• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 8:50 AM
Serikali yaahidi kukamata wafisadi zaidi

Serikali yaahidi kukamata wafisadi zaidi

Na PETER MBURU

TIMU ya pamoja iliyoundwa kwa ajili ya kupambana na ufisadi (MAT) imewaahidi Wakenya kutarajia watu zaidi kukamatwa kuhusiana na ufisadi katika siku zijazo.

Timu hiyo iliyoundwa kufuatia maelekezo ya Rais Uhuru Kenyatta ilieleza bunge kuwa faili zaidi ambazo zinahusisha watu wakubwa zinashughulikiwa na kuwa watakamatwa zikimaliziwa.

“Tuna faili nyingi katika ofisi ya kiongozi wa mashtaka ya umma (ODPP) na zingine bado zinawasilishwa. Kwa hivyo nataka kuwaambia Wakenya wasubiri visa zaidi vya watu kukamatwa kutoka kwetu ama MAT,” akasema naibu mkurugenzi wa tume ya maadili na kupambana na ufisadi (EACC) Michael Mubea alipofika seneti.

Hakikisho la Bw Mubea limekuja baada ya naibu wa Jaji Mkuu (DCJ) Philomena Mwilu kukamatwa kufuatia tuhuma za ufisadi Jimanne.

Bw Mubea alizungumza katika mkutano ulioandaliwa na kamati ya haki na masuala ya kisheria katika bunge la seneti, ambapo DPP Noordin Haji, mkuu wa upelelezi (DCI) George Kinoti, mkurugenzi wa mamlaka ya kutwaa mali Muthoni Kimani na kamishna wa mamlaka ya kukusanya ushuru nchini (KRA) Githii Mburu, pamoja na wanachama wengine wa MAT.

Bw Mubea alisema shughuli za kutwaa mali ya umma yaliyokuwa yameibiwa zilikuwa zikiendelea, akiongeza kuwa kuna kesi kortini zinazohusisha mali ya Sh10bilioni.

“Tunasonga kutoka kuwakamata tu wafisadi tukielekea kutwaa mali waliyoiba. Tunajua watu hujihusisha na ufisadi ili kupata mali, tuko kortini tukitaka kutwaa mali yaliyopatikana kufuatia ufisadi,” Bw mubea akasema.

Alisema EACC imepeleka juhudi za kukagua visa vya ufisadi katika serikali za kaunti ili kubaini udhaifu ambao umepelekea visa vya ufisadi kuongezeka.

Bi Muthoni alisema kesi zinazohusu mali ya takriban Sh61bilioni ziko katika mahakama tofauti nchini, ikiwemo ile ya benki ya Imperial iliyoanguka nay a sakata ya Ango Leasing hizo zikihusisha Sh35bilioni kwa jumla.

You can share this post!

Lazima samaki wote katika ziwa la ufisadi wavuliwe kabla ya...

Benki ya Peter Kenneth yapata hasara ya mamilioni

adminleo