• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 10:50 AM
Utata wa kesi dhidi ya Jaji Mwilu

Utata wa kesi dhidi ya Jaji Mwilu

Na RICHARD MUNGUTI

UTATA ulikumba kusitishwa kwa kesi ya ufisadi dhidi ya Naibu wa Jaji Mkuu (DCJ) Philomena Mwilu na Mahakama Kuu huku hakimu mkuu Lawrence Mugambi akikataa agizo alilopewa la kusimamisha kuendelea na kesi akisema inahusu kesi nyingine na wala sio hiyo dhidi ya jaji huyo mkuu wa pili katika Mahakama ya Juu.

Bw Mugambi alisema jinsi hali ilivyo, bado kesi dhidi ya Jaji Mwilu haijasitishwa lakini akalengeza kamba na kuruhusu agizo hilo lirudishwe kwa Jaji Enock Mwita akairekebishe.

Jaji Mwita alisitisha kusikizwa kwa kesi dhidi ya Jaji Mwilu anayetetewa na mawakili 32 akisema haki zake zimekandamizwa.

“Baada ya kusikiza ushahidi uliowasilishwa na Jaji Mwilu kupitia kwa wakili Okong’o Omogeni ni dhahiri haki zake zimekandamizwa. Amezua masuala mazito na makuu ya kisheria na kikatiba  yanayohitaji kuamuliwa. Hivyo nasitisha kesi iliyowasilishwa dhidi ya Jaji Mwilu mbele ya hakimu mkuu Lawrence Mugambi,” aliamuru Jaji Mwita.

Jaji huyo aliagiza Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji , Mkurugenzi wa  Jinai (DCI) George Kinoti na Mwanasheria Mkuu wakabidhiwe nakala za kesi hiyo katika muda wa siku saba.

Aliamuru kesi isikizwe Oktoba 7,2018. Jaji alielezwa kushtakiwa kwa Jaji Mwilu ni mbinu ya kujaribu kumong’oa kazini kwa kumsingizia alifanya uhalifu.

Ni agizo hilo la Jaji Mwita iliyozua utata huku kiongozi wa mashtaka Bi Dorcus Oduor akisema kesi iliyo kortini ni 38 ya 2018 na wala sio 292 ya 2018 kama agizo Ilivyosajiliwa.

Aliamuru mawakili James Orengo, Okong’o Omogeni , Cliff Ombeta , Wilfred Nyamu na Nelson Havi wanaomtetea Jaji Mwilu warudishe agizo hilo ikarekebishwe kwa kuwekwa nambari inayofaa.

Kesi iliyowasilishwa dhidi ya Jaji Mwilu mbele ya Bw Mugambi na viongozi wa mashtaka ni nambari 38 ya 2018 na wala sio nambari 292 ya 2018. Bi Oduor aliomba kesi dhidi ya Jaji Mwilu iendelee.

Lakini Bw Orengo alisema makosa sio yao mbali cheti cha mashtaka walichopewa na kiongozi wa mashtaka Bi Oduor kilikuwa nambari 292 ya 2018 na ndicho walikitegemea kuwasilisha kesi hiyo Mahakama kuu.

“Haya ni makosa madogo yanaypweza kurekebishwa kwa vile walalamishi ni Jaji Mwilu na wakili Stanley Kiima na wako mbele ya korti na ndio walalamishi,” alisema Bw Orengo huku akiomba apewe muda kurudi kwa Jaji Mwita kurekebisha makosa hayo kwa kuandika namba ipasayo.

Bi Oduor anayeongoza kesi hiyo dhidi ya Jaji Mwilu na Bw Kiima hakupinga kesi hiyo ikurudishwa kwa Jaji Mwita kuirekebishwa.

Lakini alisema agizo hilo inamuhusu tu Jaji Mwilu na wala sio Bw Kiima.

Mawakili Orengo, aliyekuwa makamu wa Rais Kalonzo Musyoka , Dkt John Khaminwa na Morris Kimuli wanaowatetea Jaji Mwilu na Bw Kiima walipinga washukiwa hao wakisomewa mashtaka wakisema “ hayana mashiko kisheria.”

Mabw Orengo , Musyoka na Khaminwa walimweleza Bw Mugambi hana mamlaka ya kusikiza kesi dhidi ya Jaji Mwilu kwa vile “ hakuna makosa aliyofanya Jaji Mwilu.”

Walisema mashtaka hayo ni yakumfedhesha Jaji Mwilu ni mbinu ya kumng’oa kazini.

Hakimu alifahamishwa waliokuwa DCJ Nancy Barasa na Kalpana Rawal walitimuliwa kazini kwasababu duni.

“Na sasa ni zamu ya Jaji Mwilu kutimuliwa kwa visingizio tu na watu fulani wanaoketi mahala na kupanga njama za kufanyia idara ya mahakama mabadiliko. Ni bahati mbaya wamekuwa wakliwalenga wanawake ambao wameteuliwa kuwa DCJ,” alisema Dkt Khaminwa.

Bw Orengo alimweleza Bw Mugambi kuwa kile DPP amesema ni makosa dhidi ya Jaji Mwilu ,  ni mkopo aliopewa na Benki iliyofilisika ya Imperial Bank miaka mitano iliyopita na “ aliulipa. Hadaiwi”

Alisema kuwa wakili Kiima anayeshtakiwa pamoja naye alitayarisha karatasi za kuomba mkopo na kwamba alilipa ada zote za kodi iliyoitishwa na idara husika za Serikali.

“Hii ni fitina tu dhidi ya Jaji Mwilu hajafanya makosa. Hakuna makosa aliyofanya hata! Tutawasilisha ushahidi kuthibitisha hakuna makosa ya uhalifu aliyofanya Jaji Mwilu,” alisema Bw Orengo.

Aliomba korti iamuru kesi  hiyo ipelekwe Mahakama kuu wakapinge hatua ya DPP kumfungulia mashtaka jaji huyu wa pili kwa ukuu. Korti iliambiwa DPP angelimuhusisha Inspekta mkuu wa Polisi (IG) Joseph Boinnet badala ya DCI Bw George Kinoti.

Alisema DPP alipotea njia kumfungulia mashtaka Jaji Mwilu kabla tume ya kupambana  na ufisadi kumchunguza na kupendekeza ashtakiwe.

Pia walisema tume inayowaajiri wafanyakazi wa idara ya mahakama JSC ambapo Jaji Mwilu ni mwanachama haikukabidhiwa malalamiko na kumchukulia hatua ifaayo kisheria.

Wote wawili waliachiliwa kwa dhamana ya Sh5 milioni.

 

 

You can share this post!

Mtindo wa kutimua manaibu jaji mkuu wanawake wakejeliwa

Ajabu ya mteja kuwa na mawakili 32

adminleo