• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 12:45 AM
Shinikizo kwa Kiir aachilie huru wafungwa wa kisiasa

Shinikizo kwa Kiir aachilie huru wafungwa wa kisiasa

AGGREY MUTAMBO na PETER MBURU 

RAIS wa Sudan Kusini Salva Kiir anasukumwa na watetezi wa haki za binadamu kuwaachilia wafungwa wote wa kisiasa, ili kuleta amani ya kweli kama walivyokubaliana na hasimu wake Riek Machar wiki iliyopita.

Wiki iliyopita, wizara ya mawasiliano Juba ilitangaza kuwa serikali iliwachilia huru wafungwa 21 wa kisiasa kama sehemu ya kutekeleza maelewano ya amani, ingawa walioachiliwa hawakutajwa.

Lakini wanaharakati wanasema mamia yaw engine wanaendelea kuozea jela bila kuhukumiwa, wala kutembelewa na familia na mawakili wao.

Shirika la Human Rights Watch (HRW) lilisema kuwachiliwa kwa wafungwa hao sasa kunafaa kufuatwa na hakikisho dhabiti kuwa haki za watu zitaheshimiwa na wengine walio ndani kuwachiliwa.

HRW inataka wanaharakati Samuel Dong Luak, Aggrey Idri na James Gatdet Dak, ambaye aliwahi kuwa msemaji wa Bw Machar na wote ambao wamekuwa wakosoaji wa Rais Kiir. Wote walitimuliwa Nairobi miaka miwili iliyopita.

Mwingine aliye ndani ni mchanganuzi katika vipindi vya NTV asubuhi Dkt Peter Biar Ajak, ambaye alikamatwa Julai katika uwanja wa ndege wa Juba.

“Ingawa familia yake imeruhusiwa kumtembelea, shirika la Amnesty limeshangazwa na kuzuiliwa kwake jela. Amenyimwa haki ya kumwona wakili na hajafikishwa kortini hadi sasa,” likasema shirika la Amnesty International.

Kunao viongozi wengine wengi, wengi wao wakiwa wakosoaji wa Rais Kiir ambao sasa wako jela japo hawajashtakiwa wala kuhukumiwa.

Punde baada ya Rais Kiir na Bw Machar kutia sahihi maelewano ya amani jijini Khartoum awali mwezi huu, mataifa ya US, UK na Norway yalitoa wito kwao kujitolea kuweka amani na uongozi mzuri.

“Tunaunga mkono mapenzi ya watu wa Sudan Kusini kuishi bila hofu, kuwa na amani, maendeleo na kujumuisha wote,” yakasema mataifa hayo ambayo yamekuwa yakiongoza juhudi za maelewano, kwa habari ya pamoja.

You can share this post!

China kuondoa faini ya kuzaa watoto wengi

Uhuru awarai wawekezaji Amerika wamsaidie kuafikia Ajenda...

adminleo