Nyama ya Raila haipo – Uhuru
Na PETER MBURU
RAIS Uhuru Kenyatta amepuuzilia wito wa kumtaka amuundie kiongozi wa ODM Raila Odinga nafasi katika serikali yake, baada ya kuafikiana mnamo Machi 9, akisema haruhusiwi na katiba.
Tangu muafaka huo ulioambatana na salamu ya kipekee, wengi wa viongozi wa upinzani wamekuwa wakitaka katiba kufanyiwa mabadiliko ili Bw Odinga aundiwe nafasi serikalini.
Wengine wamekuwa wakipendekeza afanywe balozi wa hadhi ya juu ambaye atazuru mataifa yaliyozongwa na vita na kutafuta amani huko.
Hata hivyo, katika mahojiano na BBC alipokuwa Marekani juzi, Rais Kenyata alisema kisheria hilo haliwezekani.
“Kwanini tutengeneze nafasi yoyote mpya? Tunafanya kazi kulingana na katiba. Lakini tutashirikiana na Raila kwa masuala ya maendeleo,” akasema Rais.
Aidha katika mahojiano hayo, Rais Kenyatta aliwakemea wale ambao humkosoa babake, Rais wa kwanza wa jamhuri ya Kenya Mzee Jomo Kenyatta kuwa alijitajirisha kwa njia zisizo za haki, akiwaambia yeyote aliye na ushahidi kuwa mali iliyo nayo familia ya Mzee Kenyatta ilipatikana kwa njia zisizoeleweka ajitokeze.
Siku chache baada ya Rais Kenyatta kutangaza kuwa maafisa wa umma watakaguliwa kuhusiana na mali wanayomiliki, Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi alisema ukaguzi huo utakuwa waki endapo hata wazee kama Mzee Kenyatta watakaguliwa namna walivyopata mali yao.