• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Raila amtaka Haji akome kuingiza siasa katika vita dhidi ya ufisadi

Raila amtaka Haji akome kuingiza siasa katika vita dhidi ya ufisadi

Na VICTOR RABALLA

KINARA wa upinzani nchini Raila Odinga amemtaka Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka ya Umma (DPP) kutobinafsisha vita dhidi ya ufisadi na badala yake ahakikishe ana ushahidi wa kutosha kabla ya kuwakamata washukiwa.

“Hakuna kurudi nyuma kuhusu hili. DPP, Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) na mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi (DCI) hawafai kuwalenga watu fulani bila kutoa ushahidi wa kutosha,” akasema Bw Odinga.

Aidha, Bw Odinga aliwataka Wakenya kuunga mkono vita hivyo ili kusaidia serikali kukabiliana na wafisadi huku akisistiza kwamba ushirikiano wake na Rais Uhuru Kenyatta unalenga kufanikisha maendeleo kwa manufaa ya wananchi wote.

Waziri huyo mkuu wa zamani alikuwa akizungumza jana katika kijiji cha Segere, Kaunti ya Siaya wakati wa ufunguzi wa makazi mapya ya kibinafsi ya Gavana Cornell Rasanga.

“Vita dhidi ya ufisadi lazima vifaulu. Najua vita hivyo vitaathiri baadhi ya jamaa zangu na marafiki zangu wa karibu. Lakini nimewambia kila mtu awe tayari kubeba msalaba wake,” akasisitiza Bw Odinga.

Alitaka idara ya mahakama kuwahukumu wanaopatikana na hatia ya kushiriki ufisadi na kuongeza kwamba hiyo ilikuwa mojawapo ya maafikiano kati yake na Rais Kenyatta mna Machi 9.

Kauli ya Bw Odinga iliungwa mkono na Seneta wa Siaya James Orengo ambaye alisema kwamba vita hivyo vitasaidia kuimarisha uchumi wa nchi.

“Kila mfanyakazi wa serikali lazima ahakikishe mambo yanatekelezwa kisheria. Kama wewe ni mwizi lazima ujitayarishe kubeba msalaba wako bila kutegemea msaada wa mtu maarufu, kukimbilia jamii yako au dini,” akasema Bw Orengo.

Aliongeza kuwa chama cha ODM hakitamtetea kiongozi wake yeyote anayekabiliwa na tuhuma za ufisadi.

You can share this post!

Wasamburu waipa serikali siku 2 wamwachilie Lesiyampe

Utawala wa Moi ulitesa Pwani, Joho aambiwa

adminleo