• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 9:50 AM
Mwanasiasa atisha kuishtaki NLC kwa kunyima wakazi haki ya ardhi

Mwanasiasa atisha kuishtaki NLC kwa kunyima wakazi haki ya ardhi

NA KALUME KAZUNGU

MWAKILISHI Mwanamke wa zamani wa Kaunti ya Lamu, Bi Shakila Abdalla ametisha kumshtaki aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Kitaifa ya Ardhi nchini (NLC), Muhammed Swazuri na tume yote kwa jumla kufuatia kile anachodai kuwa ni kuwasaliti wakazi wa Lamu na kukandamiza haki yao ya kumiliki ardhi.

Katika kikao na wanahabari mjini Lamu Jumanne, Bi Shakila alisema Swazuri amekuwa mstari wa mbele kutwaa ardhi za Lamu kiholela na kwa lazima kwa madai kwamba zilifaa kuendelezewa miradi ya kitaifa.

Bi Shakila alisema idadi ya maskwota kaunti ya Lamu imekuwa ikiongezeka kila kuchao hasa tangu tume hiyo ilipoanza kuhudumu hapa nchini.

Alisema licha ya NLC kuundwa lengo kuu likiwa ni kukabiliana na kutatua  utata wa ardhi nchini, lengo hilo halijaafikiwa tangu tume hiyo ilipoanza kuhudumu.

Bi Shakila alisema anajadiliana na wakazi wa Lamu na kwamba hivi karibuni watafika kortini kuishtaki NLC na pia Bw Swazuri kwa kuwanyanyasa haki yao waziwazi.

“Ekari zaidi ya 2000 za Lamu zimetwaliwa kiholela chini ya uelekezi wa Bw Swazuri. Wakazi wenyewe wanaomiliki ardhi hizo hawajapata fidia yoyote.

Tunaambiwa ardhi zimetwaliwa kufanikisha miradi ya serikali na maendeleo mengine. Kwa nini Swazuri kutusaliti namna hii? Hatutakubali na tuko tayari kutafuta haki yetu kisheria kama suala hilo halitazingatiwa na watu wetu kupewa haki yao ya kumiliki ardhi,” akasema Bi Shakila.

Kauli ya Mwakilishi huyo wa zamani wa wanawake inajiri wakati ambapo Bw Swazuri tayari anakabiliwa na sakata ya ununuzi wa kimagendo wa ardhi ya Sh 221,375,000 ya ujenzi wa reli ya kisasa (SGR).

Bw Swazuri pia anakabiliwa na kesi ya kutumia ofisi yake vibaya, ukosefu wa uaminifu kazini na pia ukiukaji wa sheria katika utoaji wa mali ya umma miongoni mwa mashtaka mengine.

You can share this post!

KFCB kushtaki runinga zinazopeperusha matangazo ya kondomu

Mtoto ajiua kwa kusimangwa kuwa shoga

adminleo