanapofikisha idadi ya watoto wanaohitajika, katika taifa hilo lililo na watu wengi zaidi duniani.

Gazeti la Procuratorate Daily Jumatatu lilisema sheria mpya inayoandaliwa haijarejelea kitu chochote kuhusu ‘upangaji uzazi’, kinyume na sheria ya sasa inayoweka wazi kuwa wanandoa hawafai kupata zaidi ya watoto wawili.

Sheria hiyo inatarajiwa kufikishwa katika bunge mnamo 2020 ili kuidhinishwa.

Sheria ya kupunguza idadi ya watu nchi hiyo ilianza 1979, wakati chama cha Columnist kiliweka sheria kuwa wanandoa wazae mtoto mmoja tu.

Lakini miaka miwili iliyopita, sheria ilibadilishwa na idadi ya watoto ikaongezwa kuwawili kwa kila wanandoa, baada ya idadi ya wazee kuwa ya juu kuliko vijana.

Sasa kuna hofu kuwa kutokana na idadi kubwa ya watu nchini humo kuwa wazee, maendeleo yanaweza kwenda chini, huku utofauti wa idadi ya jinsia tofauti ukizidisha hofu.

Sheria hiyo ilijadiliwa katika kikao cha bunge la nchi hiyo, wakati wa kongamano linaloandaliwa hadi Ijumaa.

Mapendekezo mengine kwenye sheria hiyo ni wanandoa kupewa kipindi cha mwezi mmoja kabla ya kutalikiana kabisa baada ya kuweka maombi ya kufanya hivyo, ili kutoa nafasi ikiwa watawaza kuendelea kuwa pamoja.

Jumla ya watoto 17.9 milioni walizaliwa 2016 nchi hiyo, idadi ya 1.3milioni juu kuliko waliozaliwa mwaka mmoja mbeleni, kulingana na rekodi za nchi hiyo. Lakini mwaka uliopita idadi hiyo ilipungua hadi watoto 17.23milioni waliozaliwa.

You can share this post!

Theresa May kukutana na Rais Kenyatta Ikulu ya Nairobi...

Shinikizo kwa Kiir aachilie huru wafungwa wa kisiasa

adminleo